esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 552
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), inajivunia ubora unaotolewa katika Kurugenzi ya Upasuaji kwa kuongeza huduma nyingi pamoja na ubora wa mashine za kisasa ambapo wameokoa fedha nyingi kama Watanzania wangefuata huduma hiyo nje ya Nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa huduma za upasuaji, Dk Sufian Baruani alisema kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano wameweza kufanya mambo mbalimbali ikiwemo upanuzi wa vyumba, ununuzi wa vifaa vipya zikiwemo mashine za kisasa pamoja na kuongeza wataalam wa kibingwa. “Hospitali ya Taifa Muhimbili tumefanya upanuzi wa vyumba vya upasuaji kutoka 11 hadi 20 na tumepunguza wagonjwa kukaa muda mrefu kusubiria huduma hii.
Awali muda ulikuwa hadi wiki sita hadi nane, kwa mfano idara ya watoto hivi sasa muda umepungua hadi wiki mbili,” alisema Dk Baruani.
Kuhusu kuongeza huduma, alisema waliweza kuanzisha huduma ya kupandikiza vifaa vya usikivu na kuweza kuwafanyia wagonjwa 34 na kugharimu Sh bilioni 1.2. Alisema ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora zaidi nchini, vifaa mbalimbali vimeagizwa na kuwa vitakuwa msaada kwa Taifa katika uboreshaji wa huduma. “Tumeagiza vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 800 kwa ajili ya upasuaji wa matundu madogo. Pia tumeagiza vifaa vya Sh milioni 700 ili kuboresha huduma za macho.
Vifaa hivi ni kwa ajili ya kupima matatizo mbalimbali ya macho pamoja na vifaa vya kutengeneza miwani,” alisema Dk Baruani. Aliongeza kuwa katika huduma ya tezi dume, wameshanunua mashine ya kisasa yenye thamani ya Sh milioni 70 ambayo itasaidia kuchukulia vipimo vya tatizo hilo na kununua vifaa vya maabara vya kutengeneza meno ya bandia.
Alisema huduma hizo za matibabu za uvimbe wa taya (Haemangioma) kwa kutumia mionzi yaani interventional radiology na tangu mwaka 2017 hadi sasa wagonjwa 302 wamehudumiwa kwa gharama nafuu ya milioni nane kwa kila mgonjwa na endapo wangeenda nje ya nchi ingegharimu Sh milioni 100 kwa mgonjwa mmoja.