Ni halali mzazi kumwachisha mtoto shule ili akamhudumie?

GoldDhahabu

JF-Expert Member
Apr 29, 2023
4,695
6,398
Kipindi fulani, nilifuatwa na kijana mmoja aliyekuwa akiishi jirani na nilikokuwa nikifanyia kazi, na kuniomba nimsadie kumtafutia nafasi ya kujifunza masuala ya ufundi kwenye kampuni fulani. Alikuwa bado kijana mdogo, under 18. Aliamua kutafuta hiyo nafasi baada ya kufeli mitihani ya kidato cha pili.

Kwa sababu ya umri wake mdogo, nilimwambia aje na mzazi wake.

Alifanya hivyo. Alikuja na mama yake. Babaye hakuwepo muda huo. Alikuwa akiishi kwingineko.

Baada ya mama yake kukiri kuwa anakubali mwanaye aende kwenye hayo mafunzo, nilionana na meneja wa kampuni husika ( nilikuwa nafahamiana naye) kwa ajili hiyo, na kwa bahati nzuri, akaliridhia ombi husika.

Lakini wakati kijana akijiandaa kwenda kuanza mafunzo, nilipata taarifa kuwa baba yake karejea kutoka alikokuwa. Kwa sababu nilikuwa ninafahamiana naye, nilimpigia simu tuonane. Nilifanya hivyo baada ya kujulishwa kuwa aliporejea kutoka alikokuwa, alianzisha "vurugu" nyumbani kwake kwa kumpiga mkewe n.k. Nilitaka nijue kama ana taarifa kuwa mtoto wake anataka akajifunze masuala ya ufundi.

Nilichobaini ni kuwa hakuwa amependezwa na hilo. Alidai kuwa mkewe na kijana wake hawakuwa wamemshirikisha, hivyo na mimi nikaamua kusitisha huo mchakato.

Lakini nilishangazwa na moja ya hoja zake. Alikuwa akijisifia kuwa yeye aliacha shule akiwa Sekondari, nafikiri "form two", baada ya baba yake kumtaka asitishe masomo akamsaidie kwa sababu alikuwa mgonjwa. Baba yake alienda mpaka shuleni kwao alikokuwa akisoma (shule ya "boarding") na kumwomba mkuu wa shule amruhusu kijana wake kuacha masomo ili akamsaidie shughuli za nyumbani kwa sababu yeye alikuwa mgonjwa na hakuwa na mtu mwingine wa kumsaidia. Japo mkuu wa shule aligoma mwanzoni, lakini kwa kuwa babaye alionesha ung'ang'anizi, mkuu wa shule aliishia kumkubalia.

Kwa mujibu wa masimulizi yake, kabla baba yake hajaaga dunia, alimshukuru na hivyo kumbariki kwa kukubali kwake kuacha masomo ili akamsaidie.

Alinisimulia hayo kunionesha kuwa kwa vile yeye alimtii baba yake, inampasa mwanaye naye kumtii pia. Jambo ambalo alilifanikisha.

Mtoto wake hakuweza kuipata tena hiyo nafasi baada ya kulazimika kusitisha huo mchakato.

Miezi michache baadaye, alinipigia tena simu kuniomba nimtafutie tena huyo mtoto wake kazi. Sikufanikiwa kufanya hivyo japo nilitamani ningeweza kuwasaidia.

Kwangu mimi, sikubaliani na huo mtazamo wa mtoto kuachishwa masomo ili akamsaidie mzazi wake . Hata huko "kwetu" haukubaliki pia.

Vipi huko "kwenu?"
 
Back
Top Bottom