Nimeitoa Facebook.
SABABU ZA MAGONJWA YA MENO NA JINSI YA KUJITIBU
Kuna tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa matibabu rasmi ya meno (yaani yale yanayotolewa na madaktari wa meno waliosajiliwa rasmi kama wataalamu wa fani hiyo), kuna wakati yanaweza kuharibu afya ya mgonjwa na kumletea magonjwa hatari ya kimfumo, yanayoweza hata kuhatarisha maisha yake
Mfano ni matumizi ya mchanganyiko wa madini ya fedha, bati, shaba na zebaki (silver amalgam) katika kuzibia matundu ya meno.Madini ya zebaki (mercury) ni sumu na yamethibitika kusababisha magonjwa mengi ikiwa ni pamoja na yale ya mishipa ya fahamu, yale yanayotokana na uharibifu wa kinga za mwili, na yale ya akili.
Kwa kawaida silver amalgam ina madini ya zebaki kwa kiasi cha 50%. 50% iliyobaki inajumuisha madini ya fedha, bati na shaba.
Tafiti zimeonyesha kuwa zebaki ndani ya silver amalgam ndani ya kinywa hutoka kidogo kidogo kama mvuke. Mvuke wa zebaki kwenye vinywa vyenye meno yenye amalgam kwa siku ni kati ya 3ug (microgram) na 27ug. Baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa kiwango cha 27ug ni cha juu sana ukilinganisha na kiwango ambacho ni salama.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Dunia (WHO) kiwango cha mvuke wa zebaki kinywani kinaweza kuongezeka sana ukilinganisha na takwimu hizi kutokana na tabia binafsi kama kusaga meno, kutafuna ubani (chewing gum) na kunywa soda.
Sasa mtu unapowekewa kwenye kinywa chako silver amalgam kwa kisingizio cha kuwa ni malighafi nzuri ya kuzibia meno matarajio yako ni nini?
Nia ya makala yetu ya leo ni kuzungumzia sababu zinazopelekea tuugue maradhi ya meno, na hatua tunazopaswa kuchukua kulinda afya ya vinywa vyetu, ili kupunguza uwezekano wa kuingia katika mazingira ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwetu.
Pamoja na mambo mengine hatua hizi zitatusaidia kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya meno. Tukipunguza uwezekano wa kupata maradhi ya meno, tutapunguza uwezekano wa kukutana na aina ya matibabu ambayo yanaweza yakatusababishia matatizo zaidi ya kiafya.
MAGONJWA YA MENO
Magonjwa ya meno, kama yalivyo magonjwa mengi mengine, ni dalili au kiashiria tu (signal) kuwa kuna tatizo katika eneo fulani la miili yetu. Aghalabu kiini cha tatizo kinakuwa kiko mbali kabisa na eneo dalili inapoibukia.
Tunapoacha kusaka kiini cha tatizo, tukahangaika kupigana na dalili, matokeo yake aghalabu huwa ni mabaya zaidi. Kwa bahati mbaya sana hii ni falsafa ambayo imeupiga chenga mfumo wa tiba za kisasa.
Na ni bahati mbaya zaidi, kuwa huu ndio mfumo tunaoutambua kama bora, ama mfumo rasmi wa tiba. Kwa kulitambua hili, makala yetu ya leo itajikita zaidi katika falsafa inayotumiwa zaidi na wadau wa tiba mbadala. Kwa wadau hawa kwao tiba ni kuondoa kiini cha tatizo na siyo kuhangaika na dalili.
Kwa mfano, unapoumwa na jino na ukakimbilia kulitoa, huko ni kuhangaika na dalili. Utaratibu mzuri ungekuwa ni kujiuliza hivi ni kitu gani kimepelekea jino hilo likaanza kuuma, na ukishagundua kiini cha tatizo uchukue hatua za kuondoa kiini cha tatizo hilo.
Kwa utaratibu huu, siyo tu kwamba utakuwa umetibu jino linalokusumbua kwa wakati huo, lakini pia utakuwa umetoa ulinzi kwa meno yako mengine ambayo kwa wakati huo yatakuwa bado hayajaanza kuuma.
