Muziki kama Pesa: Iga Akili ya Diamond, Usiige ubongo wa 20%

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
918
1,994
Karne ya 19 mwishoni, mtaalamu wa uchumi nchini Italia, Vilfredo Pareto, alitambulisha kanuni inayoitwa "The Principle of Least Effort" ambayo inajulikana pia kama 80/20, kwamba asilimia 80 ya mafanikio ya mtu, hutokana na jitihada ya asilimia 20.

Hapo ikimaanishwa kuwa binadamu anafanikiwa zaidi kwa kuweka jitihada kidogo tu. Na kwa mujibu wa uwiano ambao Pareto ameutaja, ni wazi kwamba endapo jitihada zako zitafikia angalau asilimia 50, mafanikio yatakuwa hayamithiliki.

Mwandishi Robert Kiyosaki katika kitabu chake Rich Dad's Guide to Investing, naye anatambulisha kanuni inayoitwa 90/10. Akimaanisha kuwa asilimia 10 ya watu huvuna pesa asilimia 90, halafu watu asilimia 90, hugombea pesa asilimia 10.

Alimaanisha kuwa pesa ni nyingi sana katika nyanja mbalimbali lakini kila upande, asilimia 90 huvunwa na watu asilimia 10. Akatolea mfano katika filamu ni watu asilimia 10 tu ndiyo wanavuna pesa kwa asilimia 90, vivyo hivyo kwenye soka, uwekezaji na hata muziki.

Belle-9.jpg marlaw.jpg Rich-mavoko.jpg DAYNA.jpg linah3.jpg SNURA.jpg


KWAKO MWANAMUZIKI WA KITANZANIA;

Je, wewe unataka kuwepo kwenye kundi gani? Lazima uamue leo kukataa kuwa chini, tena usikubali kuishia daraja la wastani, pambana kufika juu kabisa ya kilele. Hata hivyo, huko kunahitaji maarifa, akili ya kibunifu, utundu, ujanja, uwezo, kipaji, uvumilivu na bahati.

Muziki si kazi ya lelemama, wale wanaoamini katika sauti nzuri na kucheza peke yake, huishia katikati. Muziki ni zaidi ya kushinda studio kutunga na kuimba nyimbo nzuri. Hauishii kuwa na safu nzuri ya shoo jukwaani. Muziki kama pesa unahitaji maarifa ya kibiashara.

Katika eneo la maarifa ya kibiashara ndipo unapoweza kutambua aina ya mwanamuziki anayeweza kufika juu, atakayeishia katikati au msindikizaji. Muziki katika sura ya pesa ni zaidi ya kipaji, ni zaidi ya kusifiwa uimbaji na uchezaji.

Uvivu ni adui wa wanamuziki wengi. Kuna waliokuwa hodari kabisa lakini hawakufika popote kwa sababu walishindwa kuchangamsha ubongo kujua wanawezaje kubadili vipaji vyao kuwa pesa. Kuzifanya nyimbo zao zinazopendwa kuwa mgodi unaofoka madini.

Hakuna anayeweza kupinga kwamba Steve R&B ana sauti nzuri, uwezo mkubwa wa kuimba na anapendwa sana. Swali ni je, kipaji kikubwa alichonacho kimemsafirisha mpaka wapi ili kuvuna fedha anazostahili? Ameshaonesha juhudi ya kiwango gani?

Katika sura hiyo, ndipo utagundua ni kwa nini mkongwe Nuruel ni mwimbaji mzuri lakini hajawahi kuwa nembo sokoni. Banana Zorro na TID ni ‘brandi' kubwa sana lakini hazitengenezi pesa kulingana na uhalisia wa thamani yao.

Na itakuwa rahisi kugundua ni kwa nini Ben Pol, Barnaba, Belle 9, Rich Mavoko na wengineo wanazidiwa ‘spidi' na Ommy Dimpoz. Hutakiwi kuwalinganisha na Diamond, maana huyo tambo zake ni ndefu sana. Mwisho itakuwia wepesi kubaini namna Ali Kiba alivyofunikwa na Diamond kibiashara. Twende mdogomdogo!

NI NDOTO YA KILA MWANAMUZIKI KUWA TAJIRI KUPITIA MUZIKI;

Kama kuna mwanamuziki ambaye madhumuni yake ni kuimba nyimbo nzuri ili awe anasikiliza na marafiki zake au na nduguze halafu wanaburudika, huyo mimi simjui! Wala simfahamu mwenye ndoto za kuwa staa wa mtaa, kata au wilaya.
Namtambua anayewaza kutikisa anga la kimataifa na kutengeneza utajiri. Hata wale wanaoishia kubamba tu ndani ya mipaka ya nchi, kwa kawaida hutamani kutoka kimataifa na nyimbo zao zivume kwenye mataifa ya wengine lakini hawakufurukuta.

