Mtu asiye na Uso

Mtu asiye na Uso

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
10,884
Reaction score
18,824
By SHANWA, 1967.


SURA YA KWANZA

MGENI ANATOKEA​

TEGU, mwana wa Goja, alisimama kwenye ardhi iliyoinuka ambayo iliyatenga mabonde ya Ugweno na Usangi, mahali alipozaliwa. Ingawa alikuwa mvulana mwenye umri wa miaka kumi na sita tu, lakini alionekana kuwa alikuwa mrefu kama mtu mzima. Ngozi ya mbuzi aliyoivaa begani mwake haikuweza kuifunika kabisa miguu yake na mikono yake.

Uso wake ulionekana umejaa ghadhabu na fadhaa. Alikuwa amemwendea rafiki yake Mundula, na huko waliutumia wakati wao mwingi katika mchezo wa kutupa mishale kwa kutumia pinde zao. Mundula alikuwa na shabaha nzuri, kwani katika mishale kumi aliyoitupa, tisa ilipiga kwenye alama. Maskini Tegu alikuwa akiikosa alama kila alipoitupa mishale yake. Kwa muda fulani Mundula hakusema neno lo lote. Lakini Tegu aliutupa mshale wake mmoja vibaya sana hata ilimfanya Mundula acheke sana kwa sauti kubwa. Tegu angaliweza kumsamehe rafiki yake, lakini wavulana fulani waliokuwa wakipita pale walimcheka pia na walimtania kwa kumwita kwa jina la msichana. Wengine walimletea mtungi ili wabadilishe na uta wake. Damu ya Tegu ilichemka kwa hasira na aibu. Joto la damu yake liliweza kusikika katika mashavu yake. Kwa hasira aliyokuwa nayo karibu auvunje upinde wake kwa kutumia goti lake.

Bonde la Usangi
Njia iliyokuwa mbele yake ilikuwa na mawe na changarawe nyingi, njia yenyewe ilikuwa inateremka kwenye bonde ambalo ardhi yake imelimwa, sehemu ambayo majani ya migomba yalipepea katika upepo na yalimetameta chini ya nuru ya jua. Nyumba ziliweza kuonekana hapa na kule zikijitokeza kwenye majani mabichi, nyumba hizo zilikuwa ni za misonge. Watoto walionekana wakicheza kwenye sehemu zilizokuwa wazi na moshi ulionekana ukipanda kutoka kwenye nyumba fulani fulani. Wanawake walikuwa mashambani wakiinama sana katika mashamba yao ya viazi vitamu, huku wakilima wakitumia majembe madogo yenye mipini mifupi au wakitumia miti iliyochongwa sana na yenye ncha kali.

Tegu aliweza kuona nyumba ya chifu kwa upande wa kushoto kwenye mtelemko wa mlima. Kulikuwa na ua mkubwa kuizunguka nyumba hiyo na aliweza kumwona mlinzi amesimama mlangoni akiangalia kwenye kijia kinachotoka bondeni. Kutoka vilimani kulikuwa na vifereji vingi vya maji vilivyoungana na kufanya mto uliojipindapinda kama nyoka ukipita kwenye bonde.

Maji yenye rangi ya udongo yalikuwa yakitiririka kwenye sehemu fulani. Mayungiyungi yalionekana yakijificha kidogo mtoni, na magugu na matete yalikuwa yameota kando ya mto. Mbuzi walionekana wakitembea huko na huko karibu na vibanda, ng'ombe nao walikuwa wamesimama wakila nyasi katika sehemu za juu. Hakika ilikuwa ni hali ya amani na utulivu.


Kifo cha chifu
Ghafula wanawake walitoka nyumbani mwa chifu. Tegu aliwasikia wanalia na kuomboleza, huku wakiinama kuuchukua udongo na vumbi na kuutia katika vichwa vyao. Kutokana na kitendo hicho, alielewa kwamba chifu amefariki. Huko makondeni aliwaona wanawake wakiinuka ili kusikiliza. Wanaume walitoka kwenye nyumba zao wakikimbia kuelekea kwenye msiba. Alipozisikia ngoma zikilia, aliondoka mbio kuelekea bondeni.

Kifo cha chifu kilimfanya Tegu azisahau taabu zake mwenyewe. Chifu alikuwa ameugua kwa muda wa miaka mingi. Alikuwa akiugua ugonjwa usio wa kawaida ambao uliwaua jamaa zake mmoja baada ya mmoja na hata mwishowe hakuna hata mmoja aliyesalia hai. Baada ya Mzee Kichechi kufariki hapakuwa na mtu aliyekuwa na haki ya kukikalia kiti cha Ufalme. Watu wote waliingiwa na woga kwa ajili ya kifo cha chifu wao. Wakati alipokuwa hai chifu huyu aliweza kumzuia Mfupa, mchawi aliyeogopwa, kuzitumia dawa zake za uchawi ili kuwadhuru watu. Sasa ilionekana kuwa hapatakuwa na mtu ambaye ataweza kumzuia Mfupa katika kujitwalia mamlaka ya Uchifu.

Tegu alikimbia mbio akipita kwenye kijia kilichokuwapo kando ya mto, akapita safu za miti, akafika kwenye shamba la migomba. Kutoka hapo ilipokuwa migomba hakukuwa mbali na nyumba ya baba yake. Tegu alipoikaribia nyumba ya baba yake alisikia sauti ya mti ukichongwa.


Mchongaji na jamaa yake
Sauti hiyo haikumpendeza Tegu hata kidogo. Tegu alikuwa amechoka kumwona baba yake akishughulika na uchongaji tu daima. Baba yake alikuwa mpole, mpole sana kwake na kwa mama yake.

Tegu alipofika kiwanjani, sauti ilinyamaza. Tegu akapaaza sauti, akamwambia baba yake, 'Kichechi amefariki dunia'. Baba yake akaitikia kwa kuinamisha kichwa chake akasema, ‘Kifo hiki kimekuwa kikitazamiwa kwa muda mrefu.' Baada ya kusema hayo, alivipanga vyombo vyake vya kazi upande mmoja, akakaa na kuikunja miguu yake mbele ikipitana, akawa anafikiri sana. Mikono na miguu yake ilikuwa myembamba, na ingawa hakuwa mzee sana, uso wake ulikuwa kama kipande cha ngozi ya zamani, iliyojaa mistari.

