Njia nyembamba (Simulizi mpya by SteveMollel)

Njia nyembamba -- (msimu wa pili) 04


Mtunzi: SteveMollel


Kabla ya yeyote hajatia neno, ghafla ulisikika mlio wa risasi kisha sauti ya kuamuru:

“Wote chinii!”

Kwa hofu watu walilala chini upesi. Sauti za wanawake zilisikika zikipiga yowe ila ndani ya muda mfupi zikakoma baada ya kuamriwa hivyo na mwanaume mmoja miongoni mwa watano waliokuwa wamevamia eneo hilo.

Nyuso zao zilikuwa zimefunikwa na vinyago vyeusi na mikononi walikuwa wamebebelea bunduki ndogo na SMG. Walivalia matisheti meusi na suruali nyeusi pia.

Walinzi wa Talib hawakuweza kufanya kitu chochote kwakuwa hawakuwa na silaha hivyo nao walikuwa wamelala chini wakitulia kulinda maisha yao.

Wale majambazi walijigawa kwenda pande tofauti tofauti wakaanza kusachi mifuko ya watu na kubeba waleti na pochi za wanawake. Wakati tukio hilo linafanyika mziki uliwa umezimwa kukiwa kimya.

Wanaume wale watano walikomba kila kitu wakilazimisha wahanga kutoa kila kitu cha thamani walichonacho. Pale mhanga alipokuwa mkaidi basi nguvu ilitumika kwa kupigwa mateke ama kwa kitako cha bunduki.

Baada ya muda mfupi, mmoja wa wale majambazi alimfikia Talib. Alimpukutisha kila kitu kuanzia simu ya thamani, pete, cheni, waleti na pesa za kutosha.

Ila kabla hajaondoka, aligundua mwanaume yule aliyemtenda ni mtu mkubwa serikalini – waziri, tena waziri wa ulinzi! Alijikuta anastaajabu lakini baada ya muda mfupi akatabasamu na kupaza sauti kuwaita wenzake wamshuhudie mtu yule.

Wenzake wawili walisogea kushuhudia wakati wawili wakibakia kuendelea kudumisha ulinzi. Walimtazama Talib na kweli wakagundua ndiye yule waziri wa ulinzi.

Walijikuta wanacheka na kuanza kumdhihaki. Lakini zaidi kumtuhumu juu ya serikali.

“Nyie ndio mnafanya maisha yetu yawe magumu, mahayawani wakubwa!” Alifoka mmoja.
“Ni bora upo humu, ngoja upate kile unachostahili,” akadakia mwengine. Alimkandika Talib mateke ya tumbo na mbavu mpaka akamcheulisha damu.

“Inatosha. Tuondokeni sasa!” alishauri mwanaume mmoja. Walichukua ufunguo wa gari wa Talib kisha wakaondoka zao kwenda sehemu ya kupumzisha magari.

Huko haikuwachukua hata muda mrefu kulitambua gari la waziri, jaguar nyeusi, gari ghali kuliko yote pale. Walijiweka humo ndani na kupotea kwa mwendo mkali.

Walikimbiza gari hilo kama toy na kana kwamba vile humo ndani kulikuwa kuna magazeti, si binadamu. Ndani ya muda mfupi sio tu kwamba hawakuwa wanaonekana maeneo ya karibu, walikuwa hawaonekani kabisa!

Polisi na wanajeshi kadhaa walifika eneo la klabu baada ya dakika kama kumi na tano. Walikuwa watu wakiwa wametawanyika.

Talib, rafikiye na walinzi wake ndio walikuwa wanazungukazunguka mbele ya klabu. Nyuso za walinzi zilikuwa nyekundu kwa kuzabwa makofi mfululizo na Talib akiwatuhumu hawana faida na hawajui kazi yao.

“Nawalipa bure tu hawa nguruwe!” Aling’aka. Mdomo wake ulikuwa umepasuka kwa pembeni. Hakuonekana nadhifu; suti yake ilikuwa imechafuka na haikuwa mpangilioni.

“Nimesema hivi, leo ndio mwisho wa kazi yenu. Nahitaji watu wa kunilinda na sio kunisindikiza!”

Akamgeukia na rafiki yake. Akamtazama na macho yanayowaka moto.

“Na wewe kumbe ni punguani mzee kabisa! Ulishindwa kupiga simu na ulikuwepo VIP?”

“Nisingeweza wa…”

“Kwanini usingeweza?”

“Walikuwa wamekuja hadi kule. Sikuwa na fursa ya kufanya kitu.”

“Sasa nyie mna faida gani?” Aliuliza Talib akiwanyooshea mkono walinzi na rafiki yake.

Hakuishia tu hapo alihamia pia hadi kwa polisi na wanajeshi waliofika eneo hilo kwa kuwaita wazembe na wasiofaa kazini.

Wamechelewa kufika tukioni na hilo jambo lingeweza kugharimu maisha yake, hivyo basi kugharimu pia na taifa.

“Sasa nasema hivi …” alisema akiwa amekunja sura. “Hao washenzi walionidhalilisha wakamatwe haraka! Wakamatwe leo hii na wanyongwe mbele ya hadhara!”

Aliweka kituo na kuuliza:
“Mmenielewa?”
“Ndio, mkuu!” Akajibiwa.
“Sasa kama hamjanielewa, mtaenda kulielewa kaburi!” alitoa kitisho hicho kisha akaondoka zake kufuata mojawapo ya gari walilokuja nalo wanajeshi. Alitekenya ufunguo, akaondoka zake peke yake.

Baada ya masaa matano: Ni asubuhi ya saa mbili.

Palepale kwenye eneo lao la kawaida la kukutana, mgahawa ulio karibu na fukwe ya bahari, Kone na Rose wakiwa wamewasili ndani ya muda mfupi, waliagiza juisi za parachichi na vitafunwa vyepesi.

Kone alikuwa amevalia suti nyeusi isiyo na tai, kama apendavyo, huku Rose yeye akiwa amevalia gauni refu rangi ya udhurungi na viatu vyenye visigino virefu vilivyomfanya aonekane mrefu kuliko Kone, kitu ambacho si kweli.

Baada ya kunywa mafundo kadhaa ya juisi kwa kupitia mirija mipana, Kone alijikuta anasonya kabla ya kufungua mdomo wake kuanza maongezi rasmi ya kile kilichowaleta pale.

“Mpaka sasa simu haipokelewi,” alisema kwa sauti yenye mashiko ya huzuni. Kwa kupitia dirisha kubwa la kioo la mgahawa, alitazama mawimbi madogomadogo ya bahari yakipiga ufukweni.

“Wananipa wakati mgumu sana,” aliendelea kulalamika. “Na muda nao ndio hivyo unazidi kuyoyoma kama upepo.”

Rose alikunywa juisi yake mafundo mawili kabla hajang’ata sambusa yake ya nyama na kuirudisha sahanini.

“Sasa tunafanyaje, Kone?” Aliuliza. Uso wake haukuwa na shaka hata kidogo tofauti na ule wa Kone ulioonekana kukanganyikwa. Alikuwa anatafuna kwa madaha sambusa yake mdomoni kana kwamba ni jojo.

“Rose, inabidi ufanye jambo. Hatuwezi tukaendelea kungoja zaidi ya hapa.”

“Najua. Jambo gani sasa tufanye?”
“Mtafute Kessy!” Kone alipaza sauti. Alijishitukia kwa kutazama mazingira yake kama kuna mtu amemsikia. Alipoona hakuna, akaendelea kuongea. Sasa akiwa amepunguza sauti.

“Mtafute, hakikisha unamsumbua vya kutosha. Hakikisha unaonana naye kesho ama keshokutwa.”

Rose akanywa juisi na kung’ata sambusa yake akimtazama Kone.

“Tukikaa kumngoja akutafute, tutakesha, na hatuna huo muda. Inawezekana hata akawa amekusahau, wewe si mwanamke pekee mrembo anayekutana naye.”

“Hilo sio shida Kone. Lakini unajua kwamba tukimuua huyo jamaa, tutakuwa tumetangaza vita rasmi na wale waasi?”

Ukimya ukachukua sekunde tatu.

“Unajua walivyo vema kimapambano na namna walivyojipanga,” Rose aliendelea kudadavua. “Kwa sasa adui wao ni jamaa madarakani, kwahiyo tutakapomuondoa, sisi wakaimu ndio tutakuwa maadui.”

“Hilo lisikupe shaka, Rose.” Kone alitikisa kichwa. “Sisi tuna nchi yetu, hapa tunakuja tu kutimiza kile kilichokuwa ndani ya mkataba. Tutakapomuua huyo jamaa basi tutapata upenyo wa kufanya yetu. Mpaka waje kuunda serikali sisi tutakuwa tumeshakwenda!”

“Wale waasi watatuacha salama?”

“Watatujulia wapi? Watatuonea wapi? Watatupatia wapi?”

Rose akanywa juisi yake mpaka akaimaliza.

“Sawa,” alijibu akipandisha bega lake la kulia. “Nitafanya hicho ulichosema.”

“Saa ngapi? Fanya sasa hivi!” Kone alisihi. Rose alitoa simu yake kwenye pochi yake kubwa aliyokuwa ameilaza juu ya meza, akatafuta namba ya Kessy na kumpigia.

