Mzazi usimroge mtoto wako, mbariki

GoldDhahabu

JF-Expert Member
Apr 29, 2023
4,695
6,398
Tafadhali, kama haujatajwa, kaa mbali na huu uzi! Huu uzi ni mahsusi kwa ajili ya watajwa tu, Wababa wenye Akili na Wamama wenye akili.

Kuna mambo makuu mawili kwa walengwa: onyo na ushauri

Onyo: USIMLOGE MWANAO.

Ushauri: MBARIKI MTOTO WAKO.

Kwenye mojawapo ya vitabu vya Robert Schuller, ameelezea kilichobainishwa na kongamano la Wanasaikolojia nchini Ufaransa. Ilibainika kuwa, watoto wanaofahamika kama majiniaz, yaani, watoto wenye uwezo mkubwa sana kiakili, siyo kwa sababu wanao ubongo wa kipekee sana. Bali ni kwa kuwa walibahatika kuwapata watu wa karibu, hasa wazazi wao, waliowaaminisha kuwa ni majiniaz.

Kuongezea hilo, lilifanyika jaribio nchini Marekani, ambako walichukuliwa wanafunzi wenye uwezo mdogo darasani na kutengewa darasa lao maalum. Vile vile, walichukuliwa Walimu waliokuwa wakilalamikiwa na wanafunzi wengi kuwa hawaeleweki wanapofundisha.

Kiongozi akawaambia wale wanafunzi "vilaza" kuwa wamebainika kuwa wao ndiyo wanafunzi wenye akili kuliko wote. Kwa hiyo, wamewatengea darasa lao ili wawe wanafundishwa na walimu wenye uwezo mkubwa sana katika ufundishaji.

Na wale walimu "mzigo" waliochaguliwa nao wakapewa ujumbe unaotia moyo, kwamba imebainika kuwa wao ndiyo walimu wenye uwezo mkubwa sana kuliko wenzao wote, hivyo uongozi umeamua kuwatengea darasa maalum lenye wanafunzi "cream" pekee, wawafundishe.

Walimu wakafurahi kwa kipaji chao kutambulika, na wanafunzi nao wakatiwa moyo kugundulika kuwa ni vichwa. Kwa umakini mkubwa, na kwa siri sana, uongozi ulifuatilia yaliyojiri baada ya hizo taarifa.

Si Walimu wala si wanafunzi! Wote walichapa kazi kwa bidii, kila mmoja katika nafasi yake. Mwalimu alishughulika kama imstahilivyo Mwalimu mwenye kipaji cha kufundisha, na mwanafunzi kama mwanafunzi mwenye akili sana.

Miezi sita baadaye , mitihani ilitungwa ambayo ilifanywa na wanafunzi wote, waliokuwa wakijulikana kuwa ni vichwa na wale waliokuwa 'vilaza" lakini wakaaminishswa kuwa ni vichwa.

Kukawaje? Vilaza wa zamani waliongoza kwenye hiyo mitihani.

Waliokuwa wakifahamika kama vichwa, wa kwanza alianzia daraja C, huku kwa waliostaafu ukilaza na kujiunga na ujiniaz, A zikitamalaki.

Kulitokea nini?

Kila mmoja alifanya kama alivyoaminika. Walimu waliaminishwa kuwa wanao uwezo mkubwa sana, hivyo uwezo wao uliokuwa umejificha ukaibuka.

Wanafunzi waliaminijshwa kuwa ni cream, hivyo hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kuwa cream

Kila mtu, awe anajua au hajui, anajitahidi kufanya kama anavyotarajiwa. Watu wanaishi kwa kujitahidi kuyaishi matarajio ya watu wao wa karibu.

Kama mzazi, unaaminiwa sana na mtoto wako. Ni jukumu lako kumjengea taswira chanya kujihusu, hasa juu ya uwezo wake darasani na maishani. Ikibidi, "mdanganye" kwa uongo usio uongo, kama alivyofanya kiongozi mwenye akili nchini Marekani kwa walimu na wanafunzi wake.

Usimloge mwanao. Epuka kauli hasi, hasa za kumwonesha mwanao kuwa yeye ni toafuti na wenzake, kwamba hana akili, n.k. Kauli hasi ni uchawi hatari sana.

Maisha ya kukosoa kulikopitiliza ni sumu mbaya sana kwa mtoto.

Unaweza kumbariki mwanao. Si vibaya kuwaiga wengine, ikiwa wayafanyayo ni mema na yanawasidia.

Inasemekana, wanawake wa Kiyahudi, wana kawaida ya "kuwabariki" watoto wao pindi wanapowanyonyesha. Mtoto anapoendelea kunyonya, mama anazungumza maneno chanya juu yake, kama vile, "UNA AKILI SANA MWANGU. UATAKUJA KUWA MTU MKUBWA SANA. UWEZO WAKO NI WA HALI YA JUU MNO", n.k.

Wanafanya hivyo kwa sababu wanaojua kuwa manneno huumba. Isitoshe, maneno wanayoyatamka, fikra za mtoto zinayatunza.

Ni ajabu kuwa Wayahudi ni kati ya watu wanaosifika sana kuwa na akili duniani? Inawezekana ni kwa sababu ya kulelewa na Wababa Wenye Akili na Wamama wanaojitambua.

Wanaume wa Kizungu wenye akili, kwa kutambua umuhimu wa kusoma Vitabu, huwajengea watoto wao hizo tabia tokea wakiwa matumboni mwa mama zao.

Wake zao wakiwa wajawazito, huwasomea vitabu vizuri wakiamini kuwa kutachochea mtoto aliyeko tumboni kupenda Vitabu.

Na watoto wanapozaliwa , huendelea kuwasomea vitabu tokea vikiwa vichanga hadi watakapoweza kujisomea wenyewe.

Nasisitiza! Usimloge mtoto. Mbariki mtoto wako.

Kuna watu wamefanikiwa maishani mwao kwa sababu ya mtazamo chanya kujihusu waliojengewa na wazazi wao na watu wao wa karibu, hasa kujithamini na kujiamini. Na kuna waliokwama, na mkwamo huo umechangiwa na watu wao wa karibu. Hawakuwabariki, waliwalaani. Hawakubahatika kulelewa na watu wenye akili.

Na ninaposema watu wenye akili, simaanishi waliosoma. Kwani umeshawahi kusikia kuna shule inayowapa watu akili? Haipo popote pale duniani.

Unamfahamu mvumbuzi wa bulb ya umeme? Anaitwa Thomas Edson.

Mtu aliyevumbua bulb ya umeme ni mtu wa aina gani? Ni mwenye akili sana? Ni "kilaza" au "kichwa?"

Najua unalo jibu, lakini jiwekee akiba mpaka wakati utakaoona unafaa kulitoa.

Lakini Edson alifikaje huko? Kama mama yake angekuwa "mjinga", inawezekana maisha yake yangeishia kuwa ya kawaida tu, au ya hovyo sana. Lakini kwa sababu mama yake alikuwa na akili, kulimsaidia Thomas Edson kuwa miongoni mwa watu wengine wenye majina ulimwenguni.

Miaka miwili baada ya kuanza shule, Thomas Edson alirudishwa nyumbani akiwa na barua inayomjulisha mzazi wake kuwa mwanaye kaachishwa shule kwa kuwa hana uwezo wa kuelewa masomo ya darasani.

Mama yake, baada ya kuisoma hiyo barua, alianza kutiririkwa na machozi kiasi cha kumfanya Thomas afahamu kuwa barua aliyokuja nayo ilikuwa na ujumbe usio wa kawaida.

Thomas hakuweza kuvumilia hiyo hali. Aliamua kumwuliza mama yake kinachomliza.

Nikuulize, ingekuwa ni wewe ungejibuje?

