Mwalimu Nyerere anavyokumbukwa Tanzania na kimataifa

Diversity

Content Manager
Joined
Oct 21, 2019
Posts
140
Reaction score
231


Leo Oktoba 14, 2025 ni kumbukumbu ya miaka 26 tangu kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alizaliwa Aprili 13, 1922 na alifariki dunia Oktoba 14, 1999. Alisoma katika Chuo cha Makerere mjini Kampala, Uganda, kisha akaendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland, akiwa Mtanganyika wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza, na wa pili pekee kupata shahada ya chuo kikuu nje ya Afrika. Mnamo mwaka 1952 alirudi Tanganyika, akaoa, na kufanya kazi kama mwalimu.

Mnamo mwaka 1954, alisaidia kuanzisha Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), chama kikuu cha kisiasa katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika kutoka kwa utawala wa Uingereza. Nyerere alihubiri mapambano yasiyo ya kutumia nguvu ili kufanikisha lengo hilo. Katika uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria wa mwaka 1958–1959, Nyerere alichaguliwa kuwa mbunge. Baadaye, aliongoza TANU kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1960 na akawa Waziri Mkuu. Mazungumzo yake na viongozi wa Uingereza yalileta matokeo ya uhuru wa Tanganyika mnamo mwaka 1961.

Mnamo mwaka 1962, Tanganyika ikawa Jamhuri, na Nyerere akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza. Serikali yake ililenga kuondoa mabaki ya ukoloni na kuendeleza sera ya ‘Uafrikaishaji’ wa utumishi wa umma, huku ikihimiza umoja miongoni mwa Waafrika wazalendo. Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kisiwa cha Zanzibar kiliunganishwa na Tanganyika na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 1985, Nyerere alijiuzulu kwa hiari na nafasi yake kuchukuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi. Nyerere alikuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa Afrika wakati wa harakati za Uafrika (Pan-African Movement) zilizotikisa bara la Afrika katika miaka ya 1960. Alikuwa mtu mwenye mvuto mkubwa, asiye na tamaa ya rushwa, na aliyekuwa mzalendo wa kweli wa Kiafrika. Pia alikuwa miongoni mwa waasisi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mnamo mwaka 1963.

Nyerere anatambulika kimataifa kutokana na mchango mkubwa alioutoa, ukiwamo wa ukombozi kwa ncchi zilizokuwa zikitawaliwa na Wakoloni kwa kutoa hifadhi na makazi kwa harakati kadhaa za ukombozi barani Afrika, ikiwemo African National Congress (ANC) na Pan African Congress (PAC) kutoka Afrika Kusini, pamoja na FRELIMO wakati wa jitihada zake za kumaliza utawala wa Kireno nchini Msumbiji.

Aidha, aliunga mkono ZANLA chini ya uongozi wa Robert Mugabe katika mapambano yake dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi huko Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe).

Alijenga uhusiano ya urafiki ya karibu na Rais wa Misri, Gamal Abdel Nasser, kutokana na mradi wake nchini Tanzania uliokuwa na mwelekeo sawa na ule wa Nasser nchini Misri, ambapo wote walikubaliana na kauli mbiu ya “Ujamaa”. Rais Nasser alimuelezea Nyerere akisema: “Nyerere ni kiongozi imara na shujaa, si kwa Tanzania pekee, wala kwa Afrika yote tu, bali kwa ubinadamu wote.”

Mwalimu Nyerere anaendelea kuheshimika duniani kote, ambapo kwa Tanzania anatambulika kama “Baba wa Taifa.”
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…