CCJ yamuumbua Nape
• Alitumika kuandaa katiba, kupokea fedha, kutafuta ofisi ya CCJ
SIRI za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, zinazomhusisha na mipango ya kuwahi kukigeuka chama chake na kuanza taratibu za kujiunga na Chama Cha Jamii (CCJ), zimezidi kuanikwa na wale aliokuwa nao katika mipango hiyo.
Baada ya wanasheria na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari, kumtaja Nape kuwa mmoja wa wana CCM wanafiki, jana ilikuwa ni zamu ya Fred Mpendazoe kueleza kile alichokiita "unafiki, usaliti na uhaini wa Nape Nnauye ndani ya CCM anayojifanya kuipigania."
Mpendazoe aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kishapu kwa tiketi ya CCM katika Bunge lililopita, alijitoa mapema mwaka jana na kujiunga na CCJ kabla ya kuhamia CHADEMA.
Akihutubia mamia ya wakazi wa mji wa Mbamba Bay katika mfululizo wa maandamano na mikutano ya hadhara ya CHADEMA inayoendelea kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mpendazoe alisema sasa ameamua kuliambia taifa ukweli kuhusu Nape Nnauye ili umma wa Watanzania uepuke kudanganywa na propaganda za CCM zinazotolewa na kijana huyo.
Huku akiweka wazi kuwa yeye ni mmoja wa waanzilishi wa CCJ, Mpendazoe alisema kelele zote anazopiga Nape kuitetea CCM leo hii ni za kinafiki kwani tayari alishakiona chama hicho hakifai na akashiriki katika mipango yote ya kuanzisha CCJ.
Akitoa mfano wa jinsi Nape alivyoshiriki katika kuanzisha CCJ, Mpendazoe alisema kijana huyo alishiriki kuandika katiba ya chama hicho.
Alisema ndiye aliyepewa jukumu la kutafuta nakala za katiba za vyama vingine tawala nchini Afrika, ili kupata katiba nzuri ya kuigwa katika kuandika Katiba ya CCJ.
Aliwaambia wakazi wa Mbamba Bay kuwa Nape alilitekeleza vizuri jukumu hilo, kwani alifanikiwa kuipata Katiba ya Chama cha ANC kinachotawala Afrika Kusini, ambayo alisema ndiyo iliyotumika kwa kiasi kikubwa katika kuandika Katiba ya CCJ.
"Huyu Nape anayepiga kelele za kuitetea CCM kujivua gamba ni mnafiki mkubwa pengine kuliko wanafiki wote hivi sasa. Nathibitisha kwa wananchi wa Mbamba Bay na Watanzania wote kwa ujumla kwamba Nape Nnauye alishiriki kuanzisha CCJ. Nilikuwa naye; tulikuwa wana CCM sita. "Nape ni mhaini ndani ya CCM kwa sababu alishakula njama za kutaka kuiangusha, tofauti na Nape, mimi nilijiamini mapema na nilijitoa CCM mapema baada ya kuona hiki chama hakiwafai Watanzania.
Sasa leo wanajivua gamba halafu Nape wanampa cheo. Niwaulize, hivi kati ya Nape na Lowassa yupi ni mbaya na kwa CCM? Ni Nape aliyeona CCM haifai na kushiriki kuanzisha CCJ ili kuiangusha au ni Lowassa?" alihoji Mpendazoe na umati ukajibu "Wote hawafai." Kisha aliendelea:
Tulifanya naye vikao vyote vya siri hadi tukaanzisha CCJ, leo anaitetea CCM, ni mnafiki mkubwa", alisema Mpendazoe na kushangiliwa.
Katika hotuba yake hiyo iliyoonekana kuteka hisia za mamia ya wasikilizaji, Mpendazoe alisema CCJ ilianzishwa kwa siri kubwa na Nape alishiriki kikamilifu katika kuhakikisha mawasiliano yao yote yanakuwa ya siri kwani walifungua mtandao maalumu wa kuwasiliana kwa internet.
Hata hivyo, alisema baadaye wenzake waliufuta mtandao huo baada ya kubadili mawazo dakika za mwisho, hasa baada ya kuahidiwa vyeo na Rais Kikwete.
Alisema hata pale ilipolazimu kukutana, yeye, Nape pamoja na wengine, walikuwa wakipendelea kukutana kwenye vinywaji eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam ili wasitiliwe shaka na maofisa Usalama wa Taifa aliosema walikuwa wakiwapeleleza wana CCM wote waliohisiwa kula njama za kuanzisha chama kipya.