Pamoja na kwamba ziko sababu kadhaa zinazoweza kumpelekea mtu kupata maradhi ya meno, sababu kubwa ni mbili. Sababu hizi ni:
1. Chakula; na
2. Usafi wa kinywa.
CHAKULA
Kila chakula ni mjumuiko wa viambata vya kikemikali (chemical components) ambavyo hufanya kazi kwa pamoja vikiwa katika hali ya mizania (balance). Uchakataji (processing) hundosha mizania iliyopo na kuvuruga utaratibu wa kiambata kimoja kutegemea kingine kufanya kazi iliyodhamiriwa bila kusababisha athari mbaya.
Kadri kiwango cha Uchakataji kinavyozidi kuwa kikubwa, ndivyo mizania baina ya viambata inavyozidi kupotea, na ndivyo athari mbaya zinavyozidi kuongezeka kwa mtumiaji wa chakula kilichopitia mchakato huo.
Katika vyakula vya wanga (carbohydrates) vilivyochakatwa kwa kiasi kikubwa, mizania ya viambata imeegemea sana kwenye sukari nyepesi (simple sugars).
Hii ni kwa sababu katika Uchakataji huo viini hai (protini), mafuta (fats), vimeng’enya (enzymes) na nyuzi lishe (fibers) kuondolewa. Hii ina maana kwamba mtu anayekula sana vyakula hivi huingiza kiasi kikubwa sana cha sukari mwilini mwake; sukari ambayo haina viambata mwenza vya kuizuia isisababishe athari mbaya mwilini.
Moja ya sukari hizi, fructose, inatuhumiwa kupelekea kuzaliwa kwa kiwango kingi cha tindikali mkojo (uric acid), wakati wa kuchakatwa kwake ndani ya mwili.
Tindikali ni kitu chochote kile ambacho kinapoyeyushwa kwenye maji huongeza idadi ya chembechembe zenye kubeba umeme chanya. Kipimo kinachotumika kutambua ukali wa tindikali na vitu vingine vilivyoyeyushwa kwenye maji na kutengeneza vimiminika huitwa kipimo cha pH.
Kipimo hiki kimegawanywa katika tarakimu kuanzia 0 hadi 14. Kwa kawaida kimiminika chochote ambacho pH yake ni kati ya namba 0 na namba 7 huhesabika kama tindikali (acid), na kile ambacho pH yake ni kati ya namba 7 na namba 14 huhesabika kuwa ni alikali (alkali). Namba 7 ni pH ya maji halisi yasiyo na chochote kilichoongezewa ndani yake.
Alikali ni chumvi yoyote ile inayotokana na madini yanayojulikana kama madini ya alikali na yale yanayojulikana kama madini ya alikaline (alkaline earth metals). Yaliyo maarufu zaidi miongoni mwa madini haya ni sodiumu (sodium), potasiamu (potassium), magnesi (magnesium), na kalisi (calcium).
Kadri namba kwenye kipimo cha pH inavyozidi kuwa ndogo kuelekea 0, ndivyo ukali wa tindikali husika unavyoongezeka, na kadri namba kwenye kipimo hicho inavyozidi kuwa kubwa kuelekea 14, ndivyo ukali wa alikali husika unavyoongezeka.
Kimaumbile ukiondoa majimaji yaliyomo katika mfuko wa tumbo ambayo yana pH ya kati ya 1 na 5 kutegemeana na kama umekula, au hujala; na kama umekula, aina ya chakula ulichokula, vimiminika vingine vinavyokuwemo mwilini muda wote vina pH kati ya 7 na 8.
Pamoja na ukweli kwamba tindikali mkojo inaposimama kama yenyewe ina madhara mengi mwilini, lakini pia huchangia katika kuongeza kiwango cha mkusanyiko wa tindikali mwilini kutoka katika vyanzo vingine mbalimbali. Vyanzo hivi vingine ni pamoja na:
1. Vyakula vyote vya aina ya protini (protein);
2. Vyakula vyote vya aina ya wanga (hata kama havijachakatuliwa);
3. Matunda aina ya cranberry; na
4. Mchakato wa kuishi (yaani kupumua, kuona, kusikia, kufikiri, kutembea, nakadhalika).
Kuwa hai ni kitendo kinachohitaji matumizi makubwa ya nishati. Kila seli za mwili zinapozalisha nishati hii na kisha kila nishati hiyo inapotumika, moja ya mazao ya vitendo hivyo ni kuzalishwa kwa tindikali. Hii ina maana kwamba kila sekunde tindikali inaongezeka ndani ya mwili.
