Ndege inayotumia nguvu za jua yazinduliwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
solar-impulse-2-first-sunbath-tilt-shift-620x308.jpg

Ndege inayotumia nguvu ya jua (Solar Impulse 2) kabla ya kuanza kuruka
Ndege inayotumia nguvu za jua yazinduliwa

HISTORIA ya urushaji wa ndege inayotumia nguvu ya jua kwa kuzunguka Dunia imeandikwa.Anaandika Benedict Kimbache kwa msaada wa mashirika ya Habari.

Ndege hii iliyopewa jina Solar Impulse-2 (SI2) ilianza safari yake terehe 8 Machi huko Abu Dhabi ikielekea mashariki mwa Muscat huko Oman kama kituo chake cha kwanza, umbali wa kilometa 400, na kwa umbali huu imetumia saa 12.

Leo ni siku ya 15 tangu ianze safari yake, na ipo mji wa Mandalay huko Burma kama kituo chake cha nne. SI2 inatarajiwa kuanza mruko wake wa tano kuelekea Chongqing huko China umbali wa kilomita 1375 na itatumia saa 20, umbali huu unafanana na umbali kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba (km1394), umbali ambao basi linaweza kutumia kati ya saa 18.5 mpaka 20.

Ndege hii ya aina yake yenye uwezo wa kuruka usiku na mchana bila ya kujazwa mafuta yenye mwendo kasi wa kilomita 87-90 kwa saa (kasi ya Boeing 747 ni km 988 kwa saa). Kasi hii inaweza kupunguzwa na rubani ili kupunguza matumizi ya nguvu zilizohifadhiwa kwenye betri hasa wakati wa usiku.


Marubani wa SI2: Bertrand Piccard na Andre Borschberg

SI2 itaruka jumla ya kilomita 35,000 kwa kutua vituo 12 ikizunguka Dunia na mzunguko mzima utachukua miezi 5, hata hivyo siku ambazo ndege hiyo itakuwa angani ni sawa na siku 25. Kasi ya SI2 inaweza kupunguzwa na rubani ili kupunguza matumizi ya nguvu zilizohifadhiwa kwenye betri.

Mradi huu wa Solar Impulse ni wazo lililozaliwa Uswisi na unaofanywa na Waswisi ukiongozwa na Bertrand Piccard mwenye wazo la awali, aliyewahi kuzunguka Dunia kwa kutumia ‘baluni’ bila ya kusimama na mwenzake Andre Borschberg. Mradi huu una lengo la kuweza kutumia ndege inayorushwa kwa kutumia nguvu ya jua kuzunguka Dunia.

Mradi huu ulianza Novemba 2003 baada ya upembuzi yakinifu. Mwaka 2009 wahandisi 50 na mafundi waliobobea katika nyanja tofauti kutoka nchi sita wakisaidiwa na washauri na wadau wa teknolojia wapatao 80 walianza rasmi utengenezaji wa SI1 iliyokuja kuboreshwa na kupatikana SI2.

Kwa sasa timu nzima inayoshughulika na safari ya SI2 kuzunguka Dunia ina watu 90, ikijumuisha mahandisi 30, mafundi nchundo 25, waongozaji 22. Timu nzima inafadhiliwa kifedha na kiteknolojia na zaidi ya taasisi 100.

Lengo la mradi huu ni mkakati wa kuitangazia Dunia juu ya umuhimu wa kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kutumia nishati ya jua, ni lengo la mradi huu kuonyesha kuwa nishati mbadala na teknolojia vinaweza kukamilisha kile kinachoonekana hakiwezekani.

Utekelezaji wa mradi huu ni pamoja na kukamilisha safari ya kwanza kwa kuizunguka Dunia mwaka huu 2015 baada ya miaka 12 ya utafiti, majaribio na uboreshaji wa mfumo wa ndege hiyo isiyotumia mafuta bali nguvu ya jua, kama nishati mbadala ya miaka ijayo na hii itathibitisha kuwa ubunifu na moyo wa uveterani katika ugunduzi wa teknolojia inaweza kubadilisha Dunia.

