Mwanangu nitamuita Lissu

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,891
MTOTO WANGU NITAMUITA LISSU

Na, Robert Heriel

Wiki tatu zilizopita Niliandika Makala moja niliyoipa kichwa kisemacho "Tundu Lisu Acha kutetea Wajinga na masikini" Katika makala ile nilipigiwa simu na watu wengi mno. Wengi walionyesha hisia zao za uchungu walizonazo, walinipongeza huku wengine wakimtukuza Mungu.

Dada mmoja aambaye ndiye ananifanya niandike uzi huu, anayetambulika kwa Jina la Jacklin alinipigia simu. Aliongea kwa uchungu sana. Ingawaje nilikuwa simuoni kwani tulikuwa tukiongea kwa simu lakini niliyaona machozi yake yakitiririka kwenye mashavu yake. Alilia na kutetema wakati akiongea na Mimi. Jacklin alinambia; siku Lisu anapigwa Risasi mpaka akapelekwa Ubeligiji niliweka nadhiri kuwa nitakapopata mtoto wa kiume lazima nimuuite Lisu"

Jacklini ni moja wa wadada wenye wadhifa mkubwa hapa nchini aishiye jijini Dar es Salaam. Tofauti na watu wengine walionipigia simu, Jacklini alienda mbali zaidi na kutaka mtoto aliyekaa tumboni mwake kwa miezi tisa aitwe jina la Tundu Lisu.

Wiki tatu sasa zimepita, nimekuwa mfuatiliaji mkubwa kampeni za nafasi za wagombea Urais, huku nikiwapa Upendeleo zaidi Wagombea wawili ambao ni Mhe. Tundu Lisu na Mhe. John Magufuli kutokana na kuwa wameonekana kutoshana na wanashindana haswa.

Nami namuunga mkono Dada Jacklin, kuweka nadhiri mbele ya Mwenye enzi, ndiye Mungu wetu, kuwa endapo atanipa nafasi na muda, kisha akanibariki mtoto wa kiume basi Mtoto huyo lazima Nimuite LISU. Naye ataitwa Lisu nikimpa maana yangu binafsi isemayo " Aliyeepushwa na Kifo cha waovu".

Na kama atatokea yeyote atakayeniuliza sababu ya kumpa mwanangu wa kumzaa jina hili naam ndilo LISU, iwe ni Wewe au yule. Au Endapo mwanangu huyo nitakayekuita Lisu, utakapoulizwa kwa nini Baba yako nlikuita jina hilo, usijekosa cha kusema basi utawajibu hivi; kwa kusema hizi ndizo sababu za Mimi kuitwa Lisu na Baba yangu Taikon;

1. LISU ALIONGEZA IMANI YANGU ZAIDI KWA MUNGU.
Mimi Taikon, ndiye ndugu yenu, tena ndiye Baba yako(ewe uliyemwanangu wa kuzaa uitwaye Lisu), nalimshuhudia Mungu katika zama zangu, nikiwa kijana mdogo tuu. Mungu alishuka siku zile kutoka kwenye kiti chake cha enzi akamuokoa Tundu Lisu na mkono wa mauti. Huyo Lisu alipigwa Risasi nyingi, yatajwa; risasi zilirushwa zaidi ya hesabu ya vidole vya miguu na mikono, lakini akapatwa na Risasi kumi na sita tuu mwilini mwake. Nao watesi wake walipomuona bado yu hai hawakuisha kumuandama, wakitaka kuingamiza roho yake. Lakini Mungu yule aliyemuokoa na Mauti, ndiye Mungu wa Baba yako, aishiye Tibeli(Ambapo habari zake nilikuandikia), akamuokoa.

Basi mimi Baba yako imani yangu juu ya Mungu ikazidi kuimairika kwa maana alimuepusha na mkono wa Mauti huyo mwenye kusema kweli.

2. AGANO LANGU NA MUNGU
Nitakuita Lisu kama ishara ya agano langu na Mungu kuwa siku zote za maisha yangu, nitatenda haki, tena nitatetea hiyo haki popote pale niwapo. Nami sitakuwa na vipimo viwili vya kupimia. Nimpimie mwenye cheo kipimo hiki na yule asiye na cheo kipimo kile. Wala sitampendelea tajiri kwa utajiri wake na kumpunja masikini kwa umasikini wake. Bali wote nitawapimia kipimo kimoja bila kujali sura zao, hali zao, elimu zao au namna yoyote ile.
Kwa maana, Huyo Lisu alikuwa jasiri, hakuogopa uso wa mtu, wala hakuogopa nafasi ya mtu basli aliipenda haki na kuitetea.
Naye alihangaika kuutafuta ule uhuru wa kila mwanadamu ni sawa, wala hapana Mtu aliyemwema asiyepaswa kukemewa pale akoseapo.
Basi nitakuita kama agano langu na Mungu dhidi ya kutetea haki na kusema ukweli popote pale niwapo, bila kujali matokeo.

