Nguvu ya kufikiri pasipo kufikiri


emma115

emma115

Senior Member
Joined
Apr 28, 2012
Messages
131
Likes
109
Points
45
Age
28
emma115

emma115

Senior Member
Joined Apr 28, 2012
131 109 45
Sisi binadamu tuna uwezo mkubwa sana ambao upo ndani yetu. Wengi huwa hatufahamu uwezo huu kwa sababu tumekuwa tunafanya mambo yetu kwa mazoea. Lakini kama tukipata nafasi ya kuchunguza kwa makini yale tunayofanya, tunaona ipo nguvu ambayo wakati mwingine hatuwezi kuielezea.

Kwa mfano, kuna wakati unaweza kupata hisia kwamba kufanya kitu fulani ni sahihi, hata kama wengine wanapinga. Au kufanya kitu fulani siyo sahihi, hata kama kila mtu anafanya. Ukiulizwa kwa nini unasema ni sahihi au siyo sahihi huwezi kutoa maelezo, ila wewe unakuwa na uhakika ni sahihi au siyo sahihi. Mwisho wa siku kile unachosimamia wewe ndiyo kinakuwa kweli.

Hii ndiyo nguvu kubwa ambayo ipo ndani ya kila mmoja, nguvu ya kuweza kufanya maamuzi sahihi kwa hali fulani unayopitia, bila hata ya kufikiri, na kushindwa kujua kwa nini umefanya maamuzi hayo, lakini yanakuwa maamuzi sahihi.

Mwandishi Malcolm Gladwell amekuwa ni mtu wa kutumia tafiti mbalimbali kutetea kile anachotaka kuwaambia watu. Kwenye kitabu chake tunachokwenda kuchambua leo, BLINK, Gladwell, anatuonesha kwamba tunayo nguvu ndani yetu ya kufanya maamuzi bila ya kufikiri, na pia anatuonesha namna tunavyoweza kutumia nguvu hii vizuri na jinsi tunavyoweza kuitumia vibaya na kujikuta kwenye matatizo.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki BLINK, kuna mengi sana ya kujifunza, hasa kuhusu maamuzi tunayofanya kila siku.
1. Tafiti za saikolojia na tabia za binadamu zinaonesha kwamba hatuhitaji muda mrefu kufanya maamuzi mengi ya maisha yetu. Maamuzi mengi huwa tunayafanya ndani ya sekunde chache sana pale tunapokutana na jambo ambalo tunahitaji kufanyia maamuzi. Muda tunautumia ni sawa na ule tunaotumia kwenye kufumba na kufumbua macho.


2. Akili yetu inatumia mikakati miwili katika kufanya maamuzi ya maisha yetu.
Mkakati wa kwanza ni kutumia njia ambazo wote tunazijua, hapa unalichukulia jambo kwa ule ufahamu ambao tayari unao juu ya jambo hilo. Mkakati huu unaitwa CONSCIOUS STRATEGY. Hapa unafikiria kile ulichokutana nacho, na kuja na hatua ambazo unaweza kumweleza mtu kwa nini umefikia hatua hiyo. Mkakati huu unachukua muda mrefu kufikia maamuzi.

Mkakati wa pili pale ambapo akili yako, bila ya wewe mwenyewe kujua inafikia maamuzi. Yanakuwa ni maamuzi sahihi kwa kile unachopitia, lakini huwezi kumwelezea mtu kwa nini umefikia maamuzi hayo. Mkakati huu unaitwa ADAPTIVE UNCONSCIOUS. Mkakati huu unafanya maamuzi ya haraka, na hufikiri moja kwa moja. Hii ndiyo nguvu kubwa ambayo kila mmoja anayo, na kupitia kitabu hiki utajifunza namna ya kuitumia.

3. Nguvu hii ya kufanya maamuzi pasipo kufikiri, inatumia uzoefu ambao tayari upo ndani yetu. Katika maisha yetu, tumekutana na mambo mengi mbalimbali, uzoefu huu unakuwa umehifadhiwa kwenye sehemu ya akili yetu inayojulikana kama UNCONSCIOUS MIND. Unapofika wakati unahitaji kufanya maamuzi ya haraka, unatumia uzoefu huu kufanya maamuzi hayo.

