SEHEMU YA 35
Ilikuwa taarifa mbaya mno kwake, ilimuumiza kupita kawaida, alibadilika na kukosa tumaini kabisa moyoni mwake, alimpoteza mtoto wake mmoja na aliamini kabisa alikuwa njiani kumpoteza mtoto wake mwingine.
“Naye atakufa?” aliuliza Theo huku akimwangalia daktari.
“Theo! Ni vigumu sana kukwambia hili!” alijibu daktari.
“Niambie tu. Hata kama kuniumiza zaidi, niumize tu,” alisema Theo.
Tatizo hilo lilikuwa kubwa, kitaalamu hujulikana kama Acute decompensated heart failure (ADHF) ambapo mtu analipata mwisho wa siku anakuwa na ugumu katika mfumo wa upumuaji.
Moyo utakaposhindwa kufanya kazi yake vizuri, kutakuwa na tatizo jingine kwenye misuli yake hivyo kutampelekea mgonjwa kuwa na maumivu makali mwilini mwake.
Kwa kawaida tatizo hilo mara nyingi huwakuta watu wazima lakini kitu cha kushangaza kabisa, lilimpata mtoto mdogo kama Rachel.
Hilo liliwachanganya madaktari, walihisi kabisa uhai wa mtoto huyo haukuwa wa muda mrefu, mwaka huohuo kulikuwa na uwezekano wa kufariki dunia.
“Kwa hiyo atakufa?”
“Ila si leo!”
“Lakini atakufa?” aliuliza Theo huku akimwangalia daktari ambaye kulijibu swali hilo kwake kulikuwa na ugumu mkubwa.
Ukimya wake ulikuwa jibu tosha kwa Theo kwamba ni kweli mtoto wake angekufa kwani kwa jinsi hali ilivyoonekana, hakukuwa na ujanja wowote wa kuweza kuokoa maisha yake, na kama wangetaka kufanya hivyo basi wangetumia kiasi kikubwa cha pesa.
“Ni lazima apatiwe matibabu makubwa zaidi,” alisema daktari.
“Nitatumia hata utajiri wangu wote ilimradi mtoto wangu apone,” alisema Theo.
Kilichofuata ni kutoka humo na kwenda katika chumba alicholazwa mke wake, alikaa katika kiti cha pembeni huku akimwangalia tu jinsi alivyokuwa kimya kitandani.
Alikumbuka namna mke wake huyo alivyokuwa na hamu ya kutaka kuzaa watoto wenye afya njema, alijua ni kwa jinsi gani alikuwa na hamu ya kuwaona, je, nini kingetokea kama angemwambia kuwa mtoto wake mmoja alifariki dunia na huyu aliyebaki naye alikuwa kwenye hatari ya kufa?