Wakati wa mzunguko huo ndege itakuwa inatua kwenye maabara na nchi mbalimbali, kufanya kampeni ya matumizi ya nishati ya jua kama nishati rafiki kwa mazingira.

“Tutafanya mazungumzo na wanafunzi wa vyuo vikuu, wanasiasa, vyombo vya habari nakadhalika ili kuwaeleza umuhimu wa nishati hii mbadala, nishati inayoweza kutumika katika nyanja nyingi kama vile matumizi viwandani, matumizi kwenye ujenzi ili kuweza kuwa na Dunia safi”, marubani hao walisema wakati ndege hiyo inajiandaa kuruka kwa mara ya kwanza.

Dondoo:Solar Impulse-2

  • Idadi ya watu: 1
  • Urefu wake: mita 22.4
  • Urefu wa mabawa yake:mita 71.9
  • Kimo: mita 6.37
  • ‘Selijua’ kwenye mbawa:17,248
  • Uzito wake: Kilo 2,300
  • Chumba cha Injini: mota 4, betri 4
  • Kipenyo cha Pangaboi:mita 4
  • Kasi ya kurukia: 35 km/saa
  • Mwendo Kasi wa juu:140 km/saa
  • Kasi ya kawaida: 90 km/saa
  • Umbali wa kuruka : mita 8,500-12,000
Ndege hii inayobeba mtu mmoja tu (sehemu ya rubani) itaendeshwa na marubani wawili wa kiswiswi Andre Borschbergaliyeanza safari kwa mara ya kwanza na atapokezana na rubaniBertrand Piccard.

Akizungumza na waandishi wa habari changamoto ya kukatisha bahari za Pasifiki na Atlantiki Piccard alisema “Tunapaswa kutumia siku 5 bila ya kutua, safari ya usiku na mchana na hii ndiyo changamoto yetu kubwa”.

Hii inawezekana kwani SI2 imeboreshwa na betri zake zina uwezo wa kutunza nguvu za kutosha kuiwezesha kuruka kwa saa 120 usiku na mchana muda utakaotosheleza kuweza kukatiza bahari za Pasifiki na Atlantiki, tofauti na Solar Impulse-1 iliyokuwa na uwezo wa kuruka kwa saa 26 bila kutua.

Changamoto nyingine watakayokutana nayo marubani hao ni kujitahidi muda mwingi kuwa macho wakiwa angani. Wanaruhusiwa kusinzia si zaidi ya dakika 20. Pia watakabiliwa na kukaa kwenye eneo dogo la rubani lenye ukubwa wa mita za ujazo 3.8, eneo hili linafananishwa kuwa kubwa kidogo na eneo la dereva kwa gari ndogo.

Ndani ya chumba hiki kuna mfumo wa kuleta uhai, chakula maalumu kilichoandaliwa na wanasayansi wa lishe wa Nestlé Health Science, mfumo wa kuleta hewa ya Oksijeni, pamoja na kiti cha rubani kinachoweza kukunjwa na kukunjuliwa kwa matumizi ya rubani na kama kitanda, pia kuna kiti cha kawaida na choo.

Muundo wa Solar Impulse-2

Muundo wa ndege hii ni tofauti sana na ndege za kawaida. Solar Impulse-2 (SI2) ni maboresho ya Solar Impulse -1.

Mbawa za SI2 zina urefu wa mita 72 (karibu sawa na upana wa uwanja wa mpira wa miguu). Urefu huu ni zaidi ya urefu wa mbawa za Boeing 747 zenye urefu wa mita 64.

Ndege hii ina uzito mdogo wa tani 2.3 sawa na uzito wa gari ndogo na uzito huu umebuniwa makusudi ili kuongeza ufanisi wake. Kwenye mbawa zake ina zaidi ya seli jua 17,000 (Solar cells) zinazo chaji betri ili kutunza nguvu inayoendesha ndege hiyo hasa wakati wa usiku, ambapo kunakuwa hamna jua.

Seli Jua zinachaji betri zenye uzito wa kilo 633 na uzito huu unachukua karibu robo ya uzito wa SI2.