3. KAMA KUMBUKUMBU YA UKUU WA MUNGU.
Nami nitakuita Lisu kama kumbukumbu ya UKuu wa Mungu niliouona enzi za ujana wangu. Ili kila nikutazamapo na nikuitapo basi nikumbuke ukuu wa Mungu alioufanya enzi za ujana wangu, niliouona kwa macho yangu, na kuusikia kwa masikio yangu. Wala sio habari ya kusoma kwenye vitabu kama habari za manabii na mitume, bali habari iliyotokea katika zama zangu. Wala sikuona pekee yangu bali tuliona na kusikia habari zake watu wote na dunia nzima ikajua. Wala tukio lake halikuwa la siri ili nilijue peke yangu, bali ni tukio la wazi na watu wengi walilishuhudia. Na Mungu alitukuzwa katika maumivu na mateso ya Lisu. Basi ndio maana nalikuita LISU

4. KUKEMEA UOVU
Kama alivyoandika kwenye Zaburi, na hivi ndivyo alivyosema;
Zaburi 84:10-11 SRUV
Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu kwingineko; Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kuishi katika hema za uovu. Kwa kuwa BWANA, Mungu, ni jua na ngao, BWANA atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.
Basi nimekuita Lisu ili usione haya kuukemea uovu, na kuupinga kwa nguvu zote. Kwa maana ni heri uishi siku moja ukimpendeza Mungu na kuupinga uovu na hila zake. Kuliko miaka mingi ukinyamazia uovu. Kwa maana utapata faida gani kuishi miaka mingi ukishuhudia waovu wakitenda kwa udhalimu pasipo kuwakemea.
Basi nimekuita Lisu ili ukemee uovu pasipo macho ya hofu.

Nami nakuambia, hakuna kibali cha kukemea maovu, wala hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kukemea uovu pekeake, Wala kuombwa Ruhusa ya kukemea uovu. Kwa maana wakati waja, na sasa umekuwako kuwa wapo watu wenye hila watakaotaka kupewa mamlaka ya kutoa vibali vya ruhusa vya kukemea waovu, tena pasipo kibali watawazuia watu kukemea uovu. Lakini nakuambia mwanangu Lisu, hao ni waovu, nawe usiombe kibali kwa muovu. Kemea uovu ufanyikapo bila woga.

Kwa maana kukemea uovu ndio haki kwa yeye amjuaye Mungu. Tena kuupinga ndivyo impasavyo mtu.

5. TABASAMU MBELE YA KIFO.
Kama alivyofanya Stefano alipokuwa akipigwa mawe, akisema Mungu wasamehe kwa maana hawajui walitendalo huku akitabasamu. Hata Yesu akiwa msalabani naye alisema wasamehe kwa maana hawajui walitendalo huku akitabasamu mbele ya kifo. Nidvyo huyo Tundu Lisu alivyotabasamu wakati alipokuwa amenusuika kufa.
Mimi Baba yako, Mara kadhaa nikiwa namfuatilia Lisu tangu akiwa Nairobi, ndio huko Kenya, na baadaye akapelekwa Ubeligiji(Majina haya ni kwa wakati wangu mnamo karne ya 20-21 yanaweza kubadilika baadaye) Nalimuona mara zote huyo Lisu akiwa ametabasamu licha ya kuwa anamajeraha mwilini mwake lakini mara zote uso wake ulikuwa na nuru.

Kwa maana wapendao haki huwa na nuru usoni, lakini waovu nyuso zao hujawa na simanzi.

6. KUTOKUKATA TAMAA
Lisu kama walivyo watu wengine katika Historia, na hapa yupo Yesu wa Nazareth(nipendaye falsafa zake) hakukata tamaa licha ya kushambuliwa na kutaka kuangamizwa lakini bado aliendelea kuwapenda waliokuwa hawamtaki aliokuwa akiwatetea. Lakini bado hakukata tamaa. Pengine Mimi Baba yako ningekata tamaa na ndio maana kuna siku nilimuambia aache kutetea masikini na wajinga. Lakini bado hakuacha kutetea watu wanaomkataa, wasiomuelewa kuwa anawapigania. Kwa maana hata Yesu walimuua akafufuka na bado hawakumtaka. Hata Musa walitaka kumuua licha ya kuwa ndiye alihangaika kuwatetea.

Basi mwanangu, nimekuita Lisu ili usikate tamaa pale upiganiapo haki. Kwa maana wote waiteteayo haki huokolewa kwa haki. Nao wauteteao uovu wataangamia kwa uovu.

Basi hizo ndizo sababu chache za kwa nini nitamuita Mwanangu wa kiume, wa kumzaa Lisu endapo Mungu atanipa nafasi ya muda, na baraka ya mtoto wa kiume.

Lisu hata kama hatashinda Urais, lakini Mungu umenifunisha mambo makuu sana. Na pia naamini hata waliompiga watakuwa wamejifunza ukuu wa Mungu.
Basi wakitubu Mungu wasamehe, kwa maana wewe ni Mungu wa Rehema. Lau kama wasipotubu basi kizazi chao kiwe ukiwa, naam wakataliwe hata na kuzimu, wasiwe na kikao mahali popote pale. Nao wasiingie mavumbini kwa amani.

Wala hakuna mwenye haki isipokuwa MUNGU peke yake.

Ulikuwa nami:

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
T shirt zili zuiliwa. Majina hayatawekewa vikwazo? Utashangaa mtoto wako anakataliwa kuandikishwa jina la Lisu siku anaingia darasa la kwanza. Vinginevyo huyo Lisu awe ndio mtawala.
 
Back
Top Bottom