Mtazamo wa Mwalimu katika Ujamaa, Ubepari na Ufisadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mtazamo wa Mwalimu katika Ujamaa, Ubepari na Ufisadi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Simple, Dec 20, 2009.

 1. Simple

  Simple JF-Expert Member

  #1
  Dec 20, 2009
  Joined: Feb 6, 2009
  Messages: 249
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 35
  Profesa Issa Shivji
  Disemba 16, 2009

  Oktoba 12 mwaka huu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, iliandaa Kongamano la Kumbukumbu ya Miaka 10 tangu afariki Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Kati ya waliowasilisha mada katika kongamano hilo ni Profesa Issa Shivji, Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyezungumzia mtazamo wa Mwalimu Nyerere wa Ujamaa, Ubepari na Ufisadi. Tunaichapisha mada hii wiki hii kutokana umuhimu wake katika maisha ya sasa ya Watanzania wengi.

  Utangulizi KICHWA cha habari cha mada hii ni kigumu kidogo. Siwezi nikazungumza bila uchambuzi wa muktadha wake. Ningekuwa mwanasiasa au mwanahabari labda ningejiingiza kwa jazba katika malumbano kuhusu ufisadi kati ya wanaoitwa wapambanaji kwa upande moja, na watetezi, wa ufisadi, kwa upande mwingine.

  Lakini mimi si mwanasiasa, ingawa ninapenda siasa. Wanasiasa huwa hawapendi siasa, wanapenda madaraka! Mimi ni msomi, mwanazuoni. Wajibu wangu ni kujitahidi kuchambua viini vya mambo; si kuelezea yale ambayo ni wazi na yanaonekana.

  Mtazamo wa Mwalimu juu ya mambo haya hauwezi kuelezwa wala kuuelewa bila kuchambua mtazamo na mwelekeo wake juu ya mfumo wa kiuchumi na kisiasa. Mwalimu alikuwa mjamaa. Alikuwa anapinga ubepari. Mwalimu alikuwa mzalendo wa Kiafrika. Alikuwa anapinga ubeberu. Mwalimu alikuwa mpigania ukombozi wa binadamu. Alikuwa anapinga dhuluma na ukandamizwaji.

  Kwa hivyo, mtazamo wake juu ya masuala mbalimbali, pamoja na rushwa na ufisadi, ulijikita kwenye imani yake ya kijamaa na upinzani wake kwa ubepari na ubeberu.


  Katika kuwasilisha mada hii, nitazungumzia kwa muhtasari tu, dhana na misingi mikuu ya mfumo wa ubepari, ujamaa na ubeberu wa uliberali mamboleo, ambayo ni sura mpya ya mfumo wa kibepari. Na baada ya kuweka misingi hii, ndipo nitagusia suala la ufisadi.

  Dhana zenyewe

  Ujamaa ni imani, ndivyo alivyoamini Mwalimu Nyerere kwa muda mrefu kabla ya Azimio la Arusha. Ingawa, nionavyo mimi, baadaye alikuja kubadili msimamo huo, hasa, ukiangalia sera za serikali yake baada ya Azimio la Arusha. Kwa vyovyote vile, Mwalimu hakuamini, wala sikumbuki kwamba alisema waziwazi kwamba anaamini kwamba ubepari ni imani. Ubepari ni mfumo, si imani.

  Nikitumia msamiati wa Azimio la Arusha, ubepari ni mfumo wenye tabaka mbili: ‘tabaka la chini la watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka la juu la watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi.’ Wanaoishi kwa kufanya kazi ndio wavujajasho na wanaoishi kwa kufanyiwa kazi ndio wavunajasho. Kwa maana hii, msingi mkuu wa mfumo wa kibepari ni unyonyaji wa kitabaka. Na unyoyaji hautokani na nia mbaya ya mtu binafsi bali ni msingi wa mfumo wenyewe bila kujali nia au dhamira za watu waliomo katika mfumo huo.

  Matabaka haya mawili ni matabaka makuu ya mfumo ambao huainisha mfumo huo wa uzalishaji kama ubepari. Lakini pia, katika hali halisi ya nchi au jamii, kutokana na historia yake, kunaweza kukawa na matabaka mengine ya kati na ya chini na pia aina mbalimbali za vikundi vya kibepari na wafanyakazi. Kwa mfano, kuna tabaka la kati ambalo katika siasa-uchumi huitwa vibwanyeye, au kwa Kiingereza petty bourgeoisie. Kwa lugha nyepesi tunaweza tukayainisha matabaka haya matatu kama walalaheri, walalahai na walalahoi.

  Ili mfumo wa ubepari uendelee – yaani uwe endelevu – hakuna budi bepari ajilimbikize mtaji unaotokana na ziada anayonyonya kutoka kwa wafanyakazi. Na mtaji huo anautumia kuwekeza ili kuendelea kumnyonya mvujajasho. Ulimbikizaji mtaji ndio kiini cha mfumo wa kibepari. Uhai wa bepari kama bepari hutegemea ulimbikizaji. Bila ulimbikizaji bepari hawezi kuishi kama bepari.

  Maslahi ya matabaka hugongana kwa sababu daima wavujajasho hutaka kupunguza juhudi yao ya kuzalisha ziada wakati, kwa upande mwingine, bepari hutaka ziada zaidi na zaidi. Migongano hii ya maslahi ya kitabaka ndiyo huzaa mapambano ya kitabaka. Ingawa mapambano haya huchukua sura mbalimbali, kamwe huwezi ukawa na mfumo wa kitabaka ambao hauna mapambano. Ili kuthibiti mapambano hayo yasije yakapasua mfumo wenyewe, unahitaji chombo cha mabavu; chombo hicho ni dola. Na dola hutafuta uhalali wa kisiasa ili matumizi ya mabavu yakubalike kwa wote ingawa kiini chake ni kuulinda mfumo wa kibepari.


  Basi tuzijumuishe sifa kuu za mfumo wa kibepari. Hizi ni: Mfumo wa kitabaka wenye matabaka mawili makuu, tabaka la wavujajasho ambalo huzalisha ziada na tabaka la wavunajasho ambalo hunyonya ziada. Ulimbikizaji na uwekezaji wa mtaji ambao hutokana na ziada ili kuendeleza uzazi wa mfumo wenyewe.

  Migongano ya maslahi ya kitabaka ambayo huzaa mapambano ya kitabaka.
  Chombo cha kisiasa, yaani dola, ambacho huhodhi mabavu, kuyadhibiti mapambano ya kitabaka kwa minajili ya kuhakikisha kwamba mfumo haupasuki au kupinduliwa.
  Ujamaa
  Ujamaa ni kinyume cha ubepari, ni mfumo mbadala au mkabala wa ubepari.

  Azimio la Arusha linaeleza dhana ya ujamaa kwa ufasaha; sinabudi ninukuu:
  Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanya kazi; haina ubepari wala ukabaila. Haina tabaka mbili za watu: tabaka la chini la watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka la juu la watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi. Katika nchi ya Ujamaa kamili mtu hamnyonyi mtu, bali kila awezaye kufanya kazi hufanya kazi, na kila mfanya kazi hupata pato la haki kwa kazi aifanyayo na wala mapato ya wafanya kazi mbali mbali hayapitani mno.

  Kwa maana hiyo, Azimio liliweka wazi kwamba Tanzania haikuwa nchi ya kijamaa. Azimio likasema wazi kwamba Tanzania ina ‘misingi ya ubepari na ukabaila na vishawishi vyake. Misingi hii ya ubepari na ukabaila yaweza ikapanuka na kuenea.’ Kwa hivyo, nia na dhamira ya Azimio ilikuwa kuzuia misingi hii ya kibepari isipanuke na kuenea. Azimio likaenda mbali kwa kuchukua hatua ili misingi ya kibepari isipanuke na kupanda misingi ya kujenga Ujamaa.

  Hatua hizi zilikuwa za awali kabisa na muhimu kati ya hizo ni:
  Utaifishaji wa njia kuu za uchumi na kuweka umiliki na umenejimenti wake katika mikono ya Serikali au dola kwa maana ya kwamba dola ndio lilikuwa limechukuliwa kama mwakilishi wa wafanyakazi na wakulima, yaani chombo cha umma.

  Sera ya kujitegemea badala ya utegemezi kwa maana ya kutegemea misaada na mikopo kutoka nchi za nje. Umuhimu wa kujitegemea ulikita kwenye mambo mawili: moja, kwamba huwezi ukawa na uhuru wa kujiamulia mambo yako kama unamtegemea mwingine; na, pili, kwa vyovyote vile, hakuna mjomba huko nje ambaye atakusaidia kukuletea maendeleo.

  Gurudumu la maendeleo ni wafanyakazi na wakulima; kwa hivyo kwa mambo yote muhimu matabaka haya ya chini ndiyo yategemewe; yashirikishwe katika vyombo vya maamuzi na yapewe kipau mbele katika kuwapatia huduma za kijamii – afya, elimu, maji n.k. Kwa maneno mengine, maendeleo yawe maendeleo ya watu, si vitu au watu wachache.

  Azimio lilitambua kwamba haitoshi kuweka umiliki wa njia kuu za uchumi katika mikono ya dola kama dola yenyewe si dola ya wafanyakazi na wakulima. Pili, ni wazi kwamba ukiweka njia kuu za uchumi mikononi mwa dola maana yake ni kwamba umewapa viongozi na watendaji wa dola fursa kubwa ya kujinufaisha badala ya kuleta maendeleo ya nchi na kustawisha hali ya matabaka ya chini.

  Ndiyo maana Azimio lilisisitiza mambo mawili:
  Moja ni umuhimu wa demokrasia. Serikali iwe serikali ya kuchaguliwa na ya wakulima na wafanyakazi.

  Pili, ni kwamba kiongozi na mtendaji wa ngazi ya juu na kati ya dola na mashirika yake pamoja na ya chama asiwe bepari au kabaila na asiweze kutumia nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali au kuishi maisha ya anasa kwa jasho la wananchi.

  Ndiyo maana Azimio likaweka miiko ya uongozi. Kwamba kiongozi:

  • Asiwe na hisa katika makampuni yoyote.
  • Asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.
  • Asiwe na mishahara miwili au zaidi.
  • Asiwe na nyumba ya kupangisha.
  Na kiongozi maana yake ni mtu au mtu na mkewe au mke na mumewe. Na viongozi waliorodheshwa kama wajumbe wa vyombo vikuu vya chama, mawaziri, wabunge, wakuu wa vyama vilivyoshirikishwa na TANU, wakuu wa mashirika ya serikali, madiwani, watumishi wa serikali wenye vyeo vya juu na kati.

  Je, Azimio lilifanikiwa kujenga msingi imara wa Ujamaa? Na, kama halikufanikiwa ni kwa sababu gani? Lilikuwa na mapungufu yapi? Jambo hili limezungumzwa na kujadiliwa na wanazuoni. Lakini si nia yangu kulichambua jambo hili katika mada hii isipokuwa ni kuwakumbusha tu, hasa vijana wetu, kwamba chama chenyewe, yaani CCM, kilifanya tathmini ya miaka 14 ya Azimio katika Mwongozo wake wa mwaka 1981.

  Mwongozo huu unazungumzia kwa ufasaha na uwazi mapungufu ya Azimio na unatoa hoja ambazo zinaweza kutusaidia kuelewa vizuri hatma ya mwelekeo na mtazamo wa itikadi ya Ujamaa.

  Hoja ya msingi iliyotolewa na Mwongozo ni kwamba chini ya mwavuli wa Azimio na mashirika ya umma, lilijengeka tabaka jipya la mabepari wa kirasimu ambalo siku hadi siku lilikuwa likijipatia nguvu ya kudhoofisha na kuhujumu Ujamaa pamoja na hata kudiriki kubadili msimamo wa Azimio. Na lilijipatia nguvu zaidi mnamo miaka ya 80 kutokana na hali mbaya ya uchumi na kipindi kigumu cha miaka ya 1981-85, kabla ya Mwalimu kung’atuka.

  Bila kutoa uchambuzi kamili, kwa sababu hakuna muda wa kutosha, ninatoa hoja kwamba ingawa CCM ilifanya tathmini sahihi katika Mwongozo wa mwaka 1981, ilishindwa mbele ya tabaka hili la mabepari wa kirasimu. Na tabaka hili ndilo, likiungwa mkono na vyombo na taasisi za kibeberu, likageuza kibao.

  Nchi ikaingizwa kichwa kichwa katika mfumo wa uliberali mamboleo. Uliberali mambo leo ni sura ya ki-utandawazi ya mfumo wa kibepari wa kimataifa, kwa jina lingine, ubeberu.


  Uliberali mamboleo

  Misingi mikuu ya mfumo wa uliberali mamboleo ni:
  • Ulegezaji wa masharti ya biashara ya nje na ndani, kwa maana, ya kwamba serikali haidhibiti tena biashara.
  • Ulegezaji wa masharti ya soko la fedha na fedha kwa jumla kwa maana kwamba yeyote yule anaweza akaingiza na kutoa fedha nchini bila kudhibitiwa. Kwa kifupi, kuwa na soko huria katika bidhaa na fedha.
  • Dola kujitoa katika shughuli za uchumi, pamoja na hata katika sekta za huduma za kijamii kama elimu, afya, maji, umeme n.k.
  • Ubinafsishaji wa mashirika ya umma.
  • Ubidhaifishaji wa ardhi, misitu, maji, wanyama pori, na hata milima na mito, pamoja na ubidhaifishaji wa huduma za elimu, afya, maji, umeme n.k.
  • Uwezeshaji wa wawekezaji kutoka nje na ndani.
  Haya yote yanakuja kama masharti ya wafadhili na taasisi za kibeberu. Kwa hivyo, basi, pamoja na mahubiri ya kidemokrasia na utawala bora, serikali inapoteza uwezo na haki yake ya kujiamulia mambo muhimu ya sera na mwelekeo wa nchi kwa faida ya watu wake.

  Ufisadi

  Je, ufisadi ulikuwapo enzi za Mwalimu? Hapana haukuwapo. Je, rushwa ilikuwapo? Ndiyo ilikuwapo. Wakati wa Mwalimu wala hatukuwa na msamiati wa ufisadi. Kwa hivyo, Mwalimu hakuzungumzia ufisadi; lakini alizungumzia sana rushwa. “Rushwa ni adui wa haki,’ alirudiarudia kusema. Sasa tofauti ni nini?

  Rushwa ni kishawishi unachotoa ili mpokeaji aipinde sheria au taratibu rasmi kwa kumrahisishia mambo yake mtoaji. Mtu akimpa chochote tarishi wa mahakama ili amtafutie faili lake au alifiche faili la mpinzani wake, hii ni rushwa. Bila shaka hongo yenyewe ni ndogo na mpokeaji ataitumia kwa mahitaji yake ya lazima au ya binafsi. Rushwa ya aina hii ilikuwapo wakati wa Mwalimu lakini haikuzagaa sana isipokuwa ilianza kuongezeka katika kipindi kigumu cha uchumi mwishoni mwa miaka ya 1970 na 1980.

  Mtumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) akikupatia nafuu katika kiwango cha kodi kwa kushawishiwa na hongo, hii pia ni rushwa. Lakini hongo hili ni ya mamilioni, itatumika kwa ajili ya kujenga nyumba ya anasa au kumnunulia gari kimada wa mpokeaji. Rushwa ya aina hii ilikuwa nadra wakati wa Mwalimu, lakini pia ilianza kuongezeka mnamo miaka ya 1980s.

  Mtumishi mkuu wa serikali au kiongozi wa kisiasa akipewa asilimia kumi yake ili arahishishe utoaji wa leseni ya madini, au utoaji wa eneo la mbuga kwa ajili ya uwindaji wa kitalii, au kumuuzia mtoaji shirika la umma kwa bei ya kutupa, hii pia ni rushwa. Lakini hi si hongo kidogo na kuna uwezekano mkubwa kwamba itatumika kwa ajili ya kujilimbikizia mali au mtaji. Hii hasa ni ufisadi. Hii haikuwapo wakati wa Mwalimu kwa sababu mfumo wenyewe haukuwezesha kuwapo kwake.

  Ni mfumo wa uliberali mamboleo ndio uliozaa ufisadi. Chukua mifano yote mikubwa ya ufisadi, inatokana na sera na sheria mbalimbali za mfumo wa uliberali mamboleo. Chimbuko la mikataba ya madini ni katika sheria ya madini ambayo ilishinikizwa na Benki ya Dunia. Sheria yenyewe inatoa mwanya kwa watendaji kujinufaisha. Ufisadi wa EPA, chimbuko lake ni katika sheria iliyofanya Benki Kuu iwehuru na wala isidhibitiwe na Bunge. Ufisadi wa TTCL, TANESCO n.k. yote kwa njia moja au nyingine, uliwezeshwa na sera za ubinafsishaji.


  Ni kweli kwamba tungekuwa na viongozi wazalendo wenye uchungu na watu wao, labda mengine yasingetokea. Lakini viongozi bora hawazaliwi. Kwani wakati wa Mwalimu viongozi hawakuwa na tamaa ya hela? Walikuwa nayo, lakini wangefanya nini na mamilioni ya EPA? Wasingeweza kujilimbikizia mali – walikuwa hawaruhusiwi. Wasingeweza kujijengea hekalu! Wangeyaficha wapi? Wangeulizwa kujieleza. Kwa kifupi basi, tuone na kuchambua suala zima la ufisadi katika muktadha wa mfumo wenyewe ambao pia unazaa siasa zake za ubinafsi na ki-utandawazi ambao ni kinyume cha uzalendo.

  Haya malumbano ya wapambanaji dhidi ya rushwa kama malaika, na watetezi wa ufisadi kama mashetani, yamejengwa na vyombo vya habari na wanasiasa. Hakuna malaika wala mashetani, wote ni mashabiki wa mfumo huohuo wa uliberali mamboleo uliozaa ufisadi.
  Uliberali mamboleo ni sura katili ya mfumo wa kibepari. Ufisadi bila mipaka unadhihirisha tu usemi mmoja wa Mwalimu Nyerere: ubepari ni unyama, isipokuwa unyama huo hutendwa na wanadamu kwa sababu wanyama hawana mfumo wa kibepari!


  issashivji@cats-net.com
   
Loading...