Mheshimiwa Naibu Spika, pia limezungumzwa suala la lugha ya Kiswahili kwamba, tusiishie kutoa nyaraka na maelekezo bali tuchukue hatua madhubuti za kuhakikisha kwamba kauli za Serikali zinatekelezwa. Nataka niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba sisi katika Wizara tumejiandaa kauli ile imepelekwa kwa Waziri wa TAMISEMI na yeye amepeleka kwa Halmashauri zote zilizopo chini ya TAMISEMI, tumepeleka kwa Waziri wa Utumishi na yeye pia ameshatoa maagizo kwa Ofisi zote za Serikali kuhakikisha kwamba zinatekelezwa lakini ushauri uliotolewa na Bunge tutaufuatilia na tutajitahidi kuhakikisha kwamba maelekezo haya yanatekelezwa ikiwa ni pamoja na kuona kwamba, tunatumia Kiswahili sanifu, saa kumi badala ya masaa kumi, mrabaha badala ya mrahaba na kadhalika. (Makofi)