Kwanza kabisa napenda kutoa Pole kwako kwa Usumbufu wowote ulioupata kutokana na mgogoro uliotokea ndani ya Chama chako (Chadema). Pia natoa pole kwa wenzako wote mliokutwa na matatizo ndani ya chama.
1. Mhe. Zitto, unatajwa kwamba wewe ni msaliti ndani ya Chama. Mimi nimekuwa nikikufuatilia katika shughuli zako za kiasiasa hata hivi karibuni ulipokuwa ukifanya mikutano huko Rukwa, Kigoma na kwingineko. Umekuwa ukisisitiza ukombozi kwa Taifa hili. Kumsaidia mwananchi kuondokana na umasikini, Kutumia raslimali za nchi kwa manufaa ya wananchi. Na umekuwa ukisema ukombozi utaletwa na CHADEMA. Mimi nakushauri, Usiwe na wasiwasi, Kuwa mvumilivu, yote yatapita na siku moja utaonekana mkombozi badala ya msaliti. Kama hauna chembe ya usaliti, naamini yale yote unayoyasema yanatoka moyoni mwako na siku moja yatadhihirika.
2. Mhe. Zitto, Unatajwa kuwania uongozi hasa Uenyekiti wa Chama. Naamini hii ni haki yako na ni haki ya mwanachama yeyote wa Chadema mwenye sifa sitahiki. Naamini sifa unazo. Nashauri ufuate utaratibu wa chama katika uwapata viongozi na kila kitu kinawezekana.
3. Mhe. Zitto, Umehusisha na waraka wa siri mabadiliko ulioandaliwa na Wenzako. Bahati nzuri wamekiri kuandaa. Na jambo zuri zaidi wamesema haukuhusika lakini walitegemea kukuhusisha baadae. Mimi naamini kama huo ndo ukweli wenyewe hauna sababu ya kuwa na wasiwasi juu ya huo Waraka wa siri. Dr. Kitila Mkumbo na wenzake wanaweza kujibika juu la hilo.
4. Mhe. Zitto, Wewe ni mwanachama kijana wa Chadema, lakini wewe ni Mwanachama MKONGWE kabisa wa chadema. Si mara ya kwanza nakusikia ukisema umejiunga Chadema ukiwa na miaka 16. Na wakati huo ukiwa Kidato cha Tatu. Sasa una miaka 37 na haujawahi kuwa mwanachama wa chama kingine chochote kile hapa Tanzania na isitoshe hata nje ya Tanzania. Kwa mantiki hii wewe ni Mtoto, Baba na Mama wa Chadema. Kikisaliti chacdema ni sawa na mtoto kuwakataa wazazi wake waliomzaa, Kikisaliti chadema ni sawa na Baba na Mama kuwakataa watoto waliowazaa. Kwa mantiki hii naomba uwaeleze Viongozi wenzako Ukweli kuhusu jambo hili. Nadhani Mtaelewana na hatimaye mtasonga mbele.
5. Mhe. Zitto, Siyo kila anayekupatia ushauri na kusikitika kwa mambo yanayoendelea ndani ya Chadema ana uchungu na wewe na Chama chako. Wengine wanakudhihaki na wanapenda kukuona siku moja unakosa muelekeo wa kisiasa. Nakushauri uwe mvumilivu wa kisiasa. Wewe ni kiongozi na utabaki kuwa kiongozi Daima. Jambo la msingi ni kumaliza tofauti zenu kama zipo ili msonge mbele pamoja kwa kuaminiana.
5. Mwisho kabisa naomba msiwarudishe nyuma Watanzania walio nyuma yenu, kwani kutoelewana kwenu viongozi kunawayumbisha sana watanzania wanaopenda mabadiliko. Tunahitaji kuwaona viongozi wote wa Chadema mkiwa pamoja kwa amani, sisi watanzania tupo pamoja nanyi. Hatumbagui kiongozi yeyote. Kila kiongozi ana mchango wake ndani ya Chadema.
6. Mwisho kabisa, naamini wewe Zitto, na viongozi wenzako mtamaliza tofauti zenu na watanzania wataona mkiandika historia mpya katika medani za Kisiasa.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mimi ni Mwanachama Wa CHADEMA.