Nimekutana na Timekeeper Deus Mwafisango, hatari Sana.

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,895
NIMEKUTANA NA TIMEKEEPER DEUS MWAFISANGO, HATARI SANA.

Anaandika, Robert Heriel

Ni leo. Maeneo ya Mlimani City nilikutana na mtu hatari, jitu baya, Roho ya kale, ukimuita jitu mwitu msitu hutokuwa unakosea.
Napita Eneo la samaki samaki nasikia Sauti ikiniita. Nageuka macho yangu yanapagawa ungedhani nimeona mzimu wa Kolelo. Nikamtazama, alikuwa amekaa na mdada mmoja hivi mwenye Bleach kichwani. Hata hivyo Yule mrembo sikumjali. Yule jamaa akaita mara ya pili jina langu kunihakikishia kuwa sikusikia vibaya. Hapo nikasogea mpaka walipokuwa wameketi. Nikasimama nikiwa bado ninastaajabu labda sikuwa namkumbuka

Kabla hajataja jina lake, Akili yangu ikasafari maili zaidi ya 450 mpaka kijiji Chetu Makanya, shule ya Makanya sekondari Huko. Hapo baadhi ya matukio yakaanza kutembea katika Akili yangu kama mkanda wa filamu. Nikamuona kijana mmoja mweusi, mrefu wa kawaida lakini mwenye mwili wa ukijeba, ukisema miraba minne hautakuwa mbali kivile.
Kijana Yule alikuwa anapenda kuchomekea na kuvaa suruali za A4 labda tuseme suruali za kwaya, zenye marinda Matatu huku na huku. Shati lake lilikuwa jeupe hali iliyoleta vita baina ya weusi WA ngozi yake na Shati alilolivaa.
Mkononi alikuwa anavaa Saa Fulani hivi, ambayo isingeweza kupita dakika 30 pasipo kuitazama. Yaani yeye ilikuwa kama ameathirika kisaikolojia.

Filamu hiyo akilini ikakatika nikatazama mkono aliozoea kuiweka Ile saa yake. Sikuona saa. Kitendo hicho kilimfanya atabasamu. Sasa alijua nimemkumbuka.
Hakuwa mwingine Bali ni TIMEKEEPER Deus MWAFISANGO, kijana aliyeipenda kazi yake ya u-timekeeper na kugonga kengele enzi akiwa anasoma. Jambo hilo lilimzolee umaarufu mkubwa Kutokana na mbwembwe, ustadi, michombwezo na mikogo yake.

Mwafisango Kabla hajastaafishwa na kupewa suspension alikubalika, aliaminika, na Wakati mwingine aliheshimika.
Hujanielewa! Subiri!

Mwafisango alikuwa anatembea kulingana na kengele aliyokuwa anaenda kuigonga. Kuna utembeaji wa kugonga kengele ya mstarini, kuna utembeaji wa kugonga kengele ya kipindi, kuna utembeaji wa kugonga kengele ya Breakfast au Lunch, na kuna utembeaji wa kugonga kengele ya mstarini Kwa dharura.
Sikujua kipaji kile cha kipekee alikitolea wapi lakini nakiri kuwa kilimpendeza na kumfanya nafasi yake ionekane pale shuleni.

Kama Mwafisango asipokuweko shuleni ni rahisi kugundua. Ugongaji kengele wake ulikuwa wa kipekee. Wengi walikuwa wakimshangilia hasa pale alipokuwa akigonga kengele ya Breakfast na Lunch. Hakika utapenda. Ilikuwa Sanaa ya ugongaji Kengele.

Sasa shuleni kuna makundi ya Wanafunzi na makundi ya waalimu.
Wapo Wanafunzi wanaopenda muda uende kengele igongwe waende lunch au kwenye Michezo. Alafu wapo ambao hupenda kusoma, wale kina John kisomo.

Alafu Wapo waalimu ambao wanapenda Sana kufundisha ikibidi kuvunja ratiba, hawa huchukia Sana kengele ikigongwa. Unakuta Mwalimu akisikia kengele ikigongwa anachukia na USO wake unabadilika.
Alafu lipo lile kundi la waalimu wasiopenda kufundisha, yaani hawa wakisikia kengele huwaona kabisa pumzi na Mwili ikiwaachia. Na kuna Wakati wakihisi kengele inachelewa kugongwa wanapata kihoro. Muda wote utawakuta wanaangalia saa.

Mwafisango iwe Kwa kujua au kutokujua alikuwa MTU katili Sana Kwa waalimu wasiopenda kufundisha na Wanafunzi wapenda kusikia kengele za breakfast na lunch.

