Bi Hadija, ni kweli wapo wakina mama wengi ambao wana-support wenzi wao. Haitaisha leo. Wengi wao hawanun'guniki wala hawalaumu. Katika hali yako wewe, inaelekea uchungu wa mahusiano yenu upo sio katika yeye kuomba hela ya bia n.k, bali wewe kufika mahala ambapo huoni mwelekeo kwamba karibuni utatoka kwenye mpenzi/hawara na kuwa mke. Hapo ndipo penye tatizo. Kifupi dada ni kuwa, ni haki yako ya msingi kuidai kujua mwelekeo wenu ikiwa ni pamoja na utambulisho, posa, na ndoa. Hilo halina mjadala. Unatakiwa kusimama kidete kuwa mwenendo wa maisha yenu ya sasa ya bila hayo wewe kwako ni mtihani. Kumbuka huyu aweza kuwa mumeo kama hayo matatu yakiwekwa mahali pake. Yakirekebishwa hayo, basi bwana huyu atabanwa sio na wewe tena, bali na jamaa wote wa pande zenu mbili (mke na mume)mpaka avae tabia za wanaume wenziwe na kuiongoza nyumba yake. Kabla ya haya, uukague moyo wako kiukweli kama unampenda nje ya matatizo yake uliyoyataja kwa vile haya ni madogo na yanarekebishika haraka.