Mlalahoi, hivi Watanzania wengine weusi wote wanaipenda nchi yao? Je ni wote wamakua, warangi, wanyakyusa n.k ambao hawawadharau watanzania wenzao? Je ni watanzania wote weusi ambao hawatoi na kupokea rushwa ili wapate kila wanachotaka? Hivi ni Wahindi pekee wanaoiharibu nchi yetu? Ni kujidanganya kudhani kuwa kwa vile mtu ni mweusi basi ni mtanzania zaidi na anaipenda nchi yake zaidi! Hilo halijali mtanzania ni nani!
Kama tunataka kuzungumzia ubaguzi unaofanywa na wahindi dhidi ya watu weusi hilo linazungumzika...! Wakati watu weupe wa Marekani wanawabagua watu weusi hiko hakikuwaondolea Umarekani wao! Wakati kina Malcom X na wengine walipoanzisha jitihada za kusimama dhidi ya ubaguzi wa rangi "by any means necessary" hilo halikuwaondolea Umarekani wao! Lakini yote yale yalizungumzika! Watu weupe wakawezeshwa kuona ubaya wa njia zao na watu weusi vivyo hivyo! Na Marekani ikawa bora zaidi. Na tunajua hata hivyo bado kuna watu weupe ambao wanawadhihaki watu weusi kila siku. Na wapo watu weusi wanaowachukua watu weusi wenzao!!
Kwa upande wetu Tanzania, nitakuwa muongo na mzandiki nisipokiri kuwa Watanzania wenye asili ya uhindi wana kasumba ya kubagua watu weusi na kuwadharau, na wao kujiona bora. Lakini hilo haliwapunguzii Utanzania wao, linaonesha tu kuwa wanahitaji kueleweshwa kuwa kama Tanzania ni yao basi hawana budi kuipenda pamoja na watu wake wote! Na kushirikia katika raha na shida katika kuijenga nchi yetu. Na wapo wahindi waliofanya hivyo (labda wachache - lakini wapo)
Hata mimi najiuliza, ni Wahindi wangapi ambao watoto wao wameeingia katika ajira za jeshi la wananchi, polisi au magereza ambako ndiko chachu ya uzalendo inapandwa! Ningekuwa mimi nina uwezo, ningelazimisha kukaa chini na jumuiya ya wahindi na kuwaambia wazi kuwa kujitenga kwao hakujengi nchi! Kwa sababu hatari iliyopo ni kuwa pindi Tanzania itakapoanza kufanikiwa sana kiuchumi, Waasia hao wataanza kurejea Tanzania kwa wingi na kudai Tanzania ni nchi yao! Hilo linazungumzika.
Kuonyesha kosa la watu au kikundi cha watu katika jamii na kuwakosoa ili wajirekebishe kwa kutumia mantiki, siyo ubaguzi wa rangi. Kuwaona watu fulani ni duni, hawafai, waondoke, na wanyimwe haki fulani za kiraia kwa sababu tu ya rangi zao, huo ni ubaguzi na hauna nafasi katika Tanzania yetu. Binafsi, ni bora kuwa na Mhindi anayejali na kuheshimu watanzania wenzake, na kuisaidia kujenga nchi yake kwa kila namna, kuliko kuwa na mtu mweusi ambaye anajitahidi kuiingiza Tanzania katika mikataba mibovu, anakula rushwa kuuza madini yetu, na anatafuna pesa za serikali ubalozini kama mchwa! Ukinipa uchaguzi, nitachagua Mhindi!!!