Shirika la ndege TZ lilianza na ndege nyingi lakini zimekufa moja baada ya nyingine hadi ikabakia moja ambayo na yenyewe ilikuwa mbovu ndio imeanza kazi hivi karibuni. Ukifuatilia undani wake, utakuta ni matatizo ya kuleanaleana tu na kuogopa kuchukua maamuzi magumu. Ukweli kuna angala zile gharama za uendeshaji zinatakiwa zifahamike ili ilinganishwe na kile kinachopatikana kisha ijulikane kama kuna upungufu nani aubebe.
Kuna mchangiaji amesema TEMESA inapata fedha toka mfuko wa barabara kwa ajili ya kuendeshea vivuko, hili sio kweli hata kidogo!
Endapo TEMESA itakaa kimya bila kupiga kelele sasa wakati vivuko hivi vikiwa vipya, utafika wakati vivuko hivi vitakapoanza kuhitaji matengenezo na yakawa hayapatikani, huduma itakosekana. Ikifikia hatua hiyo, wananchi hao hao akiwemo Mh. Mbunge wao, watakuwa wa kwanza kurusha madongo.
Hii inanikumbusha rafiki yangu aliyeniomba nimwazime gari asafiri nalo umbali wa karibu km 500 kwa kigezo kuwa gari bado ni nzima yeye ataweka mafuta (dizeli) ya kwenda na kurudi. Kwa mtazamo wa watu wengi, kwao gari ni dizeli tu na kusahau kuwa kuna service, tear and wear na kwamba unatakiwa ufike mahali, gari hiyo ikizeeka inunuliwe nyingine.
Vivyo hivyo kwa upande wa vivuko, watu watasema ni vipya na vimenunuliwa na Serikali, sawa. Lakini baada ya kununuliwa vimekabidhiwa kwa TEMESA ili ivihudumia kwa ajili ya kuvusha abiria na mali zao. Vinahitaji kuhudumiwa na muda utafika vitazeeka vitahitajika vingine. Mimi nahisi huo ndio mtazamo wa TEMESA kwamba wana maono ya siku za usoni. Kwa hiyo nauli zimepanda, tuwasubiri watuonyeshe jinsi watakavyoboresha huduma zao.
Na kwa upande wa abiria, badala ya kulilia lia kuwa kuna ufisadi, watueleze nani amewahi kuuona uongozi na kuueleza kuwa fulani anahujumu kivuko hicho kimapato akadharauliwa? Kama kuna biashara mahali basi ujue kuna muuzaji na mnunuzi. Kwa maana hiyo kama kuna wizi kama wa mafuta, wananchi na wenye wanahusika kuhujumu, lasivyo, kama wasingeyataka wangetoa taarifa ili mitego iandaliwe wahusika wakamatwe!
Taarifa zilizopo, wanaokamatwa kwa kuzungusha tiketi au wizi wa dizeli wanakamatwa na viongozi wa TEMESA wakishirikiana na askari na baadhi ya raia wema.
Nafikiri tuache kulalamika, ifike mahali mtu unapotoka nyumbani kwako ama kwa miguu, gari, guta au miguu, ujiulize safari yako ina tija? Isije kuwa safari zinapangwa kwa sababu ya usafiri kuwa wa gharama nafuu!