MWANASESERE

MWANASESERE

Robert Heriel Mtibeli

Platinum Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
40,303
Reaction score
93,341
MWANASESERE

Na, Robert Heriel

Ilikuwa ni zawadi nzuri kutoka nchi za barafu. Zawadi iliyotengenezwa kwa ufundi na teknolojia ya hali ya juu. Mvuto wake uliwasogeza watoto wa nyumba ile karibu ili waweze kuona kile mama alichowaletea nyumbani. Zawadi ya Mwanasesere mtanashati kutoka nchi za mbali zenye baridi kali.

Mama alimuweka kabatini sehemu inayoonekana kwa kila atakayeingia katika sebule hiyo. Uwepo wa Mwanasesere sebuleni pale uliifanya sebule izidi kupendeza. Mama alitoa maagizo na kuwakanya watoto wasije wakaenda kumtoa mwanasesere pale kabatini wala kumchezea.

Ilikuwa ni amri ngumu kwa watoto kwani kila mmoja alikuwa anayohamu ya kutaka kumchezea Mwanasesere mwenye mvuto wa maarifa. Mtoto mmoja utii ulimshinda, naam uvumilivu uliubwaga moyo wake na kuenda kuuchezea ule mdoli ambaye Mama alisema usichezewe.

Alianza kuuchezea mdomo wake ambao aliufungua na kukuta meno matatu marefu. Meno ya mwanasesere yaliyochongoka kama meno ya paka.
"unamacho mazuri"
Mtoto alisema.
Ukaguzi uliendelea hadi mtoto aliporidhika.
"hivi kwa nini huongei?"
mtoto aliuuliza
"Naongea!"
Mwanasesere alijibu na kumfanya mtoto autupe chini kwa kuogopa. Mtoto hakutegemea kusikia jibu hilo kwani hakuwahi kuona wala kusikia kuwa mwanasesere anaongea.
Huu ulitosha kuitwa muujiza kwake. Hofu ilimuingia. Mashaka vilimpiga kikumbo akatoka mbio huku akipiga makelele kama mtu aliyepagawa.
Mama alishangaa kumuona Mwanaye akimkimbilia huku akipiga makelele. Mama aliacha kumenya viazi na kumkumbatia mwanaye.
"kuna nini mwanangu?"
Mama aliuliza akiwa kamkumbatia mwanaye.
"Huko ndani mama"
"ndani?"
"Nenda ukajionee mwenyewe"
"Nikajionee!"
"Ndio Mama"
"nini sasa si useme tu mwanangu mbona sikuelewi"
"Mwanasesere"
"Mwanasesere kafanya nini?"
"Nenda ukamuulize huko ndani"
"wewe umechanganyikiwa!"
"sijachanganyikiwa Mama. Wewe nenda tuu huko ndani ukajionee"
Mama alimuachia mwanaye na kuondoka kwenda ndani. Aliangalia kabatini alipo Mwanasesere lakini hakuona kitu chochote. Aliangaza macho huku na huku kutafuta lakini Mwanasesere hakuonekana katika mboni ya macho yake. Wasi wasi ndio jibu kwa aliyechangayikiwa ndivyo ilivyokuwa kwa Mama mwenye nyumba. Wapi alipo Mwanasesere hakuna aliyekuwa anajua.

Mtoto akasimulia yaliyotokea, masikio yao hayakuamini mpaka usiku ulipofika. Usiku wa Mwanasesere mwenye ulimi laini wa kudanganyia watu. Ulimi wa kufitinisha familia na kuifanya ivunjike. Usiku ambapo nyota zilipotea angani. Loooh ajabu kubwa.

Wakiwa wamelala sauti ilisikika sebuleni ikisema:
"Afrika! Afrika! Nimekufukia shimoni"
Wakwanza kuisikia sauti hiyo alikuwa yule yule mtoto ambaye alikutana na dhahama mchana, Wengine wote bado walikuwa katika usingizi bila ya kujua hatari inayowakabili. Baba alikuwa katika ndoto za kujenga viwanda vikubwa, wakati mama akiwa katika njozi za urembo. Mtoto pekee ndiye aliyekuwa macho akisumbuliwa na sauti ya Mwanasesere inayosikia kutoka sebuleni.

Mtoto alivuta pumzi haraka haraka kwa hofu baada ya kusikia sauti ya kitu kinachokuja kutoka sebuleni. Moja kwa moja alihisi kuwa anayekuja alikuwa ni Mwanasesere.
Mtoto alikuwa akilala peke yake katika chumba tofauti na wazazi wake. Hii ndio ilikuwa kitanzi kwa mtoto wa watu asiye na hatia. Kitasa cha mlango kilishikwa na macho yote ya mtoto yalikuwa mlangoni yakiangalia nini kinaenda kutokea. Alijilaumu kwa nini hakufunga mlango na funguo lakini mbona ndio ilikuwa kawaida yake.

Mlango ukafunguka taratibu mpaka ulipofika nusu kisha hakuna yeyote aliyejitokeza na ukimya ukatokea. Mtoto alipikicha macho kwani alihisi kama yupo katika ndoto mbaya ya jinamizi. Ukimya ulioshabihizwa na sauti za mbu kwa mbali ndio vilikuwa vikipiga ngoma ya masikio ya mtoto. Kichwani alikuwa na mjadala mkubwa kuwa ashuke au asishuke kwenda mlangoni kuangalia kama kuna yeyote. Akili moja ilimumbia amuite Mama, hapo hapo akili nyingine ikamuambia asiite.

Alishuka kitandani akaanza kutembea taratibu kwa kunyata kama paka amuwindaye panya. Moyo wake ulikuwa unadunda haswa mithili ya panya aliyekoswa koswa na mtego. Hakujua hatari gani inaweza kumpata. Alifika Mlangoni bila kuona kitu chochote akajaribu kuchungulia sebuleni lakini hakuona kitu na ukimya ulizidi kidogo kwani hata sauti za mbu zilizokuwa zikisikika mwanzo muda huu hazikusikika kabisa. Alishusha pumzi kama kobe mzee akaegemea ukuta.
" ninaota au nini kinaendelea kichwani mwangu?"
Mtoto alijiuliza na hakupa majibu. Alijiona kama mtu anayeenda kuchanganyikiwa.
Ghafla sauti ya luninga sebuleni ilisikia na kumfanya ashtuke na hofu kuurarua moyo wake.
Alijiuliza ni nani aliyekuwa sebuleni lakini hakupata majibu. Chakushangaza ni kuwa pamoja na sauti kubwa ya luninga lakini haikufua dafu kwa usingizi uliowafunika wazazi wake. Walikuwa wamelala fofofo.

Taratibu alipiga hatua kuelekea sebuleni kuona aliyekuwa sebuleni na anayeongea kwenye luninga. Hakuamini alichokiona. Alishangaa kumuona Mwanasesere akizungumza luningani.
Alikimbia haraka kwenda chumbani huku akipiga makelele. Alifunguaa mlango akaingia chumbani akiwa anatweta. Sasa aliamua kwenda kulala lakini alishtushwa kuona mtu kalala kitandani akiwa kajifunika gubi gubi na shuka.
Miguu ilipoteza nguvu, Mapigo ya moyo yaliamia kwenye ini, damu ilikuwa ikikimbia kwa kasi huku jasho jepesi la pua likichirizika. Nani aliyelala kitandani mwake hakuna aliyekuwa akijua japo akili yake ilijua kuwa atakuwa Mwanasesere.

Kama ni ujasiri basi mtoto huyu alikuwa ni jasiri. Taratibu kwa hatua za kujihami alikisogelea kitanda. Sasa alikuwa amefika kitandani akiwa anatetemeka meno kwa woga. Alipeleka mikono yake kwa hadhari kuona aliyelala katika kitanda chake. Alishika shuka taratibu mara mlango ukajifunga paaaa! hali iliyomfanya ageuke upesi kuangalia mlangoni. Hakuona kitu zaidi ya mlango uliokuwa tayari umejifunga. Alivyogeuka kitandani alishtushwa kwa alichokiona.

