SEHEMU YA 28
Kila mmoja alipigwa na taharuki mbali na bumbuwazi. Nilijihisi kutetema kwa hasira. Kuna baadhi ya watu walitaka kuwazuia kwa hasira na mshangao lakini sauti ya kiongozi wa kanisa ilisikika kuwazuia.
"Watu wa Mungu naomba tutulie chini hapa ni sehemu takatifu ya ibada. Karibuni sana watu wa Mungu kwa ujio wenu heri na iwe ndani yake mtufumbue kile kilichofumbwa mbele ya nyuso zetu kuhusu tukio la ndoa hii tarajiwa kama ni haki ama si haki. Tutulie watu wa Mungu naomba wale wa huduma ya kwanza wamsaidie mama yetu kwanza."
Macho alisema na watu wa huduma ya kwanza waliwahi pale alipodondoka mama kusaidiana na wale waliokuwa wamenyanyua na kumlaza sehemu salama kwa huduma ya kumzindua. Baadhi ya watumishi wa Mungu pia waliungana na wale watu wa huduma ya kwanza kumpa msaada mamaangu huku wengine wakiupokea ugeni ule ulioongozwa na mwanakiranga Atuganile.
Rose macho yalimtoka akiwa haamini kile alichokuwa anakiona mara baada ya watu wale kufika kanisani. Juu kwenye mikono ya yule mchungaji alishika cheti cha ndoa. mama Atu alikuwa na albamu ya picha. Hakika walijipanga. Walijipanga mno kuja kunidhalilisha na kunitibulia ndoa yangu. Wapambe wetu walifanya kazi ya ziada kutushika mimi na Rose ambaye alishaanza kuishiwa nguvu. Nilitamani kumparua Atuganile lakini nilishindwa kwa kushikiliwa na mpambe wangu ambae nae alikuwa katikati ya taharuki pia kwa heshima ya kanisa nilibaki kuwa mpole nikitamani ardhi ipasuke.
"Bwana yesu asifiwe" alisalimu baada ya kushika kipaza yule mtumishi wa Iringa ambaye nilimfahamu na ndiye aliyehusika kutufungisha ndoa.
Watu waliitika huku wakiwa na sauti za fadhaiko wakiyastaajabu ya Musa.
"Naitwa mchungaji Albert. Kutoka katika kanisa la KKT Iringa. Mimi ndiye niliyewaunganisha bwana Onesmo John ambae leo hii anataka kubatilisha maneno ya Mungu mbele ya kanisa hili tukufu, na bibi Atuganile Mwakyusa huyu aliye mkono wangu wa kuume. Tuliwaunganisha na kuwa mwili mmoja mbele ya mashahidi wa Mungu niliokuja nao leo hii kutoa uthibitisho na hiki ni cheti maalum cha ndoa yao tukufu ambayo sasa inatimiza miezi kumi na moja." Aliongea yule mchungaji huku akilionesha kanisa kile cheti cha ndoa na kuwafanya umati mzima uliojitokeza pale kuachama midomo na kubaki na taharuki kubwa. Si baba mkwe si mama mkwe, si wachungaji si marafiki, si waumini na mashahidi wote hawakuamini na wengine kushika mikono kichwani.
"Yaani kumbe ameoa hata mwaka bado? aah" sauti za minong'ono ilianza kuzoza na kusikika. Rose alinitazama akiwa ameachama mdomo akitaka kusema jambo lakini alishindwa na kubaki ametumbua macho kabla hajadondoka pamoja na mpambe wake ambae alishindwa kumzuia pindi alipokata moto.
Nilishindwa kuvumilia na kujiangusha kwa nguvu nikitamani hata nife kuliko aibu ile iliyonivaa kama upepo wa shari jangwani.
Shughuli nzima ilichafuka na kuvurugika kabisa. Vurumai lilianza kanisani waumini imani zilihamia mifukoni wengine wakiwa na hasira nami huku wengine wakiwa na hasira ya wale waliokuja kutibua shughuli. Nilijidai kuzimia nikitamani hata nisiamke kipindi hiko nikiwa sijui nini hatima ya mamaangu na mke wangu mtarajiwa ambae sasa nilijua ndio basi tena nimemkosa.