Ongezeko hili ni hatari sana kiafya iwapo hatua sahihi hazichukuliwi kukabiliana nalo.
Tindikali hupoozwa/huzimuliwa kwa alikali. Kwa sababu hii tunahitajika tuwe tunakula kwa wingi vyakula vyenye madini ya alikali au yale ya alikaline.
Vyakula pekee vinavyoweza kutupatia kiasi kikubwa cha madini haya ni vile vya mchanganyiko wa mbogamboga za majani, na vile vya mchanganyiko wa matunda.
Kwa bahati mbaya sana wengi wetu tunakula vyakula hivi vikiwa chini ya kiwango halisi cha mahitaji ya miili yetu. Hali hii huilazimisha miili yetu kutafuta njia mbadala ya kujitetea dhidi ya tindikali nyingi inayoongezeka mwilini.
JINSI MWILI UNAVYOPAMBANA NA TINDIKALI YA ZIADA
Moja ya hatua zinazochukuliwa na mwili dhidi ya ongezeko kubwa la tindikali mwilini pale kunapokuwa hakuna alikali ya kutosha kutoka kwenye lishe, ni kutoa ishara kwa mifupa kuanza kuachia madini ya kalisi (calcium) kuingia kwenye mzunguko. Kitendo hiki kinachukuliwa kama cha dharura kinacholenga kuusadia mwili kufanya kazi ya kuizimua tindikali iliyojilundika.
Hapa mwili unatatua tatizo kwa kutengeneza tatizo jingine, lengo likiwa ni kujihifadhi na hatari iliyoko usoni. Hekima ya mwili hapa ni kuwa “unaweza kuishi na mifupa iliyodhoofika, lakini huwezi kuendelea kuishi na kiwango kikubwa cha tindikali kinachojilundika mwilini!” Mwili wako unakutarajia uchukue hatua madhubuti na za haraka kujiondoa katika dharura hii.
Ni kama vile pale gari yako inapolazimika kutembelea gurudumu la akiba. Matarajio ni kwamba utachukua hatua za haraka sana kuhakikisha kuwa kitendo hicho kinakuwa ni cha muda mfupi. Kwa kifupi, kinachotarajiwa na mwili wako ni kuurejeshea mwili huo akiba ya kutosha ya madini ya alkali au yale ya alikaline, tena bila kuchelewa.
MENO NI MIFUPA PIA!
Meno, kama ilivyo mifupa mingine mwilini, huathiriwa pia na hali hii ya kupoteza madini ya kalisi pale tindikali inapozidi mwilini. Dalili kubwa kwamba mtu umeathiriwa na hali hii ni udhaifu unaodhihirishwa na meno yako pale yanapoanza, kutoboka, kukatika na kumeguka hovyo.
Tindikali pia inapozidi mwilini hufikia pahala ikaanza kubadilisha pH za vimiminika (body fluids) mbalimbali vilivyoko kwenye mwili. Vimiminika hivi ni pamoja na damu, mate, majimaji yaliyoko katika mfuko wa tumbo, majimaji yanayozalishwa na ini na kongosho kwa ajili ya uchakataji wa chakula kwenye utumbo mwembamba, majimaji ya uti wa mgongo, manii, machozi, na kadhalika.
Iwapo tindikali inayozalishwa mwilini kila sekunde na kujumuika na ile inayotoka kwenye lishe kama tulivyoona haitapoozwa, basi italundikana na kuanza kubadilisha vimiminika mwilini kutoka hali ya ualikali (pH 7 -8) na kuwa katika hali ya utindikali (pH chini ya 7).
