Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,743
- 2,601
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetangaza kuwa matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa Chama cha Wananchi (CUF) uliofanyika Desemba 2024 ni batili na kuelekeza chama hicho kurudia uchaguzi wa nafasi za juu za uongozi mara moja.
Kwa mujibu wa Jambo TV, barua ya Februari 13, 2026, iliyotiwa saini na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa CUF na walalamikaji, ofisi hiyo imetoa uamuzi huo baada ya kufanyia kazi malalamiko yaliyowasilishwa na wanachama, akiwemo Maftaha Nachuma na Miraji Mtibwiriko.
Msajili amebainisha kuwa chaguzi za Mwenyekiti wa Taifa (nafasi inayoshikiliwa na Profesa Ibrahim Lipumba), Makamu Mwenyekiti Zanzibar, na Makamu Mwenyekiti Bara, zilikiuka Kanuni ya 7.1.4 ya Kanuni za Uchaguzi za CUF za mwaka 2018.
Kanuni hiyo inataka mshindi kupata zaidi ya nusu (zaidi ya 50%) ya kura zote zilizopigwa.
Uchunguzi wa Msajili umebaini kuwa hakuna mgombea aliyefikisha kiwango hicho cha kura, lakini walitangazwa washindi kinyume na utaratibu.
“Chaguzi zote zilizofanyika katika mkutano mkuu wa CUF wa tarehe 18 na 19 Desemba 2024 ambazo hakuna mgombea aliyepata kura zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, zilipaswa kurudiwa na kwa kuwa hazikurudiwa waliotangazwa kuwa ni washindi, ushindi wao ni batili”, inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo imefafanua kuwa kitendo cha Profesa Lipumba kutochukua na kurejesha fomu mwenyewe si kosa kisheria kwa kuwa Katiba ya CUF haijaweka sharti hilo. Hata hivyo, Msajili amebaini jambo zito zaidi; kuna uwezekano mkubwa kuwa Muhtasari wa kikao cha Baraza Kuu la CUF cha tarehe 15-16 Desemba 2024 uliongezwa maneno ili kuonesha kuwa kanuni ya ushindi wa nusu ya kura iliondolewa, lengo likiwa ni kukwepa uwajibikaji.
Msajili ameweka wazi kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa wana haki ya kuwasilisha malalamiko yao moja kwa moja ofisini kwake bila kulazimishwa kumaliza mchakato wa ndani ya chama kwanza. Hii inakuja baada ya uongozi wa CUF kujaribu kupinga malalamiko hayo kwa hoja kuwa wanachama hao hawakufuata ngazi za rufaa ndani ya chama.
Kutokana na ubatili huo, Msajili amekielekeza chama cha CUF kurudia uchaguzi wa nafasi hizo tatu za juu za kitaifa (Mwenyekiti na Makamu Wenyeviti wawili) kwa kufuata Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2018.
Pia soma ~ Ngulangwa: Inawezekana CUF kutotambua Uchaguzi wa Oktoba 29 imesababisha Msajili aone Uchaguzi wetu ulikuwa batili