Mpendazoe aliyewahi kuwa msemaji wa CCJ taifa kabla ya chama hicho kunyimwa usajili wa kudumu, alisema Nape alibadili mawazo ya kujiunga CCJ dakika za mwisho baada ya Rais Jakaya Kikwete kumuahidi na hatimaye kumteua kuwa mkuu wa Wilaya ya Masasi. Alibainisha kuwa kitendo hicho kinaonyesha jinsi kijana huyo asivyo na msimamo na alivyo na uchu wa madaraka.
"Lengo letu la pamoja lilikuwa ni kupinga uongozi mbaya wa CCM na ufisadi tukiwa nje ya CCM, maana haiwezekani kupambana na ufisadi ukiwa ndani ya CCM. Ukifanya hivyo unakuwa adui. Lakini kumbe mwenzetu ndani ya moyo wake kilichomsukuma kuanzisha CCJ ni kukosa cheo kikubwa ndani ya CCM.
Sasa hilo sikulijua, nililijua baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi. Hapo alibadili mawazo ya CCJ. Ni kijana msaliti, mnafiki na asiye na msimamo, hafai kuongoza watu, ana uchu wa madaraka … kama si kupewa ukuu wa wilaya Nape asingekuwa CCM leo. "Alikuwa anatazama tu majaliwa ya tumbo lake. Huyu naye ni fisadi lakini hajavuliwa gamba, wanafiki watupu", alisema Mpendazoe na kuamsha shangwe zaidi.
Aidha, alieleza kuwa ili kuwaepuka maofisa Usalama wa Taifa, wakati mwingine walikuwa wakifanya vikao vyao vya kuanzisha CCJ ndani ya gari pamoja na Nape akiwepo.
Alieleza zaidi kuwa Nape akiwa idara ya mambo ya nje ya CCM katika ofisi ndogo ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam, ndiye aliyekuwa akiiba siri za CCM zilizohusu kuwafukuza wote waliohisiwa kuwemo kwenye mpango wa kuanzisha chama kipya cha siasa.
Alieleza kuwa Nape anayemjua yeye ni mtu asiyeukubali uongozi wa Rais Jakaya Kikwete katika chama na serikali, kwani katika vikao vyao vya mwanzoni kabisa walivyoazimia kuanzisha CCJ, kijana huyo alikuwa akimkosoa Kikwete na kuelezea udhaifu wake.
"Na ndiye tuliyekuwa tukimtuma kwa wafadhili kupokea fedha za kuanzishia CCJ. Ndiye aliyetafuta pango la ofisi ya CCJ. Kwa kuwa yeye alikuwa kijana zaidi, alifanya mambo mengi ya kufuatilia kwa siri taratibu za uanzishwaji wa chama.
"Kikwete anaongoza chama feki, CCM ina watu ambao walishamdharau kama Nape na ambao wanamuona ni kiongozi dhaifu…lakini kwa sababu mwenyewe aliwapa vyeo bila kuwajua, leo wamelazimika kubakia ndani. Mimi siwezi na ndiyo maana leo nipo CHADEMA nikiendeleza dhamira ile ile ya kuwanusuru Watanzania na ufisadi," alisema na kushangiliwa tena.
Aliwataka wakazi wa Mbamba Bay kutorudi nyuma na kurubuniwa tena na CCM inayosema imejivua gamba, kwani suala hilo limejaa usanii na unafiki mkubwa. Alisisitiza kuwa kote alikopita na CHADEMA amejiridhisha kuwa chama hicho sasa ndiyo kipenzi na tumaini pekee la Watanzania.
"Mimi sitarudi nyuma kama Nape, nitasonga mbele na CHADEMA, tumekwenda kwenye vijiji na miji mingi, CHADEMA ndiyo tumaini pekee la Watanzania….ndugu zangu tusirudi nyuma, huu ndiyo wakati wa kujikomboa. Kila haki na wakati wake…tusiipoteze fursa hii," alisema. Wakati Mpendazoe akitoa tuhuma hizo juzi, Nape alikaririwa na vyombo vya habari kuwa hajawahi kushiriki katika CCJ huku akiwatuhumu wanaomhusisha nayo wanafanya hivyo kwa lengo la kumchafua.