Nini alichokiona mtoto?
Robert Heriel
0693322300
Mtunzi na muongozaji wa filamu
 
Mwanasesere
sehemu ya 2

Movie inaanza na trela ya matukio yaliyopita katika sehemu ya kwanza yanaonekana katika luninga. Watazamaji wakiwa na msisimko wa kipekee wanasubiri kwa hamu nini kinachoenda kutokea katika sehemu ya pili. kwenye kioo cha luninga linaonekana jicho linalotisha la Mwanasesere na hapo hapo luninga inazima huku mlio wa kutisha ukisikika kwenye spika. Hofu inaonekana dhahiri kwenye macho ya watazamaji, vifua vyao vinapanda na kushuka kutokana na mapigo ya moyo yanayodunda kwa wasi wasi.

(Movie inaendelea na sauti ya kutisha katika luninga inazidi kuleta msisimko kwa watazamaji).

Mtoto alishika shuka taratibu ili kumfunua yule aliyekuwa amelala kitandani mwake. Alipokuwa akifungua mara mlango ulijifunga kwa kujibamiza kwa nguvu na kumfanya ageuke nyuma kwa kushtuka kuelekea kule mlangoni. Alikuta tayari mlango ulikuwa umeshajifunga. Alishusha pumzi kama bata dume. Alikuwa na haki ya kushusha pumzi kwani eneo lile lilikuwa ni mfano wa njia ya kuelekea kuzimu kwa muda huo.

sasa aligeuka kitandani tena kuendelea na zoezi la kumfunua yule aliyekuwa amelala kitandani lakini alishtuka kukuta hakuna mtu yeyote zaidi ya shuka lake na kitanda. Hakuweza kuamini macho yake. Alihisi anaenda kuchanganyikiwa. kama ni ndoto basi zake zilipaswa kuitwa ndoto za joka la mdimu. Joka lenye vichwa saba, lenye mikono na miguu huku vidole vyake vikiwa kama vya mwanadamu japo vina makucha marefu.

Aliangaza macho huku na huko chumbani kwake lakini alikuta chumba kipo vile vile kama kilivyokuwa.

Hizo ni harakati za Mwanasesere mjengoni. Kuchanganya vijana wajione wapo ndotoni. Kuwalewesha kwa mvinyo wa ukali wa vitisho vyake. Mwanasesere usimuweke nyumbani usije usiku ukaona mazingaombwe ukaishia kukesha kama mlinzi.

Mtoto akapanda kitandani, na hofu ikaanza kuyeyuka kama theluji wakati wa kiangazi kutokana na hali kuwa shwari kwa muda kidogo. Usingizi ukabisha hodi katika macho yake lakini kabla hajalala mara feni ya kwenye paa la nyumba ikaanza kuzunguka taratibu na kutoa mlio uliokikimbiza kimya kilichokuwepo mule chumbani hali iliyomfanya mtoto amke kutoka katika usingizi. Alishangaa kuona feni ikiwa inazunguka taratibu bila ya mtu kuiwasha. Aliangalia kwenye swichi kuona kama ipo on lakini chakushangaza aliiona imezimwa. Kama angekuwa mtafsiri wa filamu hii basi maneno ya kuchombeza ungeweza kuyasikia kama Achechee! au chunga sana! cheki maneno!.

Feni ilizidisha kasi ya kuzunguka na kufanya chumba chote kiwe na baridi. Baridi usiku wa manane. kama nilivyokwisha kusema Mwanasesere ni kutoka nchi za mbali, nchi za barafu zenye baridi kali hii ndio maana aliiwasha feni ili aweze kupata ubaridi angalau. Mtoto alizidi kuogopa, machozi yalikuwa yameshalowanisha mashavu yake. Masikini mtoto wa watu, usiku mzima ni kuhangaika wakati wazazi wamelala wanakoroma. Wanaota ndoto za mileniamu. Ndoto za kujenga biashara za soko huria wakati mtoto wao hajajiandaa kwa lolote. Mtoto ambaye hawezi kupambana na Mwanasesere. Loo! kazi kweli kweli.

Sasa mtoto alianza kuhisi baridi mara feni ikasimama kwa ghafla na ukimya ukatote huku mapzia na vitambaa vikiwa vinapepea kwa upepo uliokuwa umebakia.
Kimya kidogo kikapita mtoto akiwa ametulia akisubiri nini kinachofuata.

kwa mara ya pili alisikia sauti ya luninga sebuleni. Mtoto maswali ni mengi kupita majibu. Sasa alianza kukumbuka picha za kutisha alizowahi kuziona. Alijiona kama mhusika katika filamu za holiwood zenye kutisha mno. Aliamka kwenda mlangoni ili aweze kusikiliza.
Alisikia sauti ya mwanaume mmoja ambaye bila shaka alikuwa anamtambua. Mwanaume huyo alikuwa kiongozi fulani katika nchi yake. Maneno aliyoyasikia vizuri ya yule mwanaume kutoka katika luninga yalikuwa ni;
"tunahitaji misaada zaidi kutoka nchi za barafu kwa maana wahisani wa ndani hawatoshi."
Mtoto hakuelewa habari hizo na swali lililomsumbua lilikuwa ni zipi nchi za baraf. Yeye shuleni kwao hakufundishwa hivyo, alichofundishwa ni mabara na visiwa.

Alisikia mlango wa wazazi wake ukifunguliwa wakati luninga ikindelea kuongea. Mara sauti ya mama ilisikika sebuleni ikisema
"nani kawasha Tv?"
Aliuliza swali bila kupata majibu. Baba naye akatoka chumbani akimkuta mama akiwa anahangaika kuizima luninga ambayo ilikuwa imezimwa hivyo ni kusema hawezi kuizima kutokana na kuwa bado imezimwa lakini inaongea.
"Sijui ni nini hiki Mume wangu?"
"nani kawasha?"
"sijui nimeikuta inaongea hapa bila ya mtu yeyote"
"bila ya mtu!"
"Ndio. sasa kinachonichanganya ni kuwa siwezi kuizima kwani huku switchi ipo off. sasa nitaizimaje?"
"embu nione"
Baba mwenye nyumba aliende kwenye swichi kushuhudia maneno ya mke wake na kukuta kweli swichi imezimwa lakini luninga bado inaonyesha picha na kiongozi anayeongea.

Mtoto alitoka chumbani baada ya kusikia majadiliano ya wazazi wake.
"we ndio umewasha tv?"
baba aliuliza.
"atawashaje wakati tv inaonekana imezimwa mume wangu na wewe?"
mama alidakia na kukawa kimya kidogo wasijue nini cha kufanya.

Mara Mwanasesere akajitokeza ndani ya Luninga. Mama alishtuka kumuona Mwanasesere ndani ya Luninga. Mtoto naye alibaki ametumbua macho akiwa haamini anachokiona kwa mara hii mwanasesere alikuwa akimtizama huku tabasamu jepesi likiuvizia uso wake. Mbwa nje walianza kubweka hali iliyozua taharuki kwa kila mmoja. Bila shaka jambo la hatari linaenda kutokea. Nyuso zao zilionyesha kila dalili ya wasi wasi. Sio Mama sio Baba wote walishangazwa na mambo yale.

Wakiwa katika sintofahamu ghafla mlango wa sebuleni unafunguka lakini hakuna aliyekuwa anaingia. Punde Moshi mweusi kama wa tairi linalochomwa unaingia mlangoni na sauti ya paka ikifuatia. Mama alianguka akapoteza fahamu.



(movie inakatishwa na maandishi yanapanda yakifuatiwa na ala ya kusisimua na mwishowe yanatokea maandishi yanayosomeka "WATCHOUT PART 3". Kisha vipande vifupi fupi vya part 3 vinaonyeshwa kisha movie inameisha)

Watazamaji wamebaki wamekodoa macho wakilaani director wa movie hiyo anachowafanyia.

Niite taikon wa Fasihi
 
Back
Top Bottom