Majibu ni mepesi sana, sisi waafrika tunaamini katika kukandamizwa, tunaishi kinyonge na kuamini sisi ni wanyonge tusio na haki zozote. Ndio maana watawala wetu wanaamini hivyo na kutufanya hivyo. Suala la Lema ni moja tu kati ya milioni kadhaa ya uonevu wa dhati kabisa tunaofanyiwa na watawala na tunakaa kimya. Mfano, huu msemo wa "kuingia bure kutoka na hela" umetokana na utamaduni uliohalalishwa na Jeshi la polisi pindi wanapokamata watuhumiwa. Pia ni kitu cha kawaida sana kusikia askari akimtishia raia kumweka ndani bila kujali ni kwa kosa gani. Ni wangapi waliobambikwa kesi za ujambazi, wakati ni raia wema kabisa? Wengine kuuawa na polisi kwa visingizio kama hivyo. Rejea kesi ya Zombe na wenzake. Je, ni mara ngapi watawala wameua ama kupiga watu kwa makusudi, kisha waathirika kuonekana ndio wakosaji, mfano kesi ya marehemu Ditopile. Kwa sababu tunaishi kwa mazoea na kuonewa ndio majaliwa yetu, sishangai watu kuanza kuhoji suala la Lema kwa mtazamo wa kinyonge na kitumwa zaidi kuliko kwa fikra za binadamu aliye huru.
Dhana nzima ya ndugu Lema (Mb) kukataa dhamana sio kwamba anajitafutia umaarufu kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai, bali ni kupinga ukandamizaji wa watawala kupitia vyombo walivyojiundia. Hii haina tofauti na utawala wa kidikteta wa Nduli Iddi Amini.
Tofauti ni kwamba Amin alitoa amri moja kwa moja za kukamatwa na kuuawa wapinzani wake.
Tulipofikia hatuko huru kama tunavyojidanganya. Mbunge wa CCM, mwana mtandao anatuhumiwa kuandaa mauaji hakamatwi mpaka kibali kitoke ofisi ya bunge, wa CDM anarudi kwa miguu toka mahakamani kusikiliza kesi inayomhusu, anakamatwa ati katembea bila kibali.
Hii maana yake ni kwamba, Mh. Lema haruhusiwi kushiriki misa yoyote, misiba, kuangalia michezo, itafika wakati hata bungeni hataruhusiwa kuongozana na wabunge wengine. Sababu kote huko kuna mikusanyiko ya watu, na mkitoka ni lazima mtaandamana kwa umbali fulani.
Kuhusu, suala la Slaa na wafuasi wao hapo ni kielelezo tosha cha polisi wafanyao kazi kwa hulka pasi kutumia busara. Mkutano ni mahali ambapo watu wanajadili hoja, na kunakuwa na msemaji na wasikilizaji. Mkusanyiko ni mahali ambapo watu wamekusanyika kwa sababu fulani. Je, walimkuta Dr. Slaa anahutubia ama amekaa katika mkusanyiko wa maombolezo? Hivi ni lazima ulale kwenye nyumba? Mbona wamasai wanalala porini hawakamatwi? Hivi kwenye misiba kuna vibali vya kulala matanga?
Ni hayo tu, wapendwa wa nchi ya vibali.