Niliisikia sauti ya mchungaji aliyejiandaa kutufingisha ndoa akiihitimisha na kubatirisha ibada ya ndoa baada ya kujiridhisha na cheti cha ndoa sambamba na ushahidi wa picha. Tulikimbizwa kwenye gari baada ya kufanyiwa huduma ya kwanza huku nikiwa nina fahamu lakini nikijizimisha kwa aibu iliyonivaa. Sijajua kwa muda ule mambo yaliishaje pale kanisani kipindi tulipokimbizwa hospitali ambapo sakata letu lilikuja kujenga habari kubwa jijini kwenye vyombo vya habari hususani baada ya wapiga picha na wana habari waliokuwa pale kushuhudia harusi yetu kutoa taarifa kwa uma kile kilichojitokeza. Mtu mwengine tuliyemchafua na kumtia aibu kubwa ni baba Rose ambaye aliheshimika sana na aliwaalika marafiki zake wengi wengine wakitoka nje ya nchi.
Ingawa haikuchukua muda mlefu kwangu kujirudishia fahamu pindi nilipokuwa hospitali ili nisiwape tabu madaktari ya kunichunguza sana na kunidunga masindano wakati nina fahamu zangu timamu. Lakini nilijifanyisha kuchanganyikiwa sana ingawa muda mwingi nilikuwa na mpambe wangu aliyejitahidi kunifariji na kunituliza baada ya kufumbua macho. Sulu naye alikuwa sambamba pia na ndiye pekee alijua kila kitu ingawa yule mwengine alitamani kujua nae kulikoni niwe nimeoa hata mwaka bado halafu nifiche na kuoa tena? Nini sababu? Yepi yalitokea? Hakika haikuingia akilini kwa haraka eti ndoa ya mwaka mmoja tu iwe na migogoro mikubwa ambayo ikose vikao hata taratibu kwa wazee na watumishi wa Mungu ili watufanye tuishi kwa amani? Tena sote tukiwa katika umri wa kuheshimu watu wazima na hofu za kusikiliza nasaha? aaaaah! hakika usilolijua ni usiku wa giza. Ndoa yangu kwa Atuganile ilikuwa ni zaidi ya mwiba ulionasa katikati ya koromelo.
Sikujua nini kiliendelea kwa Rose upande wa pili wala mamaangu ambaye naye alipoteza fahamu pale kanisani.
Siku ya pili iliwadia tukiwa hospitalini ambapo watumishi wa Mungu nao walifika na kuwa karibu nasi huku wakiwa na shauku ya kujua mengi kuhusu ndoa hiyo ambayo kwa uchache tayari walishaambiwa na wenzao waliotoka Iringa na mama Atu pamoja na mwanae ambao niliamini maelezo yao yalijaa uongo wa asilimia mia wa kunipa tuhuma na unyama kwangu. Najua walijisafisha kupitia sisi. Walitupaka matope na kuonekana si watu mbele za Mungu. Waongo tulioshindikana tuliokuwa tayari kulidanganya kanisa na watu wa Mungu kwa kufanya tukio kubwa takatifu la ndoa.
Laiti isingekuwa welevu na imani ya kweli waliyokuwa nayo watumishi wa Mungu basi hata wasingetamani kuniona na kuzungumza nami kwa ukarimu wa hali ya juu pale hospitalini.
"Onesmo pole sana lakini hupaswi kuwa na mawazo kwa sababu ya matatizo hika na kunipelekea moja kwa moja upande wa nyuma ambayo isingekuwa ndoa ya kweli mbele za Mungu. Sisi ni watumishi wa Mungu na tutakusaidia kuweka sawa matatizo yako yawe ya kimatamanio ama kishetani na kusababisha utake kukiuka maandiko. Kuwa na imani weka neno la bwana kifuani mwako hakika amewabariki wale wazitakasao nafsi zao kwa kusema kweli."
