MWIGIZAJI maarufu wa maigizo wa kundi la Komedi Orijino, Lucas Mhavile 'Joti', amelazwa katika hospitali ya Muhimbili Kitengo cha mifupa MOI, baada ya kugongwa na gari maeneo ya daraja la Salenda wakati akiwa na wenzake, wakirekodi kipindi cha vichekesho cha Komedi kinachorushwa na Televisheni ya Taifa TBC1 kila Alhamisi.
Kufuatia uvumi uliojitokeza siku za hivi karibuni, kuhusiana na Mwanamama aliyekumbwa na sakati la kuota manyoya katika mkono wake, wakati akimpatia msaada wa fedha aliyedaiwa mlemavu 'ombaomba' katika eneo la Salenda.
Jana walemavu waliandamana hadi katika ofisi za Idara ya Habari Maelezo wakilalamikia uvumi huo ambao wanadai hauna ukweli wowote zaidi ya kuwaharibia mpango wa kusaidiwa na wenye magari wanaopita katika eneo hilo, ambpo walidai kwa sasa wenye magari wote wamekuwa wakipita eneo hilo na kufunga vioo vya magari yao.
Baada ya walemavu hao kutoka katika Ofisi hizo za Idara ya habari Maelezo, waliwakuta wasanii wa Komedi, wakiigiza tukio hilo katika eneo wanalokaa na kufanya shughuli za kuomba msaada na ndipo sekeseke hilo baina ya ombaomba na Wasanii hao lililopoanza wakati wakiwatimua wasanii ili wasiigize habari hiyo katika eneo hilo wakidai si ya kweli.
Akizungumza na Mtanzania Afisa Uhusiano wa MOI, Almas Juma, alisema kuwa Joti alipatwa na kasheshe hilo kwa kugongwa na gari wakati akiwakimbia ombaomba hao waliokuwa wakimtimua na magongo yao, huku akijaribu kukwepa magari na ndipo alipogongwa na kuumia shingo, na maeneo ya kichwani.
Naye Msanii mwenzake 'Masanja' alipoulizwa kuhusiana na hilo alida hawezi kuongelea chochote juu ya hilo. "Siwezi kuongelea lolote kwa sasa kwani nimechanganyikiwa na huu mkono wa Manyoya", ila hata Joti mwenyewe mbona anamanyoya kibao kwani we hujamuona miguuni??alisema Masanja
Mwandishi wa habari hizi alipofanya jitihada za kuzungumza na Joti, hakuweza kuongea lolote zaidi ya kusema kwa kunong'ona "nasikia maumivu makali kichwani na shingoni, na nyie nae nani kawaambia fasta namna hii?". alisema huku akinong'ona kwa kificho baada ya kukatazwa na daktari kuongea na kuwafanya wauguzi waliokuwapo eneo hilo kuangua kicheko.