Tegu aliutupa chini upinde wake na podo la mishale wakati Nata alipokuwa anaingia kutoka mtoni huku akiuchukua mtungi wa maji kichwani. Nata alikuwa amekasirika kwa kuwa njiani aliteleza, na maji yakammwagikia usoni. Wanawake wenzake walimcheka na wakamdhihaki kwa kuwa hakuwa na nguvu na kwamba alikuwa dhaifu. Mama yake akauliza, 'Sijui mtoto wetu ametuletea ndege au mnyama gani ili kunisaidia kuwalisha wanaume wawili?' Tegu akamjibu, 'Nimekuwa nikifanya mazoezi tu, mama.'

Mama yake akaendelea, 'Hakika unahitaji mazoezi mengi. Baba yako hakufanya lo lote kukufundisha mwanangu. Akina baba wengine wamekuwa wakiwachukua watoto wao porini kuwinda. Baba yako hakufanya kitu cho chote ila kukaa tu na kuchonga sanamu.

Goja akasema kwa ukali, 'Acheni kuongea maongezi ya namna hiyo. Ninyi mnafikiri kila kitu hakiendi sawa hapa petu.' Nata akamjibu, 'Mambo mengi hayaendi vyema hapa. Watu wengine wanakula nyama, lakini sisi hatuna nyama ya kula ingawa tunao ng'ombe wengi kama wale wa Mfupa.'

Tegu alimtazama baba yake kwa uso wa huzuni. Alijua kwamba kulikuwa na ukweli fulani katika maneno ya mama yake. Uso wa Goja ulikuwa ni wenye hasira sana kwa vile alivyolitaja jina la mganga.

Goja akajibu, 'Mfupa amewapata ng'ombe wake kwa njia mbaya isiyo ya halali. Ng'ombe wangu nimewapata kwa njia ya haki, kwa ajili ya kufanya kazi kwa bidii.'

Tegu akamwuliza baba yake, 'Mbona hukunichukua porini kuwinda na kunifundisha kuwa mpiganaji hodari? Baba yake Mundula ni mpiganaji hodari na mwindaji shujaa. Amemfundisha Mundula mambo mengi, na wavulana wengine wamefundishwa namna ya kupiga mishale vizuri.'

Goja alimtazama mwanawe, uso wake wenye mistari mistari na macho yake ya kikahawia haikuonyesha dalili yo yote ya kuwa na hasira. Baba akamwambia mwanawe, “Tazama idadi ya ng'ombe tulio nao. Utakuwa tajiri sana nitakapokufa. Huna budi kuridhika; jaribu kuelewa kwamba watu wanaopigana, wao ni kama ng'ombe, wasio na fahamu, wanaofaa kwa kuuawa tu. Mtu mmoja anayeweza kutengeneza vitu kwa mikono yake na kuvibadili na watu wengine ili kupata mahitaji yake, ni bora kuliko wapiganaji mia moja.'

Nata akaruka juu na kisha akamwangalia mumewe akamwambia, ‘Lakini kama wanaume wote wangalikuwa kama wewe, basi Wakamba na Wamasai wangevishambulia vijiji vyetu na wangechukua kila kitu tulicho nacho. Sote tungekuwa watumwa, kama nilivyo mimi.'

Hapo tena, Tegu alifikiri kwamba mama yake alikuwa amesema maneno yenye busara. Alimtazama baba yake kwa dharau kwani alijua kwamba mwanamke hapaswi kuyasema maneno kama hayo kwa mwanamume.

Mama yake akaendelea, 'Je, haiwezekani kwa mtu kutengeneza vitu kwa mikono yake na papo hapo kuwa mpiganaji hodari? Ni kweli kwamba mtu anayepigana na hali hana ngo'mbe ni sawa na mbwa asiye na mkia, lakini pia, mtu mwenye ng'ombe na ambaye hawezi kupigana ni kama mbwa asiye na meno.'

Goja aliinuka na kusimama. Alikuwa mtu mfupi na alionekana mdogo mbele ya mkewe. Goja akasema, 'Inatosha! Siku zote nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe na nina hekima pia. Kwa ajili hiyo watu wengi hunijia ili kuomba mashauri. Inawezekana namna gani, mimi ambaye sijawa mwindaji mkubwa, au sijawahi kupigana, kutazamiwa kuwafundisha watu mambo hayo? Nendeni! Kuna watu wanakuja kuniamkia sasa. Hao ni wazee wa kabila letu.'


Wazee wanaomba mashauri
Nata aliondoka kwa haraka. Goja aliendelea kukaa pale pale huku ameikunja miguu yake. Alingoja mpaka wageni wake walipokaa chini mbele yake. Wazee wakamwamkia, Salaam za heri kwako Goja.' Mmoja wa wageni akaendelea kusema, "Tumekuja kwako kwa ajili ya kifo cha Kichechi.'

Goja alikaa kimya akijua kwamba hapakuwa na neno jingine zaidi. Baada ya muda, yule msemaji aliendelea kusema, 'Kwa kuwa Kichechi amefariki, hatuna mtu tunayeweza kumchagua awe chifu. Je, unaweza kutupa shauri?' Wote walikuwa kimya kwa muda, halafu Goja akasema, 'Je, mnaweza kutengeneza halmashauri itakayotawala kwa muda mpaka mtakapomchagua yule atakayekuwa chifu?'

Mzee mwingine akamjibu, 'Mfupa atakuwa na mamlaka makubwa juu yetu.' 'Ikiwa ni hivyo, basi uite mkutano, na watu wakate shauri juu ya jinsi watakavyotawaliwa.'

Watu kadha walianza kusema kwa mara moja, lakini mmoja alipaaza sauti yake na kufanya asikiwe zaidi akasema, Mfupa hataruhusu mkutano huo kufanyika, na watu wote wanamwogopa sana.'

Goja akawaambia, ‘Uiteni kwanza mkutano na tuone utakavyotokea. Sina shauri jingine la kuwapa.' Wazee walisimama shingo upande wakasemezana, 'Afadhali tutimize jambo hili mara moja kabla Mfupa hajapata nafasi ya kufanya mipango itakayokuwa ni kwa manufaa yake.'

Goja naye aliondoka kwenda nyuma kana kwamba alikuwa anakwenda kuuchagua mti mwingine auchonge. Alipoiangalia miti yake alisema, ‘Hakuna mti utakaonifaa kwa kazi yangu nyingine. Sina budi kwenda kwenye ghala yangu nyingine.'

Tegu, aliyekuwa akiangalia namna baba yake alivyofanya wakati wale wazee walipofika, alishangazwa mno hata akalia akasema, 'Hapo ni nusu ya njia tu kwenda Ngulu. Je, huendi kwenye mkutano?'

Baba yake akamjibu, 'Sina nia ya kumwona Mfupa akikalia Kiti cha Ufalme.' Tegu alikitikisa kichwa chake. Ataweza namna gani kumwelewa baba yake? Naye pia aliinuka akasimama, na bila ya kusema neno jingine zaidi, alikimbia kwenda kwenye nyumba ya mkutano. Alikusudia kupata kiti kizuri atakachokikalia wakati wa mkutano.

Kwa kweli alifanya jambo zuri kwa kufanya haraka, kwani mara tu ngoma zilipoanza kulia, watu walianza kujazana kwenye nyumba ya mkutano ambayo iliezekwa kwa nyasi. Ndani, kwa upande mmoja, sakafu ilikuwa imeinuliwa kidogo. Watumishi wa marehemu chifu walishughulika kuvipanga viti vitakavyokaliwa na Wazee. Mbali na viti vingine, kiliwekwa Kiti cha Ufalme ambacho chifu tu ndiye aliyeruhusiwa kukikalia.


Mganga anatokea
Nyumba ya mkutano ilijaa baada ya muda mfupi tu, na hapo ndipo ngoma ziliponyamaza. Kisha, wazee walipokwisha kuketi katika viti vyao, na kabla ya mtu yoyote hajaanza kusema, kitu fulani kilitokea, kitu ambacho kilimtisha kila mtu. Mchawi, Bwana Mfupa, aliingia ndani ya nyumba ya mkutano.

Wale ambao walikuwa hawajakaa vitini mwao, ghafula walinyamaza walipomwona Mfupa anakwenda kuelekea kule kilikowekwa Kiti cha Ufalme. Pumzi za watu zilisikika kama upepo mkubwa wakati ukivuma kwenye majani makavu, walipomwona Mfupa akiuinamisha mwili wake wenye kibiongo na kuukalisha kwenye kiti cha heshima kuu. Msemaji wa Wazee aliinuka polepole, uso wake ukiwa umejaa fadhaa na mashaka, mwili wake wa kizee ukitetemeka alipokuwa akijaribu kuyashinda mawazo na hofu zake.

Msemaji huyo alimwuliza Mfupa, ‘Kwa mamlaka na uwezo gani unakaa kwenye Kiti cha Ufalme?' Bila kujibu neno, Mfupa aliwatazama watu na huku ameyafumba macho yake nusu. Itakuwa ni vigumu kueleza jinsi Tegu alivyoyachukia macho hayo, pia alivyoichukia ngozi yake iliyopayuka ikiwa na alama kadhaa za kikahawia kama za ngozi ya mbwa. Jinsi gani mtu anaweza kuwa karibu mweupe, mwenye nywele nyeupe na ngozi isiyo na afya! Mfupa alipotaka kujibu alitabasamu akasema, 'Hakuna mahali pengine pa kukaa. Pia hakuna mwingine mwenye haki zaidi yangu ya kukikalia Kiti cha Enzi.'

Mgeni anaingia
Kelele zilizofanywa kutoka nyuma zilimfanya Tegu ageuke na kutazama mlangoni. Watu wote mkutanoni nao wakatazama mlangoni. Watu walistaajabu kuona kwamba kulikuwa kimya na hata sauti ya upumzi haikusikika. Kule mlangoni alikuwapo mgeni mmoja mwenye kimo kirefu. Kichwani alivaa aina ya kilemba cha manyoya marefu na nyasi zilizotiwa rangi. Usoni alikuwa amevaa kinyago cha mti. Kinyago hicho kilikuwa na matundu mawili ambayo macho mawili ya kutisha ya yule mgeni yaliweza kuonekana yaking'aa. Alikuwa tumbo wazi lakini kiunoni alivaa vazi fupi lililotengenezwa kwa nyasi; mikononi mwake pia mlizungushwa kanda za nyasi. Hakuna mtu aliyesema neno kwa muda fulani. Kisha mgeni akasema kwa sauti ndogo, 'Mfupa, ondoka kwenye Kiti cha Ufalme.'
 
SURA YA PILI

PANGO LA KUTISHA

KABLA mtu yoyote hajaweza kusema, mgeni alitembea hatua chache mbele na akasimama karibu na Kiti cha Ufalme. Kisha aliwageukia watu akawaambia, ‘Nitakuwa na nguvu zaidi kumshinda Mfupa, kwa sababu nguvu hizo zitatoka kwenu. Sina hofu na uwezo wake. Mkinisaidia, hataweza kututawala wala hataweza kutudhuru kwa njia yo yote.' Msemaji wa Wazee akamwuliza, 'Wewe u nani lakini?' Hapakupatikana jibu kwa muda na nyumba nzima ilikuwa kimya.

'Mimi ni mmoja wenu ninyi. Lakini hapana haja kulitaja jina langu. Kama ningaliwaambia jina langu wengine wenu wangefikiri kwamba nataka mamlaka kwa ajili yangu mwenyewe na kwa ajili ya watoto wangu. Nina maoni sawasawa na maoni yenu; na nina tamaa ile ile ya kutaka utawala wa haki. Tufanyeni mambo yetu kwa hekima na akili mpaka tumpate kijana aliye shujaa na mwema. Ikiwa hatuna kiongozi, wazee wetu wanaweza kufanya makosa makubwa. Wengine watajaribu kujipatia faida wao wenyewe tukiwa hatuna chifu wa kututawala. Wazee wanamwogopa sana Mfupa, na huenda akawafanya watunge sheria mbaya. Mfupa ni mtu mbaya ambaye sote tunamjua. Mimi ni mgeni tu hapa. Hamwezi kuniogopa mimi zaidi kuliko mnavyomwogopa Mfupa.'



