SEHEMU YA 18
Wakateremka, wakachukua lifti na kuelekea juu. Walipofika huko, wakateremka, hawakuishia kwenye chumba chochote kile bali walikwenda mpaka juu kabisa ya ghorofa sehemu ambayo kulikuwa na mitambo kadhaa, madishi ambapo huko ungeweza kuliona Jiji la Dar es Salaam kwa uzuri kabisa.
Kulipambwa vilivyo, katikati kulikuwa na meza kubwa iliyokuwa na vyakula mbalimbali, kulikuwa na chupa ya mvinyo.
Pembeni kulikuwa na maua yaliyokuwa yamemwagwa kwa chini, kulikuwa na kapeti jekundu kutoka pale alipokuwa akiingilia lakini pia kwa pembeni kulikuwa na wanaume wanne ambao walishika maneno yaliyosomeka ‘I LOVE YOU’.
Mbali na hayo yote pia kulikuwa na wanaume wawili walioshika vifaa viitwavyo saxophone ambavyo vilikuwa na muonekano kama wa tarumbeta, hao kazi yao ilikuwa ni kupuliza muziki wa taratibu mahali hapo.
Ukiachana na hayo, pia kwa mbele kulikuwa na viti vingine viwili ambavyo vilielekea upande uliokuwa na uwezo wa kuliona Jiji la Dar es Salaam kwa uzuri, yaani hivyo vilitakiwa kutumika kama mapumziko baada ya kula chakula, wakae na kuangalia jiji hilo lilivyokuwa likionekana kwa usiku.
Violeth alisimama mlangoni huku akiviangalia vitu vyote hivyo, ni kama alichanganyikiwa, hakuamini kama kungekuwa na mwanaume ambaye angemfanyia vyote hivyo.
Moyo wake ukazidi kutekwa, huku akiwa amesimama kama mtu aliyepigwa na butwaa, Theo akatokea na kuanza kumsogelea.
Alivalia shati jeupe, alichomekea kwa suruali yake nyeusi, alivalia tai na moka chini, saa ya Rolex aliyonunua kwa bei ya shilini milioni arobaini na nne Afrika Kusini, alitembea kwa mapozi huku akimfuata na sura yake ikiwa imependezeshwa kwa tabasamu pana.
“Tu es la bienvenue mignonne,”
(Karibu mrembo) alisema Theo kwa Kifaransa ambacho kilieleweka vizuri masikioni mwa Violeth. Akampa mkono na kumshika, akaanza kutembea juu ya kapeti jekundu.
“Umefanya yote haya kwa ajili yangu?” aliuliza Violeth huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo! Nimefanya haya yote kwa ajili yako kwa kuwa unastahili,” alisema Theo huku akiachia tabasamu pana.