Nataka Kumuona Mwanangu!

Mentor

JF-Expert Member
Oct 14, 2008
20,328
23,879
Waliona walivyokuwa wakipendana
Wakawakubalia kuwa pamoja mwishoni
Wakafunga ndoa kubwa
Ilikuwa nderemo na vifijo, vibwebwe na vigoma
Wakapata watoto
Na wakaishi kwa furaha maisha yao yote.​
Ilikuwa ndoto yangu. Ndoto ya miaka mingi ijayo.

1998, Tanga Technical

Mwaka 1997 nilimaliza elimu ya msingi huko Moshi mkoani Kilimanjaro katika shule ya msingi Rau. Maisha ya shule ya msingi yalikuwa bora liende. Kama wazazi wako hawakuwa makini na elimu yako ilikuwa ni rahisi sana wewe kupotea. Kwa sehemu ya kwanza ya elimu yangu ya msingi, wazazi hawakuwa wakifuatilia sana maendeleo yangu shuleni.

Kazi yangu ilikuwa kutoroka shule na kwenda kula maembe na maparachichi mtaani. Kuna siku tulitoroka shule tukatembea hadi kufika Uru kijijini huko. Utoto raha sana, maana hata hatukuwa tukiogopa kupotea na hakuna kati yetu aliyekuwa akijua tunaenda wapi.

Kuanzia muhula wa pili wa darasa la sita hivi, nashukuru Mungu wazazi wangu waligutuka usingizi na kuanza kufuatilia maendeleo yangu shuleni. Yalikuwa ni mabadiliko ya ghafla na niliyaona kama ukoloni. Niseme tu kwa sasa kuwa nawashukuru sana wazazi wangu kwa kunifuatilia kipindi kile maana nisingekuwa hapa nilipo isingekuwa wao kufanya vile.

Wazazi walihakikisha kuwa wanafuatilia kama nimeenda shule na kurudi kwa wakati na kuhakikisha ninasoma ninaporudi nyumbani. Kwa muda huo mfupi wa mabadiliko yangu, nilitoka kuwa mwanafunzi anayesindikiza wenzake shuleni na hadi wakati ninafanya mitihani yangu ya kumaliza elimu ya msingi, kuwa mmoja wa waliopangiwa Tanga Technical School, shule ya kwanza ya serikali Tanzania!

Wengi hawakuamini kama Mentor ningefaulu darasa la saba. Hata leo nikikutana na watu waliokuwa wakinifahamu enzi hizo za utundu wangu shule ya msingi, hawaamini nikiwaambia kuwa sasa mimi ni daktari.

1998 Tanga Technical School, Tanga
Nilijisikia fahari kupangiwa shule hiyo maana shule tu yenyewe ilikuwa na historia yake ya pekee. Niliapa kubadilika kabisa na kuwa mwanafunzi bora katika masomo yangu. Sikuwahi kuwa mwanafunzi wa kwanza darasani tangu nianze shule, lakini hilo halikuwa lengo langu. Nilitaka kufanya kadri ya uwezo wangu ili nitakapojipima mwenyewe nisione mahali nilipozembea. Nafasi za darasani hazikuwa na umuhimu sana kwangu.

Niliianza safari yangu ya elimu mkoani Tanga chini ya mwalimu mkuu mtata hajawahi kutokea, Bwana Tetty! Kama sio kupitia chini ya mkono wa mkuu huyu wa shule sidhani pia kama ningetoka hivi nilivyo. Alijua kusimamia nidhamu ya shule maana shule ilikuwa kama nusu kijiji, tulikuwa wanafunzi wengi kutoka sehemu zote za nchi.

Pamoja na hekaheka za shule lakini pia joto la balehe lilitukumba pamoja na umri wangu mdogo wa miaka 15. Naam, nilimuona binti. Nikiwa kidato cha kwanza nilikuwa napenda kuongea labda na kuigiza kiasi. Enzi hizo kwenye ngonjera, jiving na maigizo hunikosi kabisa. Nilikuwa na umbo dogo dogo ila nilifit kwenye nafasi nyingi sana. Ilikuwa kwenye mdahalo na shule ya jirani ya Usagara. Ndiyo niikuwa kidato cha kwanza bado ingawa ndiyo tulikuwa tukimalizia miezi ya mwisho.

