Mvua zaendelea kuleta maafa katika maeneo mbalimbali Nchini, TMA watoa tahadhari kuwa mvua hizi zitaendelea maeneo tofauti

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,813
4,547
1580201058427.png

MVUA zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali zimesababisha maafa makubwa ikiwemo watu watatu kupoteza maisha na watu zaidi ya 661 katika vijiji zaidi ya sita wakikosa makazi ya kuishi katika mikoa ya Lindi na Iringa.

Pamoja na hayo, miundombinu ikiwemo madaraja na mashamba ikiharibiwa vibaya na mvua hizo.

Wakati hayo yakitokea, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya mvua kubwa katika mikoa zaidi ya 20, ikiwemo mkoa wa Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani, Mwanza na Shinyanga zitakazonyesha kwa vipindi tofauti.

Mkoani Lindi watu 600 kutoka vijiji vya Mikole, Kipindimbi, Makanganga Mitolea wilayani Kilwa jana wameokolewa kwa njia ya boti baada ya kuzungukwa na maji yatokanayo na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Renatus Mchau aliyasema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.

Alisema uokoaji bado unaendelea kwa kutumia wavuvi, pamoja na kikosi cha uokoaji kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Dar es Salaam, waliotumia boti katika uokoaji huo.

Mchau alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyefariki kutokana na maafa hayo yanayotokana na mvua kunyesha tangu juzi.

Alisema kunyesha kwa wingi kwa mvua hizo kulisababisha mito ya Matandu na Liwale kujaa maji hali iliyochangia kuwapo kwa maafa hayo.

Aidha, alisema mashamba na mali zinginezo pamoja na makazi yote yaliharibiwa na jamii inayoishi maeneo hayo kukosa makazi ya kuishi.

Alisema wakazi ambao makazi yao yameathirika wamehifadhiwa katika shule za secondari na msingi Kipindimbi wilayani humo. Alisema jumla ya boti tano zilitumika katika uokoaji huo nab ado walikuwa wakivuatilia boti nyingine ili kuokoa watu wengi zaidi kwa pamoja.

Mkoani Iringa, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha zimeleta maafa wilayani Iringa na kusababisha watu watatu kati yao wakiwemo watoto wawili kusombwa na mafuriko na kufariki dunia huku kaya 61 zikikosa makazi ya kudumu baada ya nyumba zao kubomolewa.

Pamoja na madhara hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema barabara inayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na wilaya ya Iringa katika eneo la Tungamalenga imekatika hivyo wanaotumia barabara hiyo wakiwemo watalii hawawezi kuingia wala kutoka katika hifadhi hiyo kwa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kasesela alisema mvua hizo zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo zimelizingira kwa maji gereza la wilaya hiyo lililopo katika kijiji cha Pawaga na kama hali haitabadilika ndani ya siku mbili zijazo wataangalia uwezekano wa kuwahamishia wafungwa wake wote katika gereza la Iringa mjini.

“Lakini pia kuna madaraja katika kijiji cha Nzihi na Uguruba kuta zake zimemegwa na mafuriko hayo. Hali ni mbaya na barabara zake zinapitika kwa shida huku katika eneo la Magozi barabara ikikatika,” alisema hukumvua zikishuhudiwa zikiendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo jana.

Akizungumzia vifo vya watu hao watatu, vilivyotokea katika eneo la Tungamalenga Kasesela alisema: “Watoto hao wawili walisombwa na maji baada ya kuishiwa nguvu katika mti waliokuwa wameushikilia wao pamoja na mama yao mzazi aliyenusurika katika tukio hilo.”

Bila kutaja majina yao, Kasesela alisema naye mtu huyo mzima alifikwa na umauti baada ya kushindwa kujiokoa kutoka katika maji yaliyojaa ndani na nje ya nyumba yake.

Alisema juhudi za serikali kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho cha Tungamalenga zimefanikiwa kuupata mwili wa mtu mzima na mtoto mmoja na wakazikwa juzi kijijini hapo wakati jitihada za kumtafuta mtoto mwingine zikiendelea.

Kutokana na mafuriko hayo alisema katika tarafa ya Pawaga kaya 41 na katika tarafa ya Idodi kaya 21 hazina mahali pa kudumu pa kuishi baada ya nyumba zao kubomolewa na mafuriko hayo yaliyosababisha gari lake kutitia katika moja ya barabara za vijiji hivyo wakati akikagua madhara yaliyosababishwa na mvua hizo juzi.

Kasesela alisema kuna dalili takwimu za madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo zikaongezeka na akatoa wito kwa wakulima hasa wa mpunga wenye kawaida ya kulala mashambani kuondoka mara moja.

Mvua hizo zimeleta madhara hayo huku, wananchi wilaya hiyo wakiwa hawajasahau mafuriko yaliyotokea Januari, 2016 katika kijiji cha Kisanga, Tarafa ya Pawaga ambako kaya 145 zilibomolewa na kuharibiwa makazi yao.

Wakati huo huo, TMA katika utabiri wake kuanzia Jumamosi ilitoa tahadhari ya mvua kubwa katika maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara ,Ruvuma na Kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Aidha, kuanzia siku ya Jumapili walitoa angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara ,Ruvuma, Dar es Salaam, Mororgoro, Tanga, Zanzibar, Pwani , Kisiwa cha mafia, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma na Singida.

Huku siku ya jana kulikuwa na angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na Dododma.

Katika taarifa yake, TMA pia jana walitoa angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara, Simiyu, Mwanza na Shinyanga.

TMA ilieleza kuwa katika muda huo athari zinazoweza kujitokeza ni makazi kuzungukwa na maji ,ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Imeandikwa na Kennedy Kisula Lindi, Frank Leonard Iringa na Theopista Nsanzugwanko Dar.


Habari Leo
 
Back
Top Bottom