Mgeni anakaribishwa
Palikuwa na watu wengi walioonyesha kukubaliana naye. Tegu alifikiri jinsi baba yake atakavyoshangaa kusikia habari hii. Aliendelea kumtazama Mfupa na yule mgeni mara kwa mara. Mfupa alionyesha hasira na akataka kusema. Lakini mgeni akaendelea, ‘Nataka nyote mnichague kuwa kiongozi wenu mara moja. Kisha hapatakuwa na mtu atakayekaa juu ya Kiti cha Ufalme mpaka chifu mpya atakapochaguliwa. Mnijaribu mimi kwanza, na ikiwa nitashindwa au mkiweza kutaja sababu za kutoniamini, hapo mtaweza kumchagua mtu mwingine. Je, yupo mtu anayetaka kuwa kiongozi ?'

Mara palitokea kelele za watu waliopaaza sauti zao wakisema, 'Hapana, hapana. Sisi tuna imani na wewe mgeni wetu!' Mfupa hakuweza kuizuia hasira yake na mara moja alisema, ‘Hii ni tabia na mwenendo wa watoto. Mgeni huyu ametafuta njia ya ujanja ya kujinyakulia uongozi juu yenu. Atajua namna gani ya kututawala sisi hali hayajui mazoea yetu? Nimeishi pamoja na marehemu Chifu wetu na pia nimekuwa pamoja na marehemu baba yake kwa muda wa miaka mingi. Mimi tu ndiye ninayestahili kutawala. Pepo wataniongoza mimi katika kazi zangu kwa kuwa mimi ni bwana wao. Je, kuna mtu anayethubutu kwenda kinyume cha mapenzi ya pepo?'

Umati ulinyamaza kimya kabisa mpaka mtu mmoja aliposimama ili aseme. Akauliza, 'Hatuwezi kumtaja mmoja wa wake zake marehemu ili akalie Kiti? Kwa muda watu walicheka na pande zote mbili zilionyesha kuchangamka. Watu wakasema, 'Je, anasema mwanamke? Hapana, hatuwezi kuongozwa na mwanamke.'

Ndipo tena yule mgeni akajibu, 'Haya basi, sasa hamna budi kumchagua mmoja kati yetu, Mfupa au mimi. Msiogope maneno ya Mfupa kuhusu pepo, maana pepo wote watanisaidia mimi.' Wote, isipokuwa wachache tu, waliridhika. Tegu alikuwa mmoja wa watu wa kwanza waliosimama na kunyosha mikono ili kumkubali mgeni kuwa kiongozi wao. Karibu naye alimwona baba yake Mundula, Bwana Mzima, askari hodari wa zamani, akisimama na huku akipiga makelele akisema maneno ambayo yalisikika katika midomo ya kila mtu. "Tunakuchagua wewe. Tutakuita Macho mpaka tutakapojua wewe ni nani. Macho yako yanang'aa kwenye kinyago kana kwamba yanaona kila kitu!'



Mfupa anafanya mpango
Mfupa alipoona kwamba Macho anapata kibali cha walio wengi, aliondoka kuelekea langoni. Alipofika langoni aligeuka. Akirandaranda kwa hasira aliinua mikono yake yenye rangi ya kimanjano, akasema kwa sauti ya kutisha 'Macho, mwili wako utalegea na kupungua nguvu. Mazao yako shambani yatakufa. Hakuna mtu anayeweza kupigana na Mfupa akaendelea kuishi.' Macho alisimama wima, kimya kabisa mpaka Mfupa alipoondoka kabisa. Aliwageukia watu na akawaambia waende zao kwani alitaka kuzungumza na Wazee.

Tegu aliondoka pale huku akiwaza moyoni mwake, 'Mgeni huyu anaweza kuwa ni nani?' Mgeni alikuwa amesema kuwa alikuwa ni mmoja wao, na Tegu aliamini kwa kuwa kulikuwa na kitu fulani katika mtu yule kilichofanana na mtu ambaye alimfahamu-kitu fulani kuhusu maumbile na sauti yake. Mgeni hakuwa kijana, na alianza kuwakumbuka watu wote warefu ambao wameupita wakati wa ujana. Lakini hakuna yoyote yule aliyefanana na Macho. Halafu aliwaza jinsi baba yake alivyofanya kosa kwa kukataa kuja kuhudhuria mkutano. Mara alikuwa njiani kurejea nyumbani ili akamwambie baba yake habari hiyo muhimu. Alifikiri kwamba kungekuwa na muda wa kutosha kumwezesha baba yake kwenda kwenye nyumba ya mkutano kabla Macho hajaondoka. Tegu aliuvuka mto na akapita kwenye kijia kilichokuwa na nyasi ndefu upande wa pili. Wakati huo alipokuwa njiani, kwa ghafula alikamatwa kwa nyuma na akavutwa kwenye nyasi ndefu sana. Aliingiwa na hofu kuu alipojiona yumo katika mikono ya Mfupa.

Mfupa akamwambia, Tegu, ngoja kidogo. Baba yako ni mtu mwenye hekima, naye ana ng'ombe wengi, lakini je, amepata kukupa ng'ombe hata mmoja?' Akiwa amejawa na hofu, Tegu alijibu, 'La, hajanipa bado.' Mfupa akamwuliza, 'Je, ungalipenda kuwa na ng'ombe wako mwenyewe?' 'Ndiyo ningalipenda', alijibu Tegu. Mfupa akamwambia, Ni jambo jema kwa mtu kuwa na ng'ombe wake mwenyewe. Ng'ombe wanaweza kumsaidia mtu kununua vitu vingi; wewe ni kijana ambaye hivi karibuni utafikiria kuoa.' Mpaka wakati huu Tegu alikuwa ameshikwa na hofu hata asijue la kufanya wala asiweze kusema. 'Nitampa ng'ombe wengi mtu atakayeniambia yule mgeni ni nani na anakaa wapi.'

