Mwanafunzi Mtanzania aliyefariki kwenye mapigano ya Israel na Hamas atunukiwa Shahada na Chuo cha SUA

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Jina la Clemence Mtenga, aliyefariki dunia nchini Israel, limetajwa kuwa miongoni mwa wahitimu katika mahafali ya 42 ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Wakati mahafali hayo yakifanyika hiyo jana, mwili wa Mtenga uliagwa usiku wa kuamkia jana mjini Tel Aviv, Israel na kushuhudiwa na baadhi ya Watanzania ambao walisali misa ya maziko.

Mwili wake unatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya maziko.

Mtenga alikuwa miongoni mwa Watanzania wawili na raia wa mataifa mengine waliokuwa hawajulikani walipo tangu yalipotokea mapigano kati ya Israel na Palestina.

Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 3,095 walitunukiwa na mkuu wa chuo hicho, Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Warioba, kwa ngazi ya shahada ya Uzamili, shahada za awali, stashahada na astashahada.

Mtenga na wanafunzi wenzake 91 wamehitimu Shahada ya Sayansi ya kilimo cha Bustani.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutunukiwa shahada hiyo, mwanafunzi mwenzake, Erick Christopher alisema marehemu alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakijituma darasani na hakuwahi kuwa na historia ya kufeli mitihani, bali mara azote alikuwa na ufaulu mzuri.

Alisema Mtenga alikuwa akishirikiana na wenzake na alikuwa akipewa majukumu ya kuwaongoza kwenye kazi za vikundi na za darasani.

“Hata shambani tulipokuwa tukipewa kazi, alikuwa akiwaelekeza wanafunzi wenzake namna ya kufanya na kama ilivyo ada inapotokea fursa kwenye jamii ama darasani tunafurahi kama darasa na alipopata nafasi ya kwenda Israel kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, tulimfurahia kuwa kapata fursa na tulimtakia kila la heri katika masomo yake na wenzake,” alisema Christopher.

Alisema nafasi hizo za masomo walipata wanafunzi wanane, wa kike na kiume ambao waliondoka pamoja kuelekea nchini humo.

“Ninachokikumbuka juu yake ni ile siku aliyokuwa anaondoka, Mtenga aliwasiliana na wenzetu ambao waliwahi kufika Israel kwa lengo la kutaka ushauri na maelekezo mengine, na wao walimpatia,” alisema Christopher.

Naye mwanafunzi, Irene Chaboma akimzungumzia Mtenga alisema alimfahamu kwa shughuli za kidarasa na zile walizokuwa wakifanya nje ya darasa.

Alisema mara zote alikuwa akijitoa kwa ajili ya wenzake na alikuwa akishiriki kazi zote na alikuwa msaada mkubwa hata kwa wale walioonyesha kuwa na uwezo mdogo, alijitolea kuwafundisha kwa majadiliano hadi walipoelewa.

“Mara ya mwisho baada ya kumaliza mitihani yetu tulipiga picha pamoja kama kumbukumbu na hata wakati wanaenda uwanja wa ndege, baadhi yetu waliwasindikiza, kweli tumeumia sana,” alisema Chaboma.

Marehemu Mtenga ni kati ya wanafunzi 260 wa Tanzania waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom