Mwongozo wa Ushiriki kwenye Mijadala katika JamiiForums

Status
Not open for further replies.

Maxence Melo

JF Founder
Feb 10, 2006
4,006
11,903
Wakuu,

Mwongozo huu tunauweka hapa ili wadau mtoe maoni kwani inawezekana wengi hamjausoma. Una mabadiliko kidogo lakini umekuwepo muda mrefu. Bandiko kuu lisilojadiliwa lipo hapa: JamiiForums' Community Engagement Guidelines | Mwongozo wa Ushiriki kwenye Mijadala

Unaweza kutoa maoni yako ili tuboreshe zaidi ili jukwaa letu liendelee kuwa sehemu bora zaidi kwako na kwa wasomaji ambao hata si wanachama.

============

SOMA:

Hapana shaka kuwa kutakuwa na maoni na mawazo anuai juu ya masuala mbalimbali yanayojadiliwa katika Jukwaa hili. Washiriki hawatarajiwi kukubaliana na kila jambo linalojadiliwa! Kwa msingi huo, ili kudumisha mijadala yenye heshima, ubunifu na ushiriki kamilifu, taratibu zifuatazo zimewekwa ili kuwaongoza washiriki wote:

1) Washiriki wanapaswa kutumia lugha ya kiungwana na kistaarabu ili kuhakikisha kuwa heshima na uvumilivu vinatawala katika mijadala.

2) Mpangilio sahihi wa viakifishi (uandishi) na uzingatiaji wa sarufi unatarajiwa kuonekana katika andiko lako, katika hili unapaswa kuwakumbuka wasomaji wako. Ikiwa unaweza kuhoji/kukosoa uandishi wa watu wengine, basi tarajia kuwa uandishi wako unaweza kuhojiwa au kukosolewa pia. Zingatia kuwa unapokuwa mtandaoni (si JamiiForums pekee) wapo watu ambao watahoji ubora wa uandishi wako. Hivyo, unapaswa kusoma tena andiko lako kisha lihariri ili ueleweke!

3) Kuwa mwenye mwenye adabu, mwenye heshima na muadilifu: Unapoamua kuwa mkosoaji au mtoaji wa maoni unapaswa kutambua kuwa wapo watu ambao masuala hayo yanawahusu au kuwagusa kwa namna moja au nyingine. Hivyo, unapawa kuwa mkarimu na kutumia busara ili usiumize hisia za watu wanaosoma andiko lako.

Kubali kuwa na mawazo au majibu yenye kujenga na wala yasiwe makali yenye kumshambulia mtu mwingine au kushambulia mawazo yao. Aidha, epuka kutumia herufi kubwa (CAPS), hati mkolezo au hati mlalo katika andiko lote. Kimsingi, andiko au uzi wako unapaswa kuwa wenye mawazo yenye mantiki yaliyosemwa vizuri. Hivyo, matusi yanayoelekezwa kwa mchangiaji hayakubaliki. Hata kama hukubaliani na mawazo yaliyotolewa na mshiriki mwingine haimaanishi kuwa mtu huyo hayupo sahihi (amekosea). Badala yake unapaswa toa maelezo au mtazamo tofauti ili kuchochea mjadala zaidi.

4) Epuka kutumia utani unaokera (usiofaa), uwapo jukwaani hapa, unakuwa katika mazingira ambayo hauonani ana kwa ana na washiriki wengine. Kwa hiyo, unapofanya utani ni rahisi kwa mshiriki mwingine kuuchukulia kwa mtazamo tofauti.

5) Unapotumia chanzo fulani hakikisha unakirejelea kwa usahihi: Tambua mchango wa mwingine katika andiko lako ikiwa kuna umuhimu. Weka kiungo (link) pale kinapohitajika. Hatuna jukumu la kuthibitisha maudhui yoyote, wala hatutakubali kuwajibika kwayo na wala hatuhakiki usahihi au ukamilifu wa ujumbe wowote au vigezo vya mdau yeyote.

6) Fupisha habari yako: Usipoteze muda wa washiriki wengine kwa kutoa taarifa ndefu inayojirudia rudia. Iweke hoja yako kwa uwazi, kwa ufupi na inayoeleweka.

7) Wapuuze wanachama wasumbufu: Ikitokea mshiriki yeyote jukwaani amekusumbua, tafadhali mpuuze (ignore) kisha toa taarifa kwa wasimamizi wa maudhui (moderators) huku ukiambatanisha na uthibitisho wenye kiungio kinachoonesha ulichofanyiwa ili hatua stahiki zichukuliwe. Aidha, unaweza kubonyeza kitufe cha kutoa taarifa (Report button) ili taarifa ifanyiwe kazi haraka.

8) Epuka kutukana, kushambulia au kukwaza wengine: Maandiko ya chuki na yenye mrengo wa kuwashambulia watu hayatovumiliwa na JamiiForums. Wachukulie (waheshimu) wengine kama ambavyo wewe unataka uchukuliwe (uheshimiwe). Hivyo, kuleta andiko ambalo litachochea muitikio hasi kwa watu wengine inashauriwa kuepukwa.

Jiepushe kutuma kitu chochote ambacho ni kichafu, chukizo au cha kudhalilisha ambacho kinaweza kuvunja haki miliki ya mtu au haki yake ya faragha (privacy). Ikiwa unajiuliza mwenyewe kama jambo fulani linafaa, yawezekana halifai.

9) Uradidi (Urudiaji): Uradidi wa makusudi wa ujumbe usio na maana, ujumbe mfupi sana uanolenga kuongeza idadi ya maandiko yako (posts) au kuwakera wengine hauruhusiwi kabisa. Sambamba na hilo, uradidi wa matangazo ya biashara nao hauruhusiwi kabisa. Hata hivyo, kutangaza ukurasa wako wa biashara inaruhusiwa endapo tu utaomba na kupewa kibali kutoka kwa waendeshaji wa jukwaa hili. Kutumia viungio vya nyuzi za zamani wakati wa mjadala inaruhusiwa, lakini ikionekana viungio unavyovitumia ni vile ambavyo havihitajiki au haviendani jambo husika, basi hili pia litachukuliwa kama uradidi. Vilevile, kutuma uzi wako zaidi ya mara moja huchukuliwa kama uradidi.

ZINGATIA: Ikiwa washiriki watatumia sehemu ya ujumbe binafsi kupaka/kuponda wengine kwa mambo yasiyo ya msingi jumbe zao zitafungwa. Usitume ujumbe wowote binafsi (Private Conversations) hadharani bila kuomba idhini kwa mtu aliyekutumia ujumbe huo.

10) Kuvaa uhusika wa mtu mwingine au kuingilia akaunti ya mtu: Usithubutu kuvaa au kujifanya wewe ni muhusika fulani ikiwa wewe siye. Usivae uhusika wa viongozi wa umma au mwanachama fulani au kutengeneza akaunti maalumu kwa dhumuni la kuwadhalilisha au kuwachafua wanachama wengine na wananchi wengine kwa ujumla. Kitendo cha kufanya jaribio la kuingilia akaunti ya mdau mwingine hakitavumiliwa. Kufanya matendo haya kunaweza kusababisha akaunti yako kufungiwa au kufutwa kabisa.

11) Kuitana Majina kwa mlinganisho: Hairuhusiwi Wanachama kumfananisha mdau aliyeamua kutumia jina fulani na jina jingine au majina yao halisi (aidha ni yao kweli au si yao). Kufanya hivyo kunaweza pelekea ukafungiwa akaunti yako.

12) Mijadala au andiko linaloenda nje ya mada: Hakuna adhabu yoyote kubwa inayotolewa kwa watu wanaotoka nje ya mjadala. Lakini, tuwe wawazi tu kuwa jambo hili halipendezi na linakera. Kama una jambo la kusema lakini haliendani na mada ilyowasilishwa unashauriwa kuanzisha mjadala mpya vinginevyo wazo lako litaondolewa.

13) Kujaribu kukwepa kufungiwa: Unapoingia katika akaunti yako ukakutana na ujumbe kuwa umefungiwa, tafadhali wasilisha ombi la kufunguliwa akaunti yako kwa waendeshaji wa mtandao huu ili kuwa na makuabliano juu ya sababu zilizopelekea ukafungiwa. Mkifikia makubaliano, utaruhusiwa kutumia akaunti yako bila shida. Usijisajili tena kwa jina lingine hata kama mfumo wetu ukikuruhusu. Ukijaribu kujisajili tena na tukakubaini, itasababisha kufungiwa moja kwa moja.

14) Masuala yanayohusu ponografia na utupu: Unakumbushwa kuwa jukwaa hili ni la umma, kuna watoto wenye umri mdogo na watu wazima wenye zaidi ya miaka 60 na kuendelea. Hivyo, masuala yote yanayohusu ponografia na utupu hayaruhusiwi kabisa.

15) Saini na Avata: Hatuna sheria na kanuni za uandishi wa saini wala uwekaji wa ‘avata’. Katika hili unaombwa usitumie Saini au Avata ambazo zitawakwaza watu wengine. Mathalan, saini na avata hizo zisiwe zenye maudhui yasiyofaa, kibaguzi au zinazohamasisha kutenda makosa ya jinai n.k.

16) Maudhui tata: Kwakuwa hatuwezi gusia kila kitu lakini sheria hii inagusia kila jambo... Tambua kuwa hili ni jukwaa la Umma kwahiyo unapaswa kutenda kama mtu ambaye yuko mbele ya macho au umati wa watu. Masuala mengine yote yameachwa chini ya wasimamizi wa maudhui ambayo yanajumuisha mambo yote ya uongo, upotoshaji, matusi, machukizo, udhalilishaji wa kijinsia, kutishia, uvamizi wa faragha za watu au kufanya mambo mengine yanavyovunja sheria na kuchochea uhalifu.

Kumbuka, tunayo haki ya kumfungia mwanachama yeyote kwa kipindi kifupi au moja kwa moja, kukataa andiko lolote lililotumwa, jina ambalo linachukiza au andiko baya.

Tunayo haki ya kuhariri au kufuta andiko lolote au kuweka ukomo wa mjadala wowote na kuufunga kwa sababu yoyote au hata bila sababu, pengine bila ufafanuzi wala onyo.

MSISITIZO: Kama ukikuta kuna mjadala wowote ambao unakiuka misingi iliyowekwa katika andiko hili tafadhali wasiliana nasi ili mjadala huo ufanyiwe mapitio haraka iwezekanavyo.
 
Status
Not open for further replies.

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

62 Reactions
Reply
Top Bottom