Tegu aliogopa kuwa na uhusiano wa namna yo yote na Mfupa, lakini aliogopa kumwambia hivyo. Tegu akamwambia, 'Mimi ninaenda nyumbani kwetu. Mbona umenichagua mimi kufanya kazi hiyo?' Mfupa akamjibu, "Kwa sababu mimi na baba yako mara nyingi twazifanya shughuli zetu pamoja. Kama nisingetia pumzi ya uwezo katika vinyago vyake anavyovichonga, hakuna mtu ambaye angevinunua. Utapata ng'ombe watatu iwapo utamfuata yule mgeni na kuipata habari ninayoitaka.'

Tegu, akiwa mwenye hofu na wasiwasi, alimjibu, 'Nitafanya nitakavyoweza.' Tegu alipendezwa sana na mgeni huyo hata hakuipenda tena hiyo kazi aliyopewa na Mfupa, lakini wazo la kupata ng'ombe watatu lilimsaidia kukata shauri. Aligeuka na akaanza kurudi kwenda kwenye nyumba ya mkutano huku akiwaza jinsi atakavyoringa wakati atakapokuwa akiwachunga ng'ombe wake na kuwaongoza nyumbani kwa baba yake. Alisahau kwamba angeweza kushindwa. Njiani kurudi nyumbani alikutana na Mundula.


Wavulana wanamfuata Macho
Tegu alimwita, 'Mundula! Nifuate, nahitaji msaada wako.' Alifuatana na Mundula mpaka chini ya mti ambapo watakaa na wataweza kujificha huku wakiangalia kwenye nyumba ya mkutano ili kumwona Macho akitoka. Hapo alimweleza Mundula jambo analotaka kulifanya.

Mwanzoni Mundula hakujua la kusema kwa sababu alimhusudu Macho na kumwogopa Mfupa. Tegu akamwambia mwenzake, 'Si lazima tumwambie Mfupa habari zote tutakazozigundua.' Mundula alikubali, na kwa sababu wote walitaka sana kujua habari zaidi za yule mgeni mwenye kuvaa kinyago usoni, waliazimia kumfuata Macho mpaka wamjue alikuwa ni nani.

"Yulee!', alitamka Mundula wakati Macho alipotokea nje ya nyumba ya mkutano. Mgeni alisimama mlangoni na akatazama huko na huko polepole ili kuona iwapo kuna aliyekuwa akimwangalia. Uso wake uliwatisha mno vijana hao hata wakawa karibu wakimbie. Ghafula, Macho aligeuka na kwa vile hakumwona mtu, aliondoka haraka. Tegu na Mundula mara moja waliisahau hofu yao.

Walikuwa karibu Macho awapotee mara moja kwa sababu Wazee walitoka kwenye nyumba ya mkutano baada yake, na hao wavulana nao walingoja ili wasionekane wakimfuata Macho.

Mundula akamwambia mwenzake 'Mimi nimezoea zaidi kuwinda na kunyemelea vitu kuliko wewe, kwa hivyo niache nikutangulie.' Tegu alikubali shingo upande. Wakaenda kwa haraka kupita kijia kile alichopita Macho. Mundula akasema, "Tazama! Amepita sehemu ile wazi yenye nyasi na ameelekea kwenye kilele cha mlima Mvua. Tutaonekana ikiwa tutamfuata karibu karibu sana. Njoo, sasa tushike kijia hiki cha kushoto na tuzunguke kando ya bonde ili tufike mahali pale pale. Tuwe wa kwanza. Kisha tujifiche mpaka tuone njia atakayoishika.'



Vilimani
Wavulana wawili hao walikimbia wakipitia makondeni, wakayapita mashamba ya migomba wakielekea upande wa kusini, na walipanda mabonde mpaka wakafika kwenye vilele vya vilima. Kisha walizunguka mpaka wakafika kwenye kilele cha mlima Mvua ambako walijilaza kimya karibu na kijia ambacho Macho ilikuwa lazima akipitie.

Mundula akasema, 'Sijui yeye ni nani. Nina hakika kwamba yeye ni Fasi, baba yake Ngofu, aliyekucheka leo asubuhi.' Kwa hasira sana Tegu alijibu, 'Haiwezekani. Baba yake Ngofu ni dhaifu. Nalimwona kule kwenye nyumba ya mkutano. Nyamaza! Huyo anakuja!' Macho alionekana akitokea kwa mbali, na alikuwa anatembea mbio mbio. Alivuka sehemu iliyoinuka karibu na Mlima wa Mvua, akaelekea kwenye sehemu yenye majabali ambayo mbele yao kulikuwa na nchi tambarare. Wavulana hao walimfuata.

Upepo mkali ulikuwa unavuma na sehemu ya tambarare iliweza kuonekana ikiendelea katika sehemu kubwa. Vivuli vilikuwa vinaongezeka urefu, na Tegu alikuwa akiangalia mbingu kwa uso uliojaa mashaka mengi, sehemu aliyoiangalia zaidi ilikuwa ni ile ambayo jua linatua kama mpira mkubwa mwekundu, nyuma ya mawingu mengi.

Mundula alikuwa amesimama. "Tazama anakwenda kwenye nchi iliyokatazwa. Ni hatari sana kuingia sehemu hiyo wakati wa usiku. Mfupa anatuambia kuwa pepo pepo hukaa huko.' Tegu akaendelea mbele na akasema, 'Twende. Tutaendelea mbele zaidi kidogo tukimwangalia Macho. Hapawezi kuwa na hatari.'

Mundula akamwuliza, 'Lakini je, hujasikia habari za Pango la Pepo? Hakuna mtu anayethubutu kulikaribia hata ikiwa ni mchana. Mto unatoka vilimani nyuma yake na unavipanda vilima hata juu. Kisha mto hutelemka kwenye sehemu za tambarare. Sikiliza, unaweza kusikia radi inayofanywa na maji ya mto huo sasa.'


