Mtoto Elijah (Jina si halisi) atoroka nyumbani kukwepa ukatili kutoka kwa Mama wa kambo, Akatishwa masomo ghafla ili kuuza mkaa na kuchunga mifugo

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
#SimuliziZa116 - Ilikuwa tarehe 5 Novemba 2019 tulipopokea simu ya msamaria mwema kutoka kata ya Nyehunge mkoani Mwanza ikieeleza kuwa; “Kuna mtoto mmoja hapa mtaani kwetu anayejulikana kwa jina la Elijah mwenye umri wa miaka 11 ambaye anapitia unyanyasaji na ukatili wa hali ya juu kutoka kwa mlezi wake. Mtoto huyo awali alikataliwa na mzazi wake wa damu na kwenda kuishi na mama yake wa kambo katika Kijiji cha Kahunda Ruhuma wilayani Buchosa.

Kutokana na hali ngumu ya maisha na ukatili wa hali ya juu aliofanyiwa na mama yake wa kambo, Elijah alichukua uamuzi wa kukimbilia Kijiji cha Nyehunge na kupokelewa na mlezi anayeishi nae nyumbani hapo kwa kibali cha Mtendaji wa Kijiji huku makubaliano yakiwa Elijah kuandikishwa shuleni mara moja maana hakuwahi kuipata haki hiyo ya msingi tangu akiwa nyumbani kwao”.

Msamaria huyo aliendelea kueleza kuwa, Mlezi huyo alimuandikisha Elijah shuleni kama makubaliano kati yake na Mtendaji yalivyotaka ingawa baada muda mfupi makubaliano hayo yaligubikwa na sintofahamu pale mlezi alipomkatisha masomo ghafla na kumuachisha shule Elijah kisha kumpeleka kwenye biashara za kuuza mkaa na kuchunga mifugo. Mnamo Tarehe 07 Novemba 2019, Mtoa ushauri katika Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto alimtafuta Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza kwa njia ya simu ili kujua kinaganaga cha kesi hiyo;

“Nililifuatilia kwa ukaribu suala la mtoto Elijah hasa maendeleo yake shuleni na kugundua kuwa alisoma kwa siku 4 pekee katika kipindi cha mwezi Januari alipoandikishwa hadi mwezi Novemba alipokatishwa masomo. Mara moja nilimwandikia barua mlezi wake kutaka kufahamu nini kilichomsibu hadi kupelekea kumkatisha masomo Elijah. Nikutaarifu ndugu mshauri kuwa kwenye barua niliyomuandikia pia nimemuomba tukutane tarehe 26 Novemba 2019 kwa ajili ya mazungumzo zaidi” - Alieleza Afisa Ustawi.

Ilipofika tarehe 28 Novemba 2019 Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kupitia moja kati ya washauri wake kilimtafuta Afisa Ustawi Wilaya ya Buchosa ili kujua muendelezo wa kesi ya Elijah. Afisa alieleza kuwa mazungumzo kati yake na mlezi wa Elijah juu ya ukiukwaji wa makubaliano yaliyolenga maslahi mapana ya mtoto yalifanyika. Mlezi alikiri kumkatisha masomo Elijah bila sababu za msingi na hivyo kuomba msamaha kwa alichokifanya.

Haikuishia hapo, bali pia Afisa Ustawi kwa nafasi yake alimshauri mlezi wa Elijah juu ya kanuni na taratibu zinazomhusu mtoto kwa kuitumia Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inayoweka bayana vipengele adhimu vinavyohusu maslahi ya mtoto hususan ya kimasomo. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, Mlezi wa Elijah alipata kumuelewa vyema Afisa Ustawi na hivyo kufikia makubaliano yaliyoambatana na uwekaji saini kwenye andiko maalum linaloangazia ulinzi wa mtoto na maslahi yake.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia kurasa zetu wa Facebook, Instagram na JamiiForums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Back
Top Bottom