Mtanzania gani ni mzalendo, jasiri na muadilifu?

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
ANDIKO la William Wordsworth “Character of the Happy Warrior” – “Sifa ya Mzalendo Jasiri Mwadilifu”, nitalitumia kama sehemu ndogo kujenga muktadha. Halafu nukuu “England Expects Every Man Will Do His Duty” – “Uingereza inatarajia kila mtu atatimiza wajibu wake”. Ni nukuu ya Horatio Nelson, mzalendo jasiri mwadilifu wa Uingereza.

Wordsworth ni mmoja wa zawadi katika uandishi ambao Uingereza imepata bahati kuwa nao. Mwaka 1806, Wordsworth aliandika “Character of the Happy Warrior” kama mchango wake wa kumuenzi mzalendo Nelson, aliyefariki dunia vitani mwaka 1805. Shairi la “Character of the Happy Warrior” lilichapwa mwaka 1807

Nelson, alikuwa mmoja wa makamanda wa juu kabisa wa vikosi vya Uingereza. Akafikia cheo cha umakamu jenerali. Akatambulika kwa vyeo vya Admiral na Viscount I. Aliliongoza jeshi la Uingereza kushinda vita nyingi. Kisha akajeruhiwa na kufariki dunia kwenye Vita ya Napoleon mwaka 1805.

Wordsworth katika shairi lake anamwita Nelson kuwa ni “happy warrior” wa Uingereza. Anaeleza sifa za mtu kuwa happy warrior ni uzalendo, ujasiri wa kupigania nchi katika mazingira yoyote yale, vilevile kutokuwa mbinafsi. Wordsworth alihitimisha andiko lake kwa kusema, kila mtu kwenye jeshi la Uingereza angetamani kuwa kama Admiral Nelson.

Kwa kuchambua kila sifa iliyotolewa na Wordsworth kuhusu “happy warrior”, unampata mtu ambaye ni mzalendo kwa nchi yake, jasiri anapoipigania nchi yake, asiye mbinafsi, vilevile mkweli na mwadilifu kwa nchi yake. Hivyo, tafsiri yangu, happy warrior ni mzalendo jasiri mwadilifu.

Admiral Nelson aliacha alama yake kupitia nukuu yake, kwamba Uingereza inatarajia kila mtu atimize wajibu wake. Yeye alitimiza. Ni wajibu wa kila Muingereza kutimiza huo wajibu kwa ajili ya nchi yake.

TUNA TANZANIA YETU
Kwa kukopa maneno ya Admiral Nelson ni kuwa Tanzania inatarajia kila Mtanzania atimize wajibu wake. Maswali ya msingi ni haya; ni wajibu gani Watanzania wapo nao kama taifa? Je, Watanzania wapo tayari kuheshimiana kipindi kila mmoja akitimiza wajibu wake?

Kuna maswali mengine; Tanzania ni taifa la aina gani? Mifumo yake ipoje? Tanzania ni nchi yenye Katiba, tena iliyo katika maandishi. Upi wajibu wa kila mmoja kuilinda Katiba?

Je, wajibu wa kumfanya kila Mtanzania kutambua kuwa Katiba ndio makubaliano ya muundo wa kimaisha kama nchi ni wa nani? Wajibu huo unatimizwa? Ni kwa kiasi gani Mtanzania anafahamu kuwa kuvunjwa kwa Katiba ni uhaini mkubwa kuliko hata kumpindua Rais?
Nani mzalendo jasiri mwadilifu kwa Tanzania? Anayeshangilia taarifa za Bunge la Ulaya kuinyima mikopo na misaada Tanzania kwa sababu mamlaka za nchi zinakandamiza demokrasia au yule ambaye anafurahia kusikia Watanzania wameuawa katika vurugu za uchaguzi?

Wajibu upi wa kutimizwa? Nani wa kushughulikia mgawanyiko uliopo? Kuna Watanzania hawana radhi na Tanzania yao, wanajiona wapo mateka au ukimbizini. Taarifa za nchi kunyimwa misaada wanazifurahia kana kwamba athari zake hawataakisi. Wapo wanaojiona ni Watanzania kipeo cha pili, kilio cha wenzao hata hawajali.

Nani mzalendo jasiri mwadilifu? Tundu Lissu aliyekimbilia Ubelgiji kunusuru maisha yake au IGP Simon Sirro aliyesema Tanzania ni salama? Aaminiwe nani? Lissu ambaye mwili wake umejaa matobo ya risasi au Sirro ambaye hajawezesha kupatikana waliomshambulia Lissu zaidi ya miaka mitatu imepita?

Natamani nimseme Lissu kuwa anaipaka matope nchi. Alidai kupewa vitisho vya kuuawa, badala ya kutoa taarifa polisi, akaenda kuomba hifadhi ubalozi wa Ujerumani. Kisha akaikimbia nchi kwa msaada wa ubalozi wa kigeni.

Hata hivyo, najikuta nakosa kauli ninapokumbuka kuwa Lissu alipigwa risasi 38, katika hizo 16 zilizama mwilini miaka mitatu iliyopita. Hakuna aliyekamatwa. Je, ingekuwa mimi ningekabidhi maisha yangu kwa watu walewale ambao hawakunifaa lolote katika jaribio la kutoa uhai wangu? Baada ya kujiuliza swali hilo kwa umakini, nagundua siwezi. Sasa kwa nini nimlaumu Lissu? Yeye sio binadamu?

Upande mmoja nahisi Godbless Lema anafanya usanii kuomba hifadhi Kenya. Nataka kuamini Tanzania yetu ni salama kama alivyosema Sirro. Hapohapo nakumbuka Ben Saanane, Azory Gwanda na Simon Kanguye hatupo nao. Ben, miaka minne imepita. Azory na Kanguye miaka mitatu. Hatujui walipo.

Sijitoi ufahamu, naweka akilini kuwa Lema ana mali zake, amewekeza Tanzania. Anaamua kuziacha ili kutafuta usalama nje. Nikifika hapo, najiona mimi ndiye nitakuwa na matatizo kama nitashikilia msimamo kuwa hana hoja. Naamini anayo hoja.

Mwanafunzi Akwilina Akwilini mpaka leo hajulikani nani aliyempiga risasi akiwa kwenye kiti cha daladala. Miaka miwili imepita unakaribia wa tatu. Kama wauaji hatuwaoni, hatuwajui, hawakamatwi, hawashitakiwi na hawahukumiwi. Naanzaje kumlaumu Lema anayesema anapokea vitisho vya maisha yake?

Katiba ya Tanzania, ibara ya 3 (1), inatamka kuwa Tanzania ni nchi yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kama wajibu wa kila Mtanzania ni kuheshimu na kulinda Katiba, iweje kuwepo na hali kwamba wanasiasa vya vyama vyenye kuitwa vya upinzani, wanaona ugumu kufanya siasa? Wanafanya siasa kama wapo nchi ya kukodi wakati wapo kwao.

Wajibu wa kuhakikisha siasa zinakuwa na usawa ni upi na muwajibikaji ni nani? Katiba imeandika siasa ni za vyama vingi lakini upumuaji wa vyama vya siasa unategemea hiyari ya mwenye kushika mpini. Nani mwenye wajibu wa kulitibu hili? Bunge? Bunge lipi?

Uchaguzi ni mali ya wananchi. Unafanyika. Mwananchi hana chumba cha kuhoji wala kukosoa uchaguzi na matokeo yake. Hakuna kwenda mahakamani wala kuandamana. Tena, askari wenye viapo vya kulinda wananchi na waliolishwa yamini kutogeuzia silaha raia, wanaingia barabarani kupambana na wananchi wasio na silaha.

Turudi aliposema Admiral Nelson, kwamba matarajio ya nchi ni kila mtu atimize wajibu wake. Mwananchi anayetaka kutimiza wajibu wake kwa kupinga matokeo ya uchaguzi anakwenda wapi ikiwa mahakamani hapaendeki na maandamano ya amani yanaitwa ugaidi?

NCHI NI YA NANI?
Raia si mpangaji kwenye nchi yake. Wala mtawala si baba mwenye nyumba katika taifa alilochaguliwa kuliongoza. Raia ni mmiliki wa nchi yake. Rais ni mbeba wajibu mkuu kwenye nchi kuhakikisha kila raia anafurahia umiliki wake wa nchi. Kadhalika, ni wajibu wa Rais kuhakikisha nchi inaenda kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo kwenye Katiba. Ni sawa kusema ni lazima ailinde Katiba.

Vyama vya upinzani na chama tawala wote ni Watanzania. Tofauti ni kwamba kipo kinachoshika dola vingine havina. Kuwa chama tawala sio kumiliki nchi, bali kubeba wajibu wa kuhudumia nchi na watu wake kwa usawa.

Je, watu wanatambua hayo? Kama hawatambui nani ana wajibu wa kuwafanya watambue? Ikiwa wanatambua je, wanafuata? Kama hawafuati ni nani mwenye wajibu wa kuhakikisha kinachostahili ndicho kinafuatwa?

Tumekuwa wepesi kutaka walimu watimize wajibu wao wa kufundisha, madaktari watibu inavyotakiwa. Huo ni wajibu wa kawaida katika nchi yenye utulivu. Upo wajibu wa kuifanya nchi iwe na misingi. Huo wajibu ni wa nani?

Upo mfano; wasafiri na mayai yao mabichi, wakayakabidhi kwa mwenzao waliyemuona ana nguvu sana. Njiani kilimani, yule mwenye nguvu akajikwaa. Akaanguka. Mayai yote yakaanguka na kuvunjika. Wasafiri wakajilaumu mayai yote kumbebesha mwenzao waliyemuona hodari kuliko wote.

Ni kama nchi. Hachaguliwi mtu na kukabidhiwa kila kitu kisa ameonekana ana uwezo mkubwa. Akiteleza au akijikwaa itakuwaje? Ndio maana Katiba imeweka Bunge, Serikali na Mahakama. Katiba ikasema awepo Rais, lakini awe na Makamu wa Rais. Liwepo Baraza la Mawaziri. Bunge lipo kusimamia utendaji wa Serikali nzima. Bunge limewekwa ili liwe sauti ya wananchi.

Tafsiri ni kuwa Katiba imeweka mfumo ndio uongoze nchi, sio mtu au kikundi fulani cha watu. Swali; nani mwenye kupaswa kutimiza wajibu huu wa kukumbusha kwamba nchi haiendeshwi na mtu isipokuwa mfumo? Je, akikumbusha hataitwa gaidi au adui wa umma?
Nakumbuka Joseph Stalin alipomuona Leon Trotsky ni kikwazo kwake kuitawala Soviet (USSR) kiimla, alimwita msaliti. Vyombo vya habari Urusi vikamwita Juda Trotsky. Juda (Yuda), ni yule mwanafunzi wa Yesu aliyemchuuza Masihi kwa vipande vya fedha. Yuda ni alama ya usaliti. Trotsky akaitwa msaliti wa nchi yake, Urusi na dola nzima ya Soviet.

Nelson Mandela na wenzake Afrika Kusini waliitwa magaidi walipokuwa wakipigania utawala wa kidemokrasia na usawa kwa watu wote. Ally Tamek alishatamkwa ni adui wa umma Morocco kwa sababu anapigania uhuru wa Sahrawi. Alice Paul, Lucy Burns na wenzao waliitwa magaidi walipokuwa wanapigania haki za wanawake kupiga kura Marekani.

Mifano hiyo inaenda na tafakuri hii; je, kipindi ambacho wengine wanapotimiza wajibu wao wa kusahihisha pale wanapoona watawala wanakosea, watavumiliwa? Turudi kwa Admiral Nelson, kila mtu lazima atimize wajibu wake kwenye nchi.

Ukiwa mtawala, kukosolewa pia ni wajibu. Kuvumilia ukosoaji kipindi unapokosolewa hivyo ndivyo kutimiza wajibu wako. Kama taifa likiwa na wasifiaji tu, litaanguka mithili ya wale wasafiri waliokabidhi mayai yao yote kwa mwenzao waliyemuamini.

Muhimu ni kuheshimiana na kujua kuwa wote ni Watanzania. Baada ya uchaguzi wa Rais Marekani, uliofanyika Novemba 6, 2012, mshindi, Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, alimpongeza mshindani wake, Gavana Mitt Romney kwa kampeni zenye nguvu na kura nyingi alizovuna.

Obama alisema, waliompigia kura yeye na wale waliomchagua Romney, wote waliwezesha sauti zao kusikika. Akasema: “Mimi na Romney tunaweza kuwa tulipambana sana, lakini ni kwa sababu tunaipenda sana hii nchi yetu na tunajali mno kuhusu kesho yake.” Zaidi, Obama aliipongeza familia ya Romney kwa jinsi Romney alivyojitoa kuutumikia umma.

Isingependeza? Rais John Magufuli kutamka kuwa yeye na Lissu wote wanaipenda nchi hii na wanajali mno kuhusu kesho yake, ndio maana walipambana kwenye kampeni, kila mmoja akitaka afanye kilicho bora kwa nchi yake anayoipenda?

Hatuwezi kufikia kiwango hicho cha siasa za kistaarabu kwa sababu wanasiasa wengi hawajui wajibu wao wa kisiasa. Siasa zinageuka uadui pale panapotokea ukosoaji. Kisha wananchi wanagawanyika na wanakubali kugawanywa. Wajibu ni upi?

Je, kuomba nchi inyimwe misaada kwa sababu watawala hawaheshimu haki za raia ni kutimiza wajibu au ni kufurahia wajibu unaotimizwa na wengine? Wanaofurahi wanahisi kunyimwa misaada ni kukomolewa kwa watawala au nchi inakomolewa? Utayari wetu upoje wa kuishi kwenye nchi inayokomolewa?

Je, tufurahie kukomolewa kwa kunyimwa misada na mikopo au kila mtu atimize wajibu wake? Je, tungoje adhabu ya vikwazo kwa furaha au tutimize wajibu wetu? Nani mzalendo jasiri mwadilifu?

Kwangu mzalendo jasiri mwadilifu ni yule anayetimiza wajibu wake kwa nchi yake ili wanaye, wajukuu zake mpaka wajukuu wa wajukuu zake waishi kwenye nchi safi, sio yenye amani tu, bali iliyo tulivu, yenye watu waliostaarabika na wanaoheshimiana.

Nchi ambayo Katiba ina nguvu kuliko yeyote. Taifa ambalo watawala wanaheshimu raia na haki zao bila kupepesa. Nchi ya Mahakama yenye mahakimu na majaji wanaojiheshimu na wanaofanya kazi kwa mujibu wa viapo vyao na kwa muongozo wa taaluma zao. Taifa lenye Bunge lililo na nguvu ya kuangusha Serikali. Bunge lenye msuli wa kumvua Rais urais.

Nani wa kutimiza wajibu?

©Luqman Maloto
 
Back
Top Bottom