Mentor: “I acknowledge your presence Mr. Chairman the converner of this discourse, judges, timekeeper, proposer, my fellow opposers, and the crowd at large...

Sikumbuki tulikuwa tunalumbana kuhusu hoja gani lakini wakati huo nikishuka ngeli ambayo nilikuwa nimekremu maneno magumu magumu nilimuona binti; mdogo mdogo kama mimi. Alikuwa amekaa nyuma kabisa ya ukumbi akisikiliza. Alinivutia na kunifanya kusahau mengi ya niliyopanga kuyasema.

Sikuwahi kuhisi vile nilivyohisi juu yake. Nilihisi mdomo ukipata kigugumizi cha ghafla. Nilijitahidi na kumaliza mada zangu na kwenda kuketi chini huku watu wakipiga makofi kwa sentensi yangu (punchline) ambayo nilikuwa nikipenda kuitumia ninapomalizia hoja zangu.

Akili yangu haikuwa ikiwaza tena mdahalo ule bali yule binti niliyemuona. Nilivumilia kutulia hadi mdahalo ulipoisha ndipo nilipopata fursa ya kuanza kumtafuta tena. Oh, sikumuona. Moyo wangu uliumia kama vile alikuwa ameniahidi angekuwepo pale akinisubiria. Nilitoka nje bila kujali kusalimiana na watu wengine lengo langu kujaribu kuona ni wapi binti yule ameelekea.

Alhamdulilahi, sikupata shida sana kumuona kwa mbali ila changamoto ikaja jinsi ya kumfuata. Unaanzaje kumfuata binti wa watu na hata humjui, ukiacha hata ambaco ningetaka kumuambia, tena shule tofauti na yangu na ambavyo wavulana wa Usagara walivyokuwa hawatupendi.

Dogo uko vizuriii!” Nilisikia sauti nyuma yangu na ghafla mtu akinishika bega. Nilitamani aniache ili niendelee kumfuata yule binti. Alikuwa ni mmoja wa wazungumzaji kutokea hapo Usagara. Richard baadaye nilikuja kumfahamu, yeye alikuwa kidato cha tatu. Nilizuga kumwitikia na maongezi yake lakini akili yangu yote ilikuwa inamfuatilia yule binti. Kwa wakati ule alikuwa amekaa tu na wenzake.

Uzalendo ulinishinda ikabidi nimwambie tu, “kaka Rich yule msichana ni mzuri.” Aliishia kucheka na kuniambia kuwa huyo binti ni njuka tu hata hamfahamu. Kunimaliza kabisa akamuita. Sikuwa nimejiandaa kusema lolote. Hata alipofika nilikuwa kama samaki mwenye mengi ya kusema ila mdomoni nina maji. Ila Rich alifanya ya kutosha maana alimuuliza majina yake na kuhakikisha kuwa kweli yuko kidato cha kwanza. Alikuwa na sura ya upole na alipokuja karibu yetu niliuona uzuri wake zaidi.

Nifupishe kwa kusema tu siku ile sikuweza kuzungumza hata neno moja pamoja na umahiri wangu kwenye midahalo pale kwa huyu binti nilikuwa kama bubu. Lakini kwa kuwa sasa nilikuwa nikifahamu jina lake niliporudi shuleni nilimuandikia barua na kumpa Rich. Kwangu mimi ni barua ya muhimu kuliko zote nilizowahi kuandika mpaka sasa.

Nilimuandikia barua fupi tu kumueleza kuwa nilivutiwa na upole wake na ningependa awe rafiki yangu tuandikiane barua (enzi hizo tuliita 'pen pal'). Nilifurahi siku chache baadaye kupokea majibu yake kuwa amekubali na alinitania eti nisiwe namuandikia kiingereza kama kile nilichokuwa nikiongea kwenye mdahalo.

