Huyu kwako ni makini, wengine watajifia,2. Simu ya kwanza yasema, Tia mguu njiani,
Mama yako ana homa, Imemuanza kondeni,
Fanya uje hima hima, Kupona si tumaini
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
Nianze kwenda kwa nani?
- Leo nimepata simu, Huko kwangu ofisini, Zote tena taslimu, Zimefika mikononi,
Na zote hizo muhimu, Nimezisoma yakini,
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
2. Simu ya kwanza yasema, Tia mguu njiani,
Mama yako ana homa, Imemuanza kondeni,
Fanya uje hima hima, Kupona si tumaini
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
3. Simu ya pili yasema, Hamza njoo Omani,
Mkweo anakoroma, Kakumbwa na datsani,
Ukweli hana uzima, Ajekupa buriani,
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
4. Simu ya tatu yasema, Barubaru harahara,
Mkeo wa huko Doha, leo kaumwa na nyoka,
Waganga wanavyosema, Imebakia dakika,
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
5.Simu ya nne yasema, usidharau kufika,
Mwanao Dar isalaama, Mguu umevunjika,
Homa raha alalama, Jinsi anavyoteseka,
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
6. Simu ya tano yasema, kaka yako ana kesi,
Kaiba mali ya umma, Wamemzoa polisi,
Majibu ya mahakama, Uje ulipe upesi,
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
7Watunzi huo ukweli, msidhani naropoka,
Zimeniruka akili, Nabaki kuweweseka,
Mwanakijiji na Ali, Choveki nipe hakika,
Nianze kwenda kwa nani, washairi nambieni.
Dr Hamza Yousuf Al Naamany (Barubaru)
H/N 2436, Umm hays Block.
Minal fahal Street.
Doha.
Qatar
Pokea pole wakwetu, kwa mama huko anzia,
Tena sisubiri mtu, kwa mama watimkia
Si namba mbili wala tatu, ya kwanza ashikilia
Hakuna sawa na mama, sikia baba sikia
Wala sisubiri simu, nyengine ije ingia
Umeshapata salamu, mama wasikilizia
Wajibu kwako muhuimu, safari ukianzia
Hakuna sawa na mama, sikia kaka sikia
Wengine watasubiri, kichwani hilo julia
Tulia uwe mahiri, ni mama wakimbilia
Kwa mama kweli nakiri, ni nani akaribia?
Hakuna sawa na mama, sikia ndugu sikia
Na tena una bahati, mamako anapumua
Chomoka kama baruti, usije kuja jutia
Kwa wako wote wa dhati, ni mama anaanzia
Hakuna sawa na mama, sikia shekhe sikia
Tano nasema kikomo, ni miye nakomelea
Nimeshakupa kisomo, kwa mama kuashiria
Natena hana kipimo, muhimu hiyo kujua
Hakuna sawa na mama, we Barubaru sikia!
Panapo tumika shoka,usije leta jambia,
Sifananishe na soka,na maisha ya dunia,
Mama yako shamchoka,hivi ndo watuambia?
Wakuanzia ni mama,wengine wafuatia
Tena fanya hima,usije ukajutia,
Hakuwekewa kwa bima,maisha yatalipia,
Ufanya kwake khidima,mola tampa afua,
Wakuanzia ni mama,wengine wafuatia
Kakiyo ana dhahama,kwakweli kajitakia,
Hicho kwake ni kiama,apate pa kujutia,
Umwache akale sima,kamwe sije kimbilia,
Wakuanzia ni mama,wengine wafuatia
Mkweo toka omani,mola pekee ajua,
Omba dua kwa imani,apate japo afua
Mke ombea jirani,wapate kumwangalia,
Wakuanzia ni mama,wengine wafuatia
Mtoto yupo salama,hofu ndio yasumbua,
Nenda mwangalie mama,yeye wakupigania,
Kamwe acha kulalama,nakupa japo usia,
Wakuanzia ni mama,wengine wafuatia
Nimefanya hima miye, nije na nikuambie
Barubaru usikiye, haraka ukafanyie
Shauri nikupatie, nawe ulizingatie,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia
Ukishamtoa kaka, kwa mama fanya haraka,
Wa kaka mkono shika, mwende mpate baraka,
Kwa mama mkishafika, uzima hautatoka,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia
....................
Kama wote watatoka, ukenda kumtoa kaka,
Msiba utawafika, pamoja mtawazika,
Mke wewe utazika, mama kaka atazika,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia.
.....................
M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Ikiwa hujui beti kaa mie soma tu usidanganye.Nitarudi...
Nahisi huyo ni gamba, kwa nini akimbiliwe?
Ni gwanda kama si gamba, walio wengi viwewe
Mwache apate kingwamba, atupwe selo alewe!
Awe gamba au gwanda, najuwa wote viwewe!
Kakako si kimbilio, hata aliwe na mwewe
Hata atoe kilio, kelele navyo viwewe
Asisubiri ujio, ajue yupo mwenyewe
Awe gamba au gwanda, nahisi wote viwewe!
Asake wapambe wake, aende hata msewe
Kama kaoa na mke, asake hata mkwewe
Walipokula vya kwake, malipo sasa wajuwe
Awe gamba au gwanda, najuwa wote viwewe!
Wote hao lao moja, wanagawana wenyewe
Gwanda na gamba wamoja, nishaelewa mweyewe
Watuonesha viroja, Dodoma ndiko kwenyewe!
Awe gamba au gwanda, najuwa wote viwewe!
Zangu hizi ndiyo mwisho, naomba unielewe
Nasema yeye wamwisho, foleni aielewe
Avilapo bila jasho, ajuwe vina mwishowe!
Awe gamba au gwanda, najuwa wote viwewe!
Barubaru we sikiya,wenzangu lotangulia.Nimefanya hima miye, nije na nikuambie
Barubaru usikiye, haraka ukafanyie
Shauri nikupatie, nawe ulizingatie,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia
Kwanza nakusalimia, na pole nakupatia
Yote yalokufikia, mazito nakubalia
Masahibu ya dunia, bila hodi yatujia
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia.
Swali ulilouliza, moyoni limeniumiza,
Na tena likaniliza, huzuni likinijaza,
Nikakaa nikawaza, sasa jibu nakujuza,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia.
Mama kashikwa na homa, mauti ayatazama,
Hofu yake kama mama, wanae wako wazima?
Mmoja jela katama, habari mbaya kwa mama
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia!
Ukishamtoa kaka, kwa mama fanya haraka,
Wa kaka mkono shika, mwende mpate baraka,
Kwa mama mkishafika, uzima hautatoka,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia
Kisha umtume kaka, awahi kwenda Tandika,
Kwa mwana wako hakika, mguu alovunjika,
Huko akishakufika, hali itatulizika,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia!
Nawe ufanye haraka, kwenda Doha kwa hakika,
Mauti yasije fika, habiba akakutoka,
Msiba ukakufika, wa nyonda akiondoka,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia!
Na piga simu Omani, kwa wakwe walo tabuni,
Binti yao taabani, mautiuti kitandani,
Utachelewa njiani, wauguliwa mtani,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia.
Uwaambia Omani, dua zapaa mbinguni,
Kwa Subhana Maanani, mwingi wa rehemani,
Wawatakia imani, ukiomba ahueni,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia.
Mke akinusurika, Barubaru kwa hakika,
Nenda Omani haraka, uende bila kuchoka,
Mkweo asije toka, bila ya wewe kufika,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia.
Kama wote watatoka, ukenda kumtoa kaka,
Msiba utawafika, pamoja mtawazika,
Mke wewe utazika, mama kaka atazika,
Kamtoe kwanza kaka, ya Mungu yatafuatia.
M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)