Mume alia mkewe, kichanga cha miezi miwili kulazwa mahabusu

Papaa Mobimba

JF-Expert Member
Jan 27, 2018
754
3,097
Mkazi wa Mnadani jijini Dodoma ameilalamikia polisi kwa kumuweka mahabusu mkewe mwenye mtoto mchanga kwa madai kuwa hakufanya usafi.

Lakini polisi imesema ilimkamata mwanamke huyo kwa tuhuma za wizi na kumuachia kwa dhamana baada ya kuona ana mtoto mchanga.

Mkazi huyo, Jonas Stanley alidai kuwa mke wake anayeitwa Sara Jacob na mtoto wa miezi miwili walikaa mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini hapa Julai 23, kabla ya kuachiwa baada ya kulipa faini ya Sh50,000 kwa kutofanya usafi.

Stanley, aliyezungumza na Mwananchi jana akiwa katika ofisi za mhandisi wa jiji la Dodoma, alisema alipata taarifa za mkewe kuwa mahabusu baada kutoka kazini.

“Niliporejea jioni nilikuta taarifa kwa majirani na nikaenda polisi. Hata nilipowaambia faini hiyo ninayo walikataa kuchukua kwa maelezo kuwa muda wa kazi umeisha,” alisema.

“Niliwaambia waniweke mimi mahabusu wamuachie mke wangu ili mtoto aweze kupata haki yake, lakini walikataa.”

Alisema siku hiyo ilipofika saa 3:00 usiku, alipigiwa simu na askari wakimtaka kupeleka chakula polisi kwa sababu mtoto alikuwa analia na mkewe ameshindwa kumnyonyesha kwa sababu hakuwa amekula.

“Nilipeleka chakula, lakini (mtoto na mama) waliendelea kubaki mahabusu,” alisema.

“Inaniuma sana kwa sababu niliwaomba waniweke mimi ndani wamuachie mwanangu wakakataa.”

Hata hivyo, kamanda wa polisi wa mkoa, Gilles Muroto alisema mwanamke huyo alikamatwa kwa tuhuma za kuwa na mali za wizi na si kutofanya usafi.

“Ni mmoja kati ya group (kundi) linalopokea mali za wizi ambazo tutawaonyesha (wanahabari) wiki ijayo,” alisema. Muroto.
Alisema baada ya kugundua kuwa mama huyo ana mtoto mchanga, waliona si vyema kuendelea kumshikilia, hivyo aliagiza aachiwe kwa dhamana.

Kadhia ya kukamatwa kwa suala la usafi pia imemkumba Winfrida Bernard, mkazi wa Mnadani aliyesema Julai 21, baada ya mtendaji wa kata na mjumbe kupita nyumbani kwao na kukuta hawakufanya usafi, waliamriwa kulipa faini ya Sh50,000 kila mpangaji.

“Katika nyumba tunayoishi tumepangiana zamu ya kufanya usafi wa mazingira, lakini cha kushangaza tumewajibishwa sisi,” alisema.

Alisema kwa sababu hawakuwa na fedha, yeye na mwenzake walikamatwa na kufikishwa ofisi za jiji, lakini ilipofika saa 12:00 jioni walipelekwa mahabusu hiyo ambako walitolewa siku iliyofuata.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, mkurugenzi mtendaji wa jiji, Godwin Kunambi alipinga kitendo cha kumuweka mahabusu mama aliye na mtoto mchanga na kuahidi kufuatilia suala hilo katika ngazi ya kata.

“Kimsingi mama ambaye yupo maternity leave (likizo ya uzazi), busara lazima ingetumika ili apate mapumziko na mambo mengine,” alisema.

“Kwa hiyo sidhani kama jambo hilo linafanyika na sitaki kuona linafanyika ndani ya jiji la Dodoma.”

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom