SoC02 Mwanga halisi wa mafanikio

Stories of Change - 2022 Competition

amranik

Member
Sep 13, 2019
17
15
Kutokana na maendeleo ya dunia ya leo ya sayansi na teknolojia vijana wengi wanatamani kupata mafanikio ya haraka pasipo kufanya kazi kwa bidii hii hupelekea ongezeko kubwa la vijana kutegemea michezo ya kubashiri maarufu kama kubet na wengine kujiingiza katika vitendo vya kihalifu ili kuweza kujipatia fedha kila uchao.

Dimbwi kubwa la vijana wamesahau kufanya kazi kwa bidii kuwa ndio msingi wa mafanikio na kugeuzia macho mafanikio yao yategemee bahati. Vijana wanaongojea bahati hupeteza muda mwingi wakibashiri michezo mbalimbali na kusubiri kwa matumaini lakini matumaini yao kamwe huwa ni ya muda mfupi na hawafanikiwi na kama ikitokea kufanikiwa ni mmoja kati ya laki moja.

Na hii inadumaza fikra na uwezo wa kujiamini kwa vijana katika kufanikiwa kwa kufanya kazi kwa bidii.
Wapo watu wanaamini katika bahati, wanaamini kwamba kuna wakati mafanikio ni bahati ya mtu. La, hii si kweli. Ukweli ni kwamba jinsi unavyozidi kufanya kazi kwa bidii ndio jinsi unavyosogea kwenye uelekeo wa bahati yako. Kama alivyowahi kusema Colin Powel “ ..ndoto haiweza kuwa kwenye uhalisia kwa miujiza, inahitaji jasho, malengo na kazi kwa bidii".

Siku zote mafanikio yanategemea malengo na kazi kwa bidii kwasababu kazi kwa bidii bila malengo ni sawa na jengo bila lango. Ni vipi utaingia katika nyumba uliyoijenga na hali ya kuwa haina mlango? Na ni vipi utafanikiwa kwa kufanya kazi kwa bidii bila kujiwekea malengo, yaani lango la mafanikio? Hii ni dhahiri kuwa kazi kwa bidii ni malengo tendwa katika wakati sahihi na ni moja ya onyesho la malengo yako uliyojiwekea.

Kazi kwa bidii inahusisha maamuzi sahihi katika wakati sahihi, na tofauti kubwa kati ya kufanikiwa na kutofanikiwa ni uchukuaji maamuzi. Maamuzi yako, mafanikio yako au kufeli kwako. Kwa mfano vijana wawili wenye mtaji sawa wameamua kufanya biashara tofauti na kila mmoja akitarajia faida lakini mwisho wa siku mmoja akafanikiwa na mwingine akashindwa kufanikiwa, hayo ni matokeo ya utofauti wa uchukuaji maamuzi na mawazo sahihi kwa wakati.

Aliyefanikiwa alichukua maamuzi sahihi baada ya kuona fursa sahihi lakini kijana asiyefanikiwa alikuwa na lengo la kufanikiwa lakini alishindwa kuamua wazo bora la kuja nalo ili afanikiwe. Hivyo basi kazi kwa bidii ina ambatana na utashi wa uchaguzi wa maamuzi ni kivipi uendee njia yako ya mafanikio.

Vilevile kazi kwa bidii inaambtana sambamba na ufanyaji wa tafiti kabla na baada ya kuendea jambo. Kwa kijana mwenye hamu na kiu ya mafanikio katika dunia hii ya teknolojia anahitaji kujua jambo kabla ya kuwekeza nguvu zake katika haja ya kulikamilisha jambo hilo. Hakika kuna msemo maarufu wa kigeni unaosema “ no research, no right to speak" ikiwa na maana ya kushinikiza watu kufanya uchunguzi wa jambo kwa kina kabla ya kuliongea au kulifanya. Kwa wale vijana ambao wanafanya kazi kwa bidii kwenye mambo ambayo hawajayachunguza vizur hakika mwisho wake ni kupoteza nguvu na muda. Tuamke vijana.

