Ni kosa kisheria kufanya shughuli yoyote inayoweza kusababisha kuharibu, kung'oa au kuhamisha alama za upimaji Ardhi

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,500
9,279
Serikali imewaonya wamiliki wa ardhi wanaoharibu, kung'oa au kuhamisha alama za upimaji ardhi (Beacons) na kueleza kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kulipa faini ya shilingi 750, 000 au kifungo cha mwaka mmoja jela.

Taarifa ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa umma ilieleza kuwa, ni kosa kisheria kufanya shughuli yoyote inayoweza kusababisha kuharibu, kung'oa au kuhamisha alama za upimaji.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana kupitia kitengo cha mawasiliano serikalini ilieleza kuwa wizara hiyo imebaini kuna wananchi wanaoharibu, kung'oa na kuhamisha alama za upimaji na kubainisha kwamba, kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutokana na kukithiri vitendo hivyo inawakumbusha wananchi wote kuwa mtu yeyote atakayebainika kuharibu, kung'oa, kuhamisha au kufanya shughuli inayoweza kuharibu alama za upimaji ardhi atakuwa ametenda kosa la jinai na atawajibika kulipa faini shilingi 750,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela au adhabu zote kwa pamoja.

Wizara imewaasa wananchi wote kutojihusisha na vitendo hivyo kwa kuwa vinarudisha nyuma jitihada za serikali za kuongeza usalama wa miliki ardhi kwa wananchi.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikipanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa lengo la kuongeza usalama wa miliki za ardhi kwa wananchi na maeneo yote yaliyopangwa na kupimwa yamewekewa alama za upimaji ardhini (Beacons) kwa mujibu wa sheria ya upimaji ardhi sura ya 324.

Chanzo: HabariLeo
 
Back
Top Bottom