Wenzetu wa Usagara walikuwa huru sana kutoka maana hostel zao zilikuwa nje. Hivyo ilikuwa rahisi kwa Rich kuja kuniletea barua na mimi kumuomba apite siku fulani nimpe majibu. Sisi ulikuwa ukitoroka na Tetty akakukamata adhabu yako ni kwenda kufagia manispaa.

Kirahisi hivyo ndivyo urafiki wetu ulivyoanza; barua zenye maneno ya kutiana moyo kusoma. Tulifahamiana zaidi huku nikiogopa kumtamkia yale maneno pendwa lakini haikuathiri urafiki wetu. Baadaye tukiwa kidato cha pili nilianza na mimi kutoroka na kwenda kuonana naye.

Tulikuwa tunapenda kwenda Raskazone hasa siku za mwisho wa wiki. Na ni katika kipindi hicho nilimtamkia kuwa nampenda. Sikuwa nafahamu hasa maana ya maneno yale ila nakumbuka vyema siku hiyo, nilijisikia vizuri, amani, furaha, hasa aliposema kuwa ananipenda pia. Sasa rasmi alikuwa ‘girlfriend’ wangu.

Nilikuwa najihisi natembea angani. Alikuwa anazidi kupendeza siku hadi siku. Vijana wa Usagara walikuwa wakimmezea mate. Nilishukuru sana kumfahamu kaka Rich kipindi kile maana alisaidia kuwatisha baadhi ya vijana waliotaka kunifanyia vurugu.
Kwa miaka mitatu tuliyokuwa wote pale Tanga, maisha yalikuwa kama mbingu duniani.

Tulimaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri sawa sawa na michepuo tuliyotaka kusomea. Kila mmoja alipangiwa shule tofauti, mimi nikienda Same Sekondari na yeye akienda Weruweru. Maisha niliyaona magumu maana sikuwa nimezoea kuwa mbali naye. Kwangu mimi kupangiwa Same kulikuwa na sawa na yeye alivyokuwa Usagara maana tulikuwa huru kuliko uhuru wenyewe.

Kutokana na kuwa na uhaba wa walimu tulikuwa tunapachukulia Same kama kituo cha mitihani. Kwa bahati nzuri sare zetu zilikuwa zikifanana na za shule za sekondari ya Moshi, hivyo wakati mwingi tulikuwa tukienda huko na kuhudhuria vipini vyao. Walimu hawakugundua hili lakini lilitusaidia sana kusogeza siku na elmu ilipatikana. Wakati wa mtihani ndio tulirudi shuleni kwetu kufanya mitihani.

Njia pekee ya kuwasiliana naye ilikuwa kutuma barua. Kwa minajili ya kutofichua siri za kambi, niseme tu nilifanikiwa kufanya fitna zilizoturuhusu kuwa ninapeleka barua moja kwa moja shuleni kwao. Nilikuwa nikimpelekea baadhi ya mahitaji pia na mimi barua zangu zilikuwa zikijibiwa kwa muda. Hicho ndicho kilichoniwezesha kusogeza siku.

Hadi tunamaliza kidato cha sita, maisha yetu yalikuwa murua bila shida na misukosuko yoyote. Kila mtu alirudi nyumbani kwao na kusubiria kwenda chuo, yeye kwao Tanga na mimi Moshi. Wakati huu barua hazikutosha kukidhi hitaji letu la kuonana na kuwa karibu. Tulitamani kuonana tena uso kwa uso.

2004
Nilipanga kuwa nitaenda kukaa kwa mama yangu mdogo huko Tanga na nilishaomba ruhusa kwa wazazi. Kwa bahati mbaya siku mbili kabla ya mimi kuondoka mama yangu alikuta barua kwenye moja ya vitabu vyangu nilivyoviacha sebuleni. Aliisoma na kunisubiria jioni akaanza kunipa somo. Aliniuliza sana kuhusu huyu binti na mimi bila kujua - kwa kudhani mama ana hamu tu ya kumjua - nikaanza kufunguka. Nilimueleza yote kuhusu rafiki yangu huyu.

