*
Mwanasheria Mkuu ajitosa
?
Oktoba 13, 2010
?
Mwandishi Wetu
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, wameshitakiwa wakidaiwa kufanya uchochezi kwa kutoa kauli za kuishutumu Serikali kuhusika kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM), Raia Mwema, limebaini.
Habari zilizothibitishwa na CHADEMA zimeeleza kwamba, Dk. Slaa na Mbowe wameshitakiwa kwenye Kamati ya Maadili ya Taifa, chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakidaiwa kutoa kauli zinazoitwa za uongo kwa nia ya kusababisha chuki dhidi ya serikali.
Mwenyekiti wa Kampeni za CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu, amelithibitishia Raia Mwema kwamba tayari wanasheria wa chama hicho wanalifanyia kazi suala hilo kabla ya kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwa viongozi hao.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza hoja zilizotumiwa na Serikali kuwashitaki viongozi hao wa CHADEMA ni viongozi wao kutoa lugha za uzushi, uongo na zenye mwelekeo wa kuchochea chuki dhidi ya Serikali na Taifa.
Viongozi hao wanatuhumiwa kutoa kauli hizo za uchochezi katika mkutano wao na vyombo vya habari katika ofisi za CHADEMA, Kinondoni Septemba 28, mwaka huu na kuripotiwa na vyombo vya habari.
Tuhuma ambazo zinaelezwa kutolewa na Dk. Slaa na Mbowe na ambazo Serikali imezieleza kwamba ni za uongo na zenye kuhatarisha amani ni pamoja na madai kwamba Serikali imewatuma na kuwasambaza nchi nzima maofisa wa Usalama wa Taifa ili kuhakikisha kuwa mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete anashinda.
Katika maelezo yao viongozi hao wa CHADEMA walidai kwamba wanao waraka waliodai kuwa umeandikwa na Serikali na kupelekwa kwa Wakuu wa Usalama wa Taifa wa Mikoa yote, Wakuu wa Mikoa yote, Wakuu wa wilaya zote na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya zote nchini wakielekezwa kuhakikisha CCM inashinda kwa gharama zozote.
Tuhuma nyingine ambazo zimeelekezwa kwa Serikali zilizoripotiwa na vyombo vya habari ni kwamba Serikali imetuma maofisa wake nje ya nchi kuchapisha karatasi za kupigia kura ambazo ni nje ya zile zilizoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Katika maelezo yake Serikali imekanusha tuhuma hizo ikisema kwamba hazina ukweli wowote na viongozi wa chama hicho wanatakiwa kutoa uthibitisho (kama kweli wanao) la sivyo hatua stahili zichukuliwe dhidi yao.
Akizungumzia mashitaka hayo ya Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema wiki hii hakutaka kwenda katika undani akisema ni busara zaidi kuacha mamlaka zilizoandikiwa barua hiyo kutimiza wajibu wake.
Katika mazungumzo hayo Jaji Werema alisema; Ni vizuri ukawauliza vyombo vilivyofikishiwa hayo malalamiko. Mimi na wewe (mwandishi) lengo letu ni kuendelea kuwa na nia nzuri na nchi yetu. Natumaini hata Watanzania karibu wote wana nia hiyo. Kwa hiyo kama malalamiko yamewasilishwa naamini wahusika watapewa fursa ya kujibu.
Uchunguzi zaidi unabainisha kuwa barua ya mashitaka hayo iliandikwa Septemba 30, mwaka huu na ikawasilishwa Tume Oktoba mosi, mwaka huu.
Hata hivyo, licha ya barua hiyo kufikishwa tume Oktoba mosi, ilichukua siku takriban saba kuifikisha kamati ya maadili.
Inadaiwa kuwa barua hiyo ilifikishwa hapo Oktoba 8, mwaka huu na baadhi ya wajumbe wamekuwa wakihoji sababu za kukwama au kukwamishwa barua hiyo kufika sehemu iliyokusudiwa kwa wiki nzima.
Kwa mujibu wa kanuni za kamati hiyo ya maadili mtu au chama kinachotuhumiwa au kulalamikiwa kinapaswa kuandikiwa barua rasmi na kutakiwa kutoa majibu ndani ya saa 48.
Raia Mwema ilizungumza pia na Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, ambaye pia ni mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho Jimbo la Ubungo, ambaye alisema bado chama chake hakijafikishwa rasmi malalamiko husika.
Kanuni zinataka anayelalamikiwa kuletewa malalamiko hayo rasmi na kuyajibu ndani ya saa 48. Kama hayo malalamiko yapo hayajatufikia rasmi kama taasisi. Ni kweli tunaye mjumbe wetu kama ilivyo vyama vingine kwenye kamati hiyo lakini huyu siye anayelalamikiwa.
Wanaostahili kufikishiwa malalamiko ni wahusika moja kwa moja au chama kama ndicho kinalalamikiwa. Hata hivyo, binafsi kwa niaba ya chama nimechukua hatua za tahadhari, nimeandikia barua kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujua rasmi masuala haya.
Kama kweli watatuandikia kulalamika basi nasi tuko tayari kujibu kwa mujibu wa kanuni. Na hapa ukweli ni kwamba hiki wanachozungumza kinafanyika na kutolewa matamko baada ya kufanyika upotoshaji wa makusudi.
Yaani watu wamekaa wakafanya upotoshaji, na matamko yakatolewa juu ya msingi wa upotoshaji. Ukweli ni kwamba, watu wanahangaika kufanyia kazi upotoshaji wa makusudi, alisema Mnyika.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rajabu Kiravu, naye alishindwa kuzungumzia suala hili akieleza kuwapo katika kikao.
Tathmini ya hivi karibuni ya kampeni za Uchaguzi Mkuu zinabainisha kuwa CHADEMA kwa sasa ndicho chama kinachoonekana kutoa changamoto kubwa ya kisiasa dhidi ya chama tawala-CCM, ikielezwa kuwa mgombea wake, Dk. Willibrod Slaa ndiye kinara wa changamoto hizo.
Source:
Raia Mwema - Muungwana ni Vitendo, Mwanasheria Mkuu ajitosa
?