Unaweza kuimba wimbo mzuri na usiishi, achilia mbali kuvuka mipaka ya nchi. Lazima mwanamuziki mwenyewe awe na nia ya kuufanya wimbo wake uishi, kama si yeye, basi apate menejimenti nzuri inayoweza kumfanyia kazi sahihi kwa wakati mwafaka.

Inahitaji juhudi, maarifa, ubunifu wa kupenya sokoni na kulitawala soko lenyewe. Bahati ni nguzo muhimu kufikia mafanikio hayo. Hata hivyo, upo msemo kwamba juhudi huvuta bahati. Diamond ni mwenye bahati sana kwa sababu alijitahidi. Hakukaa nyumbani mafanikio yakamfuata.

diamonds-are-forever.jpg


Chukua mfano; Floyd Mayweather Jr. ni tajiri. Mchezo wa masumbwi unamuingizia fedha nyingi. Lakini je, umeshawahi kumuona anavyoumia akiwa mazoezini? Unaweza kudhani anakufa siku hiyo kwa jinsi anavyomenyeka. Kwa akili ya kawaida baba yake (Mayweather Sr.) kwa woga na huruma, angeweza kumwambia aache.

Ni kwa sababu baba yake na Mayweather mwenyewe pamoja na timu yake yote ya ufundi wanajua mazoezi hayo ndiyo mti unaomwaga pesa kwa bondia huyo na wao kunufaika, wameendelea kukaza. Mfano huo ni kwamba hakuna pesa inayoweza kuja bila kuifanyia kazi. Utajiri ni matokeo ya kujituma katika kiwango cha juu na si vinginevyo.

Ukipata bahati ya kutazama mkanda wa mazoezi ya Christiano Ronaldo, utakiri kwamba ana haki ya kuwa tajiri na staa mkubwa wa soka ulimwenguni. Siku zote, tofauti ya mtu anayeelekea kufanikiwa sana na wengine ni jinsi anavyojituma kuonesha na kufanya vitu kuliko mazoea.

Kuna makala niliandika, nikasema Diamond ni Ronaldo na Ali Kiba ni Messi. Kwamba Diamond ana kipaji lakini si kikubwa sana ukilinganisha na Ali Kiba, ila kinachompa ubora wa daraja la kwanza ni kujituma. Hakuna ubishi kuwa Messi ana kipaji kuliko Ronaldo, lakini huoni ‘gepu' kubwa kati yao kwa sababu Ronaldo anajituma sana kujiweka katika kiwango bora.

DIAMOND ANAVUNA ALICHOSTAHILI ALI KIBA;

Rudi miaka miwili iliyopita kisha hesabu mpaka mwaka 2006, Ali Kiba alikuwa mwanamuziki anayeogopwa mno. Wanamuziki wenzake walimchukulia kama kioo cha mafanikio. Alistahili kutokana na uwezo wake lakini alichokosea ni kwamba hakukaza ili kufika mbali.

Haikuwa kuogopwa tu na wanamuziki wenzake, bali kwa mashabiki pia Ali Kiba ni kipenzi chao mpaka leo. Alikuwa na mtaji mkubwa mno wa kumuwezesha kutengeneza fedha nyingi kupitia muziki wake, vilevile kutamba kimataifa.

Alishafanya kazi na Mfalme wa R&B duniani, R. Kelly katika ‘project' ya One8 (Hands Across the World) ambayo iliwakutanisha mastaa wakubwa barani Afrika. Ulikuwa mtaji mkubwa sana kwake na hakutakiwa kurudi chini katika ‘levo' za kinyumbani, alishakuwa wa kimataifa.

one8.jpeg


Hapa namlaumu Ali Kiba mwenyewe lakini zaidi menejimenti yake. Frank Mgoyo na Seven kama mameneja wake, hawakufanya kazi inavyotakiwa kuhakikisha wanazidi kumuuza mwanamuziki wao kila kona ya Bara la Afrika na dunia kwa jumla.

Muziki ni kazi ya matangazo, Tanzania tusingewajua P Square kama menejimenti yake isingewajibika kuwatangaza katika kiwango ambacho Afrika nzima ikakubali kwamba mapacha hao wanafanya muziki mzuri.