Sikuwa na uwezo wa kujibu kitu zaidi ya kububujikwa machozi kadri sauti ya mchungaji ambaye pia alikuwa rafiki wa karibu wa baba Rose, pindi alipokuwa ananisemesha kwa hekima pale kanisani. Nilitamani kuzuzngumza mengi kwa uchungu lakini nilishindwa na kuona uongo wangu wa awali ushazifunga haki zote. Tayari nilishaonekana muongo mbele ya wakubwa na watu niliowaheshimu mno. Ni kweli nilifanya uongo lakini ulichochewa na masahibu ya ndoa yangu yaliyopamba pasipo ukomo. Atuganile walikuwa mafundi sana wa uongo na kujitetea. Kwa maelezo mafupi ya watumishi wa Mungu walibainisha yale waliyoyasikia na kuthibitishiwa makubaliano yangu na kina Atu. kuwa nilimuhmishia chuo mkoani hata miezi sita bado ili akasome vizuri lakini kumbe nilikuwa na nia ya kuoa kiujanja ndio maana nikamuachisha chuo cha awali hapa Dar. Maelezo yao yaliendana kabisa na ukweli wa picha kwa mtu ambae alikuwa mbali nasi na haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea. Uthibitisho kuwa Atu alikuwa anasoma jijini pale walikuwa nao pia na waliwaonesha wachungaji kila kitu. Kwa kweli walijipanga na walinishinda. Baba mkwe aliona kila kitu na alikuwa katika ngazi zote tokea mwanzo hadi siku hiyo ya pili ambayo hawakuwa na la ziada zaidi ya kuondoka kwa Kyela pasipo hata kusubiri hatima ya hali zetu hospitalini wakijifanya wamechukia na kukasirika huku wakiwa hawana imani nasi wakingoja hekima za watu wa Mungu kulisimamia suala hilo pindi nitapozinduka na kuwa tayari. Aaaaaaah! kwa kweli Atuganile ni zaidi ya mashetani.
Ilikuwa ni zaidi ya fadhaa ambayo sijawahi kuiota awali kama itakuja kunitokea.
Nguvu na hali ya kawaida ilishanirudia ingawa sikutamani kutoka nje ya hospitali. Lakini jioni ya siku hiyo baada ya madaktari kuridhika na maendeleo yangu niliruhusiwa kutoka pale hospitalini huku nikiwa naamini kutokufika kwa baba na mama Rose hospitali hususani kule nilipolazwa mimi huenda kulitokana na hasira ya fedheha niliyowasababishia mbele ya umati kanisani. Lakini kumbe sikujua kilichotokea pindi nikiwa hospitali kwa siku mbili tu. Hakika nilifihwa hata baada ya kufikishwa nyumbani moja kwa moja na kukuta umati umejaa. Umati ambao awali nilipokuwa nashuka garini nilijua ni wambea na waandishi wa habari walikuwa wanaendelea na maswali ya hapa na pale kuhusu tukio langu. Sikujua kabisa na nilishasahau kuwa kwenye tukio lile kumbe na mama nae alipatwa masahibu ya kushuka kwa mapigo ya moyo pindi uvamizi wa hila ulipoingia kanisani kuweka pingamizi. Vilio na sauti za maombelezo ndivyo vilinigutusha na kuwafanya waliokuwa sambamba nami (Sulu na mpambe wangu.) kunishika na kunipeleka moja kwa upande wa ndani walipokuwa wachungaji sambamba na baba Rose na watu kadha wa kadha ambao wote walinipokea kwa macho ya huzuni na kunisikitikia. Nilifichwa kwa kilichotokea mapema kwa kuwa nilikuwa hospitali kama alivyokuwa Rose ambaye kwa wakati huo sikujua maendeleo yake zaidi ya fahamu kunihama pindi nilipoiona picha kubwa ya mama ikiwa meza kuu sambamba na daftali la rambirambi. Aaaaaah! mama! Mama ! mamaaa yangu kumbe pumzi zake zilikatika siku ileile ya tukio. Alipoanguka hata kukimbizwa hospitali tayari alikuwa mfu. Alikufa kwa taharuki na kushuka presha kwa sababu ya ndoa yangu! ooooh Ndoa yanguuuuu aaaaah! Atuganileeeeee! choziii languuu litalipwaaaaaa