Simu iliita lakini haikupokelewa. Rose alimtaarifu Kone. Kone akamtaka aendelee kujaribu.

Mara tano, simu haikupata wa kuiitikia.

“Atakuwa yupo bize,” alisema Kone. “Ni mkubwa wa nchi, ana kazi nyingi. Lakini hakikisha utamtafuta tena baadae.”

“Sidhani kama kuna haja. Akikuta missed calls zangu atanitafuta mwenyewe.”
“Rose, una uhakika?”
“Asilimia zote.” Akajibu mwanamke huyo akirembua macho. Aliagiza juisi nyingine anywee sambusa yake moja iliyobakia kwenye sahani.

Baada ya masaa nane: saa kumi ya jioni.

“Unamwamini lakini?” Mou aliuliza. Macho yake yalikuwa yanamtazama Amadu kwa mashaka baada ya kutoka kumtazama mgeni wao aliyeletwa na mwenzao huyo.

Amadu alimshika Mou begani akisema:
“Niachie mimi.”

Mou akapandisha kichwa chake kabla hajaketi kitini kuwakuta wenzake: Farah, Mou, Chui, Ussein na Ulsher waliokuwa wamejaa kwenye kiti kimoja kikubwa na kirefu.

Ulikuwa ni wasaa wa Amadu kukabidhi majukumu kwa mgeni wao ambaye alijitambulisha hapo asubuhi kwa jina la Fredy. Ndani ya asubuhi hiyo Fredy alijieleza wapi alipotokea, familia yake, asili yake na nini alichokuwa anafanya kusogeza maisha.

Baada ya hapo alipewa muda wa kupumzika kabla ya tena muda huu kuwekwa kati ya THE GHOSTS kwa ajili ya kupewa jukumu ambalo lilikuwa na sura ya jaribio, kama vile alivyosema Amadu.

“Tunahitaji watu waaminifu, wasiri na wachapakazi kwa ajili ya kujiunga kwenye kundi letu.” Alifungua mjadala kwa kunena hivyo. Watu wote walikuwa wanamsikiliza, ila Fredy alifanya hilo kwa umakini zaidi.

“Umesema tunaweza tukakuamini, si ndio?”
“Ndio,” Fredy alijibu akitikisa kichwa.
“Sawa, na tumetokea kukuamini hilo. Lakini nataka nikujulishe mapema kwamba, kama hauwezi kazi ni bora ukasema sasa. la sivyo ukikiuka yale tuliyokubaliana, tutakutafuta popote pale ulipo. Tutakupata, na tutakuua!”

Baada ya maneno hayo Fredy alikabidshiwa kiasi kadhaa cha pesa kisha akapewa maelezo ya kwenda kutafuta wenzake anaowaamini wataweza kazi.

Akiwapata basi atawapeleka mahala fulani karibu na fukwe, huko THE GHOSTS watakuja kuwatwaa.

Hilo jambo inabidi liwe la siri mno. Hakuna yeyote anayetakiwa kujua isipokuwa hao wahusika tu. Na wale wote atakaowafuata kuwashawishi basi wawe ni watu ambao anawajua kwa undani, si mtu mgeni wala mtu ambaye anamjua kwa rasharasha.

Awe ni mtu ambaye akiulizwa upatikanaji wake basi litakuwa ni jambo linalowezekana ndani ya muda mfupi.

Fredy aliridhia hayo akaondoka zake. Alinyookea nyumbani kwao kwanza kuwajulia hali wadogo zake wawili walioshinda njaa siku nzima. Aliwaletea chakula alichowaachia na kisha akaenda kufanya kile alichotakiwa kufanya muda huo.

Alienda kwa rafiki yake wa kwanza ambaye aliongea naye kwa muda wa dakika kama ishirini. Alipotoka hapo akanyooka tena na barabara kama mwendo wa kilomita moja, akagonga kwenye nyumba fulani ndogo, ambapo humo alitoka msichana mweusi aliyefunga kiremba.

Aliongea naye kwa sekunde chache kabla msichana huyo hajaingia ndani na kisha kutoka mwanaume mfupi mwembamba. Alimvutia mwanaume huyo pembeni ya nyumba. Akahakikisha usalama kwanza na kuanza kuteta naye.

Alitumia hapo dakika kama kumi na kitu hivi kabla hajapaena mkono na mwanaume huyo na kuondoka. Alitembea tena kwa mwendo wa nusu kilomita ndipo akakutana na nyumba nyingine ambayo hiyo hakuhitaji kuigonga mlango maana alimkuta mlengwa wake nje.

Aliongea naye kwa dakika kama ishirini, wakapeana ‘tano’ akaondoka zake.

Usiku ulikuwa umeanza kuchukua fursa. Mataa yaliwashwa barabarani na hata majumbani. Fredy kana kwamba hakuona giza hilo, aliendelea kutembea.

Hata hakuwa amepumzika wala kutia chochote mdomoni. Alikazana na mwendo wake haukuwa umepungua tokea pale alipoanza hilo zoezi.

Alimalizia nyumba kama tatu kisha akaanza safari yake ya kurudi nyumbani. Hakuhitaji kukaba siku hiyo, kukwapua wala kukesha usiku mzima mtaani kutafuta pesa kwani alikuwa nayo mkononi.

Akilini mwake alikuwa anawafikiria wadogo zake tu na kupumzika kabla ya kuamka kesho mapemba aende fukweni.

Akiwa anatembea zake kichwani akiwa na hizo tafakuri za familia na harakati yake changa ya mapambano, ghafla kuna mtu alitokea mbele yake na kumsimamisha.

Alirudisha akili yake barabarani akamtazama mtu huyo, akagundua ni yule Rasta aliyekuwa anampatia kisago jana usiku. Alikuwa amevimba jicho lake la kulia hivyo kufanya uso wake utishe zaidi.

Rasta alisukuma Fredy akimuuliza:
“Ulidhani sitakupata?”

Fredy hakujibu kitu. Uso wake ulijikunja akimtazama mwanaume huyo mchokonozi.

“Nipe pesa yangu. Umenisikia?”

Kimya.

“Si naongea na wewe!” Rasta alimsukuma tena Fredy.
“Nipe pesa yangu!”
“Pesa ipi? Kama kuiba si tuliiba wote, na si nilikupa mgao wako?” Fredy alifungua kinywa chake kwa hasira.

Rasta alinyanyua mkono wake wa kuume amtwange Fredy ngumi, ila ajabu mkono huo ulikamatwa na mwingineo kwa nyuma. Rasta aligeuka haraka kutazama, akakutana uso kwa uso na Amadu.

“Naona bado hujajifunza,” alisema Amadu. Rasta akatabasamu kisha akatia vidole viwili mdomoni mwake kupiga mluzi. Baada ya muda mfupi wakatokea wanaume wawili waliofanana miili na Rasta.

“Leo upo kwenye himaya yangu,” alijigamba Rasta akitabasamu.

Amadu alimsogeza Fredy akamweka nyuma yake. Alikunja ngumi zake kubwa akitanua miguu yake kutafuta balansi.

“Haya naomba mnipatie hayo mazoezi,” alisema Amadu. Wanaume wale watatu wakaja kwa zamu.

Amini usiamini, hakuna aliyerusha ngumi wala teke. Amadu alipanda juu, na akiwa huko alifungua miguu yake mizito kuwashindilia mateke ya haja wanaume hao watatu waliojikuta chini ndani ya sekunde tatu tu!

Wote walikuwa wanaugulia chini wakiwa hawajiwezi kuamka, ama tuseme wakiwa wanategeana kuamka. Amadu aliwatazama kwa huruma kisha akamuuliza Fredy ni kiasi gani anachodaiwa na Rasta.

“Hanidai!” Fredy alijibu.
“Basi anataka kiasi gani?”

Fredy alijibu, Amadu akatoa kiasi hicho cha pesa na kumtupia Rasta.

“Nisikuone tena!” Amadu alisema kisha akamshika Fredy mkono kuelekea upande wa magharibi.

“Umefikaje hapa?” Fredy aliuliza.
“Nilikuwa nakufuatilia tokea umetoka getini,” Amadu akajibu.

Walitembea kidogo, wakasikia sauti ikimuita Fredy. Waligeuka nyuma wakamwona Rasta akija anachechemea huku akishikilia tumbo lake. Walimngojea mpaka mwanaume huyo akawakaribia. Walimtazama kwa hamu ya kutaka kujua wakati uso wa Rasta ukiwa rafiki.

“Naomba unifundishe,” alisema Rasta. “Nipo na wenzangu pia.”

Amadu alitumia sekunde mbili kuwaza. Akasema:

“Waite mnifuate.”



☆☆☆


☆Steve
 
hayahaya lesteve iti isi furaidei

Natamani iendelee tena na tena!
Haya njoeni wakuu wangu! Nimekuja.



☆Steve
Tuko pamoja

Leo ni jumamosi !!,......au imefikia tamati mkuu?


Yaani daaaah!! Mstue jamaa alete uhondo!!

Steve hachia kiunzi hicho


Wap Steve jaman mateja tunahangaika huku

tivu ukujeee jmos leo
 
Back
Top Bottom