BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki limeingia katika mtihani mwingine, baada ya Mchungaji Christopher Mtikila, kuweka pingamizi la kuapishwa kwa wabunge wa Bunge hilo kwa madai ya kukiuka Ibara za 50 na 51 ya Mkataba wa Jumuiya hiyo.
Bunge hilo lilikwama kuapishwa mwishoni mwa mwaka uliopita, baada ya Serikali ya Kenya kushitakiwa katika Mahakama ya Jumuiya hiyo, kwa madai ya kukiuka Mkataba huo, ambapo Serikali ya Kenya ilipigwa mwereka na kukwamisha Bunge hilo kuapishwa hivyo kukata rufaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bw. Mtikila alisema baada ya waliokuwa wabunge wa Bunge hilo, Dkt. Harrison Mwakembe na Bi. Beatrice Shekilango kuwa wabunge wa Bunge la Tanzania na kuwachagua Dkt. Norman Sigala na Bi. Hilda Kibacha, ilitakiwa kuchagua wabunge saba tu, ili kukamilisha idadi ya wabunge tisa.
Alisema kwa mujibu wa Mkataba huo, mbunge anatakiwa kuwa madarakani kwa miaka mitano, hivyo kuwaengua wabunge waliochaguliwa Machi mwaka jana ni kosa, kwani kwa mujibu wa Mkataba, sasa wabunge kutoka Tanzania ni 11 kutokana na wabunge waliochaguliwa awali kutochaguliwa kisheria.
Dkt. Sigala na Bi. Kibacha kwa mujibu wa Mkataba ni wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, ukiongeza wabunge tisa waliochaguliwa baadaye jumla Tanzania ina wabunge 11 jambo ambalo ni kinyume na mkataba huo
tumepinga hilo katika Mahakama hiyo kwa kesi namba 2 ya mwaka huu,alisema Bw. Mtikila.
Alisema pamoja na kutaka wabunge hao wawili watambuliwe, pia uchaguzi wa wabunge wengine haukua sahihi, kwani kwa mujibu wa Mkataba, wabunge wanatakiwa kutoka vyama vya siasa vya kiraia na jumuiya za kijinsia, jambo ambalo halikufuatwa, hivyo ujumla wabunge hao hawakuchaguliwa kihalali na wachaguliwe upya kwa utaratibu uliowekwa na Mkataba huo.
Lengo ni kuishikisha adabu CCM iache ukiritimba wa kuamua kufanya mambo yao wanavyotaka na si inavyotakiwa
kila Mkataba wa Jumuiya hiyo upo wazi, hivyo hakuna sababu ya kufanya mambo nje ya utaratibu huo kesi yetu iko chini ya Kampuni ya Audax & Company Advocates, aliongeza Bw. Mtikila.
Kesi ya kuwazuia wabunge wa Kenya kuapishwa baada ya Serikali kushindwa katika kesi hiyo na kukata rufaa, ilifikia mwisho juzi ambapo hukumu yake inatarajiwa kutolewa Jumanne ijayo.
Akizungumzia juu ya maoni yanayoendelea kuhusiana na kuanzishwa kwa Shirikisho, Bw. Mtikila alisema ni kinyume cha Katiba ya Tanzania na chama chake DP kinajiandaa kuweka pingamizi mahakamani kuhusiana na suala hilo.
Alisema nchi ni ya wananchi na hakuna kiongozi mwenye mamlaka na nchi hii, hivyo kila Mtanzania ana uhuru wa kushiriki kujiunga katika Jumuiya hiyo na Shirikisho kwa ujumla
Chanzo:-
http://www.majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=2228