Inafikiriwa kuwa itakapofika mwaka 2050, matumizi ya nguvu ya jua yatakuwa yamechukua nafasi kubwa duniani kuliko aina nyingine ya nishati.

Uwezekano wa nishati ya jua kutumika zaidi unathibitishwa na kushuka kwa gharama za sahani za seli jua (solar electric panel) kwa asilimia 70 kwa miaka ya hivi karibuni na gharama hizi zinatarajiwa kushuka zaidi kwa nusu ya gharama ya sasa.


Ramani inayoonesha vituo inapotua ndege hiyo

Huko Uingereza nishati ya jua inashindana na kukaribia kuipiku nishati ya upepo na inatarajiwa kuipita nishati ya gesi baada ya muda si mrefu. Huko Marekani ajira kwenye sekta ya nishati ya jua zimeongezeka na kupiku ajira za nishati ya mkaa.

Sekta hii imeshamiri nchi za Ulaya baada ya serikali kutoa ruzuku kwa taasisi zilizoamua kuwekeza kwa kuwa na ubunifu na hivyo kutengeneza soko kubwa linalowindwa na wachina.

Kuhusu warushaji wa ndege hiyo

Mradi huu ni wazo la Bertrand Piccard na Borschberg Andre ni mshiriki wa mradi.

Bertrand Piccard, ni mwanzilishi na mwenyekiti wa SI2 na anajulikana sana kwa uzoefu wake wa kusafiri kwa kutumia puto. Mwaka 1999 akiwa na mwenzake Brian Jones walizunguka Dunia kwa kutumia puto.

Kitaaluma Bertrand ana taaluma nyingi: ni daktari wa binadamu na amebobea kwenye afya ya akili; ni mtembezi mtafiti/mgunduzi na mwanaanga (aeronaut).

Sifa hizi za Bertrand ni urithi, kwani familia yao ina historia kwa kuwa na wanasayansi waliofanya mambo ya kishujaa na hivyo kuvunja rekodi. Marehemu baba yake Jacques Piccard, mhandisi na mwanasayansi wa mambo ya bahari alikuwa mtu wa kwanza kufika kwenye kina kirefu cha bahari cha Mariana mwaka 1960.

Babu yake (marehemu) Bertrand Auguste Piccard aliwahi kuvunja rekodi kwa kuruka na baluni kwa urefu zaidi mnamo mwaka 1931. Bertrand alikuwa wa kwanza kuwa na wazo la mradi huu kwa kutumia vyanzo vyake mwenyewe vya fedha na baadaye akaungwa mkono na Borschberg kama mshiriki mwenzake.

Borschberg Andre aliyesoma Massachusetts Institute of Technology (MIT) chuo kilichopo kwenye orodha ya vyuo 10 bora duniani 2014-2015. Borschberg ni Mkurugenzi (CEO) wa SI2 na kitaaluma ni mhandisi kitaaluma na aliwahi kuwa rubani wa ndege za jeshi, na mwenye utaalamu wa kurusha ndege na helikopta baadaye akawa mjasiliamali aliyejikita kwenye teknolojia ya intaneti.

Mwaka 2010 alifanya mzunguko wa kwanza kwa kutumia ndege inayotumia nguvu ya jua (SI1 pia inaitwa SIA) kwa muda wa masaa 24. Mzunguko huu uliweka rekodi ya ndege inayotumia nguvu za jua inayoendeshwa na binadamu kuruka kimo kirefu zaidi. chanzo.Ndege inayotumia nguvu za jua yazinduliwa
 

Attachments

  • Marubani wa SI2 Bertrand Piccard na Andre Borschberg.jpg
    Marubani wa SI2 Bertrand Piccard na Andre Borschberg.jpg
    6.6 KB · Views: 70
  • Ndege inayotumia nguvu ya jua (Solar Impulse 2) kabla ya kuanza kuruka.jpg
    Ndege inayotumia nguvu ya jua (Solar Impulse 2) kabla ya kuanza kuruka.jpg
    17.4 KB · Views: 74
  • Ramani inayoonesha vituo inapotua ndege hiyo.gif
    Ramani inayoonesha vituo inapotua ndege hiyo.gif
    11.2 KB · Views: 62
Back
Top Bottom