Sikutegemea kama maneno yale yangeweza kutoka mdomoni mwa mama yangu. Sikujua kuwa pamoja na kusoma kote lakini bado watu wanaweza kuwa na ukabila namna ile. Maana katika yote aliyoniambia hasa lilikuwa kwa kuwa binti ni mtu wa Tanga, wasichana wote wa ukanda huo wa Pwani si wazuri, hawana maadili na wanafundishwa kutokuwa na mwanaume mmoja (mambo ya mafiga matatu wakati huo yalikuwa yanasikika sana).

Alinionya na kunikataza hataki kabisa kusikia habari za huyo binti na kwa mantiki hiyo safari yangu ikafa. Ilikuwa ni miezi ya kuishi kwa shida, nilikonda. Tuliendelea kuwasiliana kwa barua maana kipindi hicho sikuwa na uwezo wa kununua ‘mobiteli’.

Mungu si Athumani, wakati mimi ninapangiwa Muhimbili na yeye alipangiwa chuo kikuu cha Ardhi. Tulifurahi sana maana tungekuwa karibu tena. Mama yangu alitamani anihamishe chuo maana alijua bado ninaendelea kuwasiliana na rafiki yangu huyu. Alisema maneno makali na magumu siwezi kuyaandika humu lakini niliyapuuzia. Sikuweza hata kumueleza rafiki yangu huyu. Alimueleza hadi baba yangu juu ya huyo binti na kwa pamoja wakawa kila siku wananipa somo juu ya wadada wa Tanga na mifano juu. Sikutaka kusikia, nilikuwa nimekufa na kuzikwa kwake.

Wazazi wangu walionesha kwa vitendo hata kwake kuwa hawamtaki. Nakumbuka mara kadhaa ambazo ilitokea wazazi wangu wamekuja Dar kwa kazi zao waligoma kuonana na mimi kama ningeenda na rafiki yangu huyu. Kuna wakati mmoja niligoma kwenda kuwaona kama wangekataa nisiende naye. Walikubali ila muda wote wa chakula hakuna aliyekuwa akimuongelesha mwenzake. Baada ya kula wakalipa vyakula vyote isipokuwa cha kwake. Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa hadi baadaye sana.

2009-2010
Nikiwa namalizia masomo yangu ya udaktari mwenzangu alikuwa ameanza kazi mjini tayari. Changamoto ziliongezeka kutoka kuwa wazazi wangu hawampendi hadi kwa vijana wa mjini. Kuanzia shuleni hadi kazini alikuwa akitongozwa. Sina nia ya kumsifia alimvyo mzuri wa nje, lakini alikuwa mzuri. Ukimuangalia mara moja ni lazima utatamani kumuangalia tena. Nakiri kuwa sikuwa mtu wa wivu na hilo la uzuri wake nilikwishalifahamu.

Nikiwa chuo, mara nyingi wadada walikuwa wakitamani kuwa na mimi lakini kwa ule upendo uliokuwepo katikati yetu sikuwapa hata nafasi ya kuwafikiria. Kwa upande wake hali ilikuwa vivyohivyo. Hatukuona kitu cha kututenganisha.

Kwangu mimi sikuwa nikimuonea wivu lakini mwenzangu alikuwa na wivu sana juu yangu. Mimi nilimuamini kuwa anaweza kusema hapana na nilitegemea kuwa angefanya hivyo kwangu. Mimi si muongeaji sana lakini pia si mkimya kivile. Hakuwa akipenda akinikuta naongea na wanafunzi wenzangu, wa kike. Nilimthibitishia kuwa hakuna lolote kati yangu nao.

Hakuonekana kuamini sana hili. Siku moja niligundua mawasiliano kati yake na kijana mwingine. Nilimuuliza kikawaida kabisa na akaniambia hakuna chochote cha maana bali zile jumbe za kufowadiana kwa njia ya sms (enzi hizo zilikuwa zimeshamiri sana). Nilipotezea na kuamini anachoniambia.

