WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likisema halina mamlaka ya kuzuia hati ya uhamisho wa kimataifa ya mchezaji Mrisho Ngassa kwenda El Merreikh ya Sudan kama ilivyoombwa na Simba, mchezaji mwenyewe amewataja Wekundu hao wa Msimbazi kumwacha aende kusaka maisha mapya ya soka.
Ngassa anayecheza kwa mkopo Simba akitoka klabu ya Azam FC, ameuzwa kwa dau la Sh120 milioni, lakini Wekundu wa Msimbazi wanapinga uamuzi huo wakidai winga huyo ni mali yao.
Katika madai yao, Simba imewasilisha barua TFF ikiliomba shirikisho hilo kuzuia hati ya uhamisho wa Ngassa (ITC) kwa madai ina mkataba na Ngassa.
Mtendaji Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikiri kupokea barua kutoka Simba, lakini akasema shirikisho hilo halina uwezo kuzuia ITC, kwa vile mwenye uwezo kutoa hati hiyo ni timu inayommiliki mchezaji.
Osiah alisema timu husika ndiyo huingia kwenye mtandao TMS na kuweka za mchezaji huyo ambazo ndizo zitamfanya kupata hati ya uhamisho na wao watapata taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhusu taarifa hizo.
Hatuna uwezo wa kuzuia hati ya uhamisho wa mchezaji, sisi hatuingii kwenye mtandao kwani hatuna makubaliano halali ya mchezaji na klabu. Mwenye uwezo wa kufanya hivyo ni mmiliki halali wa mchezaji na sisi tutapewa taarifa tu kutoka Fifa, alifafanua Osiah.
Osiah alisema awali kabla ya kupokea barua ya malalamiko ya Simba, walipata barua ya Azam wakidai kumchukua Ngassa waliyempeleka kwa mkopo kwa mabingwa hao wa Bara.
Akizungumzia zaidi suala hilo, Osiah alisema: Kanuni za soka ziko wazi, kwamba mchezaji hawezi kuuzwa wala kutolewa kwa mkopo na klabu anayoichezea, isipokuwa ile iliyomtoa kwa mkopo ndiyo yenye mamlaka.
Aidha, alisema klabu anayocheza kwa mkopo haina mamlaka ya kuingia naye mkataba mwingine bila kwanza kuwasiliana na klabu yake ya awali iliyomtoa kwa mkopo.
Kwa maana hiyo, Simba haina mamlaka na Ngassa isipokuwa Azam FC, na walifanya makosa tangu awali ya kumsainisha mkataba mwingine wakati ana mkataba na timu yake ya awali ambayo ni Azam, alisema Osiah.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema hawako tayari kudhulumiwa Ngassa kwa vile walishamalizana na Azam.
Kamwaga alisema uongozi wameandika barua TFF kudai haki yao na kwamba kama ni lazima mchezaji huyo kuuzwa basi warejeshewe pesa zao walizompa mchezaji huyo.
Azam wamemtoa Ngasa kwa mkopo, lakini hawajui anakula nini, analipwa shilingi ngapi na analala wapi hivyo na sisi tulitakiwa tupate mgawo wetu, alisema Kamwaga.
Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba amewataka pande zote mbili kukaa chini na kumaliza utata wa mchezaji huyo kwa faida ya pande zote mbili na mchezaji mwenyewe.
Akizungumza mjini hapa, Ngassa aliye na kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Kilimanjaro Stars) inayoshiriki michuano ya Chalenji, ameitaka klabu yake ya Simba imwongezee masilahi kama wanahitaji abaki kuichezea timu hiyo.
Ngassa alisema amesikitishwa na uamuzi wa Simba kutaka kumbania kwenda kusaka maisha mapya ya soka hasa ukizingatia kwamba hiyo ndiyo fursa yake muhimu ya kujitangaza kimataifa. Kama Simba bado wananihitaji, basi sharti la kwanza waboreshe masilahi yangu, wawe wazi kusema watanipa kiasi gani na mshahara wa mwezi utakuwa kiasi gani, alisema Ngassa.
Ngassa alisema kuuzwa kwake kwa timu hiyo ya Sudan kusihusishwe na siasa za Simba na Yanga, na kwamba Azam imeweka mbele zaidi masilahi yake.
Mchezaji huyo kinara wa mabao kwenye Michuano ya Chalenji inayoendelea Uganda, atafaidika na kiasi cha Sh75 milioni kutoka Sh120 milioni kama gharama halisi ya kuuzwa kwake.
Imeandikwa na Sosthenes Nyoni (Kampala), Kalunde Jamal na Jessca Nangawe. Source: Mwananchi