4. Nguvu ya kufanya maamuzi bila ya kufikiri ndiyo imetuwezesha sisi binadamu kuwepo mpaka sasa, hivyo kama unafikiri huna nguvu hii, unajidanganya. Kwa mfano, kama unavuka barabara na ghafla ukaona gari inakuja kwa kasi kubwa, je unaanza kufikiria ni nini ufanye? Huna muda huo, kwa haraka sana unajikuta umeshafanya maamuzi ambayo hata huwezi kuyaelezea. Unaweza kujikuta umeruka juu, ukiambiwa urudie tena huwezi. Hii ni nguvu kubwa inayoweza kutuletea makubwa kwenye maisha yetu.

5. Akili zetu huwa zinapunguza idadi ya maamuzi ya kufanya kila wakati, ndiyo maana ukishajijengea tabia, utajikuta unafanya tabia ile bila hata ya kufikia kama unafanya. Kwa mfano kama umezoea kuamka na kupiga mswaki, basi ukiamka moja kwa moja unakwenda eneo ambalo umezoea kuweka mswaki wako, unachukua na kupiga, huhitaji kufikiria hilo. Tunaweza kutumia nguvu hii kwa pande mbili; moja kujijengea tabia za mafanikio, chagua kitu ambacho unataka kukifanya kila siku, labda kuandika au kujisomea, kisha anza kukifanya kila siku kwa muda fulani, baada ya muda itakuwa tabia na utajikuta unafanya bila hata ya kufikiri. Mbili kuvunja tabia ambazo huzipendi, kama unataka kuondokana na tabia fulani usiyoipenda, anza kuvunja yale mazoea ambayo umeshajijengea kwenye tabia hiyo.

6. Pale tunapokutana na mtu kwa mara ya kwanza, tunatumia mkakati wa pili wa akili yetu kuhukumu yule ni mtu wa aina gani. Mara nyingi hatuhitaji muda mrefu kuamua mtu tuliyekutana naye ni wa aina gani, na kama ni mtu mzuri kwetu au la. Hebu kumbuka ulipokuwa shuleni, au kama upo shuleni, ilikuchukua muda gani kujua mwalimu fulani ni mzuri au siyo mzuri? Sekunde chache mno. Kila mmoja wetu ana uzoefu wa watu mbalimbali ambao alishakutana nao kwenye maisha yake, hivyo anapokutana na mtu mpya, anatumia uzoefu ambao alishajijenga kumweka mtu huyo kwenye kundi fulani.

Unaweza kutumia hili kwa faida yako, unapokutana na mtu yeyote mpya, jua una sekunde tatu tu za mtu huyo kukukubali au kukukataa, kwa jambo lolote unalotaka kumwambia, tumia sekunde hizo vizuri kuhakikisha mtu anakubaliana na wewe. Kukubalika ndani ya sekunde hizi tatu kunatokana na mavazi ulivyovaa, mwili wako ulivyo, uso wako na hata namna unavyoanza kuongea.

7. Tunaishi kwenye dunia ambayo inaamini maamuzi bora yanahitaji muda na nguvu katika kufikia maamuzi hayo. Ndiyo maana tumekuwa tunaambiwa haraka haraka haina baraka, tumekuwa tunaambiwa tusihukumu kitabu kwa ganda la nje. Tunaamini tukichukua muda na kukusanya taarifa za kutosha basi tutafanya maamuzi bora, hii ni kweli kabisa. lakini, yapo maamuzi ambayo tunaweza kuyafanya kwa muda mfupi sana, na yakawa maamuzi bora pia. Na maamuzi haya ni muhimu pale unapokuwa kwenye hali ya haraka, ambapo huna muda na huna rasilimali za kukutosha kusubiri mpaka uwe na uhakika. Hapa ndipo unapotumia uzoefu wako kufanya maamuzi bila hata ya kufikiri.

8. Nguvu hii ya kufanya maamuzi bila ya kufikiria siyo salama kwa asilimia 100, mara nyingi nguvu hii inaweza kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi. Maamuzi haya yanakuwa siyo sahihi siyo kwa mtu kupenda, bali kwa uzoefu ambao mtu huyo anao. Kwa mfano kama mtu ana pendelea vitu fulani au ana imani fulani, mara zote atafanya maamuzi yanayoendana na kile anachopendelea au anachoamini. Kwa hali hii maamuzi yanaweza yasiwe bora. Hivyo ni muhimu kuhakikisha una uelewa wa kutosha kabla ya kutegemea nguvu hii katika ufanyaji wako wa maamuzi. Muhimu ni kuhakikisha huna upendeleo wowote wewe binafsi kwenye maamuzi unayotaka kufanya.

