Mwisho wa Daudi Ballali

Mwisho wa Daudi Ballali

balali.jpg

Mkazi wa Kijiji la Luganga, Wilaya ya Mufindi, Iringa, alikozaliwa Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali analazimika kutumia saa 32 kufika katika kaburi la kiongozi huyo lililopo eneo la Silver Spring, Maryland nchini Marekani.

Ndugu wa Ballali wanaweza kutaka kwenda kuona kaburi la ndugu yao, kutokana na ukweli kwamba wengi wao hawakuwahi kupata fursa ya kumzika Gavana huyo ambaye alikuwa kiongozi wa juu kabisa wa taasisi kubwa inayosimamia masuala ya fedha na uchumi wa nchi.

Mwandishi wa gazeti hili alisafiri kwa saa 24 kutoka Dar es Salaam hadi Washington, Marekani ambako alithibitisha pasi na shaka kwamba Ballali alizikwa Mei 21, 2008 katika makaburi ya Gate of Heaven, baada ya kufariki dunia akiwa nyumbani kwake Maryland, Mei 16, mwaka huo.

Safari hiyo ya siku kumi, ilianza Alhamisi Juni 26, 2014 hadi Jumapili, Julai 6. Mwandishi wa habari hizi aliligundua kaburi hilo baada ya kwenda makaburi ya Gate of Heaven kwa siku tatu mfululizo.

Siku ya kwanza, mwenyeji wa mwandishi ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa alimfikisha katika makaburi hayo, lakini kaburi la Ballali halikuonekana na hata mwandishi alipokwenda siku ya pili peke yake, kaburi hilo pia halikuonekana kwa kutokana na ukubwa wa eneo hilo.

Siku ya tatu, Mwandishi wa Mwananchi alilazimika kuomba msaada wa Ofisi ya Makaburi ya Gate of Heaven, ambayo ilimsadia kuonyesha eneo lilipo kaburi hilo, hivyo kuwezesha kupata picha zake.

Kaburi lake liko katika msitari wa mwisho kabisa na Ukanda wa Kijani wa miti iliyozunguka makaburi ya Gate of Heaven, likiwa limeandikwa jina la kiongozi huyo, pamoja na maneno ya Kiingereza yanayosomeka “When the heart weep for what it has lost, the soul rejoices for what it has found”.

Maana ya maneno hayo ni kwamba “wakati moyo ukiomboleza kwa kile kilichopotea, roho hufurahi kwa kile kilichopatikana”. Kaburi hili limezungukwa na makaburi mengine kadhaa ambayo si ya Watanzania, kwani kwa haraka kutokana na mazingira yalivyokuwa, Mwandishi wa Mwananchi hakuweza kuona kaburi jingine lenye majina yenye asili au kuwa na mwelekeo wa asili ya Tanzania.

Uthibitisho huu ni tofauti na hekaya za miaka nenda rudi zilizogubika kifo cha kiongozi huyo, ambaye tangu alipoondoka nchini kwenda Marekani Agosti 2007, hakuwahi kurejea na badala yake zilisikika taarifa za kuugua kwake, kifo chake na baadaye mazishi yake yaliyokuwa ya siri kubwa yakiwahusisha ndugu wa karibu pekee.

Kutokana na mazingira hayo, kumekuwapo na uvumi kwamba Ballali hakufa na pengine amefichwa kusikojulikana, madai yanayochagizwa na mtu aliyejitokeza katika mitandao wa kijamii ya Twitter na facebook, akidai kwamba yeye ni Ballali na kwamba hajafa, huku akisisitiza kuwa wakati ukiwadia ukweli utafahamika.

Mtu huyo asiyefahamika hadi sasa alianza kujitokeza Twitter, Oktoba Mosi, 2012 pale aliposema “Nitakutana na Rais Kikwete (Jakaya) na ujumbe wake wiki hii hapa Marekani”. Mtu huyo alidai kwamba alikuja nchini Tanzania na kukaa karibu na Hoteli ya Hyatt Kempinski Kilimanjaro na baadaye kuondoka ghafla kwa kile alichokiita sababu za kiusalama.

Novemba 13 mwaka huo alituma ujumbe akisema:“In Dar es Salaam, Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kempinski Kilimanjaro Hotel. Feels good to be close to my former office, BoT,” akimaanisha kwamba niko Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, najisikia vizuri kuwa karibu na ofisi yangu ya zamani BoT.

Mtu huyo ambaye sasa tunaweza kuthibitisha kuwa ni feki amekuwa akiendelea kutuma ujumbe akijitambulisha kwa jina hilo la Ballali.

Ballali alifariki dunia kama ilivyotagazwa, lakini ilikuwaje akaenda safarini Washington, ugonjwa wake na hata kifo chake kilikuwaje? Je ndugu zake wanasemaje, safari ya kwenda Marekani ilikuwaje? Fuatilia mfululizo wa habari hii itakapoendelea kesho.

Source: Mwananchi
Hatudanganyikiiii- 2015 campaign trash
 
Nisaidieni jamani na huu nia uandishi wa habari wa kichunguzi wanaofundishwa? hatujaona limitation ya research yake.
Jina tu kwa kaburi inatosha kufanya hitimisho kirahisi hivyo?
 
hivi mmiliki wa hilo gazeti mwananchi sio huyo shigongo?
kama ndiye basi tunatapeliwa kwa mara ya pili kuwa gavana alifariki,maana magazeti yao ni ya udakuzi,hayajielewi kabisa..


Sent from my iPhone using JamiiForums
 
Makaburi ya America tunayajua yalivyo. Hakuna kaburi america pana kama linavyoonyeshwa hapa. Je, tangu Balalli afe hiyo sehemu wameacha kuzika? Ninauliza kwa sababu hapo linaonekana kaburi moja tu! This journalist is so ignorant that he doesn't even know how to cheat intelligently. Kajipange upya uje na better story!
 
Utata wa Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi kuhusu kifo cha David Ballali.
Kwanza, ukilisoma vizuri gazeti la Mwananchi toleo la jana 12/07/2014 kwenye ile habari inayohusiana na kifo cha David Ballali, gazeti linasema kuwa iliwachukua Siku tatu kulitafuta kaburi la marehemu Ballali.
Ilibidi wamuulize mtunza makaburi, ndiye aliyewaelekeza kaburi lilipo.

Wakati huo huo gazeti hili linadai kuwa Ballali alizikwa na ndugu zake wa karibu, ikiwa na maana kwamba, hao ndugu wa karibu walikuwa wanafahamu alipozikwa marehemu David Ballali.
Swali:-
Kulikuwa na ulazima gani wa mwandishi wa gazeti hili kumuuliza mtunza makaburi badala ya kuwauliza hao ndugu wa karibu na marehemu waliotajwa kuhusika kwenye shughuli za mazishi!

Anyway, sote tunatambua kwamba David Ballali alikuwa mtumishi wa umma nikiwa na maana kwamba, alikuwa Kiongozi mwandamizi wa Serikali tena Kiongozi wa nafasi ya juu na nyeti sana (Gavana wa Fedha), hivyo basi, ilikuwaje Serikali ikashindwa kumtuma mwakilishi toka Serikalini, ambaye angeungana na wanandugu hao katika shughuli za mazishi ya marehemu huko nje ya Nchi!
Nimeuliza jambo hili kwa sababu hakuna mahali ambapo mwandishi ametaja aidha Jina au Cheo cha mtumishi wa Serikali aliyeongozana na wanandugu wa marehemu Ballali kwenda kuhudhuria mazishi yake.
Utata bado ni mwingi sana katika habari ile ya mwandishi kuhusu kifo cha Ballali.
Pili, ukiitazama vizuri hiyo Picha iliyotolewa na gazeti hili ikilionyesha kaburi la marehemu Ballali, utaona wazi kabisa kuwa eneo hilo ni kaburi la marehemu Ballali pekee ndilo linaloonekana.
Swali:-
Kwa nini mwandishi huyu anayetuaminisha kwamba alifika eneo la kaburi, hakupiga Picha kubwa ambayo pia ingeyaonyesha makaburi mengine, kwa sababu tayari walikuwa eneo la makaburini, au hakuna Picha yoyote ya ukumbusho aliyochukua akiwa pamoja na wenyeji wake aliofika nao katika eneo hilo la makaburi, bila kumsahau mtunza makaburi aliyemwelekeza mahali kaburi lilipokuwa!