Kuna Ile Hali umekaa zako kwenye Dawati umechoka zako hapo unatamani kengele igongwe. Unaona muda umeenda lakini kengele haigongwi. Si unajua tena shule za kule kwetu kumiliki saa tuu Kwa wengi ilikuwa mitihani.

Mwafisango muda anaoenda kugonga kengele hujihisi Dunia kaimiliki. Basi akifika pale. Hutoa kile kichuma cha kugongea kengele, hapo itatokea milio ya mikwaruzo Hali itayofanya Wanafunzi waliopo madarasani kusikia, mikwaruzo hiyo huwafanya Wanafunzi kuanza kukufanya madaftari na kuyaweka kwenye mabegi.
Mwafisango anakausha kidogo pasipo kugonga kengele Hali inayowapa Wanafunzi Wakati mgumu Kwa kufikiri huenda walisikia vibaya. Basi wanataka kurudisha madaftari kwenye Dawati lakini Kabla hawajafanya hivyo, mwafisango mtu m-bad anapiga kengele moja, "Nge" kisha anatulia Kwa sekunde, hapo kila mwanafunzi hajui hiyo kengele ni Emergency au vipi, kisha wakiwa katika kutazama ikiwemo na waalimu waliokuwa darasani muda huo. Mwafisango anaongeza tena kengele nyingine "Nge" alafu Kimya. Watu wanajua kipindi, lakini wale wenye saa wanajaribu kuangalia usahihi WA saa zao. Wasio na saa wanawatazama wenye saa kama Watu wanaotaka kujibiwa maswali Yao.

Basi Mwalimu hasa wale waalimu wanoko wapenda kukaba Hadi penalty huendelea kufundisha, lakini hapo ndio TIMEKEEPER Deus MWAFISANGO huonyesha ubabe wake. Kabla hawajaandika irabu au konsonanti ubaoni, au Kabla hawajamaliza neno " Let's proceed" na kama wamelimaliza basi neno Hilo Kabla halijatafsiriwa na bongo za Wanafunzi, Mwafisango anapiga kengele ya lunch "Nge! Nge! Nge! Nge! Nge! "
Hapo utasikia kidato cha kwanza, cha pili na nusu ya kidato cha tatu na kidato cha nne Back-benchers wakishangilia, hheeeeeee!
Wengine huimba Mwafisango! Mwafisango!

Sasa nini kilimfanya Mwafisango afukuzwe shule kisha kurudi siku ya mitihani?

Swali hilo linaenda sambamba na pale nilipoona Alama ya kovu juu ya jicho la Mwafisango nikiwa natazamana naye.
Licha ya kuwa alikuwa mweusi lakini kovu lile liliweza kuukabili weusi wake na kuacha Alama ambayo MTU yeyote hata angesemama umbali WA Mita 20 angeweza kuliona.

Nimefurahi kukuona Jemedari Deusi Mwafisango, Timekeeper wa Wakati wote.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 
mwakifongo,nge alafu anatulia kwanza, nyingine Tena nge alafu anatulia ngengengengeeeeeeeee baki bencha haoooooo ...
 
Usiombe Mtu kama Mwafisango ''The Timekeeper'' apate uongozi mkubwa.

Hata hapo Makanya angeteuliwa tu kuwa Kiranja wa nidhamu mngenyooka
 
Time keepers walikuwa na UMAARUFU mkubwa sana.

1. Nadhani kengele ni UTUMWA.

2. Walizi wangekabidhiwa Hilo jukumu

3. Wanafunzi wooote nchi nzima WAWE na saa.
INAWEZA ikasaidia mno.

Binafsi sijawahi kukosa saa mkononi MWANGU.
 
Usiombe Mtu kama Mwafisango ''The Timekeeper'' apate uongozi mkubwa.

Hata hapo Makanya angeteuliwa tu kuwa Kiranja wa nidhamu mngenyooka

Mwafisango MTU hatari Kwa Hali niliyomkuta nayo sidhani kama anajeuri Ile ya nyakati zile. 😂😂
Mwafisango the Timekeeper
 
Time keepers walikuwa na UMAARUFU mkubwa sana.

1. Nadhani kengele ni UTUMWA.

2. Walizi wangekabidhiwa Hilo jukumu

3. Wanafunzi wooote nchi nzima WAWE na saa.
INAWEZA ikasaidia mno.

Binafsi sijawahi kukosa saa mkononi MWANGU.

Ni kweli Kabisa.
Lakini shule zetu za Kata, kuwa na Saa ilikuwa ni anasa. Na Dalili ya uwezo wa kiuchumi
 
Back
Top Bottom