Macho anatoweka
Vijana walikuwa bado wanamfuata Macho, lakini sasa Tegu alikuwa akimtangulia mwenzake. Nchi ilikuwa imebadilika. Palikuwa na miamba mingi iliyovunjika na kuacha mapande mengi na hapakuwa na sehemu ambayo alama za nyayo zingeweza kuonekana au sehemu iliyokuwa na alama ya njia. Sauti ya maanguko ya maji iliweza kusikika wazi, sauti hiyo ililetwa na upepo uliovuma kuelekea walikotoka. Tegu akauliza, 'Pango la Pepo li namna gani?' Mundula akamjibu 'Watu wanasema ni pango lenye giza ardhini, sehemu ambayo unaweza kuisikia milio ya pepo na maombolezo ya marehemu. Sitaweza kupakaribia mahali hapo hata ikiwa ujira ni ng'ombe wote wa Mfupa.'

Tegu akamwambia kwa sauti, 'Tazama! Macho ametoweka.' 'Twende, turudi?' 'La, tutakwenda mpaka pale alipotowekea.' Walikwenda mpaka penye jiwe ambalo walimwona Macho akiliendea,`kisha walisimama kimya, hawakuweza kuendelea zaidi kwa ajili ya hofu waliyokuwa nayo. Karibu yao walisikia sauti za vilio na mayowe kama zile za watu wanaokufa. Mundula alitetemeka kwa hofu alipokuwa akimwonyesha mwenzake shimo lililokuwa karibu sana na mahali waliposimama. Popo wachafu waliruka kutoka shimoni wakati sauti nyingine ziliposikika kutoka chini. Mundula aligeuka na kukimbia akifuatwa na Tegu. Hawakupumzika mpaka walipokivuka kilele cha mlima Mvua na walipojiona wamefika salama kwenye bonde.
 
SURA YA TATU

NCHI ILIYOKATAZWA

MFUPA alishangazwa sana alipoambiwa na Tegu kwamba Macho amekwenda kwenye nchi iliyokatazwa, na kwa mara ya kwanza, Tegu alidhani aliona dalili ya woga katika macho ya Mfupa. Mfupa akamwuliza 'Je, huyo mgeni alifanya nini alipofika mahali hapo?'

'Alikwenda zake'. 'Unataka kusema kwamba alikupotea?' 'La, hasha, alikwenda chini ya ardhi.' Mfupa akaendelea, 'Hiyo haiwezekani. Labda alikuona unamfuata, na akajificha kati ya miamba, kisha akaenda zake kwao kwa njia nyingine.'

Tegu akamjibu, "Tulikuwa tukimwangalia ili kuona iwapo atafanya hivyo, lakini tulipofika mahali alipokuwa ametoweka, tulijiona sisi wenyewe tupo karibu na Pango la Pepo. Hapo ni mahali panapotisha sana na ilitupasa kukimbia upesi sana.'

Mfupa akasema, 'Ni kweli hapo ni mahali panapotisha sana.' Kisha alisimama kimya kwa muda mrefu. Tegu akamwambia, 'Nataka ng'ombe wangu watatu.' Mfupa akamjibu, ‘Lakini hujaifanya kazi niliyokupa. Hujaniambia mtu yule ni nani, au anakaa wapi!' Tegu akasema, 'Mimi nimefanya mambo makubwa zaidi kuliko ambavyo wengine wangalifanya. Hata Mundula alitaka kurudi.' Mfupa akamwambia, 'Inawezekana, lakini tuliwekeana ahadi, na wewe hukuniambia yale niliyotaka kuyajua'. Tegu alikasirika akasema, 'Kama unakataa kunipa ng'ombe, basi sitakuambia lo lote ambalo nitagundua siku zijazo.' Baada ya kusema hayo alianza kugeuka ili aondoke lakini Mfupa alimzuia.

Mfupa akamwambia, 'Nitakupa ng'ombe mmoja sasa, na wengine wawili nitakupa utakapokwisha kuifanya kazi yangu.' Tegu alipewa ng'ombe mmoja mzee aliyekonda, ambaye alikwenda naye kwao.


Goja anazisikia habari za Macho
Mara alipofika nyumbani Tegu aliuliza, 'Baba yuko wapi?' Mama yake akamjibu, 'Sijui. Lakini natumaini atakuwapo hapa chakula kitakapokuwa tayari, kama watu wote wanavyofanya.' Tegu akauliza, 'Tutakula nini mama?' Mama akajibu, ‘Chakula cha kawaida-kande na ndizi. Unaweza kula viazi ukipenda.' Tegu akasema kwa utulivu, 'Iko nyama huko nje.' Nata akastuka akasema, 'Nyama! Umeipata wapi?' 'Nimempata ng'ombe, lakini ni mzee na hafai kufugwa.' Mama yake akasema, 'Haya basi achinjwe upesi kabla baba yako hajafika. Asipochinjwa kabla hajaja, basi atakuambia umfuge. Jamani nyama! Siwezi kukumbuka ni lini nilipokula nyama mara ya mwisho. Nenda ukamchínje na mimi ninakiweka chungu tayari.'

Katikati ya matengenezo yao, ndipo Goja alipofika. Alipokaribia moto alionekana anakoga majasho na punde tu alilitupa chini gogo zito la mti.

Goja akauliza kwa sauti kali kidogo, ‘Mnafanya nini hapa? Ng'ombe wa nani huyu anayechinjwa?' Tegu akajibu, 'Ni ng'ombe wangu, baba!' Goja akamwuliza, 'Wako? Ulimpataje?"

Ndipo Tegu alipoanza kumsimulia baba yake hadithi ya kushangaza ya Macho na jinsi Mfupa alivyomwajiri. Alistaajabu kumwona baba yake alivyocheka badala ya kumkasirikia kwa ajili ya kumchinja ng'ombe.