Sikiliza majibu ya wenye akili wenzako, maana naamini wewe nawe no miongoni mwa watu wenye akili: "Ni kwa sababu nimefurahi sana mwanangu," alisema mamaye Thomas Edson, "Walimu wako wamesema kuwa wewe una akili sana, hivyo huhitajiki kwenda shuleni bali nikufundishe mwenyewe nyumbani"

Unafikiri hilo jibu lilikuwa na athari gani kwa Thomas Edson?

Kazi alizokuja kuzifanaya zinajibu hilo. Alikuja kuwa mwanasayansi mkubwa sana, aliye na hatimiliki zaidi ya elfu moja.

Mama yake alimfundisha kusoma na kuandika, na kwa kupenda kwake kujisomea Vitabu vya Kisayansi, akawa mwanasayansi mkubwa sana.

Usimloge mwanao, bali umbariki.

Hata kama kutahitajika kumwadhibu, ufanye hivyo kwa upendo. Kamwe usimwadhibu kwa hasira. Kamwe usimtamkie maneno yatakayomfanya kujidharua au kujiona duni. Fanya ufanyalo, kuhakikiasha kuwa nafsi ya mwanao inashiba taswira chanya kujihusu.

Unaweza hata kuyaandaa mazingira ya kumsema kwa mema, huku ukijifanya hajui kuwa anakusikia.

Kwa mfano, mume na mke wanaweza wakajifanya kuwa hawajui kama mtoto wao anawasikia, halafu wakasema maneno haya, "Unajua kwa nini huwa nikitaka kitu kilichopo chumbani kwetu ninapenda kumwagiza "Junior"? Ni kwa sababu ya umakini wake. Sijawahi kumwona mtoto mwenye akili kama Junior. Katika watu waliobarikiwa kuwazaa watoto wabunifu, ni sisi. Najua atakapokuwa mkubwa, atakuja kuwa mtu mkubwa sana. Mimi nakuambia. Utaona!!!"

Mnajifanya hamjui kuwa anawasikia, kumbe mmekusudia awasikie.

Unafikiri Junior hapo alipo atajisikiaje? Fikiri tu wewe mwenyewe, itakuwaje ukimkuta mtu anakusema vizuri, tena bila huyo mtu kutarajia kuwa ungeweza kumkuta katika hali hiyo?

Hiyo kauli, nina uhakika, itamwongezea kitu kizuri kwenye ufahamu wake.

Kwanza, atajua kuwa anaaminika, hivyo atjitahidi ili aendelee kuaminika.

Pili, kutamwongezea kujiamini zaidi. Ameshajua kuwa hata wazazi wake wanamwamini.

Mengine unaweza ukaongezea mwenyewe.

Niliposema huu uzi ni kwa ajili ya wahusika tu, nilimaanisha kila mtu atakayeusoma. Unakuhusu!!!

Hata kama ni mwanafunzi, unaweza kutumia kwa wanafunzi wenzako au hata wadogo zako, bila kujali ni wa kuzaliwa nao au ni marafiki tu. Kila mtu anahitaji kuaminiwa!

Mwanaume yeyote na mwanamke yeyote anaweza kutumia mbinu zilizoelezewa kuwasaidia watoto wake na wengineo, hata kama ni watu wazima, kuwasaidia.

Ikiwa wewe ni bosi, kwa mfano, unaweza ukawafanya watu wa chini yako kuwa bora zaidi kwa kuwasaidia kujikubali. Wakigundua unawaamini, nao watajikubali, hatimaye.

Muhimu, ni kuamua kuwa baba mwenye akili au mama mwenye akili kwa mtu mwenye uhitaji huo.

Hata kama kiumri wewe ni mvulana tu au msichana tu, unaweza ukatenda kwa hekima ya baba mwenye akili na mama mwenye akili.

Wewe ni baba!

Wewe ni mama

Usiwe mchawi, bali mzazi anayebariki.

Kitendo cha kuusoma huu uzi, ni uthibitisho kuwa wewe ni "mzazi" mwenye akili.

Wasaidie "wanao" kuwa bora.
 
usimloge ❌️
usimroge ✅️
Nashukuru mkuu!

Umenisaidia kuongeza msamiati.

Nilifikiri umekosea, lakini nimeangalia kwenye kamusi, nikakuta misamiati yote miwili ni sahihi.

Kuloga ni sahihi, na kuroga ni sahihi. Yote inamaanisha kitu kimoja.

Sikukosea, na hukukosea!

Asante.
 
Miaka ya nyuma, nilisikia ushuhuda wa bibi mmoja mzaliwa wa Kilimanjaro.

Mtoto wake wa kiume alipozaliwa, ilibainika kuwa alikuwa na udhaifu wa miguu na kuongea.

Mpaka kufikia umri wa kutembea, bado mwanawe alikuwa ni wa kubebwa.

Kwa sababu ilikuwa ni kawaida watoto wengi wa huko kwao kuhudhuria ibada ya watoto Kanisani siku ya Jumapili, wa kwake alikuwa akibebwa na mtoto wake mkubwa. Ilifikia hatua kaka mtu akawa snakwepa kumbeba mdogo wake kwenda Kanisani kwa sababu wenzake walikuwa wskimcheka.

Kwa kipindi chote hicho, kila ilipotokea akamsikia mtu akimzungumzia mtoto wake kuwa ni bubu na mlemavu wa miguu, yeye aliingilia kati na kubisha. Alikuwa na kawaida ya kusisitiza kuwa mtoto wake si bubu na wala miguu ya mtoto wake haikuwa na ulemavu. Hakujua kwa nini ilikuwa hivyo, alikuwa hataki kabisa kusikia mtoto wake akitajwa kuwa mlemavu.

Miaka iliendelea, na hatimaye, siku ya siku, kukatokea jambo la kushangazwa.

Alikuwa ndani na mtoto wake mlemavu. Alikuwa amemkalisha chini huku yeye akimenya ndizi. Bila kufikiria, alijikuta akiropoka, mithili ya mtu aliyekata tamaa.

Alimwambia mwanaye ambaye alikuwa kiwete na bubu, "Ungekuwa unaweza kutembea si ungenifuatia like bakuli!". Alisema hivyo, kama vile kujisemea tu, kwa sababu alijua mwanaye asingeweza kufanya lo lote katika hilo.

Ghafla, alisikia sauti, "hili hapa!"
Alipoinua kichwa kutazama, alimkuta mwanaye aliyekuwa kiwete ndiye aliyeyafanya hayo.

Alishtuka sana, ila mshutuko wa furaha, lakini hakumwonesha mwanaye hilo. Ili kujiridhisha kuwa kweli mwanaye kapona, alimjibu, "siyo hilo, ni lile pale"

Safari hii, kwa macho yake mwenyewe, alimshuhdia mwanaye akiliridisha bakuli la kwanza na kulichukua jingine.

Ilikuwa mara yake ya kwanza kumwona mwanaye akitembea.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kumsikia mtoto wake akiongea kwa ufasaha.

Naweza nisiwe na jibu la moja kwa moja la sababu iliyompelekea mwanaye kupona ububu na ukiwete wa miguu pamoja. Lakini huenda, ni matokeo ya maneno aliyokuwa akiyatamka kuwa mwanaye si kilema wala bubu!
 
Mkuu nimefarijika sana kusoma hii mada yako, natamani sana mada kama hizi ziwe zina trend hapa jamii forum wazazi tujifunze lakini kwasababu wanachama wengi huku uwezo wao wa akili ni mdogo sana hawawezi kuelewa vitu kama hivi.

Hii ni power of positive mind mafunzo ya thomas edison nilisoma kwa napoleon hill think and grow rich
 
Back
Top Bottom