Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 260
- 998
Dar es Salaam. Makada watatu akiwamo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Tanzania Bara, Othman Omar Dunga, wamepitishwa kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho Taifa, iliyoshikiliwa kwa muda mrefu na Profesa Ibrahim Lipumba.
Wengine waliopitishwa kuwania nafasi hiyo ni Mirambo Camil Yusuf na Nkunyunyika Siwale.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, amepitishwa Mussa Mbarouk, Mohammed Ngulangwa na Miraji Mtibwiliko.Wakati Makamu Mwenyekiti Zanzibar, ni Haroub Mohamed Shamsi, Mbarouk Seif Salim na Amina Rashid Salim.
Majina hayo yamepatikana baada ya kukamilika kwa kikao cha dharura cha wajumbe, kilichofanya mchujo na kupitisha majina ya makada 20 waliojitokeza kuchukua fomu zilizotolewa bure kuanzia jana mchana, kuwania nafasi hizo tatu za juu ndani ya chama hicho.
Baada ya kupatikana kwa majina hayo, yatawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa chama unaoendelea katika Ukumbi wa Lekham, mkabala na ofisi za chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam na wajumbe wa mkutano huo watamaliza ubishi.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa mchujo huo, Mwenyekiti wa kikao hicho, Haroub, amesema orodha hiyo itawasilishwa kwa wajumbe ili wapate fursa ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
“Tumekamilisha mchujo na kwa kila nafasi tumepitisha majina matatu. Sasa tunaelekea ukumbini ambako wajumbe wanasubiri ili kuanza mchakato wa kupiga kura, ambapo kwa kila nafasi atapatikana mshindi mmoja,” amesema.
Uchaguzi huo umekuja kufuatia agizo la Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya kupokea malalamiko baadhi ya makada wa chama hicho, waliodai kuwa uchaguzi uliofanyika Novemba 2024 ulikiuka kanuni za chama hicho.