9. Nguvu hii ya kufanya maamuzi pasipo kufikiri pia inaweza kutengenezwa na kuboreshwa zaidi. Kwa sababu tumeshaona wengi tunayo nguvu hii, na pia nguvu hii inaweza kutumika vibaya, ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha tunajijengea nafasi nzuri ya kutumia nguvu hii. Unaweza kujenga nguvu hii kwa kuhakikisha una uzoefu sahihi wa kila jambo muhimu kwako, kuondokana na upendeleao au ubaguzi wowote ambao umejijengea au kujengewa, na kuweza kuweka imani yako pembeni wakati wa kufanya maamuzi muhimu.

10. Ili kuweza kufanya maamuzi pasipo kufikiri, kitu cha kwanza ambacho akili zetu zinafanya, ni kutafuta vitu vidogo kwenye hali tunayotaka kufanyia maamuzi. Kuna misingi mikuu ambayo tunaiangalia na baada ya hapo tunaweza kufanya maamuzi bora kabisa sawa na anayetumia muda mwingi kufuatilia swala zima. Hivyo ni muhimu sana kujua msingi wa kila jambo unalohusika nalo.

11. Unaweza kutabiri kama ndoa yoyote itadumu au itavunjika kwa kuangalia wanandoa wakifanya maongezi yao. Na hapa huhitaji hata dakika moja. Unachohitaji kuangalia ni mambo manne muhimu, haya ndiyo yanayoua ndoa ya aina yoyote ile. Mambo hayo ni KUJIHAMI, KULAUMU, KUKOSOA na DHARAU. Kama kwenye mazungumzo ya wanandoa utaona yametawaliwa na mambo hayo, ndoa hiyo haiwezi kudumu kwa muda mrefu. Na katika hayo manne, moja lina nguvu kubwa sana ya kuua ndoa kwa haraka, nalo ni DHARAU, watu wanaweza kuvumilia kukosolewa, lakini hawawezi kuvumilia kudharauliwa. Unahitaji sekunde mbili tu kujua kama mwanandoa anamdharau mwenzake, kwa kuangalia namna anavyoongea na mwenzake au anavyomjibu.

Somo muhimu zaidi hapa ni kama unataka ndoa yako idumu, basi wewe na mwenza wako, epukeni mambo hayo manne, na muhimu zaidi, epukeni dharau, hakuna ndoa inayoweza kudumu kama watu wanadharauliana.

12. Wanawake na wanaume wanatofautiana kwenye hisia hasi wanazokuwa nazo. Wanawake mara nyingi ni wakosoaji, wanaume mara nyingi ni walalamikaji au wanalaumu. Hivyo katika mazungumzo ya wanandoa, mwanamke anapozungumzia tatizo, huwa analizungumzia kwa kumkosoa mwanaume, wakati huo mwanaume atajitetea kwa kumlaumu mwanamke au kingine chochote. Hii inaweza kuvumiliwa, lakini inapokuja kwenye dharau, hakuna upande unaopendelea zaidi dharau, na hakuna anayeweza kuvumilia. Elewa hili na litumie kuboresha mahusiano yako na wengine.

13. Unaweza kuijua tabia ya mtu na kila kitu kuhusu yeye kama utapata dakika 15 za kukaa ndani ya chumba chake. Kukaa ndani ya chumba cha mtu, kunakupa fursa ya kumjua mtu, vizuri, hata kama hujawahi kuonana naye uso kwa uso. Kwa namna alivyopangilia vitu vyake, kwa vitu alivyonavyo chumbani kwake, unaweza kujua kama ni mtu makini au la. Unaweza kujua kama mtu ana furaha au huzuni kwa kuangalia namna alivyoanga vitu vyake.

Somo; namba tunavyopanga nyumba na vyumba vyetu, kunaeleza sana tabia zetu.

14. Watu wanaowashtaki madaktari kwa makosa waliyofanya, huwa hawawashtaki kwa sababu ya makosa hayo, bali huwa wanawashtaki kwa sababu nyingine kabisa. Tafiti zinaonesha madaktari wengi wanaofanya makosa huwa hawashtakiwi kabisa na wateja wao, na wale ambao wanashtakiwa na wateja wao ni kwa sababu ya mkwaruzano mwingine ambao ulitokea kabla ya daktari kufanya makosa. Kwa mfano kama hakumsikiliza vizuri, au kama alikuwa anafanya maamuzi bila kumshirikisha, basi mtu anakuwa na hasira ya kumshtaki daktari pale anapokosea.

Somo; watu wanafanya maamuzi yao kulingana na sisi tulivyowafanya kujisikia. Kama tumewaheshimu na kuwafanya wajisikie vizuri, watafanya maamuzi mazuri juu yetu. Kama tumewadharau na kuwafanya wajisikie vibaya, watafanya maamuzi mabaya juu yetu.

15. Nguvu ya kufanya maamuzi pasipo kufikiri ipo ndani ya mlango uliofungwa kwenye akili zetu. Hii ina maana kwamba hatuwezi kujua kwa hakika kwa nini tumefanya maamuzi ya aina fulani, lakini tunakuwa na uhakika ni maamuzi sahihi kwetu. Ili tuweze kutumia nguvu hii vizuri ni lazima tukubali maajabu yake, kwamba siyo rahisi kujua kwa hakika kwa nini tunahisi kitu fulani ni sahihi.

16. Maamuzi tunayofanya, yanaathiriwa sana na mawazo ambayo tayari yapo ndani ya akili zetu. Yale mawazo ambayo umekuwa nayo muda wa karibuni, yanaathiri maamuzi ambayo unafanya kwa muda huo. Hii inaitwa PRIMING na imekuwa inatumika kuwashawishi watu wafanye vitu fulani. Kwa mfano mtu aliyetoka kuangalia filamu ya mapigano, akikutana na mtu akamuudhi atakuwa tayari kumpiga. Wakati mtu aliyetoka kuangalia filamu ya maelewano atakuwa kwenye hali ya kuelewana.

Somo; ili kuweza kufanya maamuzi sahihi wakati wote, hakikisha una mawazo sahihi na chanya kwenye akili yako. Kwa sababu mawazo hayo yanaathiri maamuzi unayofanya. Pia kuwa makini na wale wanaokujaza mawazo fulani ili kukushawishi ufanye maamuzi ya kuwanufaisha wao.

17. Namna ambavyo tumekuzwa pia inaathiri maamuzi tunayofanya. Kile ambacho kipo kwenye jamii zetu na tumekua nacho, kinakuwa sehemu ya maamuzi yetu, hata kama hatukiamini moja kwa moja. Kwa mfano, utafiti uliofanywa, kwa wanafunzi wa vyuo, ulionesha kwamba wanafunzi weusi walifeli zaidi pale walipoulizwa asili yao kabla ya mtihani. Yaani swali la kwanza linakuwa je wewe ni mtu mweusi au mweupe, wale weusi walifeli zaidi kuliko weusi waliofanya mtihani ambao haukuwa na swali hilo. Hii ina maana kwamba mtu anapokumbushwa kuhusu jambo ambalo jamii imekuwa na kawaida ya kulibeza, anakubaliana na jamii.

Somo; maamuzi mengi tumekuwa tunayafanya kwa kuchukua jinsi jamii imekuwa inafanya mambo yake, mara nyingi imekuwa siyo sahihi lakini bado tunafanya hivyo. Ni muhimu kujirekebisha na kuondoa imani hizi ili kuweza kufanya maamuzi bora.

18. Mara nyingi kuna vitu ambavyo tunataka, lakini hatujui kama tunavitaka, na mbaya zaidi hatujui hata tunataka nini. Uwezo wetu wa kufanya maamuzi bila ya kufikiri unajua nini tunataka, ila kwa sababu tumeshaona kwamba maamuzi haya yanafanyika kwenye mlango uliofungwa, basi tunakuwa hatujui kwa hakika nini tunataka.

Tuchukulie mfano wa uchumba, mara nyingi watu kabla hawajapata wachumba, huwa wanaweka vigezo vingi, nataka mchumba awe hivi au vile. Lakini unakuja kushangaa mtu huyo ameoa au kuolewa na mtu ambaye hana kabisa zile sifa ambazo alikuwa anazitaja, lakini anafurahia ndoa yake. Hii ni kwa sababu kuna vitu anavitaka kwenye mahusiano, lakini havijui ni vitu gani, ila anapovipata anavifurahia.

19. Nguvu yetu ya kufanya maamuzi pasipo kufikiri pia inaweza kudanganywa na chuki, upendeleo au ubaguzi ambao upo ndani yetu. Kwa mfano wanaume ambao wana miili mikubwa, warefu na wenye sura nzuri, wamekuwa wanaonekana wana uwezo mkubwa kuliko wengine. Lakini hii mara zote imekuwa siyo sahihi, lakini mara zote bado tunawaamini watu wa aina hiyo. Ili uweze kufanya maamuzi bora, bila hata ya kufikiri, tunahitaji kuondokana na chuku, upendeleo na ubaguzi.

