Naibu Waziri Sagini - Mkono wa Dola Utawashukia Wahalifu Awe Mkulima Au Mfugaji

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,903
945

NAIBU WAZIRI SAGINI - MKONO WA DOLA UTAWASHUKIA WAHALIFU AWE MKULIMA AU MFUGAJI

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Jumanne Sagini amesema kuwa Serikali kupitia Jeshi la Polisi haitakuwa na uvumilivu juu ya Mwananchi yeyote awaye Mkulima au Mfugaji ambaye analengo la kuvuruga Amani na Usalama wa Raia na mali zao.

Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo kwenye ziara yake katika wilaya ya Nachingwea, Ruangwa na Wilaya ya Lindi jimbo la Mchinga Mkoani Lindi kutokana na kuwepo kwa migogoro ya Wakulima na Wafugaji ambayo imepelekea mauaji na baadhi ya Mifugo kufa na kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga.

"Kazi ya kwanza Polisi waliouwa watafutwe, wapatikane na nipate taarifa. Haiwezekani Raia amekufa haijulikani aliyemuuwa ni nani. Hawa Wananchi hawatuelewi, ndio maana wanaoongea hapa mpaka unasikitika.

Nguvu inatumika Ng’ombe amekatwa mkia wahalifu wanapatikana, anauawa Mtu asipatikane kwa nini? Wakati mwingine matendo yetu ya kuchelea yanasababisha Watu wachukue Sheria mkononi. Uwe Mkulima uwe Mfugaji zingatia Sheria kama unaenda kienyeji lazima utatuletea migogoro. Serikali ipo haikukututuma hapa kufanya masihara wala mizaha. Tutashughulika na wavunja Sheria, Wahalifu bila kuzingatia vimo vyao,unene wao,wanang’ombe wangapi au mashamba kiasi gani” Alisema Naibu Waziri Sagini.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi CP Awadhi Haji amesema kuwa Jeshi la Polisi halipo tayari kuvumilia kuona matukio ya uvunjifu wa amani yanayosababishwa na migogoro ya Wakulima na Wafugaji yanatokea ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amewahakikishia kuwa wanaovunja sheria za Nchi watashughulikiwa ipasavyo.

Awali wakizungumza katika nyakati tofauti tofauti baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Nachingwea Kijiji cha Ngunichile pamoja na wakazi wa Wilaya ya Ruangwa Kijiji cha Matambaralale wamesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la mifugo katika Vijiji hivyo ikisababishwa na Wafugaji kuhama kutoka baadhi ya maeneo ya Wilaya za Lindi kutokana na uhaba wa malisho na maji na hivyo kuingiza mifugo yao katika Wilaya za Liwale,Nachingwea Lindi na Ruangwa kunywesha mifugo katika Mto Mbwemkuru ambao ndio tegemeo kubwa la upatikanaji wa maji.

Kwa upande wao baadhi ya Wafugaji akiwemo Masanja Kabuta amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili Wafugaji hao ni baadhi ya Vijiji kutotenga maeneo mahsusi kwa ajili ya malisho na hivyo kuwafanya wenyewe kujiongoza namna gani usimsababishie mwenzio kero.

Hivi karibuni kumeripotiwa baadhi ya matukio ya kiuhalifu yakiwemo mauaji,ubakaji, uharibifu wa mazao na ushambuliaji wa mifugo kwa kukatwa mapanga katika Mkoa wa Lindi Wilaya za Ruangwa,Nachingwea,Liwale na Lindi ikisababishwa na migogoro ya Wakulima na Wafugaji.

IMG-20230901-WA0027.jpg
IMG-20230901-WA0033.jpg
IMG-20230901-WA0031.jpg
 
Back
Top Bottom