Alikata mawasiliano na huyo kijana na tuliendelea na mahusiano yetu. Tulikuwa wa mfano maana wote waliotufahamu tangu tupo kidato cha kwanza waliwahadithia wengine jinsi ambavyo tumependana muda mrefu bila kuwa na tatizo lolote. Wengi hawakujua hilo la wazazi. Miezi michache baadaye, rafiki yangu huyu alipata ujauzito. Nilifurahi sana. Najua halikuwa lengo letu hata kidogo lakini moyoni nilifurahi maana nilijua hatimaye wazazi wangu itabidi wamkubali.

Ni kweli, tulitamani kuingia kwenye ndoa kabla ya kupata watoto na tulishapanga nitakapomaliza mafunzo yangu kwa vitendo (internship) basi tutafunga ndoa na kuishi maisha ya furaha pamoja. Taarifa hii iliwaumiza sana wazazi wangu na kwa miezi kama sita ya mwanzo hawakunisemesha kabisa. Ila baadaye walibadilika kidogo na kuanza kupiga simu wakiulizia hali ya mama. Hawakuwa wakiongea sana lakini kwangu ilikuwa ni dalili njema.

Kutokana na hali hiyo, ilibidi binti ahamie kwangu, tukaanza kuishi pamoja. Ilikuwa furaha sana kwangu kuwa hatimaye ndoto ya kuishi naye inaelekea kutimia. Alizaliwa binti mzuri kama mama yake. Kwa kweli kwa huyu mtoto labda rangi ya ngozi tu ndo alichukua kwangu vinginevyo vitu vingine vyote alichukua kwa mama yake. Nililikuwa na furaha sana, hasa kuitwa baba.

Shida ya kupita njia za mkato kwenye maisha ni kuwa, tofauti na njia za mkato halisi, za maisha huwa ni ndefu. Hapo awali tulipanga nitakapomaliza 'internship' tutafunga ndoa maana tulikuwa tumeshaanza kuhifadhi fedha kwa ajili ya shughuli hiyo. Lakini fedha zote zilitumika kulea mtoto ambaye hatukuwa tumemuweka kwenye mipango yetu.

Kulea ni raha, hasa unapoitwa baba, lakini ni kazi kwenye majukumu. Hasa kwangu maana nilipomalizia tu mafunzo yangu kwa vitendo nilipata fursa ya kusomea shahada ya uzamili ya magonjwa ya ndani (internal medicine). Hivyo ilikuwa kubalance kati ya baba, kazi na shule. Kutokana na hili, njia yetu ya mkato pia ilizidi kuwa ndefu.

Tulisongeza tena mipango yetu mbele kuwa nitakapomaliza tu shule, tutakuwa tumeshajipanga tena upya tufunge ndoa tuishi kihalali. Lakini katika yote haya, nilikuwa na furaha - natamani niseme tulikuwa na furaha. Hatukugombana kwa lolote, tulilea mtoto wetu vizuri na tuliweza ku-balance kazi yake na kulea na mimi. Ni muda mfupi tu ulibaki kuvumilia turudi njia kuu.

04/23/2014 Siku ya Jumatano
Ni siku iliyobadilisha uelekeo wa maisha yangu kabisa. Siku iliyofuta ndoto yangu nzuri niliyokuwa nayo tangu utoto.

Siku hii nilitoka kazini/shule mapema na kurudi nyumbani. Kipindi hiki tulikuwa na dada wa kazi ambaye alikuwa akija asubuhi na kuondoka jioni hivyo baada ya mimi kuwasili dada aliniachia mtoto na kuondoka. Sasa mtoto alikuwa anajua kuongea kabisa. Nilijisikia furaha kama baba maana ninakumbuka hatua zote za ukuaji wake tangu anazaliwa, akiota jino la kwanza na hata siku aliyoanza kutembea.

