Nimefukuzwa kazi bila hata ya kujitetea

SJUMAA26

JF-Expert Member
Jan 25, 2012
607
167
Ndugu WanaJamii Forum wenzangu,

Naombeni msaada wenu wa kisheria, kimawazo ama ushauri.

Mimi niliwahi kuajiriwa na taasisi moja isiyo ya kiserikali (yaani NGO) kama mhasibu. Baada ya kufanya kazi kwa miezi 8 hivi, nilitofautiana na Wakurugenzi kuhusu wizi na ufujaji wa fedha waliotaka mimi, kwa taaluma yangu, niwasaidie kuuficha mbele ya wafadhili wao. Nikasimamishwa kazi kwa madai kuwa kulikuwa na wizi pale ofisini, mishahara yangu ya miezi 2 ikazuiliwa kwa madai ya "kufidia wizi" lakini wakati huo huo nikafunguliwa kesi polisi kwa tuhuma za KUGHUSHI/KUIBA!

Muda haukupita nilipata kazi kwenye taasisi ya fedha ya serikali. Wale Wakurugenzi wa NGO wakanitoa kwenye magazeti wakiujulisha umma kuwa mimi si mwajiriwa wao tena, siku 7 tu baada ya kuripoti kwenye kazi mpya! Ndipo mwajiri wangu mpya akataka kujua nini kilitokea. Nilimhadithia lakini hata hivyo akadai waandike barua kule kwenye NGO licha ya kuwatahadharisha kuwa majibu yao hayatakuwa mazuri kwangu. Wale wa NGO wakajibu kwa barua mbaya sana ya kuniharibia. Ikabidi nisimamishwe kazi.


Baada ya kukaa mwaka mmoja nikiwa "On Suspension", mwajiri wangu huyo mpya aliamua kunifukuza kazi kwa sababu mbili:-
  1. Kuficha taarifa za mwajiri wangu wa zamani (yaani wa hiyo NGO) wakati hakukuwa na uwezekano wala matakwa yoyote ya kutoa taarifa zozote za nyuma tena ndani ya kipindi kifupi (cha siku 7) baada ya kuajiriwa
  2. Kuchafuka na hivyo kutofaa tena kuwa mwajiriwa ktk Taasisi za Fedha Tanzania

Muda wote huo kesi hiyo haikuwa imepelekwa mahakamani, na kila nilipokuwa nikihoji kwanini kesi haipelekwi mahakamani naambiwa upelelezi bado haujakamilika! Baada ya mwaka 1 na miezi 7 hivi ya "Upelelezi wa Polisi", ndipo kesi ikapelekwa mahakamani!

Kesi imeendelea kuwa ikitajwa mahakamani na kuahirishwa kila uchwao kwa madai kuwa upelelezi bado haujakamilika (sasa ni zaidi ya miezi 9 tangu kesi hiyo ipelekwe mahakamani, na ni zaidi ya miaka miaka 2 na miezi 4 tangu kesi ilipofunguliwa Polisi)! Muda wote huo niliogopa kutafuta kazi kabla kesi inayonikabili haijaisha kwa kuhofia kufuatiliwa na kufukuzwa tena!

Hata hivyo, nikiwa na familia, ilinibidi nitafute kazi. Mungu si Athmani nikapata kazi kwenye Taasisi nyingine ya serikali. Hapo ikabidi nikamuone Bw. Mkubwa wa Taasisi hiyo ili kuhofia kuja kuambiwa nilificha taarifa. Baadaye ofisi iliamua kufuatilia kesi hiyo mahakamani ili kujua undani na mwenendo wake. Mwanasheria wa Taasisi hiyo akabaini kuwa hiyo kesi ilikuwa ni ya kubambikiwa tu isiyokuwa na ushahidi wowote wa kumtia mtu hatiani. Cha ajabu, Bw. Mkubwa huyo akaniambia nifanye kila ninaloweza kesi hiyo iwe imeisha mwezi wa tatu mwaka huu vinginevyo na hapo nitafukuzwa! Nilijitahidi kwenda mahakamani na kuombiwa jalada bado liko Polisi, upelelezi umeshakamilika ila "facts" hazijawa tayari na jalada lenyewe bado liko Polisi. Kwa mara mbili mfululizo, Polisi wameendelea kudai kuwa hawajamaliza kuandaa "facts".

Nilipomwambia Bw. Mkubwa kuhusu hicho kinachotokea mahakamani akadai hiyo haimuhusu na ingawa kwenye Ofisi yake sijawakosea, itabidi nifukuzwe kwa madai kuwa sistahili kuajiriwa eti kwa kuwa nina tuhuma mahakamani! Mwanasheria wake akamshauri wasubirie uamuzi wa mahakama ndipo na wao wanichukulie hatua stahiki lakini Bw. Mkubwa huyo alikataa na mwishowe nikafukuzwa.

Ndugu wadau, kesi ndio hiyo haijaanza hata kusikilizwa kwa maana "facts" hazijawa tayari na jalada liko Polisi, na wale wanaonishtaki wananifuata kuniharibia na hatimaye kufukuzwa kila ninapopata kazi. NAOMBENI WANASHERIA MAHIRI NA WAZALENDO MNISAIDIE NIFANYE NINI maana nimezunguka sana kwa takribani miaka 3 sasa tangu nipate haya matatizo bila mafanikio. Kila nikiweka wakili, jamaa wanamnunua matokeo yake siri za huku anapeleka kule ili apewe hela. Kwa sasa sina KAZI na nina Familia na Ndugu wananitegemea.

Nawasilisha.

Ahsanteni
 
Back
Top Bottom