Mara Tegu akamwuliza baba yake, 'Mbona unacheka?' Nacheka kwa vile Mfupa alivyoweza kushindwa kijanja kabisa. Umeniambia Macho ni mrefu. Ana urefu gani? Je ni mrefu kama mimi?' Tegu akamjibu, 'Ni mrefu zaidi yako, baba. Pia ana sauti ndogo.'


Wazee wanaomba mashauri zaidi
Nata aliacha shughuli zake kwa muda na akayasikiliza mazungumzo yao. Kisha akatazama njiani, akasema, 'Watu wanaweza kuisikia harufu ya nyama kutoka umbali wo wote.' Mara wazee walionekana kwenye mwangaza wa moto. Wazee walikaa ndani ya nyumba. Baada ya kuamkiana, mmoja wao alisema, "Ulimi wa ng'ombe ni chakula ninachokipenda sana.' Nata hakujibu neno, bali aliendelea kupika. Mumewe akawaambia wale wazee, 'Hamna budi kula chakula pamoja nasi. Lakini mbona mmekuja wakati huu?'

Mzee mmoja akasema, 'Hukufika kwenye mkutano leo.' Goja akajibu, 'Sikufika, maana sikutaka kumwona Mfupa akikalia Kiti cha Ufalme'. 'Unajua yaliyotokea?" Goja akamjibu, 'Ndiyo, mwanangu amenisimulia kila kitu.' Mzee akamwambia, 'Lilikuwa ni jambo la kustaajabisha sana. Watu walimwita Macho, na alipozungumza nasi alionyesha kuwa ni mtu mwenye hekima. Lakini haikuwa rahisi kuongea na mtu aliyevaa kinyago usoni. Ingalikuwa ni jambo jingine kama tungalimjua yeye alikuwa ni nani. Je, unatushauri tufanye nini siku za usoni, Goja? Tuyafuate mashauri yake au tuukatae uongozi wake na tumwulize kuwa yeye ni nani?' Goja akajibu, 'Kinyago ndicho nguvu yake. Labda watu wasingemsaidia kama wangemjua yeye alikuwa ni nani. Hapo basi, Mfupa angekikalia Kiti.'

Msemaji wao akanena, ‘Tunafurahi kwa kuwa ametuokoa na hilo. Hivyo unatushauri tumkubali Macho kuwa kiongozi wetu na kwamba tumfuate?' Goja akajibu, 'Naam, mfuateni katika mambo yote na zaidi katika kumpinga Mfupa.' Mzee mmoja akawaambia, 'Kuna habari zinazosema kwamba askari wa vita wa Wakamba wameonekana kwenye mitelemko ya vilima vilivyopo upande wa magharibi ya kaskazini. Inawezekana kuwa wana mpango wa kuvishambulia vijiji vyetu, na itatupasa tuite mkutano mwingine ili tufikirie tufanye nini. Je, utahudhuria? Goja akamjibu, 'Nitajaribu lakini nina kazi nyingi.

Tegu aliangalia gizani na huku akiwaza, 'Sijui baba yangu atafaa jambo gani huko mkutanoni ?' Adui ni huyo anataka kushambulia katika milima ya Pare, na baba yake hashughuliki hata kidogo.


Macho na Mfupa mkutanoni
Siku ya pili yake, Kichechi alizikwa. Mfupa alijifanya kana kwamba anaongea na roho ya marehemu ambaye, Mfupa alisema, alimchukia sana Macho, na alimweleza Mfupa kuwa ni mtu pekee anayefaa kuwatawala Wapare.

Mfupa aliwaelekeza Wazee fimbo yake nyeusi na akawaita wapumbavu. Wazee walikasirika sana na walichoshwa mno na mazungumzo yake ambayo hayakuwa na mwisho, waliamuru ngoma zipigwe ili kuwaita watu mkutanoni mara tu Chifu akishazikwa. Walipokuwa wakikimbilia mkutanoni, watu walishangaa kutatokea kitu gani huko.

Tegu aliwaangalia Wazee walipokuwa wanakaa kwenye viti vyao katika sehemu iliyoinuliwa mle nyumbani. Kiti kimoja kilichokuwa katikati kiliachwa kitupu. Macho aliingia kwa mlango wa pembeni na kila mmoja alimwangalia akitembea mpaka kwenye Kiti cha Ufalme na kukikalia; kinyago alichokivaa usoni kilikuwa kikiwalekea watu na vazi lake la nyasi la kiunoni liliyafunika magoti yake.

Mfupa aliingia wakati ngoma ziliponyamaza, akiwa mwenye uso wenye hasira sana. Alikaa kwenye kiti cha mbele chini ya sehemu waliyokaa Wazee, joho lake la ngozi za nyani na kofia yake nyeupe ilimtofautisha na watu wengine. Baada ya watu wote kukaa, Macho alisimama na akaanza kusema. Sauti yake ilikuwa ndogo wakati ilipokuwa ikitoka nyuma ya kinyago alichokivaa.


Mpango wa Macho unakubaliwa
"Tumesikia kwamba askari wa Wakamba wapo karibu na vijiji vyetu kwenye kingo za vilima vilivyopo upande wa magharibi ya kaskazini. Watu wetu wanaoishi kati ya Butu na Ngulu wamo hatarini, ulinzi mkubwa unapaswa kufanywa ili habari zo zote za mashambulio yao ziweze kupatikana mara moja bila kuchelewa. Mtu yoyote akishindwa kuutimiza wajibu wake hana budi kuadhibiwa. Ingawa sisi ni watu tunaotaka kuishi kwa amani bila vita, huenda ikawa ni lazima tupigane. Ni lazima tukae tayari. Ni wajibu wetu kuona kwamba kila kijana amefundishwa vema na aweza kuipigania nchi yetu na watu wake. Watu walio mabingwa wa kupigana vitani wawafundishe vijana wetu mara moja. Hatuna budi kufanya kila tuwezalo ili kuiondoa hatari inayoweza kuletwa na Wakamba wale wakaao upande wa magharibi ya kaskazini na Wamasai waishio kusini.'