20. Watu wengi wamekuwa wanatumia ubaguzi wao kukosa wateja kwenye biashara zao. Kwa mfano utafiti uliofanya umeonesha kwamba mtu mweusi anapokwenda kununua gari, anapewa bei kubwa kuliko mtu mweupe. Hii ni kutokana na ubaguzi ambao watu wamejengewa kwamba watu weusi hawana uwezo wa kununua magari kama weupe, au ni wasumbufu kwenye bei kuliko weupe.

Somo; kama upo kwenye biashara au kazi yoyote, usiwabague watu kwa mwonekano wa nje. Mpe kila mtu nafasi sawa, mchukulie kila mtu kama mteja sahihi na wape watu wote huduma sawa. Hii itakuwezesha kuwa na wateja bora kwenye kila unachofanya.

Kitu kimoja muhimu unachopaswa kujifunza kutoka kwenye kitabu hiki ni kwamba akili yako ina uwezo wa kufanya maamuzi bora bila ya kufikiri. Uwezo huu unatokana na uzoefu ambao umejijengea kwenye maisha yako, mawazo ambayo yametawala akili yako, ubaguzi, chuki na hata upendeleo ambao umejifunza kwenye jamii unayoishi.

Hakikisha unaiandaa akili yako vizuri ili iweze kufanya maamuzi bora kwako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
 
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined
Feb 4, 2009
Messages
43,207
Likes
40,727
Points
280
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined Feb 4, 2009
43,207 40,727 280
Asante sana kwa mada fikirishi
 
Red Giant

Red Giant

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2012
Messages
11,717
Likes
9,877
Points
280
Red Giant

Red Giant

JF-Expert Member
Joined Mar 9, 2012
11,717 9,877 280
kitabu kizuri sana. jamaa kichwa sana.
 
Dahafrazeril

Dahafrazeril

JF-Expert Member
Joined
Jul 28, 2015
Messages
1,509
Likes
2,006
Points
280
Dahafrazeril

Dahafrazeril

JF-Expert Member
Joined Jul 28, 2015
1,509 2,006 280
Thank you sana Mkuu kwa kutushirikisha!

Kwa mara ya kwanza nilikiona "THE BLINK" katika filamu moja ya Kanumba (Jina limenitoka kidogo),Nilikitafuta sana pasipo mafanikio mazuri.Nadhani kitakuwa kizuri mno.

Shukrani kwa kushea nasi.
 
Tutor B

Tutor B

JF-Expert Member
Joined
Jun 11, 2011
Messages
8,843
Likes
4,710
Points
280
Tutor B

Tutor B

JF-Expert Member
Joined Jun 11, 2011
8,843 4,710 280
Sina uhakika kama watanzania wenye uvivu wa kusoma wataweza kusoma thread hii hadi mwisho.
Nimeisoma na nawashauri wale wanaopitia comments pasipo kusoma wasifanye hivyo! Kuna kitu kikubwa ambacho hakifundishwi mashuleni.
Ahsante mtoa mada hii
 
red apple

red apple

JF-Expert Member
Joined
Dec 6, 2012
Messages
373
Likes
239
Points
60
red apple

red apple

JF-Expert Member
Joined Dec 6, 2012
373 239 60
Ahsante sana, namba sita hii inanisaidia sana katika shughuli zangu, nimekuwa naitumia bila kujua.
Namba 5 pia...nadhani inasaidia pia katika kuwajengea tabia watoto.
 
Tutor B

Tutor B

JF-Expert Member
Joined
Jun 11, 2011
Messages
8,843
Likes
4,710
Points
280
Tutor B

Tutor B

JF-Expert Member
Joined Jun 11, 2011
8,843 4,710 280
Ahsante sana, namba sita hii inanisaidia sana katika shughuli zangu, nimekuwa naitumia bila kujua.
Namba 5 pia...nadhani inasaidia pia katika kuwajengea tabia watoto.
Kwa ujumla wake imekaa vizuri ila kwangu mwenye kesi na wanandoa namba 11 ni babu kubwa!
 
red apple

red apple

JF-Expert Member
Joined
Dec 6, 2012
Messages
373
Likes
239
Points
60
red apple

red apple

JF-Expert Member
Joined Dec 6, 2012
373 239 60
Kwa ujumla wake imekaa vizuri ila kwangu mwenye kesi na wanandoa namba 11 ni babu kubwa!
Aisee kweli hii imekaa vizuri, hapa kwenye kukosoa pananihusu...
 

Forum statistics

Threads 1,274,695
Members 490,787
Posts 30,521,528