NEC idhibiti kwa vitendo kampeni chafu Arumeru

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
mwananchilogo.jpg
JUZI Kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilivionya vyama vya CCM na Chadema, kuacha kampeni chafu baada ya kuthibitika kuwa vimekiuka sheria na maadili ya uchaguzi kutokana na vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vinafanywa na wafuasi wao.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi alisema onyo hilo lilitolewa baada ya kukamilika kwa kikao cha kamati ya maandalizi ambacho kilipokea barua matano za malalamiko kuhusu mwenendo usioridhisha katika kampeni hizo.

CCM wamepewa barua ya onyo kutokana kitendo cha wafuasi wake kuchana picha za mgombea wa ubunge wa Chadema, Nassari siku ya uzinduzi wa kampeni za CCM zilizofanyika katika Uwanja wa Ngaresero.

Chadema nao wamepewa onyo kutokana na wafuasi wake kuwakashifu viongozi wa CCM katika eneo la Meru Garden ambako viongozi hao na mgombea wao, Sumari walisimama ili kupata chakula.


Tunachukua nafasi hii kuipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kuchukua hatua hiyo muhimu ambayo itasaidia kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu na haki.

Tunasema hivyo kwa sababu, chokochoko hizi ambazo zimeanza kufanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivi zisipodhibitiwa mapema vinaweza kusababisha umwagaji wa damu.

Sote tunajua jinsi kampeni chafu zilizofanywa na wafuasi wa Chadema na CCM zilivyotia dosari uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Igunga uliofanyika Oktoba mwaka jana.

Kuonyesha kuwa hatufurahishiwi na vitendo hivyo, hii ni mara ya tatu kuchapisha tahariri katika safu hii kutahadharisha juu ya siasa chafu katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki.

Katika tahariri mbili zilizotanguliwa tulikumbusha madhara yanayoweza kutokea endapo siasa chafu za kupakana matope zitaendelea kufanywa huku tukisisitiza kuwa wagombea viongozi wa vyama vya siasa hasa CCM na Chadema pamoja na wapambe wao wahubiri sera za vyama vyao na jinsi watakavyoshirikiana na wananchi wa Arumeru Mashariki kukabiliana na changamoto za maendeleo zinazowakandamiza.

Tulionya kuwa kampeni chafu zinaweza kusababisha vurugu kama zilizotokea Igunga na ndicho kinachoanza kujitokeza kama ambavyo tumeshuhudia matukio wanachama wa vyama hivyo kushambuliana na kesi zao ziko polisi.

Tunadhani kuwa vitendo hivyo vya ukiukwaji wa sheria ya uchaguzi zinazofanywa kwa makusudi ili kuharibu kampeni za wapinzani wao, zinafanyika huku viongozi wa juu wa vyama hivyo wakijua.

Tunasema hivyo kwa sababu hatujamsikia kiongozi yeyote wa juu wa vyama hivyo akiwakemea wafuasi wao kuhusiana na vitendo hivyo.

Ni jambo la ajabu kuona vyama hivyo vikubwa vya siasa nchi ambavyo vilipaswa kuwa kioo cha vyama vidogo vya siasa nchini, sasa vinaongoza kuvunja sheria ya uchaguzi!

Ni muda mwafaka sasa kwa viongozi wa vyama hivyo kuwaelimisha wafuasi wao kwamba fujo, au kufanya chokochoko za aina yeyote dhidi ya chama kingine kosa na kamwe haziwezi kumsaidia mgombea wao kupata ushindi.

Njia pekee ambayo vyama hivyo vinatakiwa kufanya ni kuongeza nguvu katika kuwanadi wagombea wao kwa wananchi badala ya wapambe wao kuchana picha za wagombea wa vyama vingine au kutumia lugha chafu za matusi dhidi ya viongozi wao.

Wanachohitaji wananchi wa Arumeru Mashariki kwa sasa ni kusikia namna wagombea wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo watakavyotatua matatizo mbalimbali ya eneo hilo ikiwamo maji na tatizo sugu la ardhi.

Ni wazi kwamba, wananchi wa Arumeru Mashariki hawahitaji kusikia lugha za matusi, kejeli vijembe na vitendo vingine vinavyoashiria vurugu vinavyofanywa na baadhi ya wafusia wa vyama hivyo.

Tunaamini kuwa Tume ya Uchaguzi haitaishia kutoa onyo hili, bali itachukua hatua za kudhibiti vitendo vyovyote vinavyoashiria kuvuruga uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Aprili Mosi mwaka huu.

NEC idhibiti kwa vitendo kampeni chafu Arumeru
 
Back
Top Bottom