SoC03 Ni jukumu langu kuleta mapinduzi ya kijani kwa maendeleo ya taifa

Stories of Change - 2023 Competition

Hamza Nsiha

JF-Expert Member
Jul 25, 2022
208
191
NI JUKUMU LANGU KULETA MAPINDUZI YA KIJANI KWA MAENDELEO YA TAIFA

Tanzania ni nchi iliyojaliwa kuwa na rasilimali mbalimbali ambazo huifanya Tanzania kuwa katika orodha ya nchi zilizobarikiwa duniani. La hasha! Sambamba na yote katika kuboresha na kuwezesha taifa letu kupitia rasilimali zake, tunahitaji baadhi ya mambo au misingi imara ambayo itasaidia kuleta chachu ya maendeleo kwa taifa zima na watu wake.

Katika yote, nitapenda kuzungumzia juu ya uwajibikaji wa sekta ya kilimo kama kipengele muhimu kwa maendeleo ya Tanzania. Nchi hii yenye rasilimali nyingi za kilimo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula cha kutosha pamoja na kukuza uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi Makala hii inaangazia zaidi ni jinsi gani tunavyoweza kushirikiana kwa pamoja katika kuleta mapinduzi ya kijani kwa maendeleo ya taifa.

Taifa letu, kupitia sekta yake ya kilimo imefanya kazi kubwa katika kuboresha na kusimamia vema misingi imara ya kilimo ijapokuwa kuna baadhi ya mambo bado yanaonekana kuhitaji nguvu zaidi ili kuinua zaidi sekta yetu muhimu ya kilimo kwa maendeleo ya taifa.

Sekta yetu ya kilimo, imejipambanua kwa mapana katika kuanzisha baadhi ya sera na kaulimbiu mbalimbali zenye malengo ya kuchochea kilimo nchini ijapokuwa kumekuwa na baadhi ya changamoto kadha wa kadha katika kutimiza malengo hayo. Kwa kifupi ningependa ufahamu baadhi ya kaulimbiu ambazo zilianzishwa ili kuinua sekta ya kilimo nchini;​
  • Kaulimbiu ya Kilimo Kwanza (Agriculture first), kaulimbiu hii ilianzishwa nchini Tanzania ambapo ilisaidia katika kuongeza ufanisi wa kilimo, kuboresha usalama wa chakula, pamoja na kukuza uchumi wa vijijini. Hata hivyo, kwa pamoja tunaweza onesha tathmini yakinifu kuhusiana na umuhimu wa uwajibikaji wa kina katika kaulimbiu hii ili kupanua mafanikio zaidi katika sekta yetu ya kilimo.​
  • Kilimo cha kijani, kaulimbiu hii inalenga hasa katika kuhimiza kilimo endelevu na matumizi sahihi ya rasilimali asilia kama vile ardhi na maji ili kudumisha kilimo katika taifa letu.​
  • Kilimo cha umwagiliaji, sekta ya kilimo ilianzisha kaulimbiu hii ikiwa na lengo la kukuza na kudumisha matumizi ya umwagiliaji ili kuhakikisha uzalishaji wa mazao unakuwa endelevu katika vipindi vyote.​
  • Kaulimbiu ya Kilimo biashara, pia kaulimbiu hii inalenga kuinua kilimo kama biashara na kuongeza thamani katika mazao ya kilimo.​
Hata hivyo, sekta yetu ya kilimo inakabiliwa na baadhi ya changamoto ambazo huchangia kwa kina katika kudidimiza sekta yetu ya kilimo nchini, changamoto hizo ni kama vile;

Je, ni kwanini baadhi ya wananchi wamekuwa wakiililia sekta ya kilimo katika upatikaji wa masoko ya mazao?
  • Ni ukweli usiopingika kuwa sekta yetu ya kilimo bado haijafanikiwa kikakimilifu katika kuweka mifumo sahihi ya upatikanaji wa masoko ya mazao mbalimbali nchini pamoja nje ya nchi. Wazalishaji wengi wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa masoko ya uhakika hivyo kupelekea kuwepo kwa thamani duni ya mazao.​
Je, ni kwanini baadhi ya miongozo ya kilimo imekuwa na matokeo hafifu katika kuboresha kilimo?​
  • Kuna baadhi ya miongozo iliyowahi kutolewa na sekta ya kilimo inaonekana kutofanya kazi ipasavyo kwa sasa aidha kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi au sababu zinginezo. Mfano; muongozo kuhusu zao la pamba bado ni kizungumkuti kwani hivi sasa inahitajika njia bora zaidi tofauti na zilizotolewa awali ili kuboresha uzalishaji wake sambamba na thamani yake pia.​
Je, ni kwanini kumekuwa na changamoto kadha wa kadha katika upatikanaji wa pembejeo na teknolojia bora za kilimo?
  • Ukweli ni kwamba, suala la pembejeo pamoja na teknolojia bado ni changamoto kubwa inayoathiri uzalishaji wa mazao nchini, ijapokuwa sekta ya kilimo imewekeza jitihada katika upatikanaji wa pembejeo na teknolojia mathubuti, bado suala hili ni changamoto kubwa inayodidimiza na kukatisha tamaa kwa baadhi ya wakulima nchini. Mfano; wakulima wa tumbaku huingia katika madeni makubwa ya pembejeo ambapo baadhi yao huambulia faida ndogo ya zao hilo.​
Je, ni kwanini sekta ya kilimo imejitahidi kuanzisha mikakati au kaulimbiu mbalimbali lakini zimeonekana kutofanya kazi kama ilivyodhaniwa?
  • Ni dhahiri kuwa ninaweza kusema kwamba, sekta yetu ya kilimo imekuwa ikianzisha mikakati mingi pasipo kutekeleza kikamilifu mikakati iliyopita hivyo, kila siku kuibuka na mikakati mipya ambayo ni bora lakini yenye changamoto ya kufikia utimilifu.​
Je, ni kwanini sekta yetu imekuwa nyuma katika kufanya tafiti za mara kwa mara juu ya mazao mbalimbali pamoja na masoko yake kwa ujumla?
  • Sekta yetu ya kilimo haijafanikiwa kwa kina katika kuboresha kiwango cha tafiti mbalimbali zenye kuleta tija kwa wakulima pamoja na wanufaika wake kwa ujumla. Mfano, kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi ya hivi karibuni sekta haijafanikiwa kutilia mkazo wa kina kuhusiana na ufumbuzi wa mazao sahihi kulingana na hali halisi ya sasa.​
Sambamba na kaulimbiu au mikakati makini iliyoibuliwa na sekta ya kilimo nchini Tanzania, La Hasha! Bado kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza uwajibikaji au uboreshaji katika nyanja mbalimbali ili kuing’arisha zaidi sekta hii ya kilimo katika taifa letu.

Yafuatayo ni baadhi ya mapendekezo ambayo kwa pamoja tukishikamana na kuyainua yanaweza kutia chachu na kuleta Tanzania ya kijani;​
  • Umuhimu wa kuzalisha wataalamu ambao watapelekwa katika nchi mbalimbali kwa lengo la kujifunza njia bora za kilimo kulingana na rasilimali zilizopo nchini, pia kujifunza namna ya kung’amua mifumo mbalimbali ya masoko. Mfano, Nchi ya ujerumani hupeleka wataalamu wake katika nchi mbalimbali ambapo hupata mafunzo mbalimbali ya muda mfupi juu ya masuala mbalimbali kuhusu kilimo, biashara na masoko yake kwa ujumla kwa takribani miezi mitatu (internship).​
  • Kudumishwa kwa tafiti zenye tija kuhusiana na masuala mbalimbali kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, ugumu wa masoko pamoja na hali halisi ya sasa ili kuinua uzalishaji nchini. Mfano, sekta ya kilimo inaweza kuweka utaratibu wa kupitia miongozo mbalimbali ya kilimo kila baada ya muda fulani ili kuibua maboresho au kuondoa baadhi ya miongozo ambayo haitakuwa na matokeo chanya.​
  • Kuwathamini wawekezaji wenye nia ya dhati katika kilimo lakini pia kuwaondoa wawekezaji wasiojali maslahi ya wananchi kwa ujumla. Mfano, wawekezaji wenye malengo ya kuinua miundombinu ya kilimo, teknolojia na masoko pia wawekezaji wenye kuwawezesha wakulima kupata mbegu na pembejeo bora za kisasa nchini.​
  • Sekta ya kilimo lazima itambue umuhimu wa wazawa kwa kuwainua ili kuimarisha kilimo bora nchini. Mfano, je! Itakuwa ni sahihi kuwanyang’anya ardhi wazawa na kuwapatia wawekezaji wa kigeni ilihali kuna uwezekano wa kuwainua wakulima hao kwa kuwajengea miundombinu madhubuti zitakazo inua uzalishaji wao? Hii itasaidia kuongeza ari au jitihada za kilimo kwa wazawa nchini hivyo kuinua maisha yao na taifa kwa ujumla.​
  • Pia, serikali inajukumu kubwa la kuzalisha sera bora za kilimo zenye kutekeleeka kulingana na rasilimali za nchini mwetu ili kuinua sekta ya kilimo. Mfano, serikali ilizindua mpango wa kukuza sekta ya kilimo (ASDP) ambao ni baadhi ya sera endelevu zinazofanya vema katika kuboresha sekta ya kilimo.​
  • Sambamba na yote, sekta ya kilimo ina wajibu wa kushirikiana na wananchi wake katika mikakati mbalimbali kwani wao ndio waliobeba dhamana kuu juu ya hali au changamoto wanazokumbana nazo katika shughuli za kilimo. Hivyo, kuna umuhimu wa kuibua mijadala mbalimbali ambayo itawahusisha wakulima moja kwa moja katika kutoa hoja zao ili kuleta majawabu sahihi kuhusiana na kilimo.​
Hivyo basi, si sekta ya kilimo tu bali hata sisi kama jamii kwa ujumla, kwa pamoja tunao wajibu wa kushirikiana kwa kina katika kuhakikisha tunainua sekta yetu ya kilimo na kuipandisha kileleni ambapo kwa pamoja tusimame kuijenga Tanzania mpya tena ya kijani kwa maendeleo ya taifa.​
 
Ila kuna watu huwa mnafikiria mbali sana. Kikubwa ni kwa nia njema kiukweli sekta yetu ya kilimo ni moja ya sekta ambayo inahitajika sana kwani watu hawawezi kula. Hakika yakifikiriwa haya tunaweza kufika mbali.
 
Pia ningefurahi ikiwa sekta yangu itakuja na miongozo mipya kwani hivi kuna vitu vngne bado havijakaa sawa
 
Mawazo kama haya yangefikishwa public au ungeandika katika threads pia ili wayafikie kwa uharaka
Ni mawazo mazuri kiukweli
 
Back
Top Bottom