Siku ya kwanza kutamka ‘mama’ ni mimi nilikuwa nimembeba. Nilikaa nikicheza naye pale na kukumbuka ambavyo wazazi wangu walikuwa hawapendi niwe na mama yake. Nikajiuliza ningekuwa nimewasikiliza huyu malaika mzuri hivi angepatikana kweli hata kama kapatikana nje ya mipango yetu, lakini ni wangu, ni damu yangu.

Nilielekea jikoni ambapo nilikuta dada alikwisha pika wali hivyo nikaingia kazini kuunga mboga. Nakumbuka vyema siku ile niliunga maharage. Ninapenda kupika na huwa sifanyi masikhara linapokuja suala la maakuli. Nilimweka mtoto pembeni nikaanza kukuna nazi na kukarangiza maharage yangu ambayo tulikuwa tumeshayachemsha tangu Jumapili ili kurahisisha kazi kwa siku za wiki. Nilikuwa ndiyo nimeweka mboga za majani jikoni wakati mama yake aliporudi kutoka kazini kachoka na foleni za jiji hili. Jioni ilienda haraka na ghafla ulikuwa muda wa kwenda kulala.

Kwa kuwa sikuwa na mambo mengi ya kufanya mimi ndiyo nilikuwa na mtoto siku ile. Nilikuwa naye kitandani huku nikimsomea hadithi na kumsubiria alale. Bado alikuwa akilala nasi chumba kimoja ingawa kwa wakati huu alikuwa na kitanda chake kidogo pembeni yetu. Mama yake alikuwa bize na simu ila sikuitilia maanani maana nilijua alikuwa akiwasiliana na wenzake tu. Baada ya muda alipitiwa na usingizi na kulala. Sikuwa nimechoka sana siku hiyo maana hata baaada ya mtoto kulala nilirudi kitandani kwetu na kuendelea kumalizia kusoma hadithi niliyokuwa nikimsomea binti yetu.

Ni wakati huu ambapo ujumbe uliingia kwenye simu ya mke wangu. Alikuwa amesinzia kabisa na kupotelea usingizini. Sikuweza kuusoma ujumbe lakini kwa nilipokuwa niliweza kuiona ile namba. Hapo ndipo nilipogundua akili ya binadamu ina akili sana maana kumbukumbu zangu ziliniambia ile namba si ngeni machoni pangu, niliikumbuka vyema.

Natamani nisingefanya vile, lakini niliichukua simu na kusoma ujumbe ule, ujumbe mfupi wa maneno, maneno mazito, “NATAKA KUMUONA MWANANGU!

LEO 04/23/2017
Sikumbuki kwa uwazi usiku ule uliendaje ila kwa muda mrefu niliumia. Niliumia kuwa pamoja na kufahamu mtoto hakuwa wangu, nikifikiria kumuacha na kuondoka kuliniuma zaidi. Sasa nimeshapona majeraha yale ingawa leo nimekumbuka ndoto niliyokuwa nayo zamani.

Waliona walivyokuwa wakipendana
Wakawakubalia kuwa pamoja mwishoni
Wakafunga ndoa kubwa
Ilikuwa nderemo na vifijo, vibwebwe na vigoma
Wakapata watoto
Na wakaishi kwa furaha maisha yao yote.
BADO NINAAMINI.
Wasalaam wapendwa,
mentor.
 
Is this real?!!!

Yaan nimeishiwa nguvu..please endelea utuambie ilikuaje baada ya wewe kusoma huo ujumbe?!.

Na ikawaje ukaachana na Huyo dada?

Vpi wazazi wako walilichukuliaje hilo?
 
Apart from being a Doctor, mkuu unaweza kuwa mwandishi mzuri sana wa story za movie au vitabu.
Anyway,pole sana mkuu.ila mwishoni huku sijakuelewa vzr,nahisi kama story inaendelea part two..
Na wewe mkuu, apart from being black unaweza kufaa sana kwenye matangazo ya dawa za mswaki. [HASHTAG]#joke[/HASHTAG]

Nashukuru mkuu hapo mwishoni nimekuachia msomaji nawe umalizie...mengine nikiandika nitatonesha vidonda mkuu.
 
Back
Top Bottom