Njia nyembamba (Simulizi mpya by SteveMollel)

Njia nyembamba -- (msimu wa pili) 03


Mtunzi: SteveMollel



Kone alishusha pumzi ndefu akatikisa kichwa chake. Mood yote ya tendo ya kula apple la Adamu ilikata. Kichwa chake kilitingwa na mawazo mzito juu ya THE GHOSTS na Raisi wake.


Aliona sasa mambo yanazidi kuwa magumu na yu njia panda ndefu. Ingawa mkewe alijitahidi kwa udi na vumba kupandisha hisia zake, jogoo wake alikuwa likizo na aligoma kabisa kurudi kibaruani.


Fatma anakwazika sana na jambo hilo. Atakaa na kiu yake hiyo mpaka lini na ilhali analala na mwanaume kitanda kimoja? Kwa namna moja alijiona aidha hampendezi mume wake, labda havutii na amepoteza uwezo wa kumsisimua laaziz wake.

Alisononeka na nafsiye. Mume wake alijitahidi kupooza makaa yake ya moto lakini hakufanikiwa abadani.


“Naomba unirejeshe nyumbani kwetu, Kone,” alisema na sauti ya juu.

“Kwenu kufanya nini Fatma?” Kone akauliza kwa sauti ya chini. Sauti yake ilikuwa imepooza na uso wake ulionyesha kweli ameguswa na kughafirika kwa mke wake.

“Kwetu kufanya nini?” Fatma aling’aka. “Hivi mie nimekuwa dada yako, sio?”

“Dada yangu kivipi?”

“Usijifanye mtoto, Kone. Kama haunipi haki yangu ya ndoa, ni bora nikaondoka niende kwetu. Kuna haja gani ya kukaa na mwanaume asiyenigusa wala asiye na hamu na mimi?”

“Lakini Fatma mama unaelewa ni hali …”

“Sielewi chochote, Kone. Na usidhani kama nitaelewa. Nimesema hivi, kesho nipeleke kwetu, la sivyo unipe haki yangu usiku huu mpaka n’tosheke.”

“Sawa. Nitakupa mke wangu. Hakuna haja ya kuzozana mpaka watoto huko wasikie.”

Kone alijitahidi kuvuta hisia ili apate kumhudumia mke wake, Fatma, lakini akashindwa. Uume haukupanda kabisa. Alijitahidi kumpapasapapasa mkewe lakini bado haikuleta mabadiliko. Hakuweza!

Fatma aliachana na mume wake huyo akageukia upande mwingine pasipo kuongea neno lolote. Alikuwa amevimba kwa hasira. Mwili wake ulikuwa una joto, kiu na haja lakini zilishindwa kutolewa.

Alidondosha chozi akisaga meno yake. Aliyafumba macho yake kuutafuta usingizi lakini ikamchukua muda mrefu kuupata.

Lakini kwa upande wa Kone alilala tu upesi. Sauti yake ya kukoroma ilimfikia Fatma masikioni na kumshangaza mwanamke huyo ya kwamba mume amelala haraka vile pasipo kujutia alichotoka kufanya.

Fatma aliishia kusonya na kuuminya mto alioulalia. Naye Mungu asimtupe, akampuzisha toka kwenye maumivu aliyokuwa nayo kwa kumpatia usingizi mzito. Alilala akikoroma kiwepesi.

Masaa yalijongea zaidi ndani ya usiku. Kichwa cha Kone bado kilirejelea mawazo ya kazi yake na hivyo basi ndani ya muda mfupi akaanza kuota mambo ya kazini kwake.

Alijiona yu ndani ya sebuleni kubwa iliyojazwa na sofa zenye nyama, hapo alikuwa pamoja na THE GHOSTS wakiwa wanateta mawili matatu kuhusu misheni yao ya kuupiku utawala wa Sierra Leone.

Ilikuwa ni wakati wa asubuhi na hivyo kukawa na vikombe vya kahawa mezani basi wakawa wakiteta huku wanatia kinywaji hicho mwilini. Maongezi yalikuwa ya manafanikio makubwa na yaliishia kwa kupeana mikono ya pongezi pia ikiashiria kwamba wapo pamoja.

Ila Pasipo kujua wakati akiwa ndotoni, Kone alikuwa anaongea kana kwamba ni kweli yupo katika mazingira hayo ya sebuleni. Maneno yake yalimfanya mkewe, bi Fatma, aamke kumtazama na kumsikiliza mume wake.

Na pasipo kumshitua mwanaume huyo, Fatma alisikiliza mpaka mwisho kisha akaendelea na usingizi wake.

Asubuhi na mapema Kone alipokuja kuamka, hakumkuta mwanamke kitandani. Alikuwa tayari ameshasomba nguoze na kuondoka. Alikuwa tayari ameelekea nyumbani kwao.

Kone aliamka kurupu akapepesa nyumba nzima asione mtu. Hata watoto hawakuwepo. Alichanganyikiwa na hakujua cha kufanya kwa dakika kadhaa kabla hajaamua kupiga simu ya mkewe. Simu iliita lakini haikupokelewa. Mwishowe alichoka akashika tama.

Alilaza kichwa chake sofani na mara akakumbuka jambo – kuwapigia simu THE GHOSTS! Haraka alitafuta ile namba iliyompigia jana yake usiku, akaiita na kuiweka simu sikioni.

Simu haikupokelewa. Na baada ya muda mfupi ikawa haipatikani!

Kichomi.


****



Muda wa kukaa kimya ulikuwa umetosha, kwahiyo sasa THE GHOSTS walikuwa tafakurini kipi kifuate katika misheni yao. Iliwalazimu wawe waangalifu sana na hatua zao zisiache nyayo za kumwezesha adui wao kuwapata kwa urahisi.

Walighani kadhaa ya kufanya ila kati ya hayo zito lililochomoza ni kuongeza kwanza nguvu ya kundi.

Sauti ndogo ya televisheni iliyokuwa hapo sebuleni haikuwafanya wasisikizane. Hakuna aliyekuwa anatizama televisheni hiyo hivyo kwa muda ilikuwa pweke ikitafuta mteja wakuiunga mkono.

Idadi ya watu sita wa THE GHOSTS kweli ilikuwa ndogo ukilinganisha na kazi kubwa waliyonayo mbele. Walihitaji watu zaidi. Lakini watu ambao wapo tayari kupambana kwa namna yoyote ile.

Watu wenye nia ya kweli na wapo tayari kutoa sadaka uhai wao ili kuikomboa nchi yao.

Hilo lilikuwa jema, ila shida kubwa ilikuja kwamba ni kwa namna gani watu hao watafunga vinywa vyao na kupanua vifua vyao kwa kutunza siri?

Jambo la kutafuta watu usiowajua ni hatari maana halina uhakika mkubwa wa kufuata yale mliyokubaliana, pia pana uzito na uweusi kwenye kuchambua; utajuaje wenye dhamira ya kweli na waliotumwa humo miongoni?

Hapo palikuwa pagumu sana. Na palifanya wengine waone si mpango sahihi.

“Serikali inaweza kutupata kwa urahisi endapo tukifanya hivyo,” alisema Farah.

“Ni kweli,” Mou akaunga mkono, pia akafuatiwa na Ussein na Chui.

“Wewe unasemaje?” Amadu aliuliza akimtazama Ulsher. Wote walikuwa kimya wakimtazama mwanamke huyo mwenye uso wa utulivu. Walikuwa wanangojea jibu kwa hamu pana, macho yao yalionyesha hivyo.

“Tunahitaji watu zaidi,” sauti ya Ulsher ikavuma juu ya sauti ya televisheni. Alienda kinyume na wenzake. Amadu alijikuta anatabasamu kana kwamba alikuwa anategemea jibu hilo.

“Hapana, siungi mkono!” Alisema Chui akitikisa kichwa.

“Tazama kule.” Ulsher akanyooshea kidole kwenye televisheni. Wote walitazama wakakuta taarifa ya habari ya CNN ikimuonyesha Al Saed, kiongozi wa kundi la Le tueurs la Liberia akiwa anatoa hotuba ya kwanza rasmi tangu ajiteue kuwa kiongozi wa nchi hiyo iliyopokwa kimabavu.

Chini ya kioo cha televisheni kulikuwa kuna maandishi meusi makubwa na madogo yakiwa ni machache mazito yaliyotoholewa toka kwenye hotuba husika. Mosi, nchi ya Liberia imekata mahusiano rasmi na nchi za Ulaya na Marekani, pili: hakutaruhusiwa shughuli zozote za kidemokrasia nchini, tatu na mwisho; anatazamia siku za usoni kuonana na rafikiye, bwana Kessy, wapate kuunda umoja wao utakaokuza uchumi wa nchi zao.

Kutokana na hicho alichoona, Ulsher aliamini wanahitaji watu zaidi kwani vita ni kubwa na adui hatokuwa mmoja. Hoja yake ikawa nzito masikioni mwa wenzake wasisite kukubali, ila sasa wakarejea kulekule kwenye mjadala wa mwazoni ambao kwa sasa Amadu aliomba akabidhiwe yeye hilo fukuto.

“Nadhani nitatafuta njia ya kulikwepa hilo,” alisema Amadu kwa kujiamini.

Baada ya masaa kumi na nne;

Ilikuwa ni usiku wa saa sita. Jiji la Freetown lilikuwa limepoa kwa kuwa na magari machache barabarani. Mataa yalikuwa yanawaka huku na kule, upepo nao wa bahari ya Atlantiki ukipuliza kwa mbali.

Gari moja, Suzuki Vitara yenye rangi bluu nyeusi, ilipunguza mwendo lamini na kukunja kona ya kushoto kuingia katikati ya mitaa ya Freetown. Ndani ya gari hilo alikuwamo mwanaume mmoja; Amadu. Mkono wake wa kulia uliojaza ulikuwa umekamatia usukani. Alishusha vioo vya mbele vya gari akawa anaangaza kandokando mwa barabara nyembamba za katikati ya jiji.

Kuna mtu alikuwa anamtafuta. Mwendo wake wa polepole na macho yake yaliyokuwa yanaangaza yalikuwa shahidi wa hilo.

Alizunguka kwa muda wa dakika kama kumi na tano akikaguakagua nyuso za wazururaji pasipo kupata chochote, lakini hakuchoka. Alisemea moyoni mara kwa mara:

“Lazima nimpate … lazima nimp …”

Alikata kona kama tano hivi akaona wanaume wawili wakiwa wanapigana. Mwanaume mmoja alikuwa amejaza mwili kwa mazoezi; tisheti nyeusi aliyokuwa ameivaa ilikuwa imembana haswa; kichwa chake kilikuwa kimejazwa rasta nyeusi ndefu kiasi. Aliyekuwa anapigana naye alikuwa yu mwembamba ila mrefu; tisheti lake kubwa rangi ya zambarau lilikuwa linampwerepweta; hata suruali yake alikuwa kaikabia kiunoni na kamba ya viatu.

Kwa haraka Amadu alimtambua mwanaume yule mwembamba ndiye anayemtafuta. Alikuwa ni yule mwanaume mkabaji aliyewahi kumharibia zoezi lake la ukabaji huko nyuma.

Alikuwa ni yule mkabaji aliyemwambia Amadu anafanya dhambi hiyo ili aweze kugharamia matibabu ya mama yake aliyejawa na maji kwenye figo.

Amadu alitumai atamkuta kijana huyo mtaani, na ni kweli alikuwa sahihi. Aliweka gari pembeni akachomoa funguo na kutoka ndani kufuata eneo la mpambano.

Mwanaume yule mwenye rasta alimtupia mwenzake chini kama kiroba cha magimbi alafu akamtazama Amadu kwa macho yaliyojaa shari.

“Naweza nikakusaidia?” Aliuliza.

“Ndio. Namuhitaji huyu kijana,” alijibu Amadu akimnyanyua mwanaume yule aliyetupiwa chini.

“Hauendi naye popote mpaka pale nitakapomalizana naye!” Alihororoja Rasta.

“Kwakuwa wewe ni nani?” Aliuliza Amadu. Alimsogeza nyuma kijana yule aliyemkomboa kisha akamsogelea Rasi.

Rasta alifanya makosa makubwa sana kurusha ngumi. Amadu aliikwepa alafu akamkandika Rasta kichwa kizito kilichompasua pembeni ya jicho lake la kulia na kumvujisha damu.

Rasta aliugulia maumivu yake kwa sekunde kadhaa kabla tena hajaamua kurusha turufu yake kwa ngumi za mfululizo.

Amadu alizikwepa ngumi hizo kama mtu afanyaye mchezo kisha akakamata mkono wa Rasta na kuupeleka usoni mwa mwanaume huyo kwanguvu. Ukakita puani na kumvujisha damu, alafu akasindikizwa na teke la haja lililomnyanyua juu na kumtupia chini kwa kishindo.

Amadu aliondoka na yule mwanaume aliyemtwaa kuendea gari na kutoka eneo lile.

“Naomba unisamehe, braza. Sitoiba tena!” Alisema mwanaume yule aliyekuwa na Amadu garini.

“Ina maana tokea siku ile hujaacha kuiba?” Aliuliza Amadu.

“Nimeacha.”

“Acha kuniongopea.”

Kijana yule akatazama chini.

“Siwezi kuacha braza. Sina namna nyingine ya kupata kipato cha kutunza wadogo zangu.”

“Mama yako anaendeleaje?”

Mara kijana yule akabubujikwa na machozi.

“Amekufa,” alijibu. “Wiki mbili zilizopita baada ya kushindikana kufanyiwa upasuaji.”

“Pole sana.”

Kimya.

“Nataka nikupe nafasi ya kubadilisha nchi hii. Upo tayari?”

Kijana alisita. Akili yake ilimkumbusha picha za Amadu zilizobandikwa jiji zima la Freetown ya kwamba anatafutwa. Kichwani alichambua upesi na kabla hajajibu swali, aliamua kuuliza kwanza kwanini Amadu anatafutwa.

Amadu alimjibu kiwepesi, yeye ni muasi wa serikali, kisha akarudisha swali kwa kijana huyo kama yu tayari kubadilisha hali yake na ya wenzake pia, kijana akaridhia.

“Kuna kazi kubwa nataka ufanye,” alisema Amadu. “Kwa kupitia kazi hiyo, nitapata kujua kama kweli unanifaa au lah!”

Waliyoyoma na barabara mpaka walipomezwa na giza. Mataa ya gari yaliyoyomezwa ndani ya umbali tusipate kuyaona tena.


Baada ya lisaa limoja: saa saba kasoro robo.


Ndani ya klabu ya usiku ya Aces watu walikuwa wamejaa kupata burudani, ila laiti ungelikuwa nje ya klabu hiyo pasi na shaka usingelidhani kama ndani yake kuna mziki mkubwa na makelele ya haja kwani kulikuwa kimya watu wachache wakiwa wanaongeaongea huku wakielekea ndani ya klabu hiyo ama wakiwa wamesimama.

Wanawake waliokuwa hapo nje walikuwa wamevalia vijiguo vifupi wakiwa wamejipara haswa. Magari kadhaa yalikuwa yamepakiwa nje, ila watembea kwa miguu ndio walikuwa wengi zaidi.

Ukilinganisha na huko nyuma, klabu hii maarufu ilikuwa imepoteza mvuto wake. Watu hawafuriki tena kama awali. Hao unawaona hapo klabuni ni wale tu wenye fedha zao, na wale ambao hawahofii sana juu ya usalama wao.

