Na Maggid Mjengwa,
REAL Madrid ya Hispania ni moja ya timu tajiri sana duniani. Mara nyingi, usajili wa wachezaji wa klabu hiyo huwa ni wa kufuru. Real Madrid ni mkusanyiko wa wachezaji nyota. Na hakika, kocha makini anaelewa, kuwa hakuna jambo gumu kama kufundisha timu yenye mchanganyiko wa wachezaji nyota, tena nyota wa dunia.
Kila mmoja nyota, na uwanjani hivyo hivyo. Kila mmoja anataka kuonyesha umahiri wake. Kazi na mafanikio uwanjani ni ya mmoja mmoja, si kazi ya timu. Ndio maana, Real Madrid, pamoja na kuundwa na nyota wengi wa dunia, bado huwa na kibarua kigumu sana kunyakua ubingwa wa Hispania. Juzi tu, wamenyeshewa mvua Barcelona, 5-0!
Baraza limeshaapishwa. Joe Magufuli na Harry Mwakyembe wameanza mchezo kwa kasi ya kutisha. Kabla ya kusanyiko la Jumatatu la Baraza zima la Mawaziri , wao Jumapili walishaingia Ukumbi wa Karimjee. Mbele ya kamera za wanahabari wamemwaga cheche. Yale yale, kuna tulioanza kuchoshwa na mbinu zile zile wakati mazingira ya mchezo yamebadilika. Ndio maana hatupati ushindi. Mitaani kuna hata wanaokejeli; Usanii mtupu!
Tumemwona John Magufuli akiongea kwa ukali pale ukumbi wa Karimjee. Anasema ndani ya mwezi mmoja hakuna foleni ya magari Dar es Salaam! Hapa Iringa ninakoishi jamaa mmoja aliuliza; Hayo magari ya Dar yatakwenda wapi ? Niliiona mantiki katika swali lake hilo. Magufuli akaahidi pia kujenga njia za kupita juu kwa juu. Daraja la Kigamboni, kama NSSF wameshindwa. Tulidhani angeongea na NSSF kwanza kujua wamefikia wapi.
Magufuli akasema pia kuwa kunaweza kukawapo na ferry ya kupeleka abiria mpaka Tegeta ili kupunguza foleni za barabarani. Ndio hapa tunachoshwa na wanasiasa. Hilo la Ferry ya kwenda Tegeta haliwezi kuwa Ferry kwa maana ya Kivuko bali ni usafiri wa meli kwenda Tegeta. Ni suala jingine kabisa, maana, meli hiyo itahitaji kuingia bahari kuu na pale Tegeta kujengwe bandari ndogo ya meli kutia nanga.
Ndio, Magufuli kaongea mengi na kapambwa kweli kwenye vyombo vya habari. Kuna tunaotilia mashaka staili hii ya uongozi. Tuna sababu za msingi. Inatukumbusha hata pale Waziri Magufuli alipotumia maneno mengi kutetea kuuzwa kwa nyumba za Serikali. Ni zoezi alilolisimamia Magufuli mwenyewe katika Utawala wa Awamu ya Tatu wa Rais Mkapa.
Uuzwaji wa nyumba za Serikali kwa maana ya Nyumba za Wananchi, ni moja ya vitendo vya ufisadi mkubwa uliofanyika katika Utawala wa Awamu ya Tatu. Waziri Magufuli aliyesimamia zoezi hilo na ambaye pia ni mmoja wa waliofaidika nalo, ana lazima, kwa namna yake, kuwaomba radhi Watanzania kwa dhuluma ile waliyotendewa ambayo kamwe hawataisahau.
Naam. Na kama mawaziri katika Serikali ya Kikwete watacheza kwa staili ya Kila mtu na kipaji chake , basi, nahofia, kuwa wenyewe kwa wenyewe watakwamishana uwanjani. Watanyimana hata pasi. Rais Jakaya Kikwete hahitaji Real Madrid, itamnyima ushindi. Na hilo ni Neno La Leo.
( Hii ni sehemu ya makala yangu ya Raia Mwema iliyochapwa jana Jumatano)
Maggid
Iringa
Desemba 2, 2010
http://mjengwa.blogspot.com