Moja ya vimiminika vya mwili vinavyoweza kuathiriwa na hali hii ni mate. Wingi wa tindikali mwilini unaweza kupelekea mate kupoteza hali yake ya asili ambayo ni alikali dhaifu (slightly alkaline), na kubadilika kuwa katika hali ya utindikali. Hili likitokea meno yatakuwa katika mazingira ya kupata madhara zaidi kwa sababu sasa yatakuwa yanaogelea moja kwa moja katika bahari ya mate yenye hali ya utindikali.
Hii ina maana kwamba sehemu kubwa ya madini ya kalisi yaliyoko kwenye meno itakuwa inayeyuka moja kwa moja kutoka kwenye meno na kuingia kwenye mate kwa lengo la kupooza tindikali kwenye mate hayo.
Kwa kuwa sehemu kubwa ya kalisi itakayoyeyuka ni ile ilyoko kwenye jino kwa nje, sehemu ya ndani ya jino itapoteza kinga yake dhidi ya hali kama za joto, baridi na ukakasi. Wale wote wenye malalamiko ya meno yao kuathiriwa na joto, baridi na hata vitu vyenye ukakasi, basi wajue kuwa moja ya sababu kubwa za hali hiyo ndiyo hiyo tuliyoielezea.
UMUHIMU WA MABADILIKO YA LISHE
Kujilinda dhidi ya uharibifu wa meno na mifupa mingine unaosababishwa na tindikali unahitaji kufanya mabadiliko makubwa katika lishe yako. Wataalamu wanasema ili kuuweka mwili katika viwango vya tindikali ambavyo havina madhara kiafya asilimia themanini ya chakula chako kwenye sahani iwe ni mbogamboga na matunda, na asilimia 75 ya mbogamboga na matunda hayo viwe katika hali ya ubichi.
USAFI WA KINYWA
Mabaki ya vyakula vya wanga vilivyochakatwa kwa kiwango kikubwa yanayokuwemo mdomoni baada ya kula pia yanakuwa na kiwango kikubwa cha sukari kama hivyo vyakula vyenyewe. Sukari hii ni kivutio kikubwa mno cha bakteria wa aina ya gram positive. Bakteria hawa wanapoingia kinywani kwa nia ya kufuata mabaki ya vyakula, hujikuta wakishambulia na meno pia, hasa pale meno hayo yanapokuwa ni dhaifu na ambayo hayafanyiwi usafi wa kina. Matokeo ya mashambulizi haya ni uharibifu zaidi kwa meno, na hatimaye maumivu.
Watu wengi huwa tunafanya makosa ya msingi kuhusiana na usafi wa vinywa vyetu. Makosa haya ni pamoja na kukaa na mabaki ya vyakula mdomoni kwa muda mrefu sana kabla ya kuchukua hatua ya kusafisha kinywa. Watu walio wengi wamezoea kupiga mswaki mara moja tu ndani ya masaa 24, na hii ni asubuhi baada ya kutoka usingizini.
Hii ina maana kwamba mtu mwenye tabia hiyo muda mwingi kinywa chake ni dampo la mabaki ya vyakula, na anatoa muda mrefu kwa gram positive bakteria kuweka kambi kwenye kinywa chake. Ingekuwa ni bora sana kama mtu angepata fursa ya kusafisha kinywa chake kila baada ya mlo, ili kuepukana na hali hii.
Hata hivyo, kwa sababu katika hali halisi hili ni gumu, basi ni bora mtu ukahakikisha kuwa unapiga mswaki wa hali ya juu sana usiku kabla ya kulala. Hii ina maana kwamba usiku wote utakuwa umelala huku ukiwa na kinywa kisafi, na hivyo kutoa wakati mgumu sana kwa gram positive bakteria kushambulia wakati ukiwa usingizini.
Ni vizuri pia ikafahamika kuwa kupiga mswaki pekee – hata kama mswaki huo utaupiga kila siku kabla ya kulala - hakutoshi kukiacha kinywa chako huru kwa asilimia mia moja dhidi ya uwepo wa gram positive bakteria. Njia ya uhakika ya kujihakikishia hili ni kutumia kitakasaji cha mdomo (oral disinfectant), kila baada ya muda fulani. .