Itakuwa ni vizuri kama mashirika ya umma yatajitolea kwa vijana kuwasaidia kuwapa mchanganuao wa mawazo yao kabla hawajawekeza nguvu zao katika biashara au kazi wanazo tarajia kuzifanya ili wafanikiwe. Hii inaweza kufanyika kwa kutumia watu wenye utashi wa kufanya tafiti katika eneo husika. Kwa mfano kijana akitaka kulima katika eneo fulani atapewa ushauri afanye kilimo eneo la ukubwa gani kutokana na mtaji wake, ataelekezwa apande mazao gani kutoka na eneo na ataambiwa atumie mbegu gani na mbolea gani kutokana na udongo wa shamba lake.

Na huduma itolewa bila malipo ili kuwapa vijana ari ya kufanya utafiti kwakuwa ushauri upo na ni bure wakati wowote watakapo hitaji.

Na kwa wale vijana wanaofanya kazi kwa kufuata msafara wa mamba, hakika nawakumbusha kwenye wengi kuna mengi na kwenye msafara wa mamba na kenge wapo na siku zote dunia sio mbaya ila walimwengu kamwa hawana huruma wala chembe ya aibu. Ni mara ngapi vijana wanawekeza pesa walizozipata kwa shida na kuzipoteza kwenye makampuni kama QNET, Muller, SCATEC au IDEA DEBATOR. Hii inaitwa kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata mkumbo na hii ni changamoto inayowakumba dimbwi kubwa la vijana waliopo vyuoni na wale waliomaliza vyuo na hata baadhi ya wafanyakazi wa mashirika mbalimbali.

Ipo haja sasa ya serikali kushirikiana pamoja na mashirika binafsi pamoja na wadau mbalimbali kuweza kutoa elimu kwa wananchi wa kawaida kuhusu uwekezaji wa kimtandao ili kuweza kufichua dhana ovu zinazoletwa ili kudhulumu mali za vijana wanaopenda mafanikio. Vijana wapewe elimu kupitia mitandao ya kijamii, makongamano ya vijana na katika vyombo vya habari ili kuweza kuwapa uwezo vijana wa kufanya uchunguzi sahihi kabla ya kuamini uwekezaji wake katika kampuni yoyote, iwe ya kimtandao au vinginevyo.

Na ingekuwa bora zaidi kama serikali ingeweka kozi maalumu vyuoni itakayo fundishwa biashara za mtandaoni ili kuongeza wigo mpana wa fursa kwa vijana wengi waliopo mtaani, hii ni kwasababu dunia ya sasa ni ya teknolojia na biashara za mtandaoni haziepukiki na kama serikali itaziepuka basi wananchi wengi watapoteza mali zao kwa kuwekeza sehemu ambazo si sahihi. Lakini je ni vipi tutazifanya biashara hizo hali yakuwa hatuna elimu nazo? Hivyo basi elimu kuhusu fedha na biashara za mtandao ni muhimu.

Vijana kumbukeni elimu ni muhimu na mwenye elimu hueshimiwa. Hapa sizungumzii elimu ya darsani bail elimu ya kuendea mafanikio na kukufanya uongeze bidii na juhudi katika kazi zako za kila siku. Kama wahenga walivyosema sema ‘kijana anaweza kutembea haraka lakini mzee ndio anajua njia’ hivyo basi kama kijana unatakiwa ukubali kujifunza kutoka kwa waliokuzidi elimu, uzoefu au umri. Kwa hakika biashara au kazi yoyote inaamza na elimu ndogo na uzoefu mdogo na baadae elimu inakuwa kubwa na uzoefu mkubwa na ndio wakati wa kuvuna mafanikio yako yaliyotokana na kufanya kazi kwa bidii.

Taarifa mbaya ni kwmba muda unapaa kwa kasi, na taarifa nzuri ni kwamba wewe kijana ndio rubani. Kila siku weka uso wako jua linapotoka na kivuli kitakuja nyuma yako, kamwe usichelee kufanya maamuzi pale unapoona fursa na maamuzi yako lazima yawe kwaajili ya kupata faida na wala sio kwa ajili ya kufuata mkumbo itakuwa ndio wale msafara wa mamba na kenge wapo. Kumbuka bado upo wakati wa kuweka malengo mapya na kuwa na ndoto mpya. Hujachelewa chukua hatua hatua.
PESA, NYUMBA NA MAGARI NI VITU VYA KUPITA LAKINI NI BORA VIPITIE KWAKO.

Mwandishi: CHALI
0718167997
 
Back
Top Bottom