Namlilia Mtema

Mrimu

Member
Jul 23, 2009
5
6
(1) Poleni sana poleni, poleni tena nasema
Nasema tena poleni, kifo cha dada Mtema
Hiki ni kitu kigeni, naona kama sinema
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(2) Namlilia Mtema, wa Herakuli Mrimu
Naja hapa nikihema, sikupiga hata simu
Mwili unanitetema, kikumbuka marehemu
Wa Herakuli Mrimu, namlilia Mtema.

(3) Pema usijapo pema, kipema si pema tena
Ametutoka mapema, Duniani hako tena
Tanganyika alipema, pakawa si pema tena
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(4) Taa yetu imezima, tutaiwashaje tena?
Macho yanitoka pima, ni giza sioni tena
Na ulimi umekwama, nashindwa hata kunena
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(5) Poleni sana CHADEMA, Mwenyekiti na wengine
Ni wewe Mbowe na Lema, wa Arusha si mwingine
Na Uchaggani Kilema, Tanganyika na kwingine
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(6) Wabunge wenye heshima, mliopo Tanganyika
Nawaita mje hima, mkutano kufanyika
Mkaijue hatima, nchi imegawanyika!
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(7) Dada Mdee Halima, na wewe Joni Mnyika
Wabunge wa Daresalima, mkaunde ushirika
Nyinyi sio mayatima, ni vijana wa marika
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(8) Tanganyika nilihama, sasa niko Marekani
Ni karibu na Bahama, visiwa Karibbeani
Poleni sana Kahama, na wa-Rombo wilayani
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(9) Kinijalia Karima, nitarejea mwakani
Nije Kibosho Kirima, na Holili Mpakani
Na Usseri Kitirima, nijue mu hali gani
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(10) Mbunge wetu Halima, wa Tegeta Darajani
Nakuomba kwa heshima, uje nilaki mwandani
Ndege 'kisimama wima, hapo Dar uwanjani
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(11) Ikiwa wewe mzima, andamana na jirani
Silayo au Shirima, wa Ubungo Kilimani
Mnyika iwe lazima, asikose uwanjani
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(12) Toka uwanja wa Ndege, twende zetu Ifakara
Tumuage Kambarage, nyinyi sasa ni vinara
Tupite Picha-Ya-Ndege, Morogoro Barabara
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(13) Tutanunua na Mbege, kwa Wachagga wa Kimara
'Cheze 'Iringi' na 'Rege', Moro tukifika mara
Katu hatubebi zege, hatuujengi mnara
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(14) Mi si mtu legelege, sina kukuru kakara
Na wala sina matege, nimesimama imara
Sitaki mkanitege, nifikapo Ifakara
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(15) Mimi na nyinyi wajomba, tuwe kwenye msafara
Wa Kibamba na Kwa-Komba, msitishe biashara
Siku moja ya kuomba, hamtapata hasara
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(16) Misa Kuu tutafanya, Kilombero Ifakara
Tutaanza kwa kufanya, ya Msalaba ishara
Komunyo tutagawanya, kukamilisha kafara
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(17) Sasa naita malenga, hii Jamii Foramu
Choveki sipige chenga, chukua yako kalamu
Shairi lako kulenga, utoe zako salamu
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(18) Na Barubaru malenga, tunga tupate fahamu
Uwajulishe wahenga, ni msiba si karamu
Usimtume mshenga, huyo sitamfahamu
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(19) Mzee Mwanakijiji, mkulima ndugu yangu
Najua wewe ni gwiji, la tungo za hapo tangu
Uje basi twende hiji, Ifakara kwa dadangu
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(20) Ahsante kutufariji, Waluguru na Wasangu
Na wa Kigoma-Ujiji, Morogoro ndio kwangu
Hukusahau Rufiji, na wa Mtoni-Marangu
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(21) Kaditamati wa tama, nimefika ukingoni
Bado nimeshika tama, naumia mgongoni
Huku nanguruma kama, fisi aliye pangoni
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.

(22) Salamu zao 'Wakama', na watemi wa Kingoni
Na wewe 'mangi' Maruma, Pale Moshi Korongoni
Mle kuku wa kuchoma, mwiko kumla Kongoni
Mrimu wa Herakuli, namlilia Mtema.


Mwombolezaji: Mrimu wa Herakuli (Jitu la miraba minne)
 
YU WAPI REGIA?

1. Masikini ndugu yetu, Regia twakulilia
Ulikuwa mwana kwetu, tuliye kutegemea,
Kujenga taifa letu, hili la watanzania,
Pengo ulotuachia, nani atatuzibia?

2. Habari hatuzipati, za Arumeru jimboni,
Watu hawana wakati, umuhimu hawaoni,
Wa kuweka mikakati, ku-update jamvini,
Pengo ulotuachia, nani atatuzibia?

3. Ulikuwa ukoshapu, habari kutupatia,
Ziwe zile za Kishapu, hata zile za Mafia,
Wakusanya kwenye kapu, kuja kutumiminia,
Pengo ulotuachia, nani atatuzibia?

4. Tulidhani Josephini, nafasi angechukua,
Kutuweka habarini, kila linalotokea,
Lakini haonekani, wapi amejichimbia?
Pengo ulotuachia, nani atatuzibia?

5. Halima walibaini, kwamba angesaidia,
Lakini yu vichakani, Kawe amejichimbia,
Umuhimu hauoni, habari kutupatia,
Pengo ulotuachia, nani atatuzibia?

6. Lakini nimebaini, pengo halitazibika,
Maana makaburini, hili walilitamka,
Kwamba haiwezekani, pengo hili kuzibika
Pumzika kwa amani, Regia mpendwa wetu.

7. Mrimu wa Herakuli, ona anavyojiliza,
Ameyajaza bakuli, machozi atililiza,
Hana lile wala hili, ameshindwa kujikaza
Pumzika kwa amani, Regia mpendwa wetu

8. Amealika malenga, kuja kukuomboleza,
Wale waishio Tanga, hata wale wa Muheza,
Waje hapa kujipanga, hisia kuzieleza,
Pumzika kwa amani, Regia mpendwa wetu.

9. Na miye Kilolambwani, malenga wa tangu enzi,
Najisikia huzuni, kumpoteza kipenzi,
Regia wetu jamani, katuachia simanzi,
Pumzika kwa amani, Regia mpendwa wetu

10. Kalamu naweka chini, nimeshindwa vumilia,
Naona giza usoni, kwa sababu ya kulia,
Wajua nalia nini?, namlilia Regia,
Pumzika kwa amani, Regia mpendwa wetu
 
Back
Top Bottom