Ni kweli kuwa Ali Kiba alikuwa anafanya maonesho mengi nje ya nchi kuliko ndani lakini shoo hizo mara nyingi hazina mvuto kwa sababu kule anakwenda kutumbuiza watu wachache. Tumbuizo la idadi ndogo ya watu hushusha thamani ya mwanamuziki.

Laiti wangemtengenezea video nzuri zinazomuonesha Ali Kiba ‘akipafom' kwenye maelfu ya Watanzania kisha kuzisambaza mitandaoni na katika kona mbalimbali Afrika, hapo mapromota wa nchi nyingine wangejua kumbe kuna kichwa kinachoweza kuvuta maelfu ya watu na kutengeneza fedha. Hawakufanya hivyo!

Februari 26, 2012, Ali Kiba alifanya shoo kubwa sana Dar Live na kuhudhuriwa na maelfu ya watazamaji. Kwa menejimenti makini, walipaswa kuwepo siku hiyo na kurekodi video za ‘promo', hawakuwepo. Kuanzia hapo nikatambua kwamba Ali Kiba hana menejimenti sahihi.

Ali Kiba ni fundi sana wa kuimba, ubora wake unaishia katika ‘audio' ambazo pia hazitangazwi inavyotakiwa. Menejimenti yake haikuwekeza katika video kuhakikisha nyimbo zake zinapigwa kwenye vituo vikubwa vya televisheni barani Afrika na duniani.

Channel 0 wangempa tuzo Ali Kiba kwa kazi ipi ambayo imepata nafasi kubwa katika televisheni yao? MTV wanamtambuaje ikiwa kazi zake hawajazipiga? Huwezi kumtengenezea msanii wako mazingira ya ‘kilokoloko' halafu utarajie avume kimataifa. Kwa uchawi gani?

Agosti 9, mwaka huu, wakati nampeleka Yemi Alade Airport, akirejea kwao baada ya kumaliza kufanya onesho lake katika Tamasha la Usiku wa Matumaini, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwenye gari ulisikika wimbo "Mwana" wa Ali Kiba.

Akaniambia wimbo mzuri, nikamwambia hiyo ndiyo Bongo Flava, akaniuliza mwanamuziki gani ameimba nikamtajia Ali Kiba, akaniambia hamjui kabisa licha ya kumfafanulia kuwa alikuwepo kwenye project ya One8 na aliimba Hands Across the World na 2Face, Fally Ipupa, Mr. Flavor, R. Kelly na mastaa wengine.

Katika maongezi akaniambia Diamond ni mwanamuziki mkubwa kwa sababu kwao Nigeria anajulikana. Akaniuliza kwa Tanzania kati ya Ali KIba na Diamond, nikamjibu wote ni wanamuziki wazuri, kazi zao zinakubalika sana Tanzania.

Nikamfafanulia kwamba Ali Kiba ni mwanamuziki mkubwa lakini Diamond anakua kwa kasi na anapaa kimataifa. Akaelewa!
Mwaka 2012, Diamond aliwahi kunishawishi mara kadhaa ili kampuni yetu iandae mpambano kati yake na Ali Kiba. Alijua huyo yupo juu na aliamini kwamba endapo hilo litafanikiwa angepaa. Haikuwa rahisi kwa Kiba. Alikataa na niliona sahihi kukataa.

Kushindwa kwake kujituma kutafuta njia za kulifikia soko la kimataifa, kutulia kana kwamba alipo ameshafika, ni mambo ambayo yamesababisha mafanikio aliyostahili kuyapata yeye, yamefikiwa na Diamond kabla yake. Pamoja na uzembe wa menejimenti yake, naye alipaswa kusoma alama za nyakati na kuchukua hatua.

Makosa ya Ali Kiba ndiyo hayohayo yaliyofanywa na Barnaba, anaimba vizuri lakini hafikii mahitaji ya soko la kimataifa. Matonya, MB Dog, Belle 9 na wengine wengi wapo mkumbo huo.


AKILI YA DIAMOND, UBONGO WA 20%

20%.jpg karueche.jpeg

Nilishaeleza kuwa Diamond alitamani kupambanishwa na Ali Kiba. Tamasha la Usiku wa Matumaini 2012, tulimpambanisha na Dk. Jose Chameleone, alifurahi sana na hata aliposhindana na CMB Prezzo Julai 7, 2013, alikenua.

Desemba 25, 2012, tulipompambanisha na Ommy Dimpoz alinyong'onyea, alinilaumu kwamba kufaya vile ni kumshusha kwa sababu anataka awe anapambanishwa na wakubwa. Nilimwambia mbona iliwezekana kwa yeye na Chameleone, akakubali kwa shingo upande.

Utaona kiu yake, siku zote anataka kupanda juu. Huko nyuma kabla hata hajafanikiwa kurekodi wimbo na Davido, aliniambia anatamani siku moja akutanishwe jukwaa moja na P Square, kwamba kuanzia hapo atakuwa daraja lingine Afrika na duniani.


Aprili 29, 2012, baada ya kushuka naye kwenye helikopta katika ‘Shoo ya Helikopta' Dar Live na kulakiwa na maelfu ya wakazi wa Mbagala, nilimwambia: "mdogo wangu unaona unavyokubalika? Kazi kwako."
Alinijibu: "Kaka mimi siwezi kufanya uzembe, najua nilipotoka."

Nilimkumbusha 20% alivyochezea nafasi alipokuwa juu kabisa ya kilele cha muziki Bongo. Akiwa kwenye kipindi kizuri cha kutengeneza pesa na kujitangaza kimataifa, akajifanya msela sana. Bahati ikamponyoka. Bahati bila juhudi ni kazi bure.
Ushauri wangu kwa wanamuziki ni kwamba kila mmoja awe na akili kama Diamond na asithubutu kuiga ubongo wa 20%, ni hasara kubwa.

UNAWEZA KUFANIKIWA KULIKO DIAMOND;

Unataka kuwa mwanamuziki mzuri, uuze na kukubalika kimataifa? Lengo lako ni kufanya muziki unaoishi? Kuna mambo kadhaa lazima uyafanye, hakika hautafeli, japo nakubaliana na ukweli kwamba bahati ina nafasi kubwa sana.

Kwa hapa Tanzania, kama ningekuwa mwanamuziki na nina kiu ya kufika ‘levo' za kimataifa, ningemfanya AY (Ambwene Yessayah) kuwa rafiki yangu. Angalia alipoanzia, alivyoanza kufanya ‘kolabo' na wasanii wa nje mpaka leo. Yupo pale kwa juhudi zake. Nilishawahi kuandika makala nikielezea matarajio yangu kuwa ipo siku atatikisa ulimwenguni, bado naamini hivyo.

KITU CHA KWANZA; Lazima kwanza uwe na dhamira ya kufanikiwa katika muziki. Kama huna dhamira ni kazi bure. Mafanikio hayaji bila kudhamiria.

PILI; Tambua mahitaji ya muziki. Unahitaji kusoma mzunguko wa muziki katika wigo ambao wewe unataka kufanikiwa kisha uelewe mahitaji yake ni nini?

Kwa mfano, unatakiwa ujue ukiimba nyimbo za namna gani utakubalika. Albamu haziuziki, tatizo nini? Na nini kikifanyika zitauzika? Ili uwe na mvuto hata shoo zako zijae watu inabidi uweje?
Muziki umepungukiwa nini? Mambo hayo ukishayasoma na kuyaelewa utajua mahitaji yenyewe. Kwa kifupi lazima ujue vyote, mahitaji ya muziki ya muziki na biashara.

TATU; Fanya uamuzi na usirudi nyuma. Tayari una elimu ya kutosha kuhusu mahitaji ya muziki na biashara, dhamira pia unayo, hapo ni kusonga mbele tu, maana safari yako unaielewa, changamoto lazima uzikabili na kuzishinda.

NNE; Jitengenezee thamani (branding). Mwanamuziki asiye-jibrandi hawezi kufanikiwa. Usitegemee atatokea mtu mwingine kukupa thamani, wewe mwenyewe ndiye utatengeneza thamani yako kisha itaheshimiwa. Hakikisha unakuwa wa kipekee.

TANO; Chagua mshindani. Tafuta yule anayefanya vizuri kwenye staili yako halafu mfanye awe mshidani wako. Shindanisha ladha, hakikisha unajiridhisha kwamba yako ni bora zaidi.

Nani anauza sokoni? Hakikisha unauza zaidi yake. Ukishafanikiwa kitaifa, tazama soko la kimataifa, nchi gani imefanikiwa? Mwanamuziki gani anatamba? Fanya juu chini uimbe naye. Angalia AY na Diamond wanavyofanya.

SITA; Thubutu kufanya makubwa. Hapa ni suala la kujiamini tu. Umeshajitengenezea thamani na umeshawaweza washindani. Kama hujawafunika basi upo nao sawa au umewakaribia, ni jukumu lako kuthubutu. Fanya shoo kubwa yenye jina lako, watu wakija wengi utagundua thamani yako imefikia wapi, ukifeli utajifunza.

SABA; Mwanamuziki kama kampuni. Lazima uwe na plani za kibiashara, utafute timu sahihi ya kutafuta ‘dili'. Mwanamuziki kama huna mtu wa masoko ni shida. Promo utafanyaje kwa usahihi? Lini utasaini mikataba ya matangazo na makampuni makubwa ya kibiashara kama huna timu ya kukuhangaikia kufanikisha hayo.

Meneja masoko inabidi awe mtu anayejua kazi. Atambue wewe kama mwanamuziki ni bidhaa inayopaswa kuwa juu siku zote kwa ajili ya mauzo.

NANE; Hakikisha nyimbo zako zinatamba, ila siku zote jina lako na ‘image' yako kama mwanamuziki, vinazidi nguvu ya nyimbo zako. Maana yake ni kwamba nyimbo zikiwa kubwa kuliko msanii, siku zikiacha kupigwa na mwanamuziki anaporomoka mpaka atoe mwingine.

Mwanamuziki anatakiwa kutengeneza pesa kila siku hata kama nyimbo hazitambi. Kuna kulipwa fedha kwa ajili ya matangazo na shoo. Kama nyimbo ni kubwa kuliko msanii na ndiyo hazipigwi, ataishije?

By Luqman Maloto
 

Attachments

  • MATONYA.jpg
    MATONYA.jpg
    30.5 KB · Views: 1,061
  • RACHEL.jpg
    RACHEL.jpg
    5.9 KB · Views: 997
Ulipofika kwa messi nimeacha kusoma unataka niamini kwamba Ronaldo ni zaidi ya messi ??
kwa kipi ??
Mada yako imeharibika Diamond mlinganishe na Ronaldo sawa ila kiba usimlinganishe na Messi
Messi ana tuzo nyingi kuliko Ronaldo na ana rekodi kubwa kuliko Ronaldo

Na rekodi zingine hazioti kwamba kuna siku atamkuta Messi

ni hayo tu.
 
Huyu mwandishi hunivutia sana,, aina hii ya wandishi wamebaki wachache sana,, asante sana luqman hata sis wahamiaji haramu huku Congo tuna liona hili. kwa DRC, msanii wanaemjua toka Tanzania ni Diamond Platnumz, huyu kijana wa mama Nasibu alianza kwa kuvuma mashariki ya Congo yote,, South and North Kivu, baadae akapanda mpaka mbali zaidi. Mwezi wa 11 nilikua kinshasa wenyewe wanaita KIN,,, nimekuta diamond nyimbo zake zinapigwa club. Labda niseme ukweli DR Congo kupata fursa ya kupenya na mziki wako upigwe club hasa Kinshasa na kwenye club maalrufu kama Chez ntemba. si mchezo kwa waliofika KIN wanajua nisemacho... Huyu kijana kajitangaza sana tuache ushabiki maadazi huwezi mlinganisha na na mwanamuziki yeyote east Afrika kwa sasa. Mwingine ambaye mpaka leo japo ni marehemu ni Kanumba ,, mpaka leo DR Congo hasa mashariki analiliwa,, wakati sisi msiba tukiwa tumeusahau wacongo bado wana mlilia Kanumba. ni hayo tu vijana wangu
 
Kimsingi ndani ya makala hii kuna mwangaza wa njia ya mafanikio si kwa wanamuziki pekee bali watu wote wanaoota mafanikio katika kada zao...
mie nimejfunza kuhusu mafanikio kama wewe.. hapo kwenye muzik( dimond) nimeweka kazi zangu za mikono.. swali kwa mtoa mada au hoja mimi ntapataje meneja kama mimi ni mtengeneza majiko ya kupia?? na meneja anahitaji malipo??
 
Bila jitihada,ubunifu,nidhamu,kujituma Ni ndoto kufikia mafanikio...Ni wanamuziki wengi walikuwa juu enzi zao lakini kwa kukosa kwao nidhamu...wamesahaulika.
 
Andiko zuri lakini kuna mambo ya kuangalia kwa wasanii wetu hapa Tanzania.
Ukiondoa Joseph Haule - Prof. J, wengine siwafahamu sana lakini huyu ndiye mtu ambaye kwa umri wake anafanya mambo yanayostahili kufanywa na mtu wa aina hiyo. Mfano Ana familia yenye heshima zote, hii inashabihiana na wasanii maarufu wa nchi kama Uganda maana wanaishi maisha yanayoelezeka.
Sasa huyu kijana wetu angeweka wazi lifestyle yake ingesaidia wengine, japo yeye anaita 'kazi na dawa' huenda huyu aliyempata sasa akamplekeka kusiko na sio muda atakuwa anasema 'inzi kufia kwenye kidonda...'
 
Back
Top Bottom