Tangu utawala mpya ulipoingia madarakani, uchumi umedorora mno, hamna pesa. Lakini zaidi hakuna amani ya kudumu. Matukio ya mahali penye ulinzi mkubwa kama vile benki kuu na kambi ya jeshi kuvamiwa, kuliwapa watu sababu madhubuti ya kukaa ndani ya viota vyao kwa usalama zaidi.

Ila binaadam hatufanani kama alama za vidoleni, linaeleweka hilo, hivyo wakati wengine wakiwa wamejifungia ndani, kuna wengine wenye mioyo na mifuko mipana walikuwa wameenda kutumbua. Miongoni mwao alikuwapo Talib, waziri wa ulinzi.

Alikuwa ameongozana na jopo la watu wake watano, wanne kati yao wakiwa walinzi wamlindao japokuwa hawakuwa na silaha mkononi.

Aliketi kwenye kitengo cha VIP, kule kusipo na usumbufu. Meza yake ilikuwa imechafuliwa na vinywaji vikali vya bei ghali. Alikuwa anakunywa na mwenzake aliyekaa kando wakipiga soga.

“Nimeona nitumbue mwenzangu kabla sijafa,” alisema Talib na sauti ya kilevi.

“Kwanini unasema hivyo?” Aliuliza rafiki yake kando. Naye alikuwa amebebelea glasi ndogo ilyojaa kilevi.

“Kwanini?” Talib alitahamaki. “Mpaka sasa sijawakamata wale washenzi. Yani roho yangu ipo mkononi … endapo tu wakifanya tukio lolote, basi kwisha habari yangu.”

“Usijali,” Rafiki akapooza jambo. “Utawakamata tu.”
“Lini?”

Waliendelea kuzozana mpaka pale Talib alipomuona mwanamke mrembo, mrefu mwenye shepu ya haja, akiwa anacheza mziki kwa ustadi mkubwa. Alivutiwa mno, na kichwa chake ndani ya suruali kikafanya maamuzi ya kumuwinda mwanamke yule.

Alimuagiza rafiki yake akamuitie huyo mwanamke lakini Rafiki akamtaka Talib amtume mlinzi. Talib alikataa kumtuma mlinzi kwani hakutaka kuhatarisha usalama wake, hivyo akasisitizia Rafiki aende.

Rafiki alikunywa fundo moja la kinywaji chake alafu akanyanyuka kwenda kutimiza agizo.

Alimfikia mwanamke yule na kumpasha habari, ila mwanamke akakataa. Alisema ana bwana ‘ake amekuja naye na pia hataki kampani yoyote.

Rafiki akapeleka taarifa kwa Talib. Talib alighafirika akamshutumu Rafiki ya kwamba ni mpumbavu na asiyejua kucheza na masikio ya wanawake. Aliamua kunyanyuka mwenyewe na kwenda akiwa anaongozana na walinzi wake.

Alipomkaribia mwanamke yule anayemhitaji alimshika kalio, mwanamke akashituka na kutazama aliyemtenda. Uso kwa uso akakutana na Talib.

Kumbe mwanamke yule alikuwa ni Rose! Talib aligundua ile sura si ngeni machoni mwake, lakini hakukumbuka ni wapi haswa alimuona huyo mhusika.

Kabla ya yeyote hajatia neno lolote, ghafla ulisikika mlio wa risasi kisha sauti ya kuamuru.

“Wote chinii!”



☆☆☆



☆Steve
 
Pls nitag tafadhali


Karibuni wakuu!


☆Steve
Ahsante sana mkuu. Hii story ni moto wa kuotea maili moja kando! Toa vitabu basi mkuu, mie ntakuwa mteja wako wa kwanza kabisa!



- Amini nakwambia

mkuu Steve leo vipi?

Tunaisubiri mkuu usisahau kunitag

Uko vizur mtunzi big up

ijumaa si ndio leo

hayahaya lesteve iti isi furaidei

Okey nasuburi

Pouwa mkuu, niko nasubiri next move!!
 
Back
Top Bottom