SEHEMU YA 23
“Mama.” Azra aliitika akiupamba uso wake kwa tabasamu.
“Bila shaka mgao wetu upo pia kwenye hiyo sinia,” Mama Cecilia alitania.
“Chakula ni kwa ajili ya kila mmoja wetu.”
Baada ya kujibu, watu wote, yaani Azra, mama Cecilia na Jemima, kwa sekunde kadhaa walibakia wakitabasamu mpaka midomo yao ilipofunga mfano wa mwanga wa jua unavyopotea majira ya jioni huko magharibi.
Baada ya hapo, wawili hao, mama na mwana waliendelea kumsindikiza kwa macho Azra, aliyeanza kugawa chakula kwa wagonjwa.
Toka siku hiyo Azra alianza kujenga ukaribu na wawili hao, ambapo kila siku ya jumatatu mama Cecilia na Jemima walipokuwa wakifika gerezani hapo Azra alifanya juu chini kuonana na Jemima kwa siri na kuzungumza naye mawili matatu.
Baada ya mazungumzo ya mara kwa mara, siku moja Azra aliamua kuvunja yai kwa kumwambia Jemima kwamba alikuwa na asili ya Swadege ya Rwadege na Marekani, jambo ambalo Jemima hakulitegemea na kuliamini.
Hata hivyo, baada ya Azra kumuonesha Jemima, alama kifuani kwake ya tobo lililochongwa kwa mfano wa ndege aina ya tai, ambayo ndiyo ilikuwa alama ya utambulisho wa Waswadege wote kama ilivyo alama ya chanjo ya ndui kwa ‘Wabongo’, msichana huyo alimuamini.
Machozi yakambubujika hasa aliposikiliza historia ya Azra aliyomsimulia juu ya mababu zake kupelekwa Marekani kama watumwa.
Zaidi, Azra alimsimulia mambo mengi, mengine ya uongo ilimradi kuikamilisha simulizi iliyoleta maana kwa Jemima, kwamba ndiyo ilikuwa sababu ya kumfikisha kwenye gereza hilo.
“Pole sana kaka,” Jemima alimwambia Azra huku akifuta machozi.
“Asante.” Azra alijibu. “Natamani niikanyage ardhi ya nyumbani, nifahamu kuhusu hali ya hewa na uoto wa asili.
“Baba yangu aliwahi kuniambia jua la
nyumbani ni zawadi nzuri ya kujivunia ambayo Mungu alitubariki, kwamba Swadege ni mfano wa gadeni ya Hedeni, nyumbani hakuna ugonjwa wala uzee, kuna maisha yenye uhai usio na kikomo kwani hata wafu huishi pamoja na walio hai.” “Ni kweli kabisa, lakini yakupasa kuwa mvumilivu kidogo.” Jemima alimwambia.