Haya ni maswali magumu sana ambayo ninaamini mwandishi huyu akiyaona, hatatamani ku-like au ku-comment kwenye post hii, bali atapita kwa speed ya ajabu.
Tatu, bila shaka ndugu wa marehemu ambao gazeti hili linadai ndio pekee waliohudhuria mazishi ya Ballali, watakuwa walirekodi tukio lote.
Swali:-
Kwa nini mwandishi wa gazeti hili hakuhangaika kuwatafuta hao ndugu wa marehemu Ballali waliohudhuria mazishi hayo ili wampe briefing ama more information kuhusiana na namna ambavyo mazishi yalifanyika!

Nne, mwandishi anadai kuwa pasipo na shaka, hilo ni kaburi la Ballali kwa mtizamo wa nje.
Swali:-
Mwandishi huyu anao uhakika au udhibitisho gani tofauti na huo muonekano wa nje wa kaburi la marehemu kwamba aliyezikwa pale ni yeye Ballali kweli!

Kwa sababu kitendo cha kulitazama tu kaburi kwa muonekano wa nje, hakiwezi kuwa na mashiko ya kufikia hatua ya kuuaminisha umma wa watanzania wenye nia na shauku kubwa ya kuujua undani wa utata wa kifo cha David Ballali kwamba kaburi hilo ni la kwake, kwa hili hata mtu mwenye uwezo mdogo wa kuchanganua mambo, ni lazima atapingana na wewe, manaake ni hoja dhaifu sana.
Kuna Critical thinkers, Great thinkers na wapo Poor thinkers, hivyo unapotoa habari kama hizi ambazo ni very sensitive kwa umma, utarajie kukihadaa kikundi kidogo sana cha watu.
Mhe.Msigwa aliwahi kusema, "Huu ni mfumo wa akili ndogo kujaribu kuitawala akili kubwa".
Tundu Antipus Lissu (Mb),
Singida Mashariki,
Tanzania.
13/07/2014.
***************
 
To be fair, huyu mwandishi ni budi afukuzwe kazi. Otherwise he/she must provide more evidence that will legitimize this story.
 
Kwa nnavyoijua bongo, hii habari very likely ina link na uchaguzi mkuu ujao. Stay tuned........

BTW toka lini Balali alianza kuitwa Ballali, just asking, au ndiyo yale yale ya Martin kuitwa Martine (Kuna kipindi kalizuka sana haka katabia). Fanyeni hata research hata kwa google to kuhusu jina Balali.
 
huyu mwandishi kasafiri kwenda amerika kwa gharama za nani?ili amletee nani uthibitisho?kwa lengo gani?.ebu acheni umburura kutuona watz wote ni wa shule za kata!!

akimaliza kutoa hayo majibu akafatilie ,aliyemvamia kibanda absalom
 
Yaaaani hata Neville Meena nae anaweza kutuletea utumbo km huuuu? maana nahisi ni yeye kwasababu gazeti la siku moja kabla aliripoti kuhusu watananzania wanavyofanya utapeli na kufungwa jela kule marekani. kama atakuwa yeye basi kazi ipo.
 
Kuna WanaJF wanauwezo wa kutengeneza hiyo picha kama ilivyo.
 
Binafsi sioni uhusiano wa Picha, Kaburi na Jina balali. Je ni kweli hili ni eneo la Makaburi? Perimeter ya picha hii haioneshi kaburi lingine lolote zaidi ya hili la Balali. Pia picha iliyotumika na mwandishi ni picha tuliyoizoea! Je hakuna picha nyingine aliyopiga akiwa Marekani? Je nikisema hilo kaburi limetengenezwa likapelekwa katika bustani likapigwa picha nitakuwa nimekosea? Maana tunaona kibao tu cha kaburi lakini sehemu ya chini haionekani vizuri
 
“Ni kweli nilishiriki kwenye maziko kwa sababu mimi kama Balozi wa Tanzania wakati huo ndiye nilikuwa mwakilishi wa Serikali pale Washington, lakini jambo la pili ni kwamba binafsi nilimfahamu Ballali kwa muda mrefu, kwa hiyo hata kama nisingekuwa balozi lazima ningekwenda kuzika tu.” Balozi Ombeni Sefue
sefue.jpg
 
Makaburi ya America tunayajua yalivyo. Hakuna kaburi america pana kama linavyoonyeshwa hapa. Je, tangu Balalli afe hiyo sehemu wameacha kuzika? Ninauliza kwa sababu hapo linaonekana kaburi moja tu! This journalist is so ignorant that he doesn't even know how to cheat intelligently. Kajipange upya uje na better story!
Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania BOT), Marehemu Daudi Ballali aliacha wasia unaotaka maiti yake isionyeshwe hadharani atakapofariki dunia na wala maiti yake isiletwe Tanzania kwa ajili ya maziko.
 
Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania BOT), Marehemu Daudi Ballali aliacha wasia unaotaka maiti yake isionyeshwe hadharani atakapofariki dunia na wala maiti yake isiletwe Tanzania kwa ajili ya maziko. Ballali aliyefariki Mei 16, 2008 na kuzikwa Mei 23 mwaka huohuo katika makaburi ya Gate of Heaven, eneo la Silver Spring, Maryland nchini Marekani alifahamu kuhusu kifo chake wiki mbili kabla, baada ya matibabu kushindikana.

Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa nchini Marekani kwa siku kumi kufuatilia suala hilo, alibaini kuwa kiongozi huyo alilazwa mara ya pili katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha George Washington, April 2008 na alirejea nyumbani kwake, Washington DC wiki mbili kabla ya kukutwa na mauti.

Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema baada ya madaktari kushindwa kumtibu walimwambia kwamba asingeweza kuishi kwa zaidi ya wiki mbili, hivyo walimshauri ahamie kwenye ‘hospice' ambayo ni nyumba maalumu ya kusubiri kifo kwa watu ambao magonjwa yao yameshindikana.

Hospice hutumika kwa ajili ya kuwaweka wagonjwa wanaohitaji faraja hasa kutoka na maumivu makali chini ya uangalizi wa washauri na wauguzi kwa lengo la kuwaongezea wagonjwa husika siku za kuishi.

Baadhi ya hospice hutoa huduma za kiroho, kijamii na kifedha na wakati mwingine huduma hizo hutolewa kwa wagonjwa ambao wanaugulia nyumbani. Hata hivyo, gazeti hili lilidokezwa kwamba Ballali alikataa kwenda kwenye nyumba hiyo na badala yake kutaka apelekwe nyumbani kwake.

"Alikataa kwenda kwenye hospice, aliwaambia madaktari kwamba yeye hawezi kwenda huko ijapokuwa kuna huduma nzuri na uangalizi wa nesi (muuguzi). Aliwaambia kwamba nitakwenda kufia nyumbani kwangu maana nina nyumbani kwangu," kilisema chanzo chetu na kuongeza:

"Aliporejeshwa nyumbani, alikuwa anazungumza kama kawaida lakini kadri siku zilivyosogea hali ilikuwa ikibadilika na kama sikosei siku mbili au tatu za mwisho (za uhai wake) alikuwa anajitambua lakini alikata kauli, hakuwa akizungumza chochote".

Uchunguzi wetu umebaini kuwa katika siku hizo za mwisho za uhai wake, Ballali aliacha maelekezo kwamba pindi atakapofariki dunia, mwili wake usiwekwe hadharani kwa maana ya kutazamwa na watu nje ya familia wala kusafirishwa kuja Tanzania kwa ajili ya maziko.

"He said, he doesn't like to be turned into a laughing staff (alisema asingependa kugeuzwa kichekesho), sababu watu wasingekuja kutoa heshima za mwisho, bali wangekuja kumdhihaki kuangalia Ballali aliyetuhumiwa kwa ufisadi wa EPA na siyo Gavana," kilisema chanzo hicho.



Kifo, mazishi yake

Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema Ballali alifariki Mei 16, 2008 saa 8:00 mchana saa za Marekani, sawa na saa 03:00 za Tanzania akiwa nyumbani kwake, Maryland.

Baada ya kifo chake, mwili wake ulihifadhiwa kwenye nyumba ya maiti iitwayo Vol Funeral Home iliyopo Washington DC kwa siku nne na siku ya tano Mei 23 uliondolewa na kupelekwa Kanisani kwa ajili ya Ibada kisha kupelekwa makaburini kwa ajili ya maziko.

Siku hiyo ya Mei 23 saa nne asubuhi, familia ya Ballali ikiongozwa na mjane wake Anna Muganda pamoja na watoto wake wawili, mtalaka wake na wanafamilia wengine, walikwenda Vol Funeral Home ambako walitoa heshima za mwisho kwa marehemu.

"Katika tukio hilo familia ilikubaliana kwamba matakwa ya marehemu yaheshimiwe, kwa hiyo hakuna aliyeruhusiwa kupiga picha zozote. Kwa hiyo ni ndugu tu wa familia walioruhusiwa kuona mwili wa Ballali, baadaye tulifunga casket (jeneza) na tukaondoka kwenda Kanisani,"kilisema chanzo chetu nchini Marekani.

Kauli hiyo inaungwa mkono na maelezo yaliyotolewa kwa gazeti hili Agosti 25, 2013 na dada wa Marehemu Ballali, Margaret Mpango kwamba shughuli za kuaga mwili wa marehemu, ibada na baadaye maziko vilikuwa ni kwa ajili ya familia pekee.

Akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, nyumbani kwake mjini Kigoma, Margaret Mpango aliweka bayana kwamba: "Familia isingeweza kuruhusu watu wengine kushiriki, haikuwa na maana yoyote kwani tayari kulikuwa na maneno mengi yanayomhusu".

Dada huyo anayezaliwa tumbo moja na Marehemu Ballali ni mke wa Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kasulu, Kigoma, Dk. Gerald Mpango ambaye alikuwa miongoni mwa walioongoza Ibada ya maziko ya Ballali.

Margaret alilithibitishia gazeti hili kwamba mumewe (Dk. Mpango), alishirikiana na mapadre wa Kanisa la Mtakatifu Stephen, Washington D.C. kuongoza ibada ya mwisho ya Ballali ambaye siku hiyohiyo alizikwa katika makaburi yanayomilikiwa na Kanisa Katoliki ya Gate of Heaven.

Alisema miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani wakati huo, Balozi Ombeni Sefue, ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi.



Kauli ya Sefue

Jana Balozi Sefue akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, alithibitisha kwamba kweli alishiriki kwenye Ibada ya kumuaga Ballali na baadaye kwenye maziko ya Gavana huyo katika makaburi ya Gate of Heaven.

"Ni kweli nilishiriki kwenye maziko kwa sababu mimi kama Balozi wa Tanzania wakati huo ndiye nilikuwa mwakilishi wa Serikali pale Washington, lakini jambo la pili ni kwamba binafsi nilimfahamu Ballali kwa muda mrefu, kwa hiyo hata kama nisingekuwa balozi lazima ningekwenda kuzika tu," alisema Balozi huyo.



Picha zake zasakwa

Taarifa zaidi ambazo gazeti hili lilizipata Washington DC, zinasema kulikuwa na jitihada za kutaka kupiga picha mwili wa marehemu wakati wa kutoa heshima za mwisho, lakini zilikwama baada ya ndugu wa marehemu kuzima jaribio hilo.

"Mmoja wa waliokuwapo kwenye msiba baada sisi kumaliza kutoa heshima za mwisho alitaka kupiga picha kwa madai kwamba anataka kubaki na sura ya ndugu yetu, lakini tulikataa na kumwambia kwamba tulishakubaliana kutofanya hivyo kwa heshima ya marehemu," kilieleza chanzo chetu na kuongeza:

"Baadaye tulipata taarifa kwamba wapo watu tena kutoka Tanzania ambao walikuwa wakihitaji picha hiyo kwa udi na uvumba na walikuwa wameahidi kuinunua kwa Dola za Marekani 35,000". Kiasi hicho ni sawa na Sh57.7 milioni kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni wastani wa Sh1650 kwa dola moja.



Safari ya Marekani

Safari ya Mwandishi wa Mwananchi nchini Marekani ilianza Alhamisi Juni 26, 2014 hadi Jumapili, Julai 6. Mwandishi wa habari hizi aliligundua kaburi hilo baada ya kwenda makaburi ya Gate of Heaven kwa siku tatu mfululizo.

Siku ya kwanza, mwenyeji wa mwandishi ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa alimfikisha katika makaburi hayo, lakini kaburi la Ballali halikuonekana na hata mwandishi alipokwenda siku ya pili peke yake, kaburi hilo pia halikuonekana kwa kutokana na ukubwa wa eneo hilo.

Siku ya tatu, Mwandishi wa Mwananchi alilazimika kuomba msaada wa Ofisi ya Makaburi ya Gate of Heaven, ambayo ilimsaidia kuonyesha eneo lilipo kaburi hilo, hivyo kuwezesha kupata picha zake.

Kaburi lake liko katika msitari wa mwisho kabisa na Ukanda wa Kijani wa miti iliyozunguka makaburi ya Gate of Heaven, likiwa limeandikwa jina la kiongozi huyo, pamoja na maneno ya Kiingereza yanayosomeka "When the heart weep for what it has lost, the soul rejoices for what it has found".

Maana ya maneno hayo ni kwamba, "Wakati moyo ukiomboleza kwa kile kilichopotea, roho hufurahi kwa kile kilichopatikana". Kaburi hili limezungukwa na makaburi mengine kadhaa ambayo si ya Watanzania, kwani kwa haraka kutokana na mazingira yalivyokuwa, Mwandishi wa Mwananchi hakuweza kuona kaburi jingine lenye majina yenye asili au kuwa na mwelekeo wa asili ya Tanzania.

Fuatilia mfululizo wa habari hii itakapoendelea kesho.
 
Watanzania wengi tunahitaji kuamka.. CCM ilipotufikisha imetosha...
Tutakuja kuulizwa na watoto wetu na wajukuu zetu..tulikuwa tunafanya nini..?
Mtu ameiba billions..na yeye Balali ni mhusika mkuu..akisaidiana na viongozi wakubwa sana ndani ya serikali..eti ameenda Marekani na kufia huko..na kuzikwa kimya kimya.. Hivi hii inaingia akilini..?

CCM walipotufikisha basi..deni la taifa kila siku linaongezeka.. sasa hivi tuna Escrow..

Na bado movies
 
Back
Top Bottom