Moyo wa Tegu ulijaa mapenzi kumpenda mgeni huyu shujaa, na alilisikiliza kila neno alilolisema kwa uangalifu mkuu. Macho aliendelea kusema huku akimwangalia Mfupa kusudi, 'Kichechi amekuwa mgonjwa kwa muda wa siku nyingi. Utawala wake ulikuwa dhaifu, na wale waliomshauri walifikiria njia za kujiongezea uwezo wao zaidi kuliko usalama wa raia. Ni lazima tuwe na nguvu ikiwa tunataka kuishi kwa amani.'

Macho akakaa, na watu walipiga makelele ya shangwe kuonyesha kwamba walikubaliana naye.

Wazee wengi walitazamana na kuonyesha kwamba walikuwa wameridhika, isipokuwa wafuasi wachache tu wa Mfupa. Vijana waliingiwa na msisimko mkubwa na waliendelea kupiga vifijo mpaka Mfupa aliposimama na kusema.

Umezungumza mengi', alimwambia Macho, 'lakini tutajuaje kwamba wewe ni mtu wa kufaa kutuongoza? Tungaliweza kuona uso wako, tungeweza kufahamu kwamba labda u mwoga. Hebu jifunue ili watu wauone uso wako. Acha watu wakufahamu wewe u nani na unatoka wapi.'

Macho alikaa kimya kwa muda na kisha akamjibu, ‘Umekwisha jaribu kutafuta mahali ninapoishi, Mfupa. Haya basi, wale wenye shaka na mimi wanifuate. Wale walio na ujasiri wa kutosha kunifuata mpaka mwisho, watanijua mimi ni nani.'


Watu wanamfuata Macho
Macho alitoka nyumbani na watu wote wakamfuata. Tegu hakuwa na raha kidogo. Alistaajabu jinsi Macho alivyofahamu kwamba Mfupa alikuwa akijaribu kupajua mahali anapokaa. Je, Macho aliwaona wakati walipokuwa wakijificha kwenye nchi iliyokatazwa? Tegu akawaacha watu watangulie. Alitembea taratibu nyuma nyuma mpaka alipomwona rafiki yake. Wakati huo watu walikuwa wakipita makondeni wakimfuata Macho.

Mundula akauliza, ‘Je, unadhani anafahamu ni nani waliomfuata jana? Tegu akamjibu, 'Nadhani anajua kila kitu. Nasikitika kwa sababu nataka anifikirie mema,' Mundula akamjibu, 'Nami pia nataka hivyo. Namchukia Mfupa.' Mundula akaendelea kuuliza, ‘Unajua Macho anatupeleka wapi? Hivi sasa tumekaribia sana kilele cha mlima Mvua.'

Tegu akasema, 'Ikiwa anatupeleka katika nchi iliyokatazwa, watu wachache tu watamfuata.'

Watu walipokuwa wakipita bondeni wakiwa katika mlolongo mrefu, watoto walijificha nyuma ya mama zao, na wanawake waliacha kazi zao ili kuona kulikuwa kuna nini. Watu waliokuwa nyuma walikuwa bado hawajaanza kuupanda mtelemko uendao kwenye kilele cha Mlima Mvua muda watu waliokuwa mbele walipotambua kwamba walikuwa wakienda kwenye nchi iliyokatazwa. Baadhi yao walianza kupunguza mwendo.

Mtu mmoja akamaka, ‘Anatupeleka kwenye nchi iliyokatazwa.' 'Mimi siendi,' akajibu mwingine. Mtu wa tatu akasema, 'Ni salama zaidi kwenda huko wakati wa mchana.' Askari shujaa akajibu. 'Ikiwa Macho anaweza kwenda huko kwa salama, basi nami naweza.' Kwa ajili ya maneno hayo wengi waliokuwa karibu kurudi waliazimu kuendelea na safari yao.


Mfupa anaogopa
Walipofika mahali ambapo miamba iliyovunjika iliifunika ardhi juu ya majabali, walisikia sauti za maanguko ya maji kwa mbali. Hapo, watu wengi walisimama. Hata Wazee nao walipunguza mwendo, lakini Mfupa aliendelea mbele pamoja na wale waliojipa moyo wa kumkaribia Macho. Katika kundi hilo walikuwamo Tegu na Mundula ambao walifanya haraka sana ili wamwahi. Mfupa akasema, 'Angalia usije ukatumbukia ndani ya Pango la Pepo. Utakuwa ni mtu shujaa kama ukilikaribia Pango hilo.' Uso wa kinyago na vazi lile la kichwa vilimgeukia Mfupa na kumjibu, 'Sitalikaribia tu, bali nitaliingia.'

Mfupa akauliza, 'Ulisema utaingia ndani ya Pango?' Wakati huo Mfupa alikuwa amejaa woga mwingi usio kifani na hata ilikuwa vigumu kusikia sauti yake. 'Ndiyo!,' akajibu Macho, na hapo walikuwa wakilikaribia shimo. Kama watu ishirini tu walikusanyika karibu na wengine wakiliangalia kwa mbali. Wale waliokuwa karibu walitetemeka kwa hofu waliposikia sauti kutoka chini.

Tegu akamwambia Mundula, 'Sauti hizi zilitisha zaidi jana jioni kuliko leo'. Kisha Tegu akamgeukia Mfupa na akaona kwamba mchawi alikuwa akijaribu kuificha hofu yake.'

Macho akapaaza sauti yake kwa nguvu akasema, 'Wakati umefika. Nifuate sasa Mfupa, na utagundua ninapoishi.' Baada ya kuyasema maneno hayo, aliingia pangoni mara moja na akatoweka kabisa. Watu wote walikuwa kimya kwa muda na kisha ukelele ulisikika kutoka kwenye Pango, na kisha sauti kubwa ilisikika ikigunia, 'Njoo, Mfupa. Mimi ninakungojea.'

Mfupa alilipa kisogo pango. Akachungulia nyuma kidogo mara moja na halafu akakimbia. Kicheko kikubwa na sauti ya kuguna ilisikika kutoka pangoni baada ya kuondoka kwake.

Macho akatokea tena nje akasema, 'Mtu mwaminifu hana haja ya kuogopa lakini mtu yoyote haruhusiwi kuingia katika nchi iliyokatazwa bila idhini yangu."
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom