Ndugu zangu,
Mwanafalsafa Jean- Paul Sartre anasema; Hell is the other people Kwamba jehanam ni wale wengine, anataka pia tukubaliane, kuwa pepo yaweza kuwa ni wale wengine.
Na hakika, tofauti ya mwanadamu na mnyama iko kwenye kufiri. Mnyama anaongozwa na hisia, lakini mwanadamu anapaswa aongozwe na kufikiri. Ndio maana ngombe anaweza kumpanda mama yake. Ni hisia tu zitakazoongoza tendo lake.
Hivyo, mwanadamu kwenye mambo ya msingi hapaswi kabisa kuongozwa na hisia ikiwamo ushabiki. Anapaswa kfikiri.
Vinginevyo, ni ukweli, kuwa kijamii, mwanadamu anaweza kuwa kiumbe anayeishi kwenye mahusiano ya kirafiki na kiadui na wenzake. Na katika hilo la uadui, wanadamu, kama ilivyo kwa wanyama, wanaweza kushindania na hata kugombania vingi; iwe fedha, mashamba, wanawake na hata kivuli cha mti.
Ndio, unaweza kabisa kuwakuta wanadamu wawili wanagombania kivuli cha mti, kwamba nani mwenye haki ya kukaa kivulini. Na wanaweza kugombana mpaka akatokea mwendawazimu atakayekuja kuukata na huo mti wenyewe. Na wanadamu hao watabaki wakitazama juani.
Hoja yangu hapa, kuwa lililo la msingi ni kuwa wanadamu tunategemeana. Kwamba panapo kushindania jambo, mwanadamu, tofauti na mnyama, anapaswa kufikiri sana. Atangulize kwanza hekima na busara.
Na kwenye mgogoro wowote ule, mwanadamu ayape mazungumzo nafasi ya pekee katika kufikia muafaka, na si vurugu au mapigano. Kwenye mgogoro, na kwenye kuitafuta amani, panakosekana mazungumzo ina maana ya uwepo wa mazingira ya kuvunjika kwa amani. Hapa Serikali inapaswa iandae haraka mazingira ya mazungumzo katika kuitafuta suluhu.
Ndugu zangu,
Nilikuwa shuleni miaka ile ya 80 pale aliyekuwa Waziri Mkuu, Dr. Salim Ahmed Salim alipotembelea Mtwara na kukutana na umasikini uliomstusha sana. Kule Mtwara Dr. Salim alikutana na Watanzania waliovaa magunia na miguuni hawana hata kandambili. Na kwenye jua kali walijipanga kando ya barabara kumpokea. Kwenye jua kali walikusanyika kumsikiliza Waziri Mkuu wao.
Ni kule Mtwara inasemekana Dr. Salim, kwa mara ya kwanza, alipofikia maamuzi ya kutoa ruhusa ya mitumba kuingizwa nchini. Maana, kulikuwa na Watanzania wengine wengi nje ya Mtwara waliokuwa kwenye hali ya umasikini wa kufikia kuvaa nguo za viraka na kushindwa hata kuvaa viatu vya matairi ya magari.
Tunajifunza nini?
Kwamba ni kweli Mtwara na sehemu nyingine za nchi zimekuwa nyuma sana kimaendeleo. Na leo tunaposikia Mtwara kuna gesi, nakubaliana na Rais Jakaya Kikwete, kuwa gesi hiyo haiwezi kuwa ni ya WanaMtwara tu. Ni gesi ya Watanzania wote.
Ni vema na ni busara, na kwa kuwashirikisha wazee wa Mtwara, kuwa WanaMtwara wakasikilizwa. Kuna ya msingi ambayo WanaMtwara na Serikali wanaweza kukubaliana kwenye meza ya mazungumzo.
Hata kama tunakubaliana, kuwa rasilimali za nchi ziwasaidie pia watu wa eneo inakotoka rasilimali hiyo, lakini kamwe, tusikubaliane na hoja kuwa gesi iliyo Mtwara ni ya WanaMtwara. Kwamba dhahabu ya Geita ni ya watu wa Geita, twiga wa Ruaha ni wa Wahehe na kadhalika. Haya si mawazo mazuri kuyapandikiza katika nchi.
Ni mawazo ya hatari yanayoweza kupandikiza chuki, sit u miongoni mwa wananchi na Serikali, bali hata miongoni mwa wananchi wenyewe wa maeneo tofauti. Ni mawazo yenye kupandikiza pia fikra za kibaguzi.
Na tufikiri hili, je, kama gesi ile iliyopatikana kule Mtwara, Tanzania na Msumbiji nayo ingesema ni ya kwake, WanaMtwara wangesemaje kama watu wa mikoa mingine ya nchi hii nao wangesema wapelekwe wanajeshi wa Kimakonde, Kiyao na Kimakua tu wakambapane na majeshi ya Msumbiji kutetea Gesi ya Mtwara!?
Naam, ya kule Mtwara isije ikawa yale yale ya kugombania kivuli.
Maggid Mjengwa,
Iringa,
0754 678 252
http://mjengwablog.co.tz
Brother Maggid,
Ktk watu ambao nawaheshimu ktk tasnia ya habari ni pamoja na wewe, mara nyingi nasoma makala zako kwenye magazeti na hata humu jamvini.Na mara nyingi mawazo yako au mitazamo yako huwa inafanana na yangu isipokuwa leo naomba uniwie radhi, nitakukosoa.Na natambua kuwa wewe ni muungwana, na muungwana yeyote anakubali kukosolewa.Nitakukosoa ktk kipengele kimoja tu lakini ni muhimu sana kwa kuwa ndiyo kina beba maudhui ya rai yako.Brother unaonekana hukufanya utafiti kujuwa wanamtwara madai yao ni nini hasa, umeisikiliza serikali na kutoa hukumu, hukutenda haki kwa upande wa pili yaani wanamtwara wanasema nini kuhusu suala hili.Ktk hili bro umeteleza.
Iko hivi; Nakuhakikishia kuwa
Hakuna mwanamtwara hata mmoja anayesema kuwa hataki gesi iende kwa wengine eti waitumie wao peke yao LA HASHA brother Maggid.
Huu ni upotoshaji mkubwa unaofanywa na serikali na watu wa habari(sijuwi kwa sababu gani). Na wewe ni mwana habari.
WANA MTWARA WANATAKA NINI?
1.Wanataka gesi isisafirishwe kwa bomba, anayetaka kuitumia aje aichukuwe pale na iende sehemu yoyote tz na hata nchi za nje
2.Gesi isichukuliwe ghafi. Lile bomba linalojengwa bro ni la gesi ghafi na mikataba ilishafungwa siku nyingi kwa ajili ya kusafirisha ghafi
3.Power plant ijengwe mtwara kama ambavyo imepangwa kujengwa kinyerezi na kupeleka umeme sehemu zingine za tz.
Haya yakifanyika kutakuwa na movement nyingi ambazo zitaongeza shughuli za kiuchumi hatimae kusukuma maendeleo ya lindi na mtr ambako kuna umasikini wa kutisha kuliko sehemu nyingine yoyote ya tz.
Kwa kufanya hayo, kutakuwa na umeme wa uhakika ambao mtu yeyote atakuwa na imani ya kuweka kiwanda maeneo yale hatimaye kutoa ajira za kutosha na kuinua kipato cha wanamtwara na watz wengine.
Wanamtwara wanaona hii ni fursa pekee iliyobaki kwao ktk kujikomboa ktk lindi la umasikini walilonalo ambalo limetokana na kutengwa na serikali kwa muda mrefu na kuwafanya waishi kama wakimbizi kwenye nchi yao ilihali wao wanalipa kodi kama wengine huku wakipewa ahadi lukuki kila uchao.
Namalizia kwa kurudia kusema kuwa nakuheshimu sana brother, lakini ktk hili umefanyia kazi propaganda.
Narudia
HAKUNA MWANA MTWARA YEYOTE ANAYEZUIA GESI ETI ISIWAFIKIE WATU WA MAENEO MENGINE, LA HASHA.
WANAHABARI